Dar: Wafungwa jela miaka 30 kwa kosa la kuiba simu ya laki 2

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,010
9,875
Wakazi wawili wa mkoani Dar es Salaam wamehukumiwa na mahakama ya Wilaya ya Temeke kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kuiba simu ya Sh200,000 pamoja na Sh10,000 kwa kutumia silaha.

Waliohukumiwa ni Hemed Salum na Musa Musuni ikielezwa kuwa wametenda kosa hilo Novemba 25, 2019 eneo la Mikoroshini Wilaya ya Temeke.

Walimpora Easter Asheli simu ya mkononi ya Sh200,000 na kiasi hicho cha fedha na kabla ya kufanya kitendo hicho walimjeruhi kwa kisu.

Akisoma hukumu hiyo leo Alhamisi Machi 25, 2021 hakimu mkazi, Anna Mpessa amesema mahakama hiyo imepitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na utetezi na kujiridhisha kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo.

Mpessa amesema kwa mujibu wa ushahidi wa mlalamikaji, mshtakiwa Salum alimvamia na kumjeruhi kwa kisu mkononi na kumuibia simu hiyo aina ya Sumsung pamoja na fedha na mkoba.

Amesema shahidi alieleza kuwa Salum anamfahamu kabla ya tukio hilo na eneo analofundishia lipo karibu na nyumbani kwao, kwamba wakati anampora simu hiyo alikuwa na mwenzake.

Mpessa amesema ushahidi uliotolewa unaonyesha baada ya kuiba simu waliuza na fedha iliyopatikana waliitumia kukimbilia wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Amesema katika maelezo yao waliyotoa washtakiwa hao walidai baada ya kuiba simu waliiuza Sh80,000 na kugawana Sh40,000 na kisha kukimbilia Bagamoyo.

Mpessa amesema washtakiwa hao walielezea jinsi walivyoiuza simu hiyo kutokana na hilo mahakama iliwatia hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

"Kosa la unyang'anyi limekuwa sugu sana katika jamii yetu hivyo inapelekea watu kupata ulemavu wa maisha na kurudisha nyuma maendeleo ili iwe fundisho kwa wengine hivyo mahakama hii inawahukumu kifungo cha miaka 30 jela," amesema Mpessa.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom