DAWASCO imekiuka mikataba; hatua za haraka zinahitajika kuboresha upatikanaji wa maji DSM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

DAWASCO imekiuka mikataba; hatua za haraka zinahitajika kuboresha upatikanaji wa maji DSM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by John Mnyika, Feb 23, 2012.

 1. John Mnyika

  John Mnyika Verified User

  #1
  Feb 23, 2012
  Joined: Jun 16, 2006
  Messages: 715
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 0
  Wanajamii, katika mijadala kadhaa humu mmekuwa mkigusia suala la matatizo katika upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Dar es salaam mara baada ya mafuriko yaliyotokea Disemba 2011 na wengine mmetaka kupata kauli yangu kuhusu hatua ambazo tumechukua kuhusu hali hiyo.

  Naomba kujibu kwa ujumla maswali yote yaliyoulizwa kupitia ujumbe huu, na nitaendelea kujibu maswali mengine yatayojitokeza katika mjadala huu kwa kuwa nimeamua katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo kuweka kipaumbele cha kwanza katika kazi zangu za kila siku kufuatilia masuala yanayohusiana na maji katika Jimbo la Ubungo.

  Kazi ambazo tumezifanya kuhusu ufuatiliaji wa hali ya maji na miradi ya maji katika kipindi cha toka nilipoitisha Kongamano la Maji Ubungo mwanzoni mwa mwaka 2011 mpaka mwishoni mwa mwaka huo, na mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza tutaelezana katika siku za baadaye.

  Kwa kuwa wachangiaji mmeulizia hatua ambazo nimechukua mwaka huu wa 2012 naomba niwajulishe tu kwamba toka miundombinu ya maji iharibiwe na mafuriko nilichukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa wajibu wa kibunge wa kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali, ufuatiliaji huo niliufanya wakati tunashughulikia miundombinu kwa ujumla ikiwemo barabara na madaraja yaliyoharibiwa na maafa.

  Kwa nyakati zote hizo sikutoa kauli kwa umma kwa sababu nilikuwa natumia taratibu za kawaida za kiofisi na kuziachia mamlaka husika za kiserikali kutimiza wajibu wake wa utekelezaji.

  Hata hivyo, nimelazimika kutoa mrejesho kwa wananchi walionituma kuhusu suala hili kwa kuwa: Mosi, kasi ya DAWASCO kushughulikia matatizo yaliyojitokeza mara baada ya mafuriko katika maeneo ya wananchi wa kawaida hairidhishi, ukilinganisha na hatua ambazo walichukua kwa haraka mabomba ya maji ya kwenda Ikulu yalipoharibiwa.

  Pili, DAWASCO inafanya kazi kimya kimya bila kueleza kwa umma matatizo yaliyopo na ratiba ya utatuzi wa matatizo hayo; ukilinganisha DAWASCO na TANESCO kati ya mgawo wa umeme na mgawo wa maji, walau taarifa za mgawo wa umeme zinatoka mara kwa mara. Nne, DAWASCO pamoja na kuacha kutoa taarifa kwa umma, inachelewa hata kujibu barua na kutoa taarifa kwa wawakilishi wa wananchi.

  Nilitumia taratibu za kawaida za kiofisi tarehe 14 Februari 2012 kuiandikia barua DAWASCO kuchukua hatua kuhusu tatizo la kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji katika Jiji la Dar es salaam hali ambayo imesababisha kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo; hata hivyo, mpaka ninavyoandika ujumbe huu barua hiyo haijajibiwa, imenibidi nitoe kauli jana ya kuwapa siku tatu kutoa majibu.

  Kwa mtizamo wangu, DAWASCO imekiuka mikataba miwili muhimu inayoongoza kazi zake na kusababisha matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.DAWASCO inapaswa kufanya ukaguzi wa mtandao wa maji na kurekebisha kasoro zilizopo na kutoa taarifa kwa umma kuhusu matitizo ya maji yanayoendelea katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo.

  Nakusudia kuchukua hatua zaidi za kibunge dhidi ya DAWASCO iwapo haitazingatia masharti ya mikataba husika na kushughulikia matatizo ya maji yanayoendelea hivi sasa katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo.

