Dhana ya uzalendo

SueIsmael

JF-Expert Member
Dec 11, 2013
932
1,282
Ndugu zangu wana JF,

Kwa muda mrefu nimekuwa zaidi msomaji kuliko mchangiaji katika majukwaa ya JF. Nashukuru kwa mengi niliyojifunza kutoka kwenu.

Kilicho nisukuma kuchangia leo ni swala nililokutana nalo mara kwa mara kuhusu uzalendo. Wakati mwingine mtu hutuhumiwa kutokuwa mzalendo kwa sababu ya kumpinga kiongozi wake wa serikali; wakati mwingine kuweka mitazamo hasi kuhusu nchi yake au maswala ya nchi yake. Malalamiko hutolewa kuwa wengi tunapoteza uzalendo kwa nchi zetu. Tuachilie mbali wale wanaokana uraia wao na kuasili uraia wa nchi nyingine, aidha kwasababu ya fursa katika nchi nyingine au kutokuwa na imani tena na nchi mama. Kwanini tunahitimisha mitazamo yetu katika dhana au tuhuma hizo? Pasi na yote basi, uzalendo ni nini?

Kwa uelewa wangu, ni ile hali ya kuipenda kwa dhati, kuiheshimu na kuitumikia nchi yako kwa moyo wako wote. Kuwa tayari kujitolea hadi tone la mwisho kwa nchi yako. Hili siyo swala rahisi kama wengi tunavyofikiri, na wala siyo swala jepesi. Ni imani ya hali ya juu inahitajika.

Mara nyingi kabla sijatazama na hata kupima swala kwa upana wake huwa najaribu kuliweka katika dirisha dogo kwanza. Kwa mtazamo wangu familia zetu hutufunza mambo mengi kwasababu ni darasa la kwanza la kujifunza karibu kila kitu tutakachopitia maishani mwetu. Hata kupenda, kuheshimu, kujituma, kujitolea na kuwa na imani; huanzia katika malezi ya familia. Hivi ni vigezo muhimu vya uzalendo.

Tuchukulie kigezo kimoja; heshima. ikiwa kuiheshimu nchi ni kuwaheshimu viongozi wake wananchi wake na rasilimali zake, vivyo hivyo heshima ndani ya familia ni pamoja na heshima kwa wazazi/walezi na wanafamilia wengine, wakubwa kwa wadogo, na hata rasilimali zilizomo kwenye familia. Ikiwa mtu atashindwa kujifunza heshima katika familia, ni vigumu kwa mtu huyo kuwa na heshima nje ya familia yake. Hata hivyo, heshima iliyotukuka siyo swala la kulazimisha bali hujijenga kunapokuwa na mazingira yanayoruhusu.

Tuchukulie mfano wa mzazi anayerudi amelewa, hachangii malezi ya watoto, hutukana hovyo, hajitumi, nk. Watoto na wanafamilia wengine wanaweza heshima kuwa ni baba/mama/mlezi, lakini hawatamheshimu kama kiongozi katika familia na ni vigumu kumkweza kuwa mfano wa maisha yao. Hata ile furaha na fahari ya kuwa na mzazi bora hupunguwa. Jambo la kuwa na mzazi/mlezi wa namna hii huongeza mfarakano katika familia na hata kupoteza amani.

Naam, vivyo hivyo katika mapana ya nchi. Unapokuwa na kiongozi asiye na maadili wala kujali wananchi wake, heshima atapewa kwa nafasi yake (heshima jina) lakini ni vigumu kwa wananchi kumpenda, kumtii kwa dhati au kumpa ushirikiano sawia katika shughuli mbalimbali. Heshima ni jambo la pande mbili; heshimu, uheshimiwe.

Tukija kwenye swala la ulinzi, hata familia zetu ni mfano bora. Kwa hali ya kawaida, hata kama ndani ya familia kuna mifarakano au matatizo, ikifika hatua kuwa kuna kitu au mtu anataka kuidhuru familia yenu, mtakuwa kitu kimoja katika kupambana nacho. Hata pale mmoja katika familia akitaka kumdhuru yule mdogo, au myonge au wanafamilia wengine; ndugu au jamaa wengine huingilia kati. Wakati mwingine hata majirani huingilia kati ili kunusuru. Na hapo tunaona pia katika ngazi ya taifa. Kukiwa na jambo lolote linaweza kulidhuru taifa letu, wote huwa wamoja katika kupingana nacho. Je si hivyo pale tishio linapokuwa ndani ya nchi? Je si sawa kulikemea, kulipinga na hata kuliondosha?

Ni fupishe huu mpambanuo kwa kurudi kwenye dhana ya uzalendo kwa ujumla wake; ikiwa kuwa mzalendo ni kuipenda, kuiheshimu, kuitumikia na hata kuilinda nchi yako kwa moyo wako wote na kwa kadri ya uwezo wako wote, je kupinga yale yote yanayotishia wewe kutotekeleza hayo, si uzalendo pia?

Naomba niishie hapa, niwasilishe tafakuri hii na niwaombe tutafakari pamoja.
 
Back
Top Bottom