Demokrasia ni kupinga, kupingwa, kukataa na kukataliwa

Allan Harold

Member
May 5, 2014
32
67
UKIAMUA kupinga kitu uwe tayari kupingwa na wewe. Msimamo wowote unaouchukua kinyume ama na msimamo wa wengi au ule unaoonekana kukubalika na wengi si lazima ukubaliwe na wengine – hata kama ni sahihi kwa kiasi gani.

Katika demokrasia haki ya kukataa msimamo wa wengi ni alama kuu ya demokrasia. Wapo wanaofikiria kuwa alama ya demokrasia ni vyama vingi, uchaguzi au kupiga kura; kwa maoni yangu alama kuu ni jinsi gani watu wanavumiliana na kwa namna gani wanavumilia watu wasiokubali.

Kuna tofauti ya kupinga na kukataa japo yote mawili yanahusiana na kutokukubaliana. Mtu anapoamua kupinga si lazima sana aanishe sababu za kupinga kwake au kwanini hakubaliani na kile kilichokubaliwa na wengine. Anaweza kusema “sitaki tu” na ikatosha. Hata hivyo mtu anapoamua kukataa japo anakuwa anapinga lakini hapa anaonesha kwanini anamsimamo huo na zaidi sana anaweza kuonesha makosa ya kile kilichokubaliwa na wengine ili awashawishi wakubaliane naye.

Katika siasa hata hivyo watu wana haki ya kutokufuata mkumbo. Hatuwezi kuwalazimisha watu wawe kama sisi tulivyo au wakubaliane na misimamo yetu au kutumia mbinu za kuwalazimisha ili wakubaliane nasi. Tunachoweza kufanya ni kuonesha makosa ya misimamo yao na kuwashawishi kwa nguvu ya hoja si vitisho kwanini sisi tuko sahihi na siyo wao.

Mwalimu Nyerere akiandika katika kijitabu kidogo cha “Tujisahihishe” akionesha umahiri wake katika kuelewa Sanaa na ufundi wa kujenga hoja anasema hivi

Mara nyingi hoja tunazotumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda, au kukubali mawazo yetu, huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayoyjadili.

Na anatoa mfano wa jambo hili – japo anauita ni mfano wa kipuuzi:

Ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali ya kwako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana.

Hoja ya Nyerere hapa iko wazi sana; kuwa hoja hujibiwa kwa hoja na hoja yenye nguvu ndiyo inapaswa kukubaliwa. Kwamba, hoja haiwi mbaya au haikubaliki kwa sababu aliyeitoa hatumpendi! Kwamba, tuko tayari kukubali hoja ya “mwenzetu” hata kama ni hoja mbaya na tunakataa tena vikali na kwa kebehi hoja ya “mwingine” kwa sababu tu si mwenzetu! Kumbe ukweli wa hoja hautegemei nani katoa hoja hiyo.

Nyerere anaendelea kusema hivi kuhusu hili kwenye Kijitabu hicho cha “Tujisahihishe”:

Kosa jingine kubwa ni kuwagawa watu katika makundi; kundi “letu” na kundi “lao”… Kosa hili kwa pande zote mbili ni baya. Linagawa viongozi katika makundi, na ni wazi kwamba viongozi wakigawanyika katika makundi chama pia huwa katika hatari ya kugawanyika katika makundi na kukosa shabaha yake.

Ni wazi kuwa ni muhimu watu kutofautisha tofauti za hoja na tofauti za kibinafsi. Watu wanaweza kuwa kwenye chama kimoja lakini wakawa na maono tofauti kuhusu mambo mbalimbali. Kwa mfano, watu kwenye chama kimoja wanaweza kudhamiria kabisa kuwa wanataka kuhakikisha kuwa wananchi wanajenga nyumba za kisasa kwa bei nafuu. Wanapokuja kutofautiana ni katika namna ya kufikia lengo hili. Wapo ambao labda kwa kuamini katika Ubepari zaidi wanaona kuwa suala hili si jukumu la serikali na wanataka “soko” liamue nani anajenga nini na kwa gharama gani huku wengine wanaona kuwa ni jukumu la serikali kuweka mazingira yatakayochangia gharama za ujenzi kushuka.