  Ikumbukwe kuwa DAWASCO ni shirika la umma lililoundwa kwa tangazo la Serikali nambari 139 la tarehe 20 Mei 2005 kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992.Tarehe 1 Julai 2005 DAWASCO ilipewa mkataba wa ukodishaji (lease agreement) na DAWASA ambao unaitaka DAWASCO kuendesha miundombinu ya maji na kuhakikisha matengenezo ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam.

  Aidha, katika kutekeleza mkataba huo DAWASCO inapaswa kuzingatia mkataba wa huduma kwa wateja (Client Service Charter) ambao unaitaka DAWASCO kushughulikia kwa muda maalum malalamiko ya wateja na kutoa taarifa kwa umma kila panapokuwa na matatizo ya maji.

  Kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa wateja DAWASCO inapaswa kushughulia malalamiko ya wateja na kuyajibu ndani ya siku tano na iwapo matatizo yaliyopo yanahitaji hatua za kiufundi; DAWASCO inatakiwa kushughulikia matatizo hayo ndani ya siku 30.

  Kuanzia mwishoni mwa mwezi Disemba 2011 mara baada ya maafa ya mafuriko katika Mkoa wa Dar es salaam mpaka leo tarehe 22 Februari 2012 nimepokea malalamiko mbalimbali toka kwa wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo sio nzuri kama ilivyokuwa baada ya hatua ambazo tulichukua kwa nyakati mbalimbali kuanzia Januari 2011 mpaka Septemba 2011.

  Itakumbukwa kwamba tarehe 5 mwezi Septemba 2011 nilifanya maandamano ya kwenda DAWASCO nikiwa na wawakilishi wa wananchi wa kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo ambapo tulifanya mkutano na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO.

  Kufuatia mkutano huo DAWASCO ilichukua hatua mbalimbali ambazo ziliboresha mgawo wa maji katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo kabla ya ratiba ya mgawo kuvurugika kufuatia mafuriko yaliyokumba mkoa wa Dar es salaam.

  Hata hivyo, baada ya mafuriko hayo DAWASCO haikuchukua hatua zinazostahili kwa wakati na kuachia kurejea tena kwa mtandao haramu wa biashara ya maji wenye kuhujumu wananchi hususan wa kipato cha chini katika Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.

  Hivyo, bodi ya wakurugenzi ya DAWASCO chini ya uenyekiti wa Mhandisi Suleiman Said Suleiman na Mtendaji Mkuu wa kampuni Jackson Midala wanapaswa kurekebisha kwa haraka mfumo mzima wa ufuatiliaji wa DAWASCO kuwezesha ukaguzi wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji.

  Katika kipindi hiki cha matatizo makubwa ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo DAWASCO iache kuwatumia wafanyakazi wanaohusika na ukaguzi kufanya kazi tofauti za kusoma mita na kugawa Ankara badala yake wafanyakazi tajwa wafanye ufuatiliaji wa dharura wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji katika maeneo mbalimbali.

  Baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kutembelewa ni kata za Makuburi, Kimara, Saranga, Mbezi Luis, Msigani, Kwembe, Goba (hapa kuna tatizo pia kwenye mradi unaoongozwa na kamati, baada ya kuunganisha nguvu ya umma mtendaji kata ameondolewa na hatua za haraka zinaendelea kuchukuliwa na Manispaa ), Kibamba , Sinza, Makurumla, Mabibo, Manzese, Ubungo na Mburahati.

  Kwa upande mwingine, kwa kuwa mkataba wa huduma kwa wateja unatoa haki kwa wateja wa DAWASCO lakini pia unaeleza wajibu; natoa mwito kwa wanajamii ambao mmekuwa mkitoa malalamiko ya ujumla kuhusu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam kutimiza wajibu wa kuwaelekeza wakaguzi husika mitaa yenye matatizo katika mtandao wa maji ili hatua ziweze kuchukuliwa.

  Mkataba huo unawataka wateja wa DAWASCO kutoa taarifa kuhusu uharibifu wa miundombinu, wizi wa maji na kuhusu matatizo ya maji hivyo mnaweza kutoa taarifa husika na kufuatilia wakaguzi kufika maeneo yao kwa kupiga nambari ya bure 0225500240 au 0762979627 za DAWASCO makao makuu.

