Dhima ya TBC katika kazi ya elimu kwa umma: Mbona Festus Makerubi anatumia Roho Mtakatifu kulijingisha Taifa?

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478
1605449715642.png

Dr. Ayub Rioba, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa, TBC

Katika kipindi cha Nyimbo Zetu kilichorushwa asubuhi ya tarehe 15 Novemba 2020, kupitia luninga ya TBC, mtangazaji wa TBC, Festus Makerubi, amerudia mara nne maneno ambayo meseji yake ya msingi inawakilishwa na maneno yafuatayo:

"Mungu amejenga ukuta wa Roho Mtakatifu kuizunguka nchi yetu ya Tanzania. Hivyo, nchi ya Tanzania imekingwa na ugonjwa wa korona. Lakini majirani zetu bado wanafunika pua na midomo yao kwa sababu ya korona. Wote tumshukuru Mungu kwa muujiza huu." (My paraphrase).

Lakini, huu ni uwongo ambao haupswi kusambazwa na TV ya Taifa inayoongozwa na wasomi, yaani watu ambao wamefuzu katika mafunzo ya kutafiti, kuhakiki na kuchuja habari kabla ya kuzisambaza kwa umma.

Hannah Beech, Alissa J. Rubin, Anatoly Kurmanaev na Ruth Maclean, kupitia Jarida la New York Times, la tarehe 25 Septemba 2020, tayari wamechapisha utafiti unaomtia hatiani mtangazaji wa TBC na mabosi wake.

Utafiti huo una kichwa cha maneno haya:

"THE COVID-19 RIDDLE: WHY DOES THE VIRUS WALLOP SOME PLACES AND SPARE OTHERS?"

Yaani, "MAAJABU YA UGONJWA WA KORONA: KWA NINI KIRUSI CHA COVID-19 KINAZIADHIBU BAADHI YA NCHI NA KUZIHURUMIA NCHI NYINGINE?"

Waandishi hawa wametoa mifano mingi kuonyesha kwamba swali hili halina jawabu la kisayansi, kifalsafa, wala kiteolojia.

Mifano hiyo ni pamoja na Dominika vs jirani yake Haiti, Indonesia vs jirani yake Malaysia, Singapore vs jirani yKe Japan, na Thailand vs jirani yake India.

Hawa ni majirani ambao wanaonyesha pengo kubwa la kesi za korona, wakati wote wako eneo moja la kijiografia, wana utamaduni mmoja, muundo wa demografia unafanana, na hatua zilizochukuliwa na serikali ni sawa.

Vivyo hivyo, hapa Tanzania hakuna kesi nyingi za korona, lakini jirani zetu wa Kenya wanazo kesi nyingi.

Hivyo, mfano wa Tanzania na majirani zaKe sio mfano pekee duniani, na haupswi kubebwa kichwa kichwa kama ushahidi wa kutendeka kwa muujiza.

Yaani, nadharia ya Mungu mwenye kuwapendelea baadhi ya watu na kuwaua watu wengine wasio na hatia haina mashiko. Hayo ni mawazo ya kubahatisha.

Kwa hiyo, nina tatizo na ujumbe huu kwa sababu za kisayansi, kifalsafa, na kiteolojia.

Lakini tatizo kubwa zaidi ni dhima ya vyombo vya habari kama vile TBC, chombo cha kitaifa kinachoongozwa na kaulimbiu ya UKWELI NA UHAKIKA.

Maneno ya Makerubi yanakinzana na kaulimbiu ya TBC. Ni maneno yenye madhara ya KULIJINGISHA TAIFA.

Kujingisha taifa ni kusindika raia wenye maarifa haba ama kwa njia kuwanyima taarifa kabisa, au kuwapa taarifa haba au kuwapa taarifa potofu--disinformation.

Katika masomo ya ujasiriadola na usalama wa nchi hii huwa ni ajenda kubwa.

