Demokrasia Ya Funga Ndoa Africa

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
Ratifa Baranyikwa


WENGI walifikiri kuwa suluhu pekee ya kuirejesha Kenya katika hali yake ya amani wakati ule ilipotumbukia kwenye mgogoro wa kisiasa ni kuundwa kwa serikali ya mseto.

Baada ya Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja, watu walishangilia na kusema kuwa hatimaye suluhu imepatikana, bila kujiuliza iwapo kama mahasimu hao walikuwa wamejiandaa kuachana na misimamo mikali waliyokuwa nayo muda mchache kabla ya kufikia makubaliano.

Tunatambua kuwa serikali za mseto zinazoundwa katika nchi nyingi barani Afrika zimekuja kutokana na viongozi kutoheshimu misingi ya demokrasia.
Lakini sasa upo ushahidi wa kutosha kuwa uanzishwaji wa serikali za mseto kama suluhu ya kumaliza migogoro ya kisiasa inayotokana na kuvurugika kwa chaguzi barani Afrika si suluhu ya kudumu.

Na sasa kuna dalili kubwa kwamba ile serikali ya mseto iliyoundwa nchini Kenya baina ya Chama cha PNU cha Rais Mwai Kibaki na Orange for Democratic Party (ODM) cha Raila Odinga ambaye sasa ni Waziri Mkuu inaelekea kushindwa.

Kama hili litatimia litakuwa ni pigo kubwa katika medani za siasa barani Afrika kwa kuwa serikali hiyo inategemewa kuwa ni mfano mzuri kwa nchi nyingine zilizokumbwa na migogoro ya kisiasa.

Zimbabwe tayari imeingia kwenye orodha, Rais wake, Robert Mugabe, aliyekuwa akikaidi makubaliano ya kugawana madaraka kwa uwiano wa haki, naye ametumbukia humo, kutokana na yale yanayojiri Kenya.

Sote tumesikia na wengine kushuhudia yanayotokea nchi jirani ya Kenya hivi sasa ambako baadhi ya viongozi wameamua kujiondoa serikalini, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua, kutokana na migogoro isiyokwisha ndani ya serikali ya mseto, kila mmoja akishutumu na kudharau mamlaka ya mwingine.

Na hivi karibuni tu, Waziri Mkuu Raila Odinga ameingia katika mgogoro mpya na bosi wake, Mwai Kibaki, baada ya kujichukulia maamuzi ya kuwatimua mawaziri wawili wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Wakati Raila akiona ametekeleza jukumu lake kama inavyostahili kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu na kwa mamlaka yake, Kibaki anaona kiongozi huyo anataka kuvuka mipaka.

Matatizo haya yanakuja huku mamilioni ya Wakenya wenye kipato kidogo wakiwa wanakabiliwa na tatizo la njaa, na ufisadi wa wakubwa ukifikia hali ya kutisha. Wachambuzi wanaona serikali imeshindwa kukabili ipasavyo hali hiyo.

Migogoro kama hiyo haitaishia hapo, itaendelea siku hadi siku kwa kuwa serikali nzima ni kielelezo cha kutokuwepo kwa chaguzi zinazoheshimu misingi ya demkorasia.

Wachambuzi mbalimbali wamekuwa wakionya kuwa viongozi barani Afrika lazima wajifunze kuheshimu matakwa ya wapiga kura na kukubaliana na matokeo ya uchaguzi, kwani uchaguzi bado unabaki kuwa njia bora ya kupata viongozi.

Hata wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Arusha mwaka jana, mwandishi wa habari mkongwe hapa nchini alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa serikali za mseto zinaweza kuwa na maana kama zitatumika kama mpito kwa ajili ya kuandaa katiba.

Leo hii hapa nyumbani inasikitisha kuona kuwa watu wameanza kubishana juu ya jambo ambalo hata kama wakikubaliana na kulitekeleza kama lilivyo, haliwezi kuwa suluhu ya matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yanayoikabili Zanzibar hivi sasa.

Achilia mbali mlolongo wa migogoro iliyosababisha kukua kwa mpasuko visiwani humo, hivi sasa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Wananchi (CUF) wapo katika mchakato kuhusiana na namna ya kutekeleza makubaliano ya kuunda serikali ya mseto, kama moja ya dawa za kumaliza mpasuko kisiwani humo.

Lakini wapo ambao wanashangilia na wanaamini kuwa kuundwa kwa serikali ya mseto ndiyo suluhu ya matatizo ya Zanzibar.

Hawa, naamini kuwa wakati walipoliangalia tatizo linaloikabili Zanzibar leo hii, walipofushwa na kile kinachotokea hivi sasa, bila kuchunguza kwa kina sababu ya hayo yanayotokea.

Ni kweli kuwa serikali ya mseto inaweza kuwa sehemu ya dawa ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar, lakini siamini kuwa aina ya serikali hii inaweza kuwa suluhu ya kudumu ya mpasuko wa kisiasa nchini humo.

Kwa hatua tunayoelekea tunaweza tusiangalie nyuma sana kutafuta historia katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.

Lakini kuna kila haja ya kutafuta namna ambayo itahakikisha kuwa chaguzi zinakuwa huru na haki, na kama tutaweza kufukia mazingira kama hayo, kila mgombea ataweza kukubaliana na matokeo ya uchaguzi hata kama atashindwa kwa kura chache.

Katika mazingira kama hayo sidhani kama tutahitaji serikali ya mseto kwa sababu atakayeshindwa atakuwa anajua kuwa ameshindwa kwa haki, hivyo hakutakuwa na sababu wala kitu cha kulalamikia uchaguzi.

Kukosekana kwa mazingira ya uchaguzi huru na wa haki Zanzibar ndiyo chanzo cha migogoro yote kisiwani humo, hata kama itakubaliwa kuwa serikali ya mseto ianze sasa, mpaka utakapofika wakati viongozi watakapoanza kuheshimu chaguzi.

Pamoja na kuwa CCM imependekeza kuwapo kwa mchakato wa kupata kura ya maoni, inapaswa kufahamu kuwa chimbuko la migogoro ya sasa ni nidhamu mbaya ya kutoheshimu demokrasia katika masanduku ya kupigia kura.

Hivyo, kulikuwa hakuna haja ya kukimbilia kwenye upigwaji wa kura za maoni bila kuanza kuweka mazingira ya kupiga kura za haki kama njia ya kupata jawabu la matatizo yanayoikabili Zanzibar. Hata kama pendekezo la kura ya maoni litakubalika, inapaswa kwanza yaandaliwe mazingira ambayo yataifanya kura hiyo ionekane na wote kuwa ni huru na ya haki, kinyume na hayo, tutakuwa tunaandaa mgawanyiko mwingine. Zanzibar inakabiliwa na matatizo mengi katika nyanja mbalimbali lakini ufumbuzi ni kukubali na kuheshimu matokeo ya chaguzi tu na si vinginevyo na kama tutaweza kufikia hapo, tutakuwa tumepata suluhu ya migogoro kisiwani humo.


h.sep3.gif
 
Back
Top Bottom