  Pia, mnaweza kuwasilisha kero za maji kwa ofisi ya DAWASCO zilizo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam na kupitia nambari zifuatazo: Temeke +255 775016184, Ilala +255 775048556, Magomeni +255 775016179, Boko/Tegeta +255 775048553, Tabata +255 775016181, Kawe +255 775016185, Kinondoni +255 775016180 na Kimara +255 775048554. Mtumie pia nafasi hiyo kuwasilisha kwa DAWASCO maelezo na vielelezo kuhusu maeneo ambayo hakuna miundombinu ya maji kabisa au miundombinu iliyopo haijawahi kutoa maji kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kutaka hatua za ziada.

  Matatizo ya maji katika maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo yamedumu kwa miaka mingi, wananchi wametupa wajibu wa kuwawakilisha kuisimamia serikali na mamlaka zake kupunguza kero husika kwa haraka hivyo nawaomba tuendelee kuunganisha nguvu za pamoja ili kuwezesha vitendo zaidi vya kushinikiza uwajibikaji kwenye sekta ya maji katika kipindi cha karibuni. Nitawapa taarifa zaidi hatua kwa hatua, kuhusu nini kitafuata. Maslahi ya UMMA kwanza.

  JJ

   
 2. W

  WildCard JF-Expert Member

  #2
  Feb 23, 2012
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Mh Mnyika,
  Fuatilia kwa bidii ile kauli ya JMK ya Maji Dar 2013. Hii ikitekelezwa angalau kwa nusu yake tu nafuu kubwa utaiona. Vinginevyo kugawana haya maji kidogo yaliyopo haisaidii kitu. Hayatoshi na yanapotea sana kwa ajili ya miundombinu chakavu iliyopo. Hakuna muujiza mwingine kwa sasa zaidi ya kuwekeza upya kwenye maji ya Dar na kwingineko nchi hii. Tulijisahau mno huku miji ikikua na mahitaji ya maji yakiongezeka kwa kasi ya ajabu.
   
 3. R

  Rickshaw Member

  #3
  Feb 23, 2012
  Joined: Feb 21, 2012
  Messages: 15
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nushukuru sana kwa kuwa inaelekea ulinielewa vyema katika uzi wangu "Mnyika Mkonge unakuhus nini, kachape kazi jimboni? japo moderators hawakunitendea haki kwa kuufuta.
   
 4. zomba

  zomba JF-Expert Member

  #4
  Feb 23, 2012
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 17,081
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 0
  Mnyika hizi ndio kazi za mbunge, sio kapayuka payuka hoovyo kama wabunge wengine.

  Hapo tupo pamoja na nakupongeza.
   
 5. Albedo

  Albedo JF-Expert Member

  #5
  Feb 23, 2012
  Joined: Feb 24, 2008
  Messages: 5,566
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 135
  Mkuu JJ sometimes hawa watu wanatakiwa kupewa Kupewa Ultimatum, Wakishindwa Nguvu ya Uma inabidi Ichuke Nafasi yake. Haya Majitu hayaendi pasi na Kusukumwa
   
 6. Michael Scofield

  Michael Scofield JF-Expert Member

  #6
  Feb 23, 2012
  Joined: Jul 30, 2011
  Messages: 1,218
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Hawa DAWASCO tangu wameingia hiyo 2005, hawana walichokifanya zaidi kwa wananchi wa Dar, hakuna jipya, miundombinu ni ile ile walioikuta, imechoka, hawajabuni njia mbadala kutatua kero ya maji jijini.
  Mara ya mwisho kuyaoga maji ya DAWASCO (kipindi hicho CITY WATER) ni 2004, sasa hivi ni mwendo wa maji ya chumvi tu.
   
 7. zomba

  zomba JF-Expert Member

  #7
  Feb 23, 2012
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 17,081
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 0
  Ikishindikana mnaenda Ikulu kumuona Rais. Juisi, kashata ukitoka huko unamualika akuchangishie ujenzi wa visima, au sio?
   
