Dhana ya Mazao ya Kimkakati: Taswira kuelekea Tanzania ya Viwanda

Jul 18, 2020
14
12
Na: Norbert Mporoto
– Tanzania.

Uchumi wa taifa la Tanzania umekuwa ukipigiwa chapuo na kupewa tafsiri nyingi ambazo hazivuki mipaka ya kukitambua kilimo kama sekta adhimu ambayo ndiyo uti wa mgongo wa taifa hili. Kulingana na Taasisi ya Takwimu Tanzania (NBS) sekta ya kilimo na madini zikiwa kama shughuli za msingi zimechangia pato la taifa kwa wastani wa asilimia 33.7 kwa miaka mitano mfululizo yaani 2015-2019. Miaka kenda, wataalamu wa sera za maendeleo na nguli wa eneo la Kilimo wamekuwa wakija na mbinu, mikakati na ujuzi mpya ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha pato la taifa kupitia kilimo linakua siku baada ya siku. Kwa tathmini ya miaka mingi sekta ya kilimo imefanya vizuri katika kukuza pato la taifa kupitia mazao makuu ambayo ni Korosho, Kahawa, Pamba, Chai, Mkonge na Tumbaku na hivyo kupelekea mazao haya kuingia katika orodha ya mazao ya kimkakati nchini.

Mchango wa mazao haya katika biashara za nje (foreign trade – major export) kwa kipindi cha miaka mitano yamekuwa ya kutia hamasa kiasi kwamba nguvu ikiwekezwa yanaweza leta tija zaidi, na kuwezesha wanufaika wa mnyororo huo wa thamani kujikwamua kiuchumi mara dufu. Mwaka 2015 orodha ya mazao haya ya kimkakati iliingiza kiasi cha shilingi bilioni 1745.9, mwaka 2016 shilingi bilioni 1994.5, mwaka 2017 shilingi bilioni 2164.4, mwaka 2018 shilingi bilioni 1420.8 na mwaka 2019 grafu iliongezeka na kuwa shilingi bilioni 1784.5 na kufanya wastani wa shilingi bilioni 1822.02 kuzalishwa katika mauzo ya nje ya mazao haya ya kimkakati ndani ya kipindi hicho.

Tafsiri nyepesi na kwa tathmini iliyo wazi ni kwamba endapo uzalishaji wa mazao haya ukiongezeka na kupewa kipaumbele na watu wote ambao mnyororo wake wa thamani huwagusa basi miaka ijayo eneo hili litachangia pato la taifa kwa ufanisi na kiwango kikubwa zaidi.

Katika kipindi cha pili cha miezi sita ya mwaka 2020, nimebahatika kuwa nasoma na kusikia matamko ya viongozi mbalimbali wa Wizara ya Kilimo na wale wa kitaifa wakisisitiza juu ya uwekezaji wa zao jipya la kimkakati. Kigoma sasa si mwisho reli wala si sehemu ya kwenda kushangaa Migebuka wakipiga mbizi, bali kitovu cha uzalishaji wa zao la Mchikichi. Na iko wazi dalili zinaonekana, jitihada zinafanyika. Na hivyo orodha ya mazao hayo ya kimkakati imeongezeka kwa kuufanya Mchikichi kuwa zao jipya linalojumuishwa katika orodha ya awali.

Hasira imetuingia, nasi nadhiri tumeweka. Huenda lililotukera wengi ni ile historia ya taifa la Malaysia na Indonesia kuja kuchukua mbegu ya Mchikichi mkoani Kigoma miaka ya 1960’s na leo hii Malaysia inashikilia rekodi ya dunia kwa uzalishaji wa mafuta ya mawese ambayo ni zaidi ya tani milioni 18. Tanzania ikiwa ni moja ya walaji wa bidhaa hiyo, inakadiriwa katika matumizi yetu ya mafuta hayo kwa kiwango cha asilimia 65 huagizwa kutoka nje ya nchi, hasa nchini Malaysia.

