Dk. Gideon Shoo: Tuwapime walioteuliwa kwa kazi na si kwa majungu

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
HAKUNA ubishi hata kidogo kwamba siasa ni kitu muhimu sana katika jamii yoyote ile. Ni katika siasa ndipo tunapokutana na mahusiano mbalimbali iwe ni kiuchumi au kijamii. Haiyumkiniki kuishi bila kuwa ndani ya siasa kwa namna moja au nyingine.

Hata hivyo, katika nchi yetu kwa miaka mingi sasa kumekuwapo na mazingira ambayo tunaweza kuyaita kwamba yasiyokuwa na neema yanayotokana na jinsi ambavyo siasa inatumika. Tumekuwa ni taifa la siasa kwa kila namna.

Siasa imeachiwa kutawala maisha yetu kiasi kwamba kila linalofanyika linaangaliwa kwa jicho la kisiasa.

Hili lina sura nyingi na athari zake ni mbaya na nzuri. Ni nzuri kwa sababu tunatambua kwamba kila kitu ambacho kinafanyika katika jamii yetu ni matunda ya siasa zetu. Tunapozungumzia upatikanaji wa huduma zozote zile tunamaanisha utekelezaji wa uamuzi wa kisiasa. Hilo halina ubishi.

Kwa miongo kadhaa sasa tumekuwa taifa la watu wa siasa. Hii pengine inatokana na historia ya taifa letu hususan katika miaka ile ya kushiriki kikamilifu katika harakati za kupigania ukombozi wa Afrika na kutokomeza ukoloni na ubeberu duniani.

Wanahistoria wanajua kwamba Tanzania imo ndani ya vitabu kwa kiasi kikubwa kutokana na ushiriki wetu kama taifa katika mapambano ya ukombozi na hilo bila shaka ni sifa kubwa.

Tulikuwa taifa la watu waliotambua kwamba uhuru wa mtu mmoja hauwezi kukamilika kama aliye jirani nawe yupo utumwani. Ni falsafa sahihi kabisa.

Lakini pengine baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa na kujiingiza katika mfumo wa uchumi wa soko huria tulitakiwa kuangalia upya namna ya kuingiza siasa katika maisha yetu ya kila siku.

Inaelekea kwamba tulipokea mageuzi ya kiuchumi lakini hatukutaka kupokea mageuzi ya kisiasa. Tukabaki kuwa ni taifa la siasa za ukombozi lakini katika mazingira ya uchumi wa soko huria au tuseme uchumi wa kibepari ambao sheria zake ni tofauti na zile za uchumi wa kijamaa ambao soko lake linahodhiwa na dola.

Kwa muda mrefu sasa kila uchao mada kuu zinazojadiliwa hapa nchini ni za kisiasa. Siasa imeachiwa kutawala kila kitu na kinachosikitisha zaidi ni siasa zisizokuwa na tija sana katika uchumi wetu.

Watanzania wameaminishwa mambo mbalimbali ya kisiasa na ukichunguza utagundua kwamba ama ni hoja zinazolenga katika kuwanufaisha watu fulani kiuchumi au ni hoja ambazo zinalenga kuvuruga ustawi wa kiuchumi na kijamii wa wananchi walio wengi.

Zinatupwa hoja kwa wananchi kama vile ni hoja nzito zinazolenga katika kuboresha ustawi wa walio wengi lakini ukichunguza unagundua kwamba ni hoja hafifu zinazolenga katika kufanikisha malengo binafsi ya mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu. Linainuliwa bango la maslahi ya umma kiupotoshi ili kufanikisha lengo lililojificha la maslahi ya kikundi kidogo cha watu wenye malengo ya kiuchumi, kijamii au kisiasa.

Hili limejitokeza tena wiki iliyopita wakati Rais John Pombe Magufuli alipotangaza Baraza la Mawaziri ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi.