 8. John Mnyika

  John Mnyika Verified User

  #8
  Feb 23, 2012
  Joined: Jun 16, 2006
  Messages: 715
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 0
  WildCard,

  Asante, hili suala la kufuatilia ahadi ya JK ya 2013 nimelifanya na naendelea kulifanya; hata hivyo walivyo wazito wa kutekeleza ahadi wameisogeza mbele mpaka 2014; katika mkutano wa nne wa bunge wakati wa bajeti niliwabana si tu kuzingatia ahadi ya yao ya 2013 bali kurudisha nyuma mpaka 2012, na ni kitu ambacho kinawezekana suala hili likionekana kuwa ni dharura linalohitaji hatua za haraka. Hata hivyo, hii ni mikakati ya muda wa kati na muda mrefu.

  Ujumbe huu niliotoa unahusu hatua za dharura ambazo zinahitajika kwa kiwango hiki hiki cha maji kilichopo sasa; kinatakiwa kugawiwa kwa usawa kwa kuzingatia ratiba ya mgawo wa maji na pia kugawiwa moja kwa moja kwa wateja wa DAWASCO badala ya kuongezeka kwa watu wa kati wenye kufanya biashara ya maji na kuongeza mzigo wa bei kwa wananchi wengi zaidi. Hizi ni hatua zinazowezekana katika kipindi kifupi sana kama kukiwa na ukaguzi wa mtandao wa maji na usimamizi thabiti kwa upande wa DAWASCO. Iliwezekana katika kipindi cha kati ya Septemba mpaka Disemba 2011 na watu wengi zaidi wakapata maji. Tatizo ni kwamba mara baada ya mafuriko ya DSM pamepatikana kisingizio cha kurudi nyuma, ndio maana nataka mamlaka zaidi za DAWASCO zitoke ofisini waende mitaani na kurekebisha hali ya mambo.

  Najua yapo mambo ambayo yapo nje ya uwezo wa DAWASCO, kwa hayo nitaendelea kuzifuatilia mamlaka zingine ikiwemo DAWASA, EWURA, Wizara ya Maji na hata Rais Kikwete mwenyewe. Kazi ambayo wananchi walinichagua ni ya kuwawakilisha na kuzisimamia mamlaka zingine za kiserikali ili kero hii ya maji ipungue; na ndio wajibu ninaoendelea kuufanya; mamlaka hizi zisipochukua hatua zinazostahili kwa wakati wasitarajie kwamba itakuwa kama kipindi kilichopita ambapo mbunge anakaa mpaka baada ya miaka mitano ndio anarudi kwa wananchi; mimi nitaunganisha nguvu ya umma mwaka huu huu mpaka kieleweke.

  JJ
   
 9. John Mnyika

  John Mnyika Verified User

  #9
  Feb 24, 2012
  Joined: Jun 16, 2006
  Messages: 715
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 0
  Rickshaw,

  Sijausoma huo uzi, lakini vyote mkonge na maji vinanihusu kama mtanzania na mwakilishi wa wa wananchi. Kwa aliyekuwepo kwenye mikutano niliyohutubia Mombo na Korogwe anaweza kueleza vizuri zaidi nilichowaeleza watu wa Tanga kuhusu haja ya kuwa na Mpango wa haraka wa kunusuru uchumi wa nchi na kudhibiti mfumuko wa bei kwa pamoja na mambo mengine kuongeza uzalishaji katika taifa na ajira kwa vijana. Hali ya sasa ya kupanda kwa gharama za maisha ni tishio kwa uchumi na usalama wa nchi. Mkoa wa Tanga ulikuwa kati ya maeneo yenye uzalishaji sio wa mkonge tu bali hata viwanda. Na nilizungumza kwa kirefu kuhusu Kiwanda cha Tembo Chipboard pale Mkumbura na magogo toka msitu wa Shume.