Barani Afrika rekodi ya uzalishaji inashikiliwa na nchi ya Nigeria ambayo inazalisha zaidi ya tani milioni mbili kwa mwaka na kuifanya kuwa nchi ya tatu kiuzalishaji duniani. Nchi washindani ambazo tutatakiwa kuhakikisha tunaingia nao ulingoni kupambana katika soko la dunia ni Cameroon, Benin, Ghana na jirani zetu Kenya. Wakati tukiendelea kujipanga na kufunga kamba, rekodi yetu ikumbukwe tunazalisha tani 2000 kwa mwaka (hizi ni takwimu za Mkoa wa Kigoma pekee ikiwa kama kitovu cha uzalishaji). Hii inatoa picha halisi ya jumla ya uzalishaji ikiwa mikoa ya Pwani, Kagera, Rukwa, Mbeya (Kyela), na visiwani Zanzibar itajumuishwa kwa pamoja. Sina hakika kama zao hili lilipewa na kuwekewa umakini, huenda wananchi waliitumia miti ya Mchikichi kwa kivuli au makuti ya kuezekea vibanda na baadhi walipoishiwa mafuta walitumia zao hili kama mbadala, na wachache tena walitumia kama zao la biashara baada ya kujaribu shughuli nyinginezo na kuambulia patupu na hivyo kuweka rekodi hiyo ya uzalishaji nchini. Kongole kwa uthubutu.

Licha ya kwamba mazao haya yana historia ndefu juu ya ufanisi wake na nguvu iliyowekezwa hapa nchini, si ajabu bado ukakutana na changamoto zilezile za kiutendaji. Malalamiko ya mkulima wa kahawa, chai, tumbaku, korosho, pamba na mkonge huwa ni mithili ya watoto wa mama mmoja wanaolilia chakula, uliaji wao hutaja shida ileile. Tathmini ya vilio vyao vinaashiria uwekezaji mdogo wa mazao haya katika ngazi ya wakulima wadogo kiasi kwamba wengi hawazalishi kwa tija, na wengine wamesusia kabisa mashamba yao na kugeuza machungio.

Kama tumeshindwa kuzalisha kwa hiyari basi tuzalishe kwa sheria zenye weledi. Nakumbuka Azimio la Arusha liliazimia kuvifanya vijiji kuwa vitovu vya uzalishaji lakini leo hii ni matusi makubwa kumchukua Afisa au msomi yeyote na kumpeleka kijijini akazalishe, baada mwaka tu atakimbia kijijini na kurudi mjini. Vijijini kunaogopwa, vijijini wanakwenda kuzika na kutambika tu. Lakini huko ndiko uzalishaji wa sekta ya kilimo unafanyika, nani atafanya kwa weledi wakati wasomi na nguvu kazi wako mjini wanagonga glasi za mvinyo? Nani atazalisha ikiwa nadharia za kilimo bora zimegomea mjini kwa watu wanaolimia mdomoni na kwenye makaratasi?

Dunia iko kasi sana! Ukizubaa watu watakuuza na wakikuonea huruma watakuvua utu wako kwa kipande kidogo cha fedha. Mkulima anayetoka shamba na mazao yake hauzi bila kukutana na jabari linaloamua bei ya mazao yake, wamejipa majina mapya wanajiita madalali au mawakala. Tembelea masokoni utawaona na vitambi vyao, kalamu pembeni na kijidaftari kidogo kama wahesabuji sensa. Wamejenga hatari, wanalimia mdomoni huku mkulima akidhoofu siku baada ya siku. Inachekesha sana lakini ndipo tulipofika. Utatoka wapi uzalishaji wenye tija katika mfumo huu wa kimaslahi?

Kila Halmashauri na Wilaya nchini zipo katika maeneo ambayo ni yenye uzalishaji mzuri. Kama si katika kilimo basi ufugaji, kama si ufugaji basi sekta nyinginezo. Ni ajabu leo hii bado tunalia na ruzuku ama mikopo nafuu kwa wakulima. Ukweli ni kwamba kwa taswira ya kilimo nchini ni vigumu kwa mkulima mdogo kukopesheka katika taasisi za kifedha. Kwanini Wilaya ama Halmashauri zisitumie mbinu ya ‘kutengeneza uhitaji katika masoko na kuzalisha kwa wingi ili kukidhi mahitaji’ kwa kutumia wakulima wao na baadae waigawe faida kwa misingi ya kunufaisha pande zote kadri ya uwekezaji. Au kutoa elimu ya ushirika na kuwashawishi wakulima kujiunga kwenye vyama vya ushirika vitavyoweza kutetea maslahi ya wakulima kwa ujumla. Lengo ni kumtoa mkulima kwenye vita ya kibiashara ambayo kamwe hawezi kufurukuta. Kwanini Halmashauri au Wilaya zisizalishe kwa misingi hiyo kisha wafanye biashara na wahitaji wa bidhaa hizo ili kulinda thamani?

