Demokrasia ya Tanzania Ipanuliwe Yaanzishwe Majimbo ya Uchaguzi ya Vyuo Vikuu

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,216
3,587
OIP.Wlq5QE9XhUe-XLCdlun5ZwHaFj
OIP.AuciYjfaYtIp9gZZHUGLCAHaEK
OIP.OrZHbwY0_31iS7B-YcXS8gHaEK
1632221516533.jpeg
1632221255562.jpeg

Taswira zote kwa hisani ya:
Kwa kuzingatia historia ya utendaji wa bunge letu na mabaraza ya madiwani na jukumu la msingi sana la kizalendo ambalo kila mwanazuoni anajivika pale anapokuwa amehitimu mafunzo yake na kuapa kutumikia jamii yake na pia jukumu la taasisi za elimu hasa ya juu la kuandaa rasilimali watu katika kulitumikia taifa letu, muda sasa ni muafaka kwa taifa letu kuanzisha majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu. Hii ni hoja ambayo naileta kwa Watanzania wenzangu wote bila kujali jinsia, kada ya utumishi, kazi, taaluma, taasisi nk ili iweze kuamsha mjadala mpana toka kwenye makundi yote yenye fikra pevu na mtazamo chanya juu ya umuhimu wa mabadiliko katika jamii pana. Naipa changamoto Tanzania kuchukuwa nafasi ya kwanza kabisa kuongoza njia ya kupanua demokrasia yake kwa namna hii na hatimaye isambae barani Afrika.

Yatosha kutamka kwamba taasisi za elimu ya juu ambazo kwa miaka yote kabla na baada ya uhuru wa taifa letu yamefanyika chanzo cha mijadala na tafiti za kuibua hoja za msingi sana zenye hekima, busara na mawazo ya kimapinduzi katika kuitumikia jamii ya kitanzania; zinastahili kuchukuwa nafasi ya kwanza kabisa ya kuongoza mjadala huu na madai haya ya kupanua wigo wa demokrasia ya Tanzania kwa kuanzisha majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu. Historia itakumbuka milele yote kuwa taasisi za elimu ya juu e.g. chuo kikuu cha Dar es Salaam wakati huo kikiitwa chuo kikuu cha Afrika Mashariki kilisimama kidete kudai uhuru kwa kuandaa rasilimali watu ambao walikuja kushiriki harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na ukombozi wa bara la Afrika kwa namna mbalimbali ikiwemo chimbuko la falsafa, hekima, busara, itikadi na nadharia kadha wa kadha zilizotafitiwa ambazo zilitia hamasa harakati za kudai uhuru na ukombozi na kuzifanya taasisi hizi kikiwemo chuo kikuu cha Dar es Salaam kuwa na charter zao kama utambulisho wake.

Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwenye nembo yake tunasoma maneno “Hekima ni Uhuru”, chuo kikuu cha Ardhi tunasoma maneno “Utafiti, Elimu, Ushauri”, chuo kikuu cha Mzumbe tunasoma maneno “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”, chuo kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili tunasoma maneno “Elimu, Tiba, Utafiti”, chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine tunasoma maneno “Ardhi ni Hazina”, chuo kikuu Huria cha Tanzania tunasoma maneno “Elimu Bora na Nafuu kwa Wote”, chuo kikuu cha Tanzania cha Mt. Agustino tunasoma maneno “Ujenzi wa Ufalme wa Mungu”, chuo kikuu cha Tumaini tunasoma maneno “Utafiti, Mafunzo, Huduma”, chuo kikuu cha Tanzania cha Mt. Yohana tunasoma maneno “Kujifunza Kuhudumia” nk.