  Masuala ya mikoa mingine yanauhusu sana mkoa wa Dar es salaam ikiwemo jimbo la Ubungo, Mosi; jimbo la Ubungo lina wakazi toka mikoa yote nchini. Pili, kusuasua kwa maendeleo ya vijijini kuna athari kubwa kwa mijini kama Ubungo, kwa kuwa rasilimali za mikoa mingine zikishindwa kutumika vizuri utegemezi kwa mikoa hiyo kwa Dar es salaam unaongezeka na sisi kukosa fedha za kuelekeza kwenye miradi mingine muhimu kama ya maji, ukweli ni kwamba mkoa kama Tanga ungeweza kabisa kuichangia DSM fedha za kuwekeza kwenye maendeleo ya jiji ikiwemo miundombinu ya maji, lakini sasa ni kinyume chake; vyanzo vya Dar es salam vya kodi vinaingia kwenye kapu la taifa ambapo lugha ya kila wakati ni kuwa 'kasungura kadogo'. Tatu, vijijini uchumi usipoinuka kwa kuongeza uzalishaji na ajira ongezeko la wimbi la wananchi kuja mijini ikiwemo katika jimbo la Ubungo linazidi, hali hii inafanya jitahada zetu za kuisimamia serikali kuleta maendeleo kila wakati zinaathiriwa na ongezeko la watu kila kukicha; hali yenye athari kwenye mipango miji, mikakati ya ajira nk.

  Ukitazama picha pana, utabaini kwamba nawajibika kuungana na wabunge wote nchini, iwe ni wa Mtwara au Zanzibar na popote kwingine. Wao pia wanawajibika kuungana nami kuja kufanya kazi za maji Ubungo kwa sababu Dar es salaam ni ya wote, wapo wabunge ambao tunaishi nao Ubungo hii, pamoja na kuwa wana makazi pia katika majimbo yao. Hili suala la maji ni letu sote.

  JJ
   
 10. nitonye

  nitonye JF-Expert Member

  #10
  Feb 24, 2012
  Joined: Dec 18, 2011
  Messages: 7,167
  Likes Received: 508
  Trophy Points: 280
  Tunashukuru kwa juhudi zako mheshimiwa, nadhani kero ya maji ni kwa jiji zima sasa unaonaje ukaorganize na wabunge wa majimbo mengine ili kutatua tatizo hili? Maji ya Dawasco siku hizi imekuwa kama anasa maana kupatikana kwake ni kama unatafuta dhahabu vile
   
 11. R

  Rickshaw Member

  #11
  Feb 24, 2012
  Joined: Feb 21, 2012
  Messages: 15
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nashukuru sana kwa majibu mazuri yaliyoshaheni nadharia bila real situation on the ground. Unafahamu kabisa kuwa lipo tatizo kubwa la wananchi kutokufahamu majukumu hasa ya mbunge hususan jukumu ya la "kuisimamia na kuishauri serikali" kama ambavyo unatakakuonyesha kuwa ni bingwa.

  Lakini kumbuka kutokana na mfumo uliopo uliomba kura za wanaubungo wasiokuwa na elimu ya uraia kwa kuwaahidi kuwashughulikia matatizo yao kwanza. Baada ya kupata unajifanya kusahau tatizo kubwa lililopo la ukosefu wa elimu ya uraia na wananchi waliokuchagua 2010 wanakupima kwa vigezo gani si katiba, si kuwasimamia mawaziri, serikali n.k badala yake watakupima na ahdi ulizotoa mdomoni mwaka kuhusu kero zao wakazi wa jimbo la Ubungo.

  Tunachokiogopa sisi tunakukosoa ni kupoteza such a resourceful person kama wewe bungeni kwa ujinga wa wananchi kutokuwa na elimu ya uraia.

  Unachotaliwa kufanya wewe na Chadema ni kuwa na ujasiri kama aliouonyesha Rais Mkapa kutumia Ilani ya uchaguzi ya 2000 kuomba kura na baada ya miezi sita tu akatanaza hadharani kuwa ilani haitekelezeki na akamua kama Raisi kuanza kulipa madeni ya taifa, jambo lilirejesha imani ya wahisani kuifutia Tanzania madeni na ikaweze kukopesheka tena na hivyo kudhibiti mfumuko wa bei, kukuza uchumi n.k

