Dawa ya Mbu yasababisha nyumba kuteketea kwa moto na watoto wawili kufariki

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,495
9,275

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WATOTO wawili wa familia moja wanaoishi shehia la Limbani wilaya ya Wete, wamefariki baada ya kuungua moto, wakati wakiwa wamelala.

Waliokumbwa na ajali hiyo ni Ah-lamud Hamad Salum (3), na Azahar Hamad Salum mwenye umri wa miaka tisa.

Mashuhuda wa tukio walisema, watoto hao ilipofika majira ya saa 2:30 kama kawaida waliingia chumbani mwao kwa ajili ya kulala na mama yao alikwenda kuwafungia chandarua kwa ajili ya kuwakinga na mbu.

Walisema pamoja na kuwafunika chandarua, alikuwa na kawaida na kuchoma dawa ya mbu, ili kuhakikisha usalama zaidi kwa watoto hao.

Walieleza ilipofika saa 3:00 usiku huo walianza kuona moshi kwenye mianya ya dirishi ikienea hadi kwenye nyumba za jirani na kuanza kupata wasiwasi.

Walisema dakika tano, baadae waliamua kugonga mlango wa mbele kwa nguvu na wenyewe wakashituka.

Walisema walipofika walishuhudia moshi na moto unaowaka kwa kasi na tayari mtoto mmoja alikuwa ameungua hali iliyotajwa kwamba alifariki kabla ya kufikishwa hospitali ya Wete.

Sheha wa shehia Limbani, Massoud Ali, alithibitisha tukio hilo akisema limesababishwa na moto.

Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Shehan Mohamed Shehan, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuzitaka jamii kuwa na uangalizi wa hali ya juu kwa watoto.

Alisema japokuwa chanzo kwa hatua za awali ni moto ulioanzia kwenye uchomaji wa dawa za mbu, lakini chandarua walichokuwa wametumia watoto hao ndio kilichoondoa uhai wao.

Hili ni tukio la tano la ajali ya moto ndani ya mwezi wa Agosti mwaka huu kisiwani Pemba.
 
Back
Top Bottom