Ni katika muktadha kama huo wa chuo kikuu kushiriki harakati za kudai uhuru na ukombozi barani Afrika; ambao siku hizi umepotoka [ama haupo tena au umepungua kasi katika taasisi hizi] ndiyo andiko hili kinaegemeza hoja yake hii. Tunahitaji kutambua kuwa upatikanaji uhuru na ukombozi barani Afrika havikuishia hapo vilipoishia, la hasha, bali tunahitaji kuendeleza harakati za mapambano ya kuendeleza kile tulichokwishajipatia na pia kuleta mengine mapya ambayo ni lazima yatukie kulingana na mabadiliko ya dunia ambayo hayakwepeki hivi sasa. Na hii tutafanikiwa endapo tutakuwa na watu wenye busara na kaliba ya kuratibu mfumo mzima wa jamii kwa usahihi, haki na kwa kuzingatia misingi ya sheria zinazoongoza jamii husika. MUNGU ameweka wasomi ili waweze kuiendesha dunia na katika msaafu wa Kikristo katika kitabu cha mithali kuna maneno yanayosomeka kuwa “Mkamateni sana elimu, msimuache aende zake, maana ni uzima wenu” hapa tunahakikishiwa kuwa academia imepewa dhamana ya kuifanya dunia ikalike kwa usalama zaidi kwa kusambaza elimu hata na ya uamsho wa fikra za watu na kwamba swala la kushika elimu ni agizo la Mungu na haki kwa kila mtu na ikumbukwe kuwa maneno hayo kwenye msaafu huo wa Kikristo yametaja elimu kama nafsi iliyo hai ndiyo maana msaafu umetumia viwakilishi vilivyopigiwa msitari hapa kama ifuatavyo; mkamateni usimuache aende zake, maneno ambayo yanatumika kuelezea kitu chenye nafsi hai.

Ni umuhimu huu na uzito wake ndivyo miongoni mwa mambo mengine unachagiza madai ya kuwepo kwa majimbo haya ambayo ni muafaka sasa kwamba yatasaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya jamii yetu kwa kuongoza mijadala yenye tija zaidi na yenye uelewa zaidi wa jamii yetu na matatizo yake; mijadala ambayo kama ikifanyika bungeni ambapo maazimio yake huwa hayapuuzwi katika kuisimamia mhimili wa serikali basi mabadiliko katika jamii ya kitanzania yatafikiwa kwa namna za kisayansi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Ni sauti zenye nguvu za hoja za kisomi za wabunge na madiwani hawa wa majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu zitakazoweza kuchagiza na kuathiri kwa matokeo chanya mabadiliko katika jamii yetu kupitia mhimili wa bunge na mabaraza ya madiwani ambavyo ni vyombo vya wananchi.

Naamini katika nguvu za wasomi kwa ushahidi wa nyakati zile baada ya uhuru wa taifa letu ambapo inasemekana walikuwa wasomi wazalendo saba tu lakini nguvu zao zilikuwa na mshindo mkuu sana mpaka kufanikiwa kuliweka taifa letu katika msitari wa maendeleo tunayojivunia hivi leo. Swali ni kuwa, kama wasomi saba waliweza kuongoza mawazo ya wananchi wote wakati huo je, leo hii ambapo tunao wasomi hadi soko la ajira limefurika mbona jamii inaonekana kuchanganyikiwa na taathira za chagizo za sayari hii na kutoa mwanya kwa wanajamii kulalamikia mfumo uliopo wa uendeshaji jamii yetu na kuleta kiu ya mabadiliko ambayo haijulikani ni kundi lipi kati ya wanasiasa, wasomi na wafanyabiashara ambalo ndilo lina thubutu ya kujaribu kushika hatamu ya harakati za kuleta mabadiliko hayo yanayohitajika kwenye jamii yetu?