  Kama ulivyo msema wa kiingereza "You cannot eat your cake and have it" haiwezekanai ukaomba kura kwa ahadi za kutatua kero za jimbo fulani halafu na baada ya ukapata ubunge ukajifanya wewe ni wa kitaifa zaidi kabala ya kutangaza hadharani mgongano wa kimaslahi katika ya maslahi ya jimbo na taifa uliopo vichwani mwa wapiga kura wako. Cha kushangaza mgongano huu ni mkubwa sana hata miongoni mwa wasomi hata waliobobea ambao tuliwatarajia wawe wa kwanza kuelimisha umma kuhusu ibara 63 ya Katiba; lakini naye utamkuta anamlalamikia mbunge kwa kukosa maji, barabara n.k
   
 12. R

  Rickshaw Member

  #12
  Feb 24, 2012
  Joined: Feb 21, 2012
  Messages: 15
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nashukuru sana kwa majibu mazuri yaliyoshaheni nadharia bila real situation on the ground. Unafahamu kabisa kuwa lipo tatizo kubwa la wananchi kutokufahamu majukumu hasa ya mbunge hususan jukumu ya la "kuisimamia na kuishauri serikali" kama ambavyo unatakakuonyesha kuwa ni bingwa.

  Lakini kumbuka kutokana na mfumo uliopo uliomba kura za wanaubungo wasiokuwa na elimu ya uraia kwa kuwaahidi kuwashughulikia matatizo yao kwanza. Baada ya kupata unajifanya kusahau tatizo kubwa lililopo la ukosefu wa elimu ya uraia na wananchi waliokuchagua 2010 wanakupima kwa vigezo gani si katiba, si kuwasimamia mawaziri, serikali n.k badala yake watakupima na ahdi ulizotoa mdomoni mwaka kuhusu kero zao wakazi wa jimbo la Ubungo.

  Tunachokiogopa sisi tunakukosoa ni kupoteza such a resourceful person kama wewe bungeni kwa ujinga wa wananchi kutokuwa na elimu ya uraia.

  Unachotaliwa kufanya wewe na Chadema ni kuwa na ujasiri kama aliouonyesha Rais Mkapa kutumia Ilani ya uchaguzi ya 2000 kuomba kura na baada ya miezi sita tu akatanaza hadharani kuwa ilani haitekelezeki na akamua kama Raisi kuanza kulipa madeni ya taifa, jambo lilirejesha imani ya wahisani kuifutia Tanzania madeni na ikaweze kukopesheka tena na hivyo kudhibiti mfumuko wa bei, kukuza uchumi n.k

  Kama ulivyo msema wa kiingereza "You cannot eat your cake and have it" haiwezekanai ukaomba kura kwa ahadi za kutatua kero za jimbo fulani halafu na baada ya ukapata ubunge ukajifanya wewe ni wa kitaifa zaidi kabala ya kutangaza hadharani mgongano wa kimaslahi katika ya maslahi ya jimbo na taifa uliopo vichwani mwa wapiga kura wako. Cha kushangaza mgongano huu ni mkubwa sana hata miongoni mwa wasomi hata waliobobea ambao tuliwatarajia wawe wa kwanza kuelimisha umma kuhusu ibara 63 ya Katiba; lakini naye utamkuta anamlalamikia mbunge kwa kukosa maji, barabara n.k
   
 13. John Mnyika

  John Mnyika Verified User

  #13
  Feb 26, 2012
  Joined: Jun 16, 2006
  Messages: 715
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 0

  Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO ameeleza kuwa watafanya ziara na mbunge Ubungo kati ya Machi Mosi mpaka Machi 3 mwaka huu katika maeneo ya Kwembe, Saranga, Msigani, Makuburi , Sinza na Makurumla kushughulikia matatizo ya maji.
  Wamesema matatizo ya maji yanayokabili baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam yanatokana na kuharibika kwa pampu moja kati ya tatu za kusukumia maji iliyopo Ruvu na kuongeza kuwa mafundi wapo katika matengenezo na wakati wowote hali inaweza kutengemaa.
  (Chanzo: Gazeti la Habari Leo 24/02/2012)
   
 14. S

  Serayamajimbo Senior Member

  #14
  Feb 29, 2012
  Joined: Apr 15, 2009
  Messages: 191
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Vipi kuhusu hii ziara kamanda?

  serayamajimbo
   
Loading...