DED MALINYI AFUFUA MATUMAINI YA WATOTO WA RUMBANGA

acer

JF-Expert Member
Apr 4, 2012
1,595
142
DED Malinyi alivyofufua matumaini ya watoto wa Rumbanga

Na Oscar Mbuza

NI shule inayopatikana katika kijiji kidogo cha wafugaji cha Rumbanga katika Halmashauri ya Wilaya mpya ya Malinyi mkoani Morogoro ikiwa imevaa sifa zenye pande kuu mbili, moja ikiwa ni hasi na nyingine chanya.

Pande hasi kwa shule hii ya Msingi Rumbanga yenye madarasa kuanzia la kwanza hadi la nne, ni mazingira yasiyo rafiki kwa mwanafunzi kuweza kujifunza.

Wanafunzi wa shule hiyo kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwake wamekuwa wakisoma katika majengo ‘yaliyovaa suti’ kwa maana ya kuta za shule na hata dali la juu kuezekwa kwa nyasi, huku madawati yakiwa ni miti iliyolazwa sakafuni, huku choo kikiwa ni jengo la nyasi pia lisilo na ubora wala usalama kwa wanafunzi.

Hata hivyo upo upande wa pili ambao ni chanya kwa shule hii, nao ni taarifa kwamba shule hiyo imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kiwilaya kila mwaka katika kufaulisha wanafunzi katika mitihani ya darasa la nne.

Hata hivyo kivutio kikubwa katika ufaulu huo wa wanafunzi, kimekuwa ni shule hiyo kutokuwa na walimu wa serikali, badala yake kuwategemea walimu wawili wa kujitolea ambao ni watoto wa wanakijiji wenzao ambao baada ya kumaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri waliamua kurudi kijijini ili kuwafundisha wadogo zao.

Ni mchanganyiko wa sifa za pande zote mbili, ile ya shule hiyo kukosa mazingira rafiki ya wanafunzi kusoma, lakini pia ile ya kufanya vizuri kwa wanafunzi wake katika mitihani ya darasa la nne kila mwaka, ndio ulioifanya serikali wilayani Malinyi kuamua kuitazama shule hiyo kwa jicho la huruma.

Ulazima wa kuwepo kwa shule hiyo katika eneo hilo la wafugaji ulitokana na awali wanafunzi kulazimika kutembea umbali mrefu wa hadi kufikia kilometa 34 kwenda na kurudi kufuata masomo katika Shule ya Msingi ya Mwembeni, hatua ambayo ilikuwa inawasababishia wanafunzi vikwazo mbalimbali na baadaye kukatisha masomo yao.

Kama hatua za awali za kuboresha mazingira ya kutoa elimu kwa shule hiyo, serikali ya Malinyi iliamua kubuni mkakati wa makusudi wa kuihamasisha jamii hiyo ya kifugaji katika kijiji cha Rumbanga kuunganisha nguvu zao pamoja ili kuanza ujenzi wa jengo jipya na la kisasa la shule hiyo muhimu.

Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Marcelin Ndimbwa ilikuwa ni kuagiza fedha zilizonusurika katika safari iliyofutwa na Rais John Magufuli kwa watendaji wa juu wa serikali za mitaa kwenda mkoani Simiyu kushiriki sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru Oktoba 14, mwaka huu, zipelekwe kwenye shule hiyo ili zianze kugharamia ujenzi wa jengo jipya la kisasa.

“Ili kutii agizo la Rais (Magufuli) nialigiza zaidi ya Sh milioni 4 ambazo ilikuwa sisi watendaji wa Halmashauri ya Malinyi tuzitumie kwa safari ya kwenda Simiyu, ziletwe hapa katika Shule ya Msingi Rumbanga ili tuanze ujenzi huu,” anasema Ndimbwa.

Mkurugenzi huyo anasema pamoja na nia ya dhati ya serikali ya kuhakikisha kuwa inaboresha miundombinu ya shule katika maeno yote nchini, ikiwemo Malinyi, lakini serikali katika wilaya hiyo ilifurahishwa na mwamko wa wakazi wa kijiji hicho ambao mara baada ya kuuziwa wazo la kuanzisha ujenzi huo kwa nguvu zao wenyewe, waliitikia mwito huo kwa kasi ya ajabu.

“Niseme wazi kuwa namna walivyopokea mpango huu ilitutia sana moyo sisi kama serikali.Wananchi hawa walijikusanya na kuanza kufyatua matofali na hivyo ile fedha tuliyopanga kuwapa tuliitumia kununua mifuko ya saruji na kazi ya ujenzi waliifanya wao pia,” anasema Ndimbwa.