Sekta zote muhimu zinapitia changamoto kadhaa ngumu ambazo majibu yake siku zote yametegemezwa kwa wataalam wa nje na warasimu wa kisiasa wa ndani ya jamii yetu ambao nao wameonyesha kuelemewa na kuhitaji wasomi wazalendo wenye moyo wa kizalendo ambao tunaweza kuwapata kupitia academia; watakaopelekwa bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani baada ya kuonekana kuwa wasomi hawa wakibaki kwenye taasisi zao na kutoa ushauri wa kitaalam wakiwa huko wamekuwa hawasikiki na ushauri wao umepata vikwazo na changamoto nyingi za kisiasa katika utekelezaji wake.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa majimbo haya kuanzishwa nyakati hizi tulizonazo ambazo taifa letu limepiga hatua kubwa sana ya maendeleo kwa muda wa nusu karne iliyopita kwa kuzingatia mfumo wa ujamaa na kujitegemea ulioongoza taifa kwa takriban miaka 25 ambapo dola lilijivika jukumu zito na kubwa sana ambalo hata mataifa ya viwanda yalishindwa; la kuhudumia umma kwa mambo yote ya msingi sana kumwezesha mwanadamu akamilike huku utu wake ukitangulizwa mbele ambapo kupitia maazimio mbalimbali kama Azimio la Arusha, Azimio la Musoma, Azimo la Iringa nk taifa letu liliweza kujiweka katika nafasi ya heshima kubwa sana katika medani za kimataifa.

Kuna haja ya kudurusu sheria ya uchaguzi na sheria ya vyuo vikuu ili ziweze kuakisi mahitaji haya mapya ili kuyapa haya majimbo nguvu na uhalali wa kisheria. Katika hili napendekeza kwa moyo wa uzalendo kabisa upanuzi wa wigo wa demokrasia ili kutoa fursa ya kuanzishwa majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu ambapo napendekeza nguvu ya katiba inayotoa mamlaka kwa taasisi ya Urais ya kuteua wabunge ibadilishwe ili wabunge hao wanaoteuliwa na taasisi ya Urais sasa wapatikane kupitia majimbo ya taasisi za elimu ya juu.

Kwa vile bunge ni chombo cha wananchi basi ni dhahiri kuwa wabunge wanaoteuliwa na taasisi ya Urais huwa hawawakilishi maslahi ya umma moja kwa moja [indirect democracy] isipokuwa wanafanya hivyo kupitia taasisi ya Urais ambapo uwajibikaji wao haupo kwa wananchi bali kwa mteuzi wao na ukweli huu unadhihirishwa na dhana nzima ya uwakilishi wa mbunge kwa wateuzi/wapiga kura wake ambapo mbunge anakuwa ni mwakilishi wa maslahi ya mteuzi wake [rais au wapiga kura wa jimbo lake]. Ili kuondokana na kadhia ya kuhojihoji madaraka ya taasisi ya Urais katika kutenda shughuli zake za ki-uteuzi, ni wakati muafaka sasa kwamba wabunge wanaoteuliwa na taasisi hiyo nyeti sana na ya juu katika uongozi wa taifa, nafasi hiyo sasa ichukuliwe na majimbo mapya yatakayoanzishwa ya taasisi za elimu ya juu. Vinginevyo kutegemea gharama kwa taifa, uwezekano uangaliwe wa kuwa na wabunge wote wa makundi haya mawili ya majimbo ya uchaguzi ya vyuo vikuu na lile la kuteuliwa na taasisi ya Urais. Mabadiliko ya sheria kadhaa zilizoanzisha taasisi hizi ikiwemo sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi yafanyike.

Andiko linatoa changamoto kwa wadau wa msingi sana wa demokrasia nchini Tanzania kama; TCD [Taasisi ya Demokrasia Tanzania], Taasisi za elimu ya juu, vyama vya siasa, Mashirika ya Habari, Taasisi za kidini hasa zinazomiliki vyuo vikuu, TLS [Chama cha Wanasheria Tanganyika], Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, TEC [Tume ya uchaguzi Tanzania], Mashirika yasiyo ya kiserikali [NGOs] yanayojihusisha na masuala ya demokrasia, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, TAMISEMI kupitia halmashauri ambazo ni wenyeji wa taasisi za elimu ya juu nk wawe kwenye hatamu ya mjadala wa kuanzishwa kwa majimbo haya ya uchaguzi kwa faida ya jamii yetu na nchi yetu.

majwalaoriko@yahoo.co.uk

1632221193971.jpeg
 
Back
Top Bottom