Diwani wa CCM akusudia kuhamia upinzani

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797


na Sitta Tumma, Mwanza


DIWANI wa kata ya Lugata, jimbo la Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, Adrian Tizeba (CCM), ametangaza kutaka kukihama chama hicho kwa madai ya kuundiwa fitna chafu na baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwemo mtu aliyemtaja kuwa ni Mbunge wa jimbo la Buchosa, Dk. Charles Tizeba (CCM).


Diwani huyo ambaye ana uhusiano na mbunge wa Buchosa, Dk. Tizeba, alisema anataka kujiondoa na kujiunga na upinzani baada ya kuchoshwa kupakwa matope kunakofanywa na makada wenzake wenye nia ya kumdhoofisha kisiasa.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Mwanza hivi karibuni, Diwani Tizeba alisema viongozi hao akiwemo mbunge wa Buchosa wanamhofia huenda mwaka 2015 akagombea ubunge jimbo hilo kwa tiketi ya chama cha upinzani.


"Kuna barua nimeikamata ikiwa imeandikwa na mbunge wa Buchosa, Dk. Tizeba, kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, akitumia kivuli cha wananchi wa kata ya Lugata ambao baadhi yao ni marehemu. Barua hii imelenga kunichafulia heshima, jina na sifa yangu ndani na nje ya CCM, na jamii kwa ujumla.


"Barua hii ni ya Septemba 20, mwaka huu, inasema, Tizeba kutokana na utovu wake wa nidhamu inasemekana anajiandaa kugombea ubunge ili apambane na mdogo wake Dk. Charles Tizeba ambaye ni mbunge wa sasa wa jimbo letu kupitia CCM katika uchaguzi ujao wa 2015," alisema.

Alisema baada ya kuikamata hiyo barua, alifanya uchunguzi kubaini majina ya walioorodheshwa kwenye barua hiyo, na kwamba baadhi yao alibaini ni marehemu wa muda mrefu na kwamba baadhi yao walikuwa si wakazi wa kata ya Lugata.

"Mimi nina akili timamu, naamini asilimia zote 100 aliyeandika hii barua ni mdogo wangu ambaye ni mbunge wa Buchosa. Niko tayari kwenda kwenye vipimo katika hili na itathibitika hivyo. Kwa maana hiyo nafikiria kuihama CCM muda wowote, naamini wananchi wataniunga mkono," alisema diwani Tizeba.


Kwa mujibu wa diwani huyo wa Lugata, ambaye amewahi kuwa Katibu wa NCCR-Mageuzi mkoa wa Mwanza kuanzia mwaka 1994-2005, amechoshwa na siasa za fitna, majungu na siasa uchwara ndani ya CCM, hivyo anatarajia kutimiza azma yake hiyo ya kuondoka ndani ya chama hicho tawala na kuhamia chama kimojawapo cha upinzani, ikiwemo CHADEMA.


Alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo dhidi yake, mbunge wa Buchosa, Dk. Tizeba, alibeza na kusema: "Mambo hayo hayana mashiko, si jambo la kufuatilia. Huyu ni kaka yangu kabisa ninayemfuata...anatakiwa aniite aniambie niweze kujitetea. Ila hiyo barua na mimi nimeisikia."



 
Back
Top Bottom