Demokrasia; kwa faida ya nani na kwa wakati gani?

sulphadoxine

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
2,257
644
KAMA kuna kitu ambacho watu wanakosea, basi ni kuhimiza demokrasia kwenye vyama vilivyopo kwenye harakati za kusaka utawala wa nchi badala ya kusisitiza hilo ndani ya vyama mbalimbali duniani, vilivyopewa ridhaa na wananchi kushika dola.

Nasema hivyo kwa sababu kumekuwepo na kasumba ama tuseme unafiki wa kuhimiza demokrasia ndani ya katiba za vyama vya kisiasa, hasa vile ambavyo havijapata ridhaa ya wananchi kuunda serikali kupitia uchaguzi mkuu, bila kujali kwamba nafasi ya demokrasia ndani ya vyama pinzani vya kisiasa siyo muhimu sana kama ilivyo kwa chama tawala, kwa vile vyama hivyo bado viko kwenye harakati za kusaka utawala (ama ukombozi wa nchi) kama wanavyoita wao.

Limekuwa ni jambo la kawaida siku hizi kuwasikia viongozi wa serikali na wale wa chama tawala, wakihimiza mabadiliko ya utawala hasa kwenye ngazi za juu za uongozi wa vyama vya upinzani, wakilenga nafasi za Mwenyekiti Taifa na ile ya Katibu Mkuu wa Chama taifa, huku pia wakipinga uteuzi wa majina yale yale kwenye nafasi ya kuwania Urais wa nchi!

Naweza kusema kwamba siyo kweli kuwa wamekuwa wakifanya hivyo ili kuonesha umuhimu wa kuimarisha misingi ya demokrasia ndani ya vyama hivyo, bali kinachoonekana hapo ni hofu ya ukubwa wa majina ya watu wanaoshika nyadhifa hizo za juu kwenye vyama hivyo vya upinzani na namna ambavyo wamekuwa na ushawishi mkubwa kwa wananchi, hivyo kukihatarisha chama tawala! Historia ya dunia inaonesha kwamba vyama vingi vya kisiasa vinapokuwa kwenye mapambano ya kusaka uhuru ama hata mabadiliko ya utawala wa nchi, vimekuwa vikiongozwa au kubebwa na majina makubwa kupitia umaarufu wa viongozi wake, kuliko ukomavu na ubora wa demokrasia inayooneshwa ndani ya uongozi wa vyama hivyo.

Ni ukweli usiopingika kwamba mfumo wa utawala wa kidemokrasia una umuhimu wake katika uongozi, lakini ni lazima ieleweke pia kuwa ni wakati gani demokrasia inapaswa kutumika na wakati gani siyo muhimu kuitumia; Nasema hivyo kwa sababu siyo wakati wote ni muhimu ama lazima kutumia mfumo wa demokrasia ndani ya vyama vya kisiasa hasa vile vilivyoko kwenye harakati za kusaka kushika dola, ama wakati mwingine pia ndani ya taasisi, asasi, nchi ama vikundi mbalimbali vya kijamii.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa siyo vyama, asasi, vikundi au nchi zote za kidemokrasia ndizo zenye mafanikio kuliko nchi nyingine zinazofuata mfumo mwingine wa kiutawala, ingawa sikatai kwamba mfumo huo una faida na hasara zake pia kama ilivyo mifumo mingine ya kiutawala duniani, bali cha muhimu zaidi ni kuangalia ‘manufaa ya demokrasia kwa wananchi' na siyo ‘manufaa ya watawala' kupitia mfumo wa demokrasia ama mwingine wowote ule.

Sina muda wa kutosha kutaja nchi nyingi za kifalme zenye mafanikio makubwa kuliko zile za kidemokrasia, wala sina haja ya kutaja nchi zinazotawaliwa kijeshi au hata kidini ambazo pia ziko mbali kiuchumi kuliko zile za kidemokrasia; ingawa sipendi pia kueleweka vibaya kwamba napinga mfumo wa demokrasia Tanzania, la hasha; ninachokisisitiza kwenye makala hii ni umuhimu wa ‘demokrasia ndani ya chama tawala kwa faida ya wananchi' na siyo ‘demokrasia ndani ya vyama vya upinzani kwa faida ya chama tawala'!