Na kama Mkurugenzi wa TBC, Dr. Rioba, anavyojua fika, hapa duniani, baada ya uovu wa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia, uovu wa pili dhidi ya ubinadamu ni kuwajingisha watu, yaani stupefaction of humanity.

Kusema uwongo ni kitendo cha kuinyima akili nafasi ya kufanya kazi yake ya kuuongoza mwili katika matendo mbalimbali.

Yaani, uwongo unasababisha psycho-somatic disintegration kama itokeavyo pale mtu anapokunya pombe hadi kupoteza balance wakati wa kutembea.

Kwa hiyo nina ombi maalum kwa DR. AYOUB RIOBA, MKURUGENZI MTENDAJI WA TBC:

Naomba usimamie vizuri chombo hiki ili kisiwe chanzo cha ujingishaji wa kitaifa.

Ukumbuke kuwa, ili kaulimbiu ya ukweli na uhakika iwe na maana lazima TBC izingatie msingi wa kiepistemolojia na kielimu usemao kuwa:

"KNOWLEDGE IS JUSTIFIED TRUE BELIEF."

Yaani,

"MAARIFA NI IMANI AMBAYO UKWELI WAKE UMETHIBITISHWA KWA NJIA YA KUKUSANYA USHAHIDI MWINGI WENYE KUIBEBA IMANI HIYO NA HIVYO KUUPIKU USHAHIDI KIDOGO WENYE KUTHIBITISHA IMANI ILIYO KINYUME CHA IMANI INAYOPENDKEZWA."

Kuna mambo matatu hapa: belief (imani), justification(uthibitisho), na truth (ukweli). Tuone moja baada ya jingine.

Imani aliyo nayo mtu ni taarifa juu ya ulimwengu unaomzunguka mtu huyo zikiwa zimehifadhiwa katika kichwa chake. Taarifa hizi zinaweza kuwa ukweli mtupu, uwongo mtupu au mseto wa haya mawili.

Kwa kuzingatia mtazamo wa falsafa mamboleo, kuna imani za aina tatu: imani za kiufafanuzi (descriptive beliefs), imani za kikanuni (normative beliefs), na imani za kitunu (evaluative beliefs).

Imani za kiufafanuzi (descriptive beliefs) ni matamko juu kuwepo au kutokuwepo kwa vitu fulani fulani hapa ulimwenguni. Mfano ni tamko kwamba:

-- wachawi wapo,

-- Mungu yupo,

-- Malaika wapo,

--kuna ukuta wa Roho Mtakatifu uliojengwa kuizunguka Tanzania ili kuilinda dhidi ya ugonjwa wa korona,

-- Mungu aliyefunuliwa katima Biblia anazo nafsi tatu,

--Mungu wa Wakatoliki anakataza matumizi ya kondomu,

-- Mungu wa Waislamu anakataza unywaji wa pombe na ulaji wa kiti moto,

-- kila binadamu ni mbinafsi,

-- kila binadamu ni mkarimu,

-- dunia ni sayari ambayo ni tambarare kama meza,

-- dunia i sayari ambayo ina muundo wa tufe kama mpira wa miguu,

-- Nchini Tanzania hakuna ugonjwa wa korona,

-- Nchini Tanzania iko katika ukanda wa tropiki,

-- tendo la ngono ya jenitalia kwa jenitalia likifanyika katika msimu wa rutuba ya uzazi kwenye mwili wa mwanamke huweza kuleta mimba,

-- tendo la ngono ya jenitalia kwa jenitalia likifanyika nje ya msimu wa rutuba ya uzazi kwenye mwili wa mwanamke haliwezi kuleta mimba,

-- kila tendo la ngono ya jenitalia kwa jenitalia ni alama inayobeba maana ya umoja wa ndoa ya mwaname na mwanamume,

-- kila tendo la ngono ya jenitalia kwa jenitalia ni alama inayobeba maana ya familia iliyotokana na uzazi uliofanywa na wanandoa wenyewe,

-- kuna muungano usioweza kuvunjika kati ya maana mbili za tendo la ngono ya jenitalia kwa jenitali, yaani maana ya umoja wa ndoa ya mwaname na mwanamume na maana ya familia iliyotokana na uzazi uliofanywa na wanandoa wenyewe, n.k.

