Dini ilivyotumika kuwaunganisha watanganyika dhidi ya ukoloni visomo vya Qur'an na dua zilizofanyika wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,849
30,189
1553782537291.png

Mkutano wa TANU Mnazi Mmoja 1950s

Inategemea watu watakavyoitumia dini.

Dini inaweza kutumika kuwaunganisha watu na pia inaweza kutumika kuwagawa.

Mikutano ya mwanzo ya TANU pale Mnazi Mmoja ilifunguliwa kwa dua na watu wakisoma Surat Fatha na kutikia dua hiyo kwa pamoja.

Aliyekuwa akiongoza dua hii alikuwa Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU.
Leo ni tabu sana kwa mtu kuamini kuwa hali ilikuwa hivi kuwa hata mikutano ya ndani ya TANU pale New Street ilikuwa ikifunguliwa na kufungwa kwa dua na Nyerere akiwapo.

Mwalimu Nyerere katika hotuba yake maarufu kwa Wazee wa Dar es Salaam Ukumbi wa Diamond wakati wa kustaafu urais mwaka wa 1985 alieleza kuhusu dua aliyofanyiwa na akashiriki nyumbani kwa Mzee Jumbe Tambaza.

Hotuba hii imekuwa maarufu sana khasa kipande hiki anachoeleza jinsi yeye Mkristo alivyopokelewa na Waislam wa Dar es Salaam akiwa na vijana wenzake Abdul Sykes na Dossa Aziz.

Hawa vijana wawili Abdul Sykes na Dossa Aziz, marafiki wa Baba wa Taifa ndiyo waliompeleka Mwalimu Nyerere kwa Mufti Sheikh Hassan bin Ameir kumtambulisha na kutaka msaada wake akubalike kwa Waislam na kuanzia siku ile Sheikh Hassan bin Ameir na Nyerere walikuwa wazalendo wawili wakisaidiana katika kudai uhuru wa Tanganyika Sheikh Hassan akiuza kadi za TANU ndani ya misikiti ya Dar es Salaam alikokuwa akidarsisha.

Turejee kwenye visomo na dua wakati wa kudai uhuru.

Lilikuwa jambo la kawaida sana wakati ule kwa Waislam waliokuwa katika mapambano na ukoloni kutanguliza mambo yao yote kutaka msaada wa Allah.

Hili lilikuwa jambo lililokuwa linakuja hata bila ya kufikiri.

Mwaka wa 1949 kabla ya mgomo wa makuli wa Bandari ya Dar es Salaam, walifanya kisoma na dua kubwa na baada ya hapo ndipo walipoingia barabarani kwa maandamano kama ishara ya kuanza mgomo.
Abdul Sykes alihusika sana katika mgomo huu.

Mwalimu Nyerere kwa hiyo hakuwa kiongozi wa kwanza katika harakati kufanyiwa kisomo na Waislam.
Mwalimu Nyerere yeye haya hakuyajua kwani alizikuta harakati katikati.
Abdul Sykes alikuwa Market Master Kariakoo Market nafasi kubwa sana wakati wa ukoloni na yenye wasaa na fursa za kutosha.

TANU ilipoanza Abdul Sykes akawa anauza kadi za TANU pale sokoni na Nyerere alikuwa hapungui ofisini kwake.

Special Branch wakiwafuatilia na siku moja Abdul Sykes akavamiwa na mkubwa wake Mzungu, Town Clerk ambae soko lilikuwa chini yake.

Abdul na huyu Mzungu walipambana kwa maneno makali Abdul akidai kuwa TANU kilikuwa chama halali na si kosa kuwa na kadi zake.

Hofu iliyotanda pale sokoni ilikuwa Abdul atafukuzwa kazi.
Abdul wakati ule Abdul alikuwa kijana wa miaka 30.

Wazee wafanyabiashara pale sokoni akina Sharif Mbaya Mtu, Mshume Kiyate, Shariff Abdallah Attas, huyu alikuwa mfanyakazi wa soko, mkusanyaji ushuru wa nafaka pale sokoni walijikusanya na pakafanyika dua kubwa ya kisomo na wakachinja mnyama.

Hii ilikuwa ndiyo dua ya kwanza kwa TANU kufanya kisha zikafuata dua aliyofanyiwa Rashid Ali Meli na ile ya Nyerere.

Rashid Ali Meli yeye alikuwa mweka fedha wa Dar es Salaam Municipal Council.

Rashid Ali Meli alifungua safe yake ofisini akatoa fedha kuikopesha TANU akamkabidhi Iddi Faiz Mafungo aliyekuwa Mweka Hazina wa TANU ili aziingize katika mfuko wa safari ya Nyerere UNO.

Siku ya pili wakaguzi wakaja ofisini kwake kufanya ukaguzi bahati nzuri hawakuanza na kukagua fedha taslimu.

Ilikuwa wazi kuwa endapo wakaguzi watagundua kuwa kuna upungufu wa fedha Rashid Ali Meli atashtakiwa kwa wizi na atafungwa.

Taarifa hizi ziliipofika ofisi ya TANU kitu cha kwanza kabisa ikawa pafanywe dua.

Baada ya kisomo hiki cha Rashid Ali Meli kikafuatia kisomo cha Lindi alichofanyiwa Baba wa Taifa na Sheikh Mohamed Yusuf Badi mwaka wa 1956 kisha ikafuatia dua ya Mnyanjani, Tanga kabla ya kwenda Tabora kwenye mkutano wa Kura Tatu uliotishia kuigawa TANU katika mapande mawili.

Picha hizo hapo chini ni Mkutano wa TANU Mnazi Mmoja miaka ya mwanzo ya TANU, picha ya pili ni kushoto Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia naJulius Nyerere. Picha ya tatu ni Soko la Kariakoo kama lilivyokuwa katika miaka ya 1950 na picha ya nne ni Shariff Abdallah Atttas. Picha ya mwisho kulia ni Lawi Sijaona, Abdul Sykes, Julius Nyerere na Dossa Aziz katika hafla Ukumbi wa Arnatouglo kumuaga Nyerere safari ya pili UNO 1957.

Namaliza kwa kusema kuwa hivi ndivyo Waislam walivyoitumia dini yao katika kuleta umoja wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika umoja ambao hivi sasa haupo tena kwani uhuru ulikuja na changamoto zake na moja ya changanoto kubwa ikawa kuzuka kwa uadui dhidi ya Uislam ikawa chochote kinachowahusu Waislam hakiangaliwi kwa jicho la kheri na wale walioshika madaraka ya serikali.

Taratibu hata historia hii ya wazalendo hawa waliopigania uhuru ikawa haitakiwi na zikafanyika juhudi kubwa na za makusudi kuwafuta mashujaa hawa katika historia ya Tanganyika.

Wazee wetu wameonyesha kuwa dini inaweza kutumika kuwaunganisha watu.
Bahati mbaya sana leo dini inatumika kuwabagua watu.

MWISHO
 
Back
Top Bottom