Mara baada ya Dk. Magufuli kutangaza Baraza kulianza kusikika maneno ya hapa na pale kujadili uteuzi wake huo. Hakuna tatizo hata kidogo kujadili uteuzi wa Rais Magufuli. Ni haki kabisa wananchi kujadili majina ya walioteuliwa na kila mmoja wetu anayo haki ya kumkubali au kumkataa ye yote yule, kwa mtazamo wake.

Jambo linalochosha na kukera ni pale zinapoonekana wazi jitihada za makusudi za kutaka kumlazimisha Rais atengue uteuzi wa baadhi ya watu kwa sababu ambazo kiuhalisia hazina mashiko hata kidogo.

Zimekuwapo na jitihada kubwa za kumlazimisha Rais eti ukifikiria upya uamuzi wake wa kuwateua baadhi ya watu kushika nyadhifa za uwaziri akiwamo Profesa Sospeter Muhongo.

Si jambo baya hata kidogo kumshauri Rais ili afanye maamuzi yenye faida kwa taifa. Lakini siamini kwamba Rais katika uteuzi huu alioufanya alikosea kiasi cha baadhi yetu kuanza kuwasakama wale walioteuliwa kwa kusambaza ujumbe na hata kuandika habari zinazowahusu kwenye vyombo vya habari.

Nikichukua mfano wa hoja inayotolewa dhidi ya Profesa Muhongo kwamba eti alijiuzulu kutokana na suala la akaunti ya Escrow ya Tegeta na kwa maana hiyo hana hadhi wala sifa ya kuteuliwa kuwa waziri, tena wa wizara ile ile ambayo alikuwa akiiongoza kaika awamu ya nne, ni wazi kwamba kuna walakini wa hoja hiyo.

Suala la Escrow lililochukua muda wetu mwingi kama taifa lilijadiliwa kwa marefu na mapana. Kwa wale waliokuwa wanafuatilia kwa karibu mnyambuliko mzima wa mgogoro huo uliotishia uhai wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete watakumbuka kwamba katika mnyukano huo suala la kujiuzulu kwa Profesa Muhongo lilikuwa kwa kiasi kikubwa ni uwajibikaji wa kisiasa na sio matokeo ya ushiriki katika uhalifu wowote ule kama ulikuwapo.

Upo ushahidi usiopingika kwamba Profesa Muhongo alijiuzulu kutokana na kuwajibika kisiasa na siyo kwa kuhusika katika uhalifu wa aina yoyote ile kama ulikuwapo. Ni jambo la kusikitisha kwamba inaendeshwa kampeni dhidi ya mtu ambaye hana makosa na hiyo inafanyika kwa namna ya kutaka kumkatisha tamaa.

Ni wazi kwamba moja ya mambo ambayo yanasababisha hofu kubwa miongoni mwa wale wanaoendesha kampeni dhidi ya Profesa Muhongo ni umahiri wake katika kuchambua masuala yote yanayohusu madini na nishati, uzalendo wake katika kufanya uamuzi unaohusu rasilimali za taifa na kutambua kwamba ni haki ya Watanzania wote na kamwe si kwa ajili ya wateule wachache ambao wanataka kumilikishwa rasilimali kwa niaba ya Watanzania.

Profesa Muhongo anasema kwamba ushiriki wa Watanzania katika uchumi mpana, hususan katika sekta ambazo ni za mitaji mikubwa sana kama vile utafutaji wa mafuta na gesi baharini utafanyika kupitia mashirika ya umma. Kwa mashirika ya umma kuwa na vitalu vya mafuta na gesi ni kwamba itatoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kushiriki kwa kununua hisa.

Hata hivyo, msimamo huo wa Profesa Muhongo unapingwa na wanaompiga vita ambao wanadai kwamba njia ya Watanzania kushiriki katika sekta ya mafuta na gesi ni kwa wizara husika kuwamilikisha Watanzania wachache vitalu vya mafuta na gesi.

Kwa kuwamilikisha vitalu vya mafuta na gesi si kwamba Watanzania wanafaidika bali wanaomilikishwa ndiyo watakaoamua wafanye nini na vitalu hivyo. Uzoefu na ushahidi upo, unaonesha kwamba vitalu hivyo huishia kuuzwa kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi. Kwa maneno mengine, watu hawa wanaojivisha koti la uzalendo huishia kuwa madalali wa mabepari.