Leo hii ukizunguka katika Wilaya na Halmashauri ambazo zinastawisha mazao ya kimkakati ni ukweli kwamba inatumika ile dhana ya (the strong will survive, the weak will perish) mwenye nguvu atastahimili na mnyonge atapotea. Walio na nguvu ya kumudu uzalishaji ni makampuni, taasisi na mashirika ya umma ambao hawa kwa lugha nyingine wanawabemenda wakulima wadogo ambao kimsingi wao ndiyo wazalishaji wakuu. Nani atamkumbatia mkulima wa kawaida ili azalishe katika mazingira rafiki kama sio serikali?

Ni kweli tunapiga hatua, lakini hatuna uhakika wa usalama wa mahali tunapokwenda kutua hatua moja zaidi. Uendelevu wa mazao ya kimkakati unahitaji mabadiliko ya kimfumo hasa ufufuaji wa viwanda vya mazao ya kimkakati, ufufuaji wa mashamba yaliyotekelezwa, uboreshaji wa mifumo ya usafirishaji yenye kulinda uthamani wa mazao na bidhaa hizo, ujenzi wa viwanda vipya na vya kisasa vya utengenezaji bidhaa zitokanazo na mazao hayo na zaidi kuweka mifumo rafiki ya kiuzalishaji. Kubwa katika yote ikiwa ni kuwalinda wakulima wadogo na wazalishaji wa sekta ya kilimo, kwani kufanya hivyo itakuwa tumelinda na kuzuia upotevu wa mazao na nguvu kazi katika mnyonyoro wa thamani wa uzalishaji wetu.

Norbert Mporoto.
Tanzania.
NB: Picha haina umiliki. Ni kwa matumizi fikirishi tu

IMG-20181110-WA0018.jpg
 
Unasema turudi kwenye azimio la Arusha ili tukalime tena? Watanzania kama hatuutaki umaskini, utatukimbia. We have everything with us. Ila ni wavivu sana. Na wapiga porojo
 
Kwa nini mkakati usiwe hata uvuvi huko kigoma, kigoma mmeiona ni ya mawese tu.Wazee was kigo.a wanataka kipanda korosho, parachichi nyie mmekazania mawese tu.Serikali kapandeni mawese kwa wingi wananchi wataamua mazaovyanayolipa.
Lita ya mawese in sh.1500 wakatu alizeti 3000-6000.Mawese yatashuka sana bei iwapi miti milioni Mona itapandwa kwa hio Lita ya mawese inaweza shika had I 500-1000.
Hakuna mkakati wowote wa kiviwanda ila kina mkakati was kupanda.
Je kuna maandalizi gani ya maana ya viwanda maana baada ya miaka 2 miti mingi itaanza kuzaa.
Mpaka sasa hakuna umeme wa gidi nani ataenda kuwekeza sehemu ambayo haina umeme wa viwanda.
Msiongee hadithi hadithi,ongeeni mkakati inayopimika vinginevyo mambo yatakuwa vilevile.
Maweze yataweza badili uchumi wa kigoma na TZ kama kutakuwa na commitment ya ukweli.
 
