Dhamira ya Kuhakikisha Kila Mmoja Ananufaika na Huduma ya Intaneti Bado Inakwamishwa Sehemu Mbalimbali Duniani

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,799
HUDUMA YA INTANETI NI MUHIMU.jpg

Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wanaweza kuzuia huduma ya kufikia mtandao kwa njia nyingi. Kwa mfano, serikali zinaweza kukata gridi ya umeme au kuhujumu miundombinu ya huduma ya mtandao kama vile minara ya simu za mkononi na kebo za fibre optic.

Serikali pia zinaweza kuzuia ufikiaji wa tovuti au majukwaa ya mawasiliano—kama vile Facebook, Telegram au WhatsApp—kwa kuzuia URL maalum au anwani za IP kwa malengo fulani – ambayo mara nyingi huwa ni yasiyo na manufaa kwa wananchi wake.

Kwa vyovyote vile, kunyima watu uwezo wa kufikia huduma ya intaneti ni ukiukaji wa haki za binadamu, kwani mtandao umekuwa sehemu muhimu ya maisha kwa sehemu kubwa ya dunia. Ni ukweli huu uliyosababisha Umoja wa Mataifa kutangaza kwamba unazingatia ufikiaji wa mtandao kama haki ya binadamu.

Hata hivyo, pamoja na dhamira nzuri ya dunia kuhakikisha kila mmoja popote alipo anaweza kufikia huduma hii, bado mazuio ya ufikiaji wa intaneti yanaendelea kutekelezwa na serikali mbalimbali duniani ili kuzuia haki za wananchi kuandamana, kupata taarifa au kuzuia hatua fulani za wananchi.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Access Now inayoitwa Weapons of control, shields of impunity: Internet shutdowns in 2022, kuzuiwa kwa intaneti katika nchi nyingi kumeendelea kuchochewa na maandamano, migogoro, mitihani, chaguzi, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na matukio mengine makubwa ya kitaifa.

Ripoti hiyo ambayo inatolewa kupitia kampeni ya #KeepItOn inayounganisha mashirika mbalimbali duniani katika juhudi za kukomesha uzimaji wa intaneti, pia imeeleza kuwa kwa mwaka 2022 intaneti ilizimwa mara 62 katika nchi 16 wakati wa maandamano, huku ikizimwa mara 8 katika nchi 6 ili "kuzuia udanganyifu wa mitihani", mara 33 wakati wa migogoro na ilizimwa mara 5 katika nchi 5 wakati wa uchaguzi.

SABABU ZA KUZIMWA INTANETI DUNIANI 2022.jpg

Pia inaeleza kuwa kwa mwaka 2022 pekee, serikali na watendaji wengine walitatiza ufikiaji wa intaneti kwa angalau mara 187 katika nchi 35 - na kuvunja rekodi ya juu katika kampeni ya #KeepItOn kwa idadi ya nchi zilizozima intaneti katika mwaka mmoja.

Kuzuia ufikiaji wa intaneti ni ukiukaji wa uhuru wa raia kwani kunazuia umma kukusanyika na hivyo kunaharibu mtiririko huru wa habari. Hii inaweza kuruhusu serikali za kimabavu kunyamazisha wakosoaji na kukwepa uwajibikaji kwa wananchi wake.

Kuzima mtandao sio tu kunavuruga uwezo wa raia kupata taarifa muhimu na kuwasiliana wao kwa wao, lakini pia kunaharibu muingiliano wao na dunia nzima, na hivyo kutengeneza mwanya wa serikali dhalimu kuendeleza upotoshaji na propaganda zisizo na tija kwa wananchi wake.

Kuzuia ufikiaji wa intaneti kunaathiri vibaya sio tu wapinzani wa kisiasa na vikundi vya waandamanaji lakini jamii kwa ujumla. Hili ni jambo baya sana kwani katika dunia ya leo intaneti ni muhimu katika kuokoa maisha ya watu katika taasisi za afya lakini pia linaweza kuathiri hata mfumo mzima wa elimu na vipato binafsi.

Ni muhimu kudumisha ufikiaji wa huduma za mtandao, mifumo ya kidigitali na teknolojia hasa wakati wa uchaguzi, maandamano na vipindi vya migogoro. Kukatizwa kwa makusudi kwa ufikiaji wa mtandao na huduma za mtandaoni huathiri haki za watu za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiraia.

Serikali zinapaswa kuepuka kuzuia au kuweka masharti magumu ya udhibiti wa huduma za mtandao. Serikali badala yake zinapaswa kushughulikia hatari zozote zinazoletwa na mitandao ya kijamii kupitia mifumo iliyopo ya kidemokrasia kwa kushauriana na mashirika ya kiraia na walioathirika.

#KeepItOn
 
Back
Top Bottom