Haishangazi kuona baadhi ya watu hawa wakitumia pesa nyingi kwenye kampeni za kumchafua Profesa Muhongo au mtu mwingine yeyote anayeonekana kukwamisha azma yao ya kutaka kuwanyonya zaidi wananchi, huku wakizuga kwamba wanapigania maslahi ya wazawa.

Hizi jitihada za kuiweka nchi katika mijadala ya kisiasa ya kudumu hazina faida hata kidogo.

Na haziwezi kuwa na faida kwa sababu mijadala yenyewe hailengi katika kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi bali inalenga katika kuchafuana kwa lengo la kuwakatisha tama watendaji wazuri ambao wanao uwezo wa kutatua matatizo na kuboresha maisha ya Watanzania.

Hili hatutakiwi kulikubali hata kama wanaolitaka liwe hivyo wanao ukwasi mkubwa na vyenzo za kusambaza sumu mbaya.

Tunatakiwa kujitambua kama taifa. Aidha, ni muhimu tukajua maslahi yetu kama taifa yako wapi na nani anayeweza kwa dhati kabisa kusimamia maslahi yetu na kuhakikisha kwamba tunafaidika wote.

Hatuwezi kukaa kimya kama taifa tunaposhuhudia jitihada za makusudi zinazofanywa na mtu au kikundi cha watu kwa lengo la kuhakikisha kwamba hakuna mabadiliko ya kweli katika maisha yetu. Mabadiliko ya kweli hayaletwi kwa majungu na kuhukumiana pasi na ushahidi wowote wa maana na mbaya zaidi bila ya kufuata sheria.

Rais amewateua wasaidizi wake.

Tuwaache wafanye kazi ambayo amewaagiza kuifanya. Kazi yetu iwe ni kuhakikisha kwamba tunapeleka mrejesho kwake kuhusu utendaji wa hao wateule wake na si kumlazimisha awatimue hata kabla ya kuanza kazi.
Tuwape muda na kisha tuwapime walioteuliwa kwa kazi si kwa majungu.

Mwandishi wa makala haya Dk. Gideon Shoo, ni mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Chanzo:
Raia Mwema
 
Dr.Shoo asante kwa uandishi wako mahiri.Haiwezekani watu wachache wakayumbisha Nchi kwa maslahi binafsi.
 
Dr Shoo umepiga vizuri sana, mawakala wa mafisadi wasitake kumlazimisha Rais JPM atengue uteuzi wa Prof Muhongo
 
Hayo ni maoni yake Dr shoo, pengine anabembeleza ukurugenzi wa mawasiliano je, hatujasahau ulaji alopata msharika mwenzie Salva. Mponde asiyekubaliana na watawala upate urojo.
 
Dr.Shoo asante kwa uandishi wako mahiri.Haiwezekani watu wachache wakayumbisha Nchi kwa maslahi binafsi.

Bahati mbaya baadhi ya watu wanashindwa kutofautisha mazingira na taratibu zinazozingatiwa wakati wa kujiuzuru.Kuna kujiuzuru kwa kutunza heshima(resignation with honour).Hii inamsafisha muhusika na kumuongezea hadhi,sifa au thamani.Pia kuna kujiuzuru kwa kuwa muhusika au mshiriki katika kashfa au makosa(resignation with stigma).Hii inampunguzia sifa au hadhi kiongozi muhusika katika jamii na wakati mwingine anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.Dr Shoo ameelezea vizuri kuhusu Prof.Muhongo kwani hakuhusika kwa namna yoyote ile tukiachia kuwa alikuwa ni waziri mwenye dhamana.
 
Ili kumpima Magufuli na timu yake itaraishwe cheki list ya vipaumbele vyake, ili tuje kumhukumu navyo next time.
 
Prof. Muhongo anatosha. mwenye ushahidi wowote dhidi yake asipoteze muda.aende mahakamani.
 
Back
Top Bottom