Kwa ujumla, matamko haya yanaweza kubeba ukweli (positive truth value) au uwongo (negative truth value). Ushahidi wa kitafiti ndio kigezo pekee cha kutofautisha kati ya haya mawili.

Imani za kikanuni (normative beliefs) ni imani juu ya tabia gani ambazo ni mbinu halali katika kufukuzia malengo na kinyume chake. Mfano ni imani kwamba:

-- kuua mtu asiye na hatia ili kutafuta madaraka ni tabia halali,

-- kuzini kwa lengo la kutafuta mtoto wa kiume atakayerithi mali za baba ni tabia halali,

-- kuiba fedha za jirani ili kujenga nyumba nzuri na kununua gari ni tabia nzuri,

-- kula rushwa ili kutafuta karo ya watoto ni tabia halali,

-- kusema uwongo ili kulinda heshima ya bosi ni tabia halali,

-- kumtesa raia ili atoe siri anazozijua kuhusu walikojificha magaidi ni tabia halali,

-- wanawake wanapaswa kuwatii waume zao kila wakati na kila mahali, n.k.

Imani za kitunu (evaluative beliefs) ni imani juu ya malengo gani ambayo ni mema na malengo gani ambayo ni haramu. Mfano ni imani kwamba malengo yafuatayo yanapaswa kupiganiwa na kila mtu, kila mahali na kila wakati:

-- kuwahi kazini,

-- kufanya kazi kwa bidii,

-- kuwa na afya njema,

-- kupata elimu bora,

-- kuishi katika mazingira salama,

-- kuwa na ofisi zenye utawala bora, na

-- kujenga uchumi unaojali maslahi ya watu wote ni m.

Kiwango cha ukweli wa imani kinapimwa kwa kuangalia ukubwa wa ushahidi uliopo kwenye kapu la utafiti lililoko mezani.

Ni hivi: mara zote, kila sentensi, kama vile "Ni kweli kwamba Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona," husindikizwa na sentensi nyingine mbili nyuma yake.

Sentensi hizo ni: "Sio kweli kwambaTanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona" na "Ama ni kweli kwamba Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona au Sio kweli kwamba Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona."

Tukisema kuwa, maneno "ni kweli kwamba Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona" yasomeke kama "ni kweli kwamba P," herufi ya P itawakilisha maneno "Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona."

Hivyo, "Sio kweli kwamba Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona" itasomeka kama "Sio kweli kwamba P."

Na maneno "Ama ni kweli kwamba Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona au Sio kweli kwamba Tanzania ni nchi pekee iliyo huru dhidi ya korona" yatasomeka kama "Ama ni kweli kwamba P au Sio kweli kwamba P."

Kwa kuwa, mara zote, ushahidi ulioko katika kapu la utafiti ni sawa na100%, basi kuna mambo matatu yanawezekana hapa.

Mosi, inawezekana kwamba, maneno "ni kweli kwamba P" yanaungwa mkono na ushahidi ulio zaidi ya 50% na maneno "sio kweli kwamba P" yanaungwa mkono na ushahidi ulio pungufu ya 50%.

Katika mazingira haya tunasema kuwa maneno "ni kweli kwamba P" yanapaswa kukubalika kama hitimisho la kitafiti.

Pili, inawezekana kwamba, maneno "ni kweli kwamba P" yanaungwa mkono na ushahidi ulio pungufu ya 50% na maneno "sio kweli kwamba P" yanaungwa mkono na ushahidi ulio zaidi ya 50%.

Katika mazingira haya tunasema kuwa maneno "sio kweli kwamba P" yanapaswa kukubalika kama hitimisho la utafiti.

Tatu, inawezekana kwamba, maneno "ni kweli kwamba P" yanaungwa mkono na ushahidi wa 50% na maneno "sio kweli kwamba P" yanaungwa mkono na ushahidi wa 50%, kwa maana kwamba ushahidi umefugana.