Sasa tofauti kama hizi ni tofauti za msingi katika jukwaa la majadiliano ya kidemokrasia. Ni muhimu watu wenye mawazo tofauti wapewe nafasi ya kutoa mawazo hayo na kuwashawishi wengine. Na pale ambapo mawazo ya upande mmoja yanapokubaliwa wale waliokataliwa mawazo yao si lazima wajione kuwa wanaanzisha mapambano ya kujaribu kuhujumu kilichokubaliwa na wengi. Hii si demokrasia; demokrasia ni pamoja na kukubali maamuzi ya wengi hata kama yanaweza kuwa na makosa. Mwanademokrasia wa kweli ni mtu mvumilivu ambaye anaweza kutumia muda na uwezo wake kuwashawishi wengine waone makosa ya maamuzi yao.

Ni lazima tufike mahali tujue kuwa kukataliwa kwa hoja za watu au mtu haina maana ni kukataliwa kwa watu wenyewe. Nyerere analieleza hili vizuri kwenye kijitabu hicho nilichotaja hapo juu:

‘Wanaopingwa hawana budi wakubali kuwa kinachopingwa ni zile hoja zao, siyo wao wenyewe. Bila mazoea haya mazungumzo hayana maana; yanakuwa ni kupoteza wakati…Kadhalika, hoja zetu zikijibiwa kwa kupingwa halafu tukawakasirikia waliozipinga tunafanya mazungumzo yasiwe na maana, kwa sababu tunapenda hoja zetu zikubaliwe hata kama SI HOJA SAFI (Msisitizo wangu).

Katika siasa zetu za Tanzania sasa hivi tumefika mahali inakuwa vigumu watu ndani ya chama hicho hicho kuwa na maoni au mitazamo tofauti. Wanachama wanaonekana kutaka kulazimishwa kuwa katika mtazamo wa aina moja au maoni ya aina moja kuhusiana na jambo fulani na wakati wowote kunapotokea watu kutokukubaliana basi kunaanza kujengwa uhasama na hata chuki dhidi ya mtu au watu.

Hii si demokrasia!

Chama kinapochukua msimamo kuhusu jambo fulani ni jukumu la viongozi wake kusimamia msimamo huo. Wanachama wa kawaida wanaweza kutokubaliana nao sana na hata kujadili mawazo mbadala lakini viongozi wanapaswa ama kuunga mkono msimamo au uamuzi wa chama au kama hawawezi kuunga mkono kuachia ngazi (kujiuzulu) katika kupinga na hapo ndipo wanaweza kuonesha kukataa kwao.

Lakini pia ni vizuri kuweka wazi kuwa mtu anapochukua msimamo wa kukataa na kupinga uamuzi au msimamo wa chama ni lazima pia awe tayari kukubali matokeo ya kufanya hivyo. Huwezi kupinga au kukataa maamuzi ya chama halafu ukabakia ulivyo hasa kama ni kiongozi. Mwanachama wa kawaida anaweza kufanya hivi bila matokeo makubwa lakini kiongozi wa chama hawezi kwenda kinyume na chama chake au msimamo wa chama chake tena hadharani halafu akabakia kuwa kiongozi; ni lazima kuwe na matokeo.

Hili ni jambo la kutafakari kidogo. Nimrudie Nyerere kidogo (kwani mimi ni mmoja wa wanafunzi wazuri wa Falsafa ya Mwalimu). Katika kijitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania Nyerere anaelezea vizuri sana dhana hii ambayo bado haijakolea miongoni mwa viongozi wetu. Kiongozi wa ngazi ya chini unaposhindwa kutetea msimamo wako wa kwanza (wenye makosa) huwezi kuendelea kuwa kiongozi halafu utoe ushauri mwingine. Ni vizuri ukajiuzulu ili aje kiongozi mwingine atoe maoni mengine.

