Dharula-model ya utendaji serikali ya ccm 2005-2015

rrm72

JF-Expert Member
Mar 10, 2015
508
299
Wakati tukiwa shule ya msingi, tulisikia kila mara wakubwa zetu wakimtaja Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa jina la Musa. Walielezea kuwa jina hilo lilitokana hasa na jinsi Raisn huyo wa Serikali ya Awamu ya Kwanza alivyozoea kushika fimbo kila alipoonekana hadharani. Busara zake, maono yake na jinsi alivyokuwa na uwezo wa kuelewa mambo akiwa kiongozi wa nchi iliyokuwa katika safari ngumu ya kutoka kuwa koloni kuelekea kwenye maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ni mambo mengine yaliyomfanya Nyerere apachikwe jina hilo la kiongozi wa Waisraeli waliotoka utumwani Misri kuelekea nchi ya ahadi.

Ni dhahiri kuwa Nyerere alikuwa ametutoa huko utumwani na alikuwa katika kazi ngumu ya kuliongoza Taifa kuelekea kwenye uhuru wa kweli, ambao ungemaanisha maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mussa hakufika nchi ya ahadi. Na nyerere hakufika kule alikoona ndio kuwa maziwa na asali na kama ilivyokuwa kwa Mussa, Baba wa Taifa alilazimika kuwaachia wengine waiongoze nchi kuelekea huko kwenye maono yake.

Iliwachukua miaka 40 wana wa Israeli kufika nchi ya ahadi, lakini sisi baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru bado hatuna uhakika na tulipo. Hatujui tumefika nchi ya ahadi au tumeikaribia.

Hata hivyo, ukweli kwamba mambo mengi sasa yanafanywa kwa dharura na inadhihirisha kuwa bado hatujafika. Mambo yanayohitaji subira, upembuzi yakinifu na ushirikishwaji kikamilifu wa wahusika ili kurahiusisha utekelezaji wake, yanafanywa kwa dharura. Kila jambo, hata jema, linafanywa kwa dharura.

Kwa nchi ambayo Katiba mpya imekuwa ikidaiwa kwa miaka mingi, mchakato wa kutekeleza hilo usingekuwa wa dharura-mfano ni kutotumia muda wa kutafuta sifa wa wajumbe wa Bunge la Katiba, kutokuwa na chombo cha uhakika cha maridhiano iwapo kunatokea kutoelewana, kuanisha mambo ambayo yangezua utata na kuyatafutia majibu mapema, kama suala la Muungano, na kutoangalia athari za kujaza wakereketwa wa vyama badala ya wazalendo wa nchi.

Matokeo yake kila jambo lilijadiliwa kidharura na Katiba Inayopendekezwa kupitishwa kwa dharura kiasi kwamba mchakato huo sasa hauna maana kwa wengi.

Hata suala la Askofu Josephat Gwajima, ambaye amekamatwa “kwa dharura” baada ya kumponda hadharani Kardinali Polycarp Pengo kuhusu msimamo wake dhidi ya Tamko la Jukwaa la Wakristo lililotolewa na maaskofu takriban wiki tatu zilizopita, ni la dharura. Polisi ilimkamata askofu huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ikidai alitoa matusi dhidi ya Kardinali Pengo, lakini kinachoendelea sasa ni dharura. Haijulikani hayo “matusi” yake yanahusiana vipi na mali zake, kama helikopta iliyozinduliwa kwa mbwembwe huku nchi nzima ikijua lakini leo polisi hawajui iliingiaje! Sijui matusi yake yanahusiana vipi na hati ya usajili wa kanisa, muundo wa utawala wa kanisa, namba ya usajili wa kanisa, waraka wa maaskofu na nyaraka za kuonyesha ritani.

Maana yake ni kwamba kuna watu waliotakiwa kufanya hiyo kazi kwa muda muafaka, lakini hawakuifanya kwa kuwa walijua kuna dharura itatokea ndipo wahoji.

Bunge, ambalo sasa linaonekana kuwa na watu wachache wenye uzalendo, weledi, wakereketwa wa nchi na wanaotumia muda mwingi kuchambua mambo, sasa linalazimika kuwa chombo cha kuilazimisha Serikali kukumbuka kuwa uendeshaji wa nchi haufai kuwa wa dharura. Wiki mbili zilizopita, wabunge wachache wa upinzani walilazimika kuilazimisha Serikali ishughulikie kwanza suala la kiongozi wa wafanyabiashara ndogondogo, Johnson Minja ambaye alikamatwa kwa “dharura” baada ya madai ya muda mrefu ya wajasiliamali hali kutopatiwa ufumbuzi na badala yake akajikuta akifunguliwa mashtaka mahakamani.