Katika mazingira haya tunasema kuwa maneno "ama ni kweli kwamba P au sio kweli kwamba P" yanapaswa kukubalika kama hitimisho la utafiti.

Na kuthibitisha ukweli wa imani, ni mchakato ambao, katika milenia ya tatu unaongozwa na modeli sanifu ya kiepistemolojia iitwayo OPHETA.

Yaani,
O-bservation (Ona),
P-uzzle definition (Baini kitendawili),
H-ypothesis formation (Otea jawabu),
E-vidence collection (Kusanya ushahidi),
T-heory formation (Toa hukumu), na
A-nnouncement for application (Tumia nadharia).

Yaani, Kuona jambo, Kubaini kitendawili, Kuotea jawabu, Kukusanya ushahidi wa kuthibitisha au kubatilisha maoteo, Kutengeneza nadharia kama hitimisho la mchakato, na Kutangaza matokeo ya utafiti ili watu wayatumie.

Hatua ya kukusanya ushahidi ("Evidence collection") inaweza kufanyika kwa kutumia mbinu za kisayansi, kifalsafa, kiteolijia au vinginevyo kulingana na kitu kinachochunguzwa.

Kama hatua hii ikifanyika kisayansi tunatarajia kuona controlled experiement ikitumika.

Walimu wote wanaujua na wanapaswa kuzingatia msingi huu wa OPHETA. Lazima wawafundishe wanafunzi wao kuuzingatia msingi huu pia.

Hata waandishi wa habari za uchunguzi wanapaswa kuzingatia kanuni ya OPHETA katika utendaji wa kazi zao.

Viongozi wa dini, watawala, na wanasiasa pia wanawajibika kuheshimu kanuni ya OPHETA kila mahali na kila wakati.

Baada ya kusema hayo, sasa namtakia Dr. Rioba na rimu yake kazi njema inayozingatia misingi ya ukweli na uhakika.

Hapa niseme tu kwamba, swaga za uchaguzi zimepitwa na wakati kwa kuwa uchaguzi sasa umekwisha.

Turudi kwenye misingi ya kitaaluma na kitafiti.

1605449921764.png

Mtangazaji wa TBC, Festus Makerubi.
 
Nimepata msamiati Mpya walau "kujingisha" uma au mtu, hii naamini itakua ni dhambi kubwa sana, ngoja nitafute kwenye mkate wa katekisimu (CCC).
 
Tatizo la wabongo wengi hatuna elimu na hata wale walio na elimu wameendekeza uoga na tumbo mbele. They are blinded either by fear or hunger.

Hata wanaosema kuwa hapa Tanzania hakuna cases za Covid19 bado wanatakiwa wajifikirie kwasababu kitu ambacho 'sirikali' imeamua ni kutokupima watu na kutoa updates tu lakini haimaanishi kuwa Covid-19 haipo.
 
Nimepata msamiati Mpya walau "kujingisha" uma au mtu, hii naamini itakua ni dhambi kubwa sana, ngoja nitafute kwenye mkate wa katekisimu (CCC).

Kazi njema. Lkn, hutaupata. Neno hili ni tafsiri ya maneno "STUPEFY" na "STUPEFACTION" alilopenda kulitumia sana Emmanuel Kant wakati wa kujadili dhana ya hadhi ya ubinadamu--human dignity--na jinsi uwongo, pombe, kazi za mikono na ngono zinavyosababisha psychosomatic disintegration na hivyo kusigina hadhi ya ubinadamu.
 
Kujingisha ndo nini iyo...?

Neno hili ni tafsiri ya maneno "STUPEFY" na "STUPEFACTION" alilopenda kulitumia sana Emmanuel Kant wakati wa kujadili dhana ya hadhi ya ubinadamu--human dignity--na jinsi uwongo, pombe, kazi za mikono na ngono zinavyosababisha psychosomatic disintegration na hivyo kusigina hadhi ya ubinadamu.
 
Back
Top Bottom