Dhana ya Mofimu, Viambishi na aina zake katika lugha ya Kiswahili

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,813
4,544
Wakuu salaam,

Katika kuendelea kukumbushana vipengele mbalimbali vya lugha katika somo hili tutaangalia Mofimu na Viambishi huku tukipitia dhana ya mzizi na shina. katika andiko hili tutaanza kufafanua mofimu, aina zake kisha viambishi na mwisho mzizi na shina kama ifuatavyo:

Maana ya Mofimu
Mofimu ni kipashio kidogo kabisa cha lugha ambacho kina uwezo wa kusitiri maana ya neno ambalo kwalo limeundwa. AU ni kipashio kidogo kabisa cha lugha chenye maana kisarufi au kileksika.

AINA ZA MOFIMU
Mofimu huru
ni aina ya mofimu ambayo huweza kusimama pekee na kujitosheleza kimaana yaani huwa na sifa ya neno. Mfano; mama, Baba, Dada, Kaka, Mjomba, Shangazi n.k. Kwa mifano hiyo utagundua kuwa mofimu huru haziwezi kugawanyika zaidi na kubeba maana kisarufi, kwa maana kwamba mofimu ‘baba’ ikigawanywa ba-ba, ‘ba’ hii haina maana yoyote kisarufi zaidi ya kuwa silabi.

Mofimu tegemezi ni aina ya mofimu ambayo huweza kuvunjwavunjwa na kubeba maana kisarufi, mofimu tegemezi hutegemeana ili kuleta maana kamili ya neno.

Mfano; neno ‘anakula’ limeundwa na mofimu zifuatazo:- [a-na-kul-a] ambazo kila moja hubeba dhana Fulani ya kisarufi.

VIAMBISHI

Ni mofimu zinazopachikwa nyuma au mbele ya mzizi wa neno ili kubadilisha dhana ya neno. Kwa kuwa mofimu hizo hupachikwa sehemu tatu tofauti, tunapata aina tatu za viambishi kwa mujibu wa nafasi zake katika neno, yaani; viambishi awali ambavyo hupachikwa mwanzoni au nyuma ya mzizi wa neno,viambishi kati ambavyo hupachikwa katikati ya neno (Kiswahili hakina viambishi hivi) na viambishi tamati ambavyo hivi hupachikwa mbele au mwishoni mwa mzizi wa neno.
Mfano:-

VIAMBISHI AWALIMZIZI WA NENOVIAMBISHI TAMATINENO JIPYA
A na chez ew aAnachezewa
Wa li chez ean aWalichezeana
Tu ta chez e aTutachezea

1. Viambishi awali Hivi hupachikwa kabla ya mzizi wa neno na huwa ni vya aina tisa:

i. Viambisha awali vya nafsi-
Hivi hudokeza upatanishi wa nafsi katika kitenzi, zipo nafsi tatu, nafsi ya kwanza, ya pili, naya tatu.

NAFSIUMOJAUWINGI
Ya KwanzaNi-Tu-
Ya PiliU-M-
Ya TatuA-Wa-

Mfano:-Ninalima
Tunacheza

ii. Viambishi awali vya ngeli
hivi hupatikana mwanzoni mwa nomino au vivumishi ili kudokeza hali ya umoja na uwingi.
Mfano:-Mtu (umoja) – Watu (uwingi)
Msafi (umoja) – Wasafi (uwingi)

iii. Viambishi awali vya ukanushi
hivi hudokeza hali ya uhasi wa tendo. Huwakilishwa na mofimu (ha-) na (si-)
Mfano:- Amekula (uyakinifu) – Hajala (ukanushi), Nakula (uyakinifu) – Sili (ukanushi)

iv. Viambishi awali vya Njeo
Hivi hudokeza nyakati mbalimbali ambazo ni wakati uliopita, uliopo na ujao.

NYAKATIMOFIMU
Uliopo-Na-
Uliopita-li-
Ujao-Ta-
Mfano:- Mlituona
Utakuja

v. Viambishi awali vya hali
Hivi hudokeza hali mbili za nyakati ambazo ni mazoea ambayo huwakilishwa na mofimu {hu} na timilifu inayowakilishwa na mofimu {me}.
Mfano:-Hucheza
Amelima

vi. Viambishi awali vya masharti
Hivi hudokeza hali ya masharti au uwezekano katika tendo. Mofimu hizo ni kama –ki-, nge-, ngali- n.k.
Mfano:- ukija
Ungekuja
Angalimkuta

vii. Kiambishi cha urejeshi wa mtenda (kiima)
mhiki hudokeza urejeshi wa nomino inayotenda katika kitenzi.
Mfano: - Aliyekuja {-ye-} hudokeza urejeshi wa mtenda.

viii. Kiambishi kiwakilishi cha mtendwa au mtendewa (shamirisho)
hivi huwakilisha mtendwa au mtendewa wa jambo.
Mfano; Nilimpiga, Uliukata, Nimeipenda, Wameniteta.

ix. Kiambishi awali cha kujirejea (kujitendea)
hiki huwakilishwa na mofimu (-ji-)
Mfano; kujipenda

2. Viambishi tamati
Hivi hudokeza kauli mbalimbali za vitenzi.
Mfano: - Anacheza – kutenda
Unachezwa- Kutendwa
Utachezewa- Kutendewa
Nimemlia- Kutendea
Wamewasomesha- Kutendesha n.k

MziziKiambishi cha KauliKiambishi tamati maanaNeno jipyaKauliViambishi vya kauli
ChezaChezaKutenda-a
eaChezeakutendea-e-
PigianaPigianaKutendeana-ian-/-ean-
iwaPigiwaKutendewa-iw-/ew-
SomeshaSomeshaKutendesha-ish-/esh-
eshwaSomeshwaKutendeshwa-ishw-/eshw-
LimikaLimikaKutendeka-ik-/-ek-
anaLimanaKutendana-an-
waLimwaKutendwa-w-

DHANA YA MZIZI NA SHINA LA KITENZI
Mzizi wa kitenzi
ni sehemu ya neno inayobakia mara baada ya kuondoa viambishi vyote vya awali na tamati katika neno hilo.

Mfano: - a-na-chez-a {-chez-}, m-ku-lim-a {-lim-}
Mzizi funge ni ule ambao hauwezi kujikamilisha kimaana yaani hauwezi kusimama kama neno. Mfano; -lim-, -chez-, -imb- n.k.

Mzizi huru ni ule ambao huweza kusimama kama neno na ukichanganuliwa zaidi hupoteza maana yake ya msingi. Mfano; Kinu, Kazi, Arifu, Sali n.k.

Shina la kitenzi ni sehemu ya neno ambayo huongezwa viambishi fuatishi (tamati) au ni sehemu ya neno ambayo hubakia baada ya kuondolewa viambishi tangulizi. Mfano:- chez+a = cheza, lim+a = lima. Sehemu hii ya neno hutumika kuundia neno jipya.

Shina sahili – hili ni shina ambalo huundwa na mofimu moja tu ambayo ni mzizi wa neno hilo, huwa ni mofimu huru, Mfano; Kesho, jana, kitabu, jarida n.k.

Shina changamano – shina hili huundwa na mzizi na kiambishi tamati maana. Mfano; cheka, lala, lia, kula n.k.

Shina ambatani – shina hili huundwa na mofimu mbili ambazo ni huru. Mfano; mwana + kwenda = mwanakwenda, mbwa + mwitu = mbwamwitu
 
Back
Top Bottom