Mkurugenzi huyo anasema nia ya serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 25, mwaka huu, jengo hilo linakuwa limekamilika na kupigwa bati ambazo zitatolewa pia na halmashauri ya wilaya ya Malinyi huku akisema mabati hayo yameshaandaliwa tayari.

“Shule itakapofunguliwa Januari mwakani wanafunzi hawa hawatasoma tena katika mabanda haya ya nyasi na badala yake watakuta jengo jipya la kisasa pamoja na choo cha kisasa vikiwa vimekamilika.

“Ni imani yetu kuwa mazingira mapya watakayoyakuta yatawapa chachu ya kufanya vizuri zaidi na hivyo waongoze kitaifa na si kiwilaya tena,” anasema Ndimbwa.

Mkakati huo wa serikali wilayani Malinyi, unaungwa mkono na Diwani wa Kata ya Malinyi ilipo shule hiyo Said Tira anayeeleza pia kufurahishwa na namna jamii ya wafugaji katika Kijiji cha Rumbanga ilivyohamasika katika ujenzi wa shule hiyo na kwamba wananchi hao wanapaswa kuungwa mkono na serikali kwa nguvu zote.

“Na mimi kwa dhati niwapongeze Mkuu wa Wilaya Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji Ndimbwa kwa namna walivyolipokea suala hili na kulipa msukumo baada ya mimi kama diwani wa eneo hilo kuanzisha uhamasishaji kwa wananchi wale.

“Kitendo hiki ndicho kinachosisitizwa na Rais (Magufuli) kwamba wananchi waanzishe miradi ya maendeleo bila kusubiri serikali iwaanzishie. Watu wa Rumbanga ni mfano wa kuigwa,” anasema Tira.

Katibu wa Kamati ya Ujenzi wa shule hiyo Joseph Paschal anasema kwa vile shule hiyo ni ya darasa la kwanza hadi la nne, iliazimiwa kujenga jengo lenye madarasa mawili ili kuwawezesha wanafunzi kuingia kwa mikupuo miwili, awamu ya kwanza ikiwa ni ya darasa la kwanza na pili na baadaye darasa la tatu na la nne.

“Tunashukuru serikali yetu katika awamu ya kwanza tayari ilitupatia Sh 2,580,000 ambazo tulinunua saruji kwa ajili ya kuanzia ujenzi. Wananchi wamefurahi sana kwa ushirikiano huu ambao serikali inatupatia.

“Mbali ya shule kutokana na hamasa tuliyoipata, tayari tumejenga daraja katika mto Rumbanga ambako wanafunzi walikuwa wanashindwa kuvuka wakati wa mvua na hivyo kukosa masomo. Sasa watapata majengo bora na pia watavuka bila shida katika mto Rumbanga,” anasema Paschal.

Kwa upande wao wakizungumzia changamoto wanazokumbana nazo katika kujifunza katika shule hiyo, mwanafunzi Salu Kuba wa darasa la kwanza katika shule hiyo na Kulwa Paul wa darasa la pili, wanasema ni pamoja na kulowana na mvua wakiwa darasani wakati wa masika.

“Mvua ikija tulikuwa tunapewa maturubai yapo pale shuleni ndio tunajifunika, lakini bado tulikuwa tunalowana na mvua na kuanza kutetemeka. Wakati mwingine mvua ilikuwa inatusababishia kupata homa na kushindwa kusoma vizuri,” anasema Kulwa.

Anasema mbali ya mazingira hayo magumu shuleni, lakini pia ukosefu wa daraja katika mto Rumbanga pia ulikuwa ni kikwazo kikubwa katika kuhudhuria masomo darasani kwani kuna wakati walikuwa wakilazimika kurejea makwao pale wanapofika mtoni na kukuta maji yamejaa na hivyo kuathiri ushiriki wao katika masomo.

Mtoto Salu anasema kitendo cha kukaa kwenye magogo wawapo darasani kilikuwa kinawasababishia kuumwa na wadudu watambao chini na kupata madhara mbalimbali na hivyo kushindwa kushiriki masomo itakiwavyo.

Kama vile michango iliyotolewa na halmashauri bado haijamridhisha Mkurugenzi Ndimbwa aliyevutiwa na kujitolea kwa wananchi hao, anasema mara jengo hilo litakapokamilika serikali itapeleka walimu katika shule hiyo ili kuongeza nguvu.

Anasema pia serikali itaingiza katika mpango wake wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha baadhi ya barabara za kijiji hicho ili kuziboresha na kuzifanya kupitika kirahisi na kwa uhakika wakati wote wa mwaka na hivyo kukuza maendeleo ya eneo hilo.

Source; HabariLeo 26/12/'16
1482771034589.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom