Dirisha lilinusuru maisha yetu: SIMULIZI YA MJANE AMBAYE NYUMBA YAKE ILIBOMOLEWA NA TEMBO | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dirisha lilinusuru maisha yetu: SIMULIZI YA MJANE AMBAYE NYUMBA YAKE ILIBOMOLEWA NA TEMBO

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by HUNIJUI, Oct 20, 2012.

 1. HUNIJUI

  HUNIJUI JF-Expert Member

  #1
  Oct 20, 2012
  Joined: Oct 10, 2012
  Messages: 1,441
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 135
  “NIKIWA na wanangu ndani ya nyumba, ghafla tukasikia paa la nyumba yetu linasukwasukwa, mkonga wa tembo ukiwa tayari uko ndani, tulitamani dunia ipasuke….Watoto wakanikumbatia….hakuna wa kulia…wote tukawa tumepigwa
ganzi!”

Ni mjane Eliada Astablo Msilikale (46), mkazi wa Kijiji cha Makundusi, 
Kata ya Natta, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara ambaye na wanaye watano hawana makazi baada ya tembo kuezua paa la nyumba yao akitafuta chakula.
  

Hali hiyo inamfanya aishi kwa majirani yeye na familia yake kutokana na kukosa makazi akitafakari namna ya kuendesha maisha yaliyojaa kila aina ya taabu.

Ilivyotokea
 Ilikuwa Septemba 26, mwaka huu saa 2:05 usiku akiwa ndani ya kibanda chake, alisikia kwa nje uwepo wa kitu kisicho cha kawaida hali iliyowafanya kuzidisha utulivu zaidi ili waweze kusikia ni nini kinachojiri.

Utulivu wao ulijengwa na hofu baada ya kubaini kuwa anayezunguka ni
tembo katika eneo la uwanja wa nyumba.

  Wakiwa katika taharuki hiyo, 
waliona mkonga wa tembo ukinyanyua paa la nyumba yao ya nyasi.

“Watoto wangu wakaniangukia kwa hofu huku paa likizidi kusukwa
sukwa…kibatari kikazima ikawa giza… nyasi zinatudondokea, baada ya muda kukawa kimya…nikawazoa zoa wanangu wakiwa katika taharuki kubwa
nikawaomba wajikaze,” anasema kwa masikitiko.


  Mama huyo kwa ushujaa anadai kuwa alipobaini tembo amesogea shambani akawachukua watoto wake na kuwapitisha dirishani kisha wakakimbilia kwa jirani yao.

“Haikuwa kazi rahisi maana ilikuwa giza. Kwa jirani ni mbali…na kama
tembo akiamua kutufukuza atatumaliza.

  “Kwanza nilitafuta upepo
unakoelekea nikabaini, ikawa rahisi kumkwepa maana kama angesikia
harufu yetu alivyokuwa na hasira angetumaliza,” anabainisha.

Wakiwa kwa jirani yao, walikokimbilia hata hawajaingia ndani, tembo huyo
kwa hasira alirudi kwenye mji huo na kuangusha paa lote, kitendo
kilichowafanya kuishiwa nguvu kabisa kwa kuwa huenda angewakuta ndani angewaua kabisa.
  

Kilichomsukuma tembo kuezua paa

Kwa mujibu wa mama huyo na majirani zake, wanadai kuwa tembo huyo alikuwa akitafuta chakula hasa baada ya kusikia harufu ya mahindi kwa ndani ndipo alipoamua kuezua paa hilo aweze kupata chakula ,kwa kuwa mashambani hakuna mazao tena.


  Hatima ya maisha yake
 Anasema kwa sasa hana mbele wala nyuma kwa kuwa nyumba hiyo ndiyo ilikuwa tegemeo la yeye na watoto wake.

Eliada anadai kuwa alihamia kijijini hapo mwaka 2005 na kuanza
kujishughulisha na kilimo. Hata hivyo, amekuwa havuni vizuri
kutokana na mazao yao kuliwa na wanyama.
  

Mwanaye asimulia
 Rehema Msilikale (12), mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Makundusi anasema tukio hilo hatalisahau katika maisha yake na haamini kama bado wako hai.


  “Binafsi niliishiwa pumzi kwa muda. Mwili ukaganda kwa hofu…nilishtuka
baada ya kushtuliwa na mama yangu akitutaka tupitie dirishani.

  “Tulipita na mdogo wangu hadi tukafika kwa jirani na sikuamini na siamini hadi sasa kama tuko hai maana ule mkonga ulivuruga sana paa,” anasema Rehema.

Kijana aeleza alivyonusurika Paulo Elias (25), kijana mkubwa wa mama huyo anasema wakati tukio linatokea alikuwa kwa jirani yake lakini alisikia vurugu zikiendelea.

  “Wakati ninakwenda nyumbani, nilipomulika kwa tochi nilimwona tembo mkubwa anazunguka hapa nyumbani, nikajaribu kumtisha akimbie, mama akasema nisipige kelele atatushambulia humu ndani,” anadai.

Pamoja na kuwa ana kibanda chake pembeni alishindwa kulala huko kwa
madai kuwa ingekuwa rahisi kushambuliwa na tembo, wakahamia kwa jirani yao wote.

Jirani yao
 Sadoki Majura (65) anasema kuwa amelazimika kuwapokea waathirika hao kwa kuwa hawana namna ya kujisitiri wakati wakisubiri utaratibu mwingine wa kuwasaidia kwa kuwa tatizo la wanyama hao ni sugu na hawajawahi kupata nafuu.
  

“Ndani ya mwezi huu tu, tembo wamevunja maghala na nyumba za watu zaidi ya sita na kula mazao tena usiku na hata alfajiri watu wakiwa shambani…tunapotoa taarifa hatupati msaada kwa wakati,” anasema.


  Anadai kwa Mugasa Machandi jirani yake walifika jioni na kuangusha
ghala kisha wakala mtama wote, wakaenda kwa Amosi Mathias na kula mahindi, lakini nyumbani kwa Samo Sadoki walivunja mlango hawakuingia isipokuwa kwa Wanchota Masaigana waliingia ndani kwa kuvunja mlango
wakala mtama huku familia ikijificha uvunguni hadi walipomaliza.

Ofisa Mtendaji wa kijiji, 
Suzana Charanga anadai kuwa matukio ya tembo kuvamia makazi ya watu na kubomoa maghala yanazidi kushamiri lakini la kubomoa nyumba kama ilivyofanyika ni la kwanza.

  Matukio hayo yakiachwa yaendelee jamii inazidi kuwa maskini kwa kuwa kila wanacholima hawavuni na wanachovuna
kinaliwa kikiwa ghalani.


  Diwani
 Jumanne Kwiro, Diwani wa Kata hiyo anasema wahifadhi hawana msaada kwa wananchi kwa kuwa wakiitwa hawafiki kwa wakati ikiwa ni tofauti wakiambiwa kuna jangili magari hufika kwa wingi na silaha nzito nzito.
  

“Kuna kila sababu ya kuangalia upya uamuzi wa kusitisha uwindaji wa
kisheria maana kabla ya mwaka 2004 matatizo kama haya
hayakuwapo,” anasema.

Kwiro ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo anasema wananchi hawanufaiki na hifadhi zaidi ya hasara na madhara kwani hata bidhaa za kibiashara, hoteli na kambi zinazowazunguka hazifanyi biashara nao.
  
Alitoa gunia la mahindi akiahidi kuwa wanashauriana na wadau wengine ili kusaidia ujenzi wa nyumba ya mama huyo kwa kuwa matukio kama hayo yanajenga uadui kati ya wahifadhi na jamii.
  

Mbunge
 Dk Stephen Kebwe, Mbunge wa jimbo hilo alilazimika kukatisha shughuli zake na kwenda kwa mama huyo akiwa na gunia la mahindi na anavunja ukimya na kudai matatizo yanayosababishwa na wanyama kwa wakazi yamezidi na matokeo yake ni ongezeko la familia maskini.


  “Hakuna Mazingira rafiki kati ya wananchi na wahifadhi, madhara kama haya ni makubwa kwa familia hii…mwananchi akikutwa anachanja kuni anatozwa faini kubwa ama kifungo sasa kwa tukio hili hakuna aliyekuja kusaidia,” anasema.

Anabainisha, wizara imeishaelezwa lakini hawajachukua hatua kwa kuwa inatakiwa kuangaliwa vyema maana watu na wanyama wanaongezeka lakini ardhi ni ileile lazima migogoro inaongezeka.

  Anashauri uwekaji uzio ama ufugaji nyuki kama njia ya ulinzi kazi
ambazo zinatakiwa kusaidiwa na wahifadhi lakini anashangazwa na
kujikita zaidi kununua silaha nzito za kupambana na wananchi badala ya
kutumia njia shirikishi.

Mkurugenzi Mtendaji

  Kimulika Galikunga, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kupitia kwa diwani anaahidi kutoa mabati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mama huyo, ahadi ambayo diwani anadai itatekelezwa kwa kushirikisha uongozi wa kijiji na wadau wengine kuhakikisha wanamjengea nyumba mjane huyo.

Matukio mengine

  Katika Kata ya Manchira, matukio ya tembo kubomoa maghala na kula mazao ya wakulima ni ya kila siku, lakini wataalamu wa uhifadhi wanadai ongezeko la tembo kwenye makazi ya wananchi inatokana na kukithiri kwa ujangili ndani ya hifadhi na mapori ya akiba ikiwamo Kenya.

Hali hiyo inawafanya wakimbilie maeneo tulivu ambako ni kwenye makazi ya wananchi kusaka chakula.

Hao ndio tembo wa Serengeti wanaotafuta chakula hadi ndani ya nyumba
   
 2. z

  zamlock JF-Expert Member

  #2
  Oct 20, 2012
  Joined: Dec 25, 2010
  Messages: 3,849
  Likes Received: 53
  Trophy Points: 145
  aise hiyo ni hatari sana Mungu ni mkubwa sana
   
Loading...