Kwa nini mkakati usiwe hata uvuvi huko kigoma, kigoma mmeiona ni ya mawese tu.Wazee was kigo.a wanataka kipanda korosho, parachichi nyie mmekazania mawese tu.Serikali kapandeni mawese kwa wingi wananchi wataamua mazaovyanayolipa.
Lita ya mawese in sh.1500 wakatu alizeti 3000-6000.Mawese yatashuka sana bei iwapi miti milioni Mona itapandwa kwa hio Lita ya mawese inaweza shika had I 500-1000.
Hakuna mkakati wowote wa kiviwanda ila kina mkakati was kupanda.
Je kuna maandalizi gani ya maana ya viwanda maana baada ya miaka 2 miti mingi itaanza kuzaa.
Mpaka sasa hakuna umeme wa gidi nani ataenda kuwekeza sehemu ambayo haina umeme wa viwanda.
Msiongee hadithi hadithi,ongeeni mkakati inayopimika vinginevyo mambo yatakuwa vilevile.
Maweze yataweza badili uchumi wa kigoma na TZ kama kutakuwa na commitment ya ukweli.
Makala imejikita zaidi kutathimini hali ya kilimo, hasa mazao mkakati. Uko sahihi kwamba commitment ya watu na uwezekezaji lazima iwe ya hali ya juu. Lakini mbali na uwepo wa changamoto za uzalishaji, bado uhitaji wa zao hilo kwa matumizi ya ndani bado ni mkubwa kiasi kwamba tuna 'import' kwa wingi sana bidhaa ambayo inaweza zalishwa nchini.

Lakini secondary impact ni kushindana katika soko la dunia, ikizingatia barani Afrika nchi wazalishaji wa zao hilo ni chache.

Lakini katika yote, bado kuna changamoto nyingi (nyingine zikiwa zimeorodheshwa) ambazo nakubaliana nawe kuwa zinahitaji ufumbuzi ili kuleta tija ya uzalishaji.
 
Unasema turudi kwenye azimio la Arusha ili tukalime tena? Watanzania kama hatuutaki umaskini, utatukimbia. We have everything with us. Ila ni wavivu sana. Na wapiga porojo
Hapana kurejea katika Azimio la Arusha si kurejea kulima, bali kuna mifumo rafiki ya uzalishaji ambayo ilijadiliwa katika Azimio la Arusha (hasa kuvifanya vijiji kuwa vitovu vya uzalishaji).
 
Makala imejikita zaidi kutathimini hali ya kilimo, hasa mazao mkakati. Uko sahihi kwamba commitment ya watu na uwezekezaji lazima iwe ya hali ya juu. Lakini mbali na uwepo wa changamoto za uzalishaji, bado uhitaji wa zao hilo kwa matumizi ya ndani bado ni mkubwa kiasi kwamba tuna 'import' kwa wingi sana bidhaa ambayo inaweza zalishwa nchini.

Lakini secondary impact ni kushindana katika soko la dunia, ikizingatia barani Afrika nchi wazalishaji wa zao hilo ni chache.

Lakini katika yote, bado kuna changamoto nyingi (nyingine zikiwa zimeorodheshwa) ambazo nakubaliana nawe kuwa zinahitaji ufumbuzi ili kuleta tija ya uzalishaji.
Nilifanya analytical research kuhusu hill zao nikiwa mzawa wa Kigoma.Sua hawana research za maana kuhusu hill zao ambacho ndio kioo cha utafiti wa kilimo TZ.
So unawezaje kuwekeza ktk kitu ambacho hakina utafiti.Zao hili linasukumwa kisiasa badala ya utaalamu. Nilighaili kwenda kununua ardhi kwa dhumuni la kulima chikichi nakuanzisha kilimo kingine ambach napambana nacho.
Kama uwekazaji wa zao hilo utafanyika kisiasa bila utalaamu basi watu wa kigoma lazima waje walie.
Naomba uchambuzi wako uende mbele zaidi kutoka shambani na uende ktk processing na marketing.
Mkakati usiwe tu kuhamasisha watu kupanda bali hata jinsi ya kusindika na kuuza.Tatizo la Tanzania sio kulima bali kuuza.Mwanasiasa huwa halimi kazi yake ni kusema mwisho wa siku mkulima hulia peke yake mifano ni mingi.
 
Hapana kurejea katika Azimio la Arusha si kurejea kulima, bali kuna mifumo rafiki ya uzalishaji ambayo ilijadiliwa katika Azimio la Arusha (hasa kuvifanya vijiji kuwa vitovu vya uzalishaji).
Tumeisha hama kwenye ujamaa mkuu, tusilazimishe mawazo yaliofeli kurudi tena.Ujamaa ulifeli vibaya mno sema tu watu humstahi muasisi wake. Nipe mfano wa kijij kimoja kilichoweza kufaulu na Sera za ujamaa.
 
Back
Top Bottom