Nasema hivyo kwa sababu wanaosisitiza mabadiliko ndani ya uongozi wa juu wa vyama vya siasa eti kwa kigezo cha kuonesha demokrasia ndani ya vyama vyao, siyo wananchi ama wanachama wa vyama hivyo, bali ni viongozi wa Serikali na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakilenga zaidi kuwadhohofisha viongozi wa vyama hivyo ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa mwiba kwa utawala wao!

Kinachoshangaza zaidi na kuonesha unafiki na pengine hofu yao kwa viongozi hao, ni pale mabadiliko hayo ya kidemokrasia kwenye ngazi za juu za uongozi ndani ya vyama vya upinzani, yamekuwa yakielekezwa zaidi kwa vyama tishio vya upinzani kama vile Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema na kile cha Wananchi, CUF.

Majina maarufu kama vile Wilbrod Slaa, Freeman Mbowe, Ibrahimu Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad yamekuwa yakihofiwa sana na chama tawala kiasi cha kudhaniwa kuhusika kuhimiza au kuchochea kwa njia mbalimbali mabadiliko ya uongozi ndani ya vyama hivyo vya upinzani, yatakayo zipoteza walau sura hizo kwenye siasa za Tanzania ili watawala wa nchi hii wapate uhuru wa kujitanua madarakani na kufanya watakalo, maadamu hakuna ‘mjanja' wa kuhoji na kuibua maovu yao.

Kama ilivyokuwa enzi za wakoloni waliolivamia bara letu la Afrika, wao pia walihimiza na kuchochea mabadiliko ya uongozi ndani ya vyama vya siasa vilivyokuwa kwenye harakati za kuwang'oa wakoloni na kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika;

Lengo kuu likiwa siyo kujenga demokrasia ndani ya vyama hivyo bali ilikuwa ni njama tu za kupenyeza viongozi dhahifu ama vibaraka wao kwenye uongozi wa juu wa vyama hivyo, ili wapate kuwatawala milele! Kwa kulitambua hilo, viongozi wa vyama hivyo barani Afrika walisimama kidete kuendeleza mapambano ya ukombozi kupitia vyama vyao, bila kujali makelele ya wakoloni ya kuhimiza demokrasia ‘bandia' ndani ya vyama vya kiharakati, ili kuvidhohofisha kwa lengo la kujinufaisha wao madarakani kama watawala kupitia viongozi dhahifu waliowapenyeza na kuwasimika kwa hila ndani ya vyama hivyo!

Wakitambua kuwa ‘demokrasia ni muhimu wakati wa kushika dola' na siyo wakati wa harakati za kusaka ukombozi; vyama hivyo vya ukombozi kamwe havikuruhusu mabadiliko ya viongozi wao mahiri na machachari kwenye harakati hizo za ukombozi, bali walibadilishana nyadhifa hizo za juu wao kwa wao kwa kadili walivyoona inafaa kimajukumu, bila kuathiri vuguvugu la harakati zao za ukombozi.

Ndiyo maana Mandela alidumu na waandamani wake wale wale ndani ya chama cha ANC, Samora pia vivyo hivyo na kundi la watu wake walioaminiana ndani ya chama chao cha Frelimo, Mugabe na wenzake wale wale wa chama cha ZANU-PF, n.k; hivyo basi ikiwa wananchi bado wanawakubali, kwanini wakoloni ama watawala wahimize mabadiliko kama siyo hofu yao tu?

Kwa mfano hapa kwetu Tanganyika enzi hizo, pamoja na kuwepo watu maarufu katika harakati za kutafuta uhuru wa taifa letu, lakini nafasi za juu za uongozi wa chama cha TANU zilimilikiwa na sura zile zile za viongozi ‘tishio' kwa wakoloni kama vile Rashid Kawawa, Bibi Titi Mohamed, Oscar Kambona na Julius Kambarage, ambao hawakuona umuhimu wa demokrasia ndani ya chama chao, mpaka pale kazi ya ukombozi ilipohitimishwa mwaka 1961.

Je, nani alithubutu kuhoji demokrasia ndani ya chama cha TANU kabla hakijashika dola, kama siyo wakoloni ambao kwa hofu ya kupokonywa utawala wao, hawakutaka kabisa kuziona sura za viongozi wetu hao mahiri waliotuletea uhuru?

Hata leo hii siyo wananchi wanaodai demokrasia ndani ya vyama vya upinzani, bali ni utawala ulioko madarakani ndio unaosisitiza hilo ili kupandikiza viongozi dhahifu ndani ya vyama hivyo kwa faida yao wenyewe! "Mungu Ibariki Tanzania"
 
Back
Top Bottom