Nafasi ya kiongozi kupingana na viongozi wengine ndani ya chama ni katika vikao vya chama; ni humu ambapo kila kiongozi anapaswa kuwa na haki ya kulindwa kutoa maoni yake na kuyatetea. Itakuwa hatari sana kama kwenye vikao vya chama viongozi wanashindwa kutoa maoni kwa uhuru wakiogopa kuonekana wako kinyume cha chama. Ni humu wanatakiwa viongozi wawe na uwezo wa kushawishi wengine na maamuzi yanapoamuliwa kwa kura basi yaonekane kweli yametokana na mjadala huru na wa wazi. Kama hili ni gumu kutokea ndani ya chama basi demokrasia inakufa zaidi ndani ya chama kuliko nje ya chama.

Lakini kama kiongozi anashindwa au anaogopa kutoa msimamo wake ndani ya chama halafu anaenda kupingana na chama nje ya chama chake kwa sababu hakutaka kuonekana anapingana na chama ndani basi anapaswa kujiuzulu; kwa sababu tu alikuwa na nafasi ya kuwashawishi wengine ndani ya chama kuchukua msimamo wake na hakufanya hivyo.

Lakini inakuwaje kama haki ya kupinga hailindwi ndani ya chama? Hili ni jambo la kufikirisha kidogo. Chama cha kisiasa ambacho hakina mfumo wa kulinda na kukubali watu kupingana kwa hoja – si kwa vioja – kitajikuta kwenye matatizo kwani kitakuwa kinalazimisha watu kuwa sawasawa kiasi kwamba kitakuwa kinajinyima chenyewe hoja za kikosoaji na fikra mbadala. Maana kama watu wote kwenye kikao wanatoa maoni ya kuunga mkono tu hata kama wengine wana mawazo kinyume na ya wengi basi maoni na mawazo yatakayokuwa yanatoka kwenye kikao yanaweza kuwa siyo ya kina sana.

Ni katika kupingwa, kupinga na kupingana kwa hoja ndipo hoja bora na madhubuti inapoweza kupatikana. Adui mkubwa wa demokrasia ni watu kulazimishwa kukubaliana; alama kuu ya utawala wa kiimla ni kulazimisha watu kukubaliana. Madikteta na tawala za kibabe zinaogopa na hazikubali sana kupinga.

Wakati mwingine ni hawa wenye kupinga ndio wanakuwa upande sahihi wa historia siyo wale wengi wanaokubali bila kujiuliza au kupinga. Tulipoanzisha mapambano ya kifikra kazi kubwa zaidi ilikuwa ni katika kukataa misimamo na maelezo ya serikali ambayo wengi waliyakubali kwa sababu “Waziri Mkuu kasema” au “Ikulu imetoa tamko” au “Rais kasema”. Tulionesha wakati ule kuwa katika demokrasia ni jukumu la wasomi na wanaharakati kusimama mbele ya watawala na kuwahoji na hata kuwakatalia.

Leo hii tunapoelekea chaguzi mbalimbali za mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani; vyama vya siasa vitajikuta vinalazimishwa kuamua mapema zaidi vinasimama upande gani; vinakubali kukosolewa, mawazo tofauti na fikra tofauti? Au vyama vinajikuta vinalazimisha watu wote kuwa na mawazo yanayofanana kama senene wanaoruka pamoja? Baada ya malengo ya mipango kukubaliwa au kuwekwa wazi ni muhimu wanachama wawe huru kutoa maoni na misimamo yao kuhusiana na kufikia malengo hayo bila hofu ya kuonekana wasaliti. Hili ni kweli hata katika kujadiliana mikakati. Mikakati si lazima ikubaliwe na kila mtu; lakini wanaopinga mikakati hiyo ni lazima wafanye hivyo kwa uwazi na watumie njia zote zilizo wazi mbele yao kufanya hivyo. Kama njia hizo haziko wazi.

Ni jukumu lao kulazimisha zifunguliwe. Na hili ni sehemu ya demokrasia. Vinginevyo, tutaishia kutishana, kukosana kwa kukosoana, na kupingana kunakozaa kupigana.

Demokrasia ina gharama; na sehemu yake ya gharama ni kukubali kupingwa na kuwa tayari kupinga kwa hoja.
 
Back
Top Bottom