Hata suala la Kura ya Maoni ni kama limeangusha ghafla leo. Serikali haikujiandaa kwa vifaa vya uandikishaji na badala yake ililazimika kwenda kuazima Nigeria. Hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haikupangiwa fedha, badala yake Hazina imeombwa kwa dharura kuipa fedha kadri itakavyohitaji-dharura.

Bunge lilitakiwa lipitishe “kwa hati ya dharura” miswada miwili ya habari, lakini baada ya kelele nyingi, likalazimika kuiondoa. Haikueleweka ni kwa nini jambo lililokuwa linahitajiwa kwa muda mrefu na wanahabari, lipelekwe bungeni kwa dharura bila ya wahusika kushirikishwa katika uandaaji wake.

Jana ndio ilikuwa kali zaidi. Baada ya ajali za barabarani kuua watu wengi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Maji na Nchi Kavu (Sumatra) iliibuka na kanuni mpya za udhiti wa usafiri. Inaonekana kanuni hizo zilitungwa “kwa dharura” bila ya kutumia muda mwingi kutafiti chanzo halisi cha ajali hizo na namna ya kuzipunguza, na ikazipitisha kwa dharura bila ya wadau kushirikishwa kikamilifu.

Kutoshirikisha kikamilifu kwa wadau kuliweka mazingira magumu ya utekelezaji wa kanuni hizo, ambazo pamoja na mambo mengine zinataka madereva kupata upya mafunzo baada ya leseni zao kuisha kwa gharama ya Sh500,000 kutoka mifukoni mwao, kufutiwa leseni zao kabisa, kudhibiti mwendo wa mabasi ya mikoani na kulazimisha yale yanayofanya safari ndefu kupumzika mara jua linapozama na kuendelea na safari kunapopambazuka.

Hapa wadau kama shule za udereva, wamiliki wa mabasi, wawakilishi wa madereva hawakushirikishwa kikamilifu na badala yake Jeshi la Polisi ambalo linaweza kuwa moja ya sababu za kupitisha madereva wasio na sifa, ndiyo pekee linaonekana kuelewa kanuni hizo. Kanuni hizo zinaonekana kuwa ngumu katika mazingira ambayo siyo rafiki kwa ufanyaji wao kazi wa madereva- wengi hawna mikataba na hivyo kuwa hatarini kupoteza ajira iwapo watakuwa nje ya ajira kwa wiki mbili kuhudhuria mafunzo hayo.

Badala yake, nguvu kubwa iliandaliwa kuhakikisha kanuni hizo zinafanya kazi. Lakini hali imekuwa tofauti. Wananchi ndio wameumia zaidi na makovu yake yatachukua muda kuyatibu. Uchumi pia umejeruhiwa jana. Wengi walichelewa makazini na wengine kushindwa kwenda kabisa. Baadhi waliumia kwenye vurugu zilizosababishwa na mgomo wa madereva wa daladala wanaopinga kanuni hizo mpya, na wengine kujeruhiwa na vibaka ambao walitumia mgomo huo kama fursa ya ajira ya muda, huku baadhi wakilazimika kuvuruga bajeti zao ili kupata usafiri uliokuwa wa bei ghali kutokana na mabasi kukosekana.

Bidhaa zilizotakiwa kusafirishwa jana hazikwenda kwa wakati, rasimali watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine hazikutumika na hivyo uzalishaji kutetereka na kwa ujumla shughuli ambazo zilitakiwa zifanyike jana, sasa zitafanyike siku nyingine na hivyo kuongeza gharama ya utekelezaji wa shughuli hizo. Maana yake Serikali ilikosa mapato mengi ambayo yangeiwezesha kutoa huduma za kijamii.

Hata tamko la Waziri wa Kazi, Gaudencia Kabaka la kusitisha utekelezwaji wa kanuni hizo mpya limekuja “kwa dharura” kwa kuwa Serikali ingeweza kufanya mazungumzo mapema na madereva. Cha ajabu uamuzi huo umekuja wakati mgomo umeshatekelezwa kwa kiasi kikubwa?

Hivi usafiri ni wa dharura?

Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yanafanyika kwa dharura na kusababisha nchi kuyumba bila ya sababu za msingi. Kashfa ya fedha za escrow, Epa, Richmond, migomo ya walimu, migomo ya madaktari, wamiliki wa malori, migomo ya wanafunzi, mapigano ya wakulima na wafugaji na mingine mingi ilitatuliwa kwa dharura.

Ndiyo kusema nchi hii sasa ni ya dharura?
SOURCE; Mwananchi 12/04/2015
 
Back
Top Bottom