Dk Magufuli awawashia moto Tanroads

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,422
911,172
Dk Magufuli awawashia moto Tanroads Saturday, 11 December 2010 20:59

Habel Chidawali, Dodoma

WAZIRI wa Ujenzi Dk John Magufuli amewashukia watendaji wa wizara yake na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na kuwataka waepuke rushwa wanayoikwapua kupitia ujenzi wa barabara za lami.

Dk Magufuli amewataka watumishi hao kuongeza umakini katika utendaji wao wa kazi kabla hajamfukuza mmoja baada ya mwingine na kuwaacha watumishi wazalendo, wanaoguswa na umaskini wa mtanzania.

Dk Magufuli alisema hayo alipokuwa anakutana na viongozi wa serikali mkoani Dodoma ambako pia alieleza kuwa, kama aliweza kumfukuza kazi Meneja Mkuu wa Tanroad hivi karibuni, Ephrem Mrema hataona shida kuwatimua watumishi wa chini wasiokuwa waadilifu.

Waziri Magufuli ambaye wakati wa utawala wa awamu ya tatu, alikuwa waziri wa ujenzi kabla ya kuhamishiwa wizara nyingine, amewaeleza watendaji hao kuwa ameanzisha mkakati maalumu kuisafisha wizara ya Ujenzi ambayo kwa muda mrefu, imeonekana kuwa kinara wa ufisadi katika kupitisha zabuni za ujenzi wa barabara.

Alisema ikilinganishwa na nchi zingine barani Afrika, Tanzania ndiyo yenye gharama za juu za ujenzi wa barabara. Hii inachangia maskini wa nchi na watu wake.

"Sitaki tena kusikia eti kilometa moja ya barabara inajengwa kwa Sh1.2 bilioni. Huu ni wizi mkubwa. Watu wanapanga bei za juu kisha wanazifuata fedha hizo kwa wajenzi na kuzichukua. Nasema hiki kitengo nitakufa nacho," alisisitiza Magufuli.

Akitolea mfano wa nchi kadhaa duniani na bila kutaja angependa gharama za ujenzi ziwe kiasi gani, Dk Magufuli alisema hakuna sababu ya kutumia fedha nyingi kiasi hicho, kujenga barabara wakati nchi ni maskini.

Dk Magufuli alieleza mikakati yake katika kipindi cha uongozi wake kuwa ni kufanya kazi na watu wenye weledi na ambao ni wazalendo, wanaoipenda nchi yao na kuionea huruma siku zote katika kubana matumizi ya fedha za walipa kodi.

"Mnaniangalia tu, naomba sana mniombee kwa kuwa nimeanza kazi hii kwa nguvu zote na tayari nimeshamtuma Naibu Waziri wangu kutembelea mikoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa wakati mimi naanza na mikoa hii ya Dodoma na Morogoro lazima tukimbie," alisema.
Katika hatua nyingine Dk Magufuli alizungumzia tabia ya watu kujenga katika maeneo ya akiba ya barabara akisema kuwa sio sahihi kwani ni hatari kwao kuwa wakibomolewa, hawatalipwa chochote.

Alitolea mfano wa barabara ya Dar es Salaam- Mlandizi ambayo upanuzi wake ulihusisha kubomoa zaidi ya nyumba 3,000, lakini waliolipwa ni nyumba saba tu na hivyo akasema wale wote waliojenga nyumba zao katika maeneo ya akiba ya barabara wajiondoe mapema wenyewe.

Dk Magufuli ambaye ni Mbunge wa Chato, mkoani Kagera alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwakamata na kuwaweka rumande matajiri wote waliojenga nyumba zao katika maeneo barabara bila ya kujali fedha zao na nafasi zao kitaifa.

Alimtaka Mkuu huyo wa mkoa kutowaogopa watu hao kama alivyofanya yeye wilayani Chato ambako aliwabomolea nyumba na wananchi wa Jimbo hilo, bado wakampitisha bila kupingwa kuwa mbunge wao.
 
Yeye na msaidizi wake ni - the right tool for the right job
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom