#COVID19 DAR: Kasi ndogo ya wanaochanja yamshtua Mganga Mkuu

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
422
1,049
Kasi ndogo ya chanjo ya kujikinga na Ugonjwa wa UVIKO-19 imemshtua Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Rashid Mfaume, na kuwahimiza wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupata chanjo.

Dk. Mfaume alitoa msisitizo huo jana Aprili 5, 2022 baada ya kubaini kuwa kasi ya watu kupata huduma hiyo bado ni ndogo licha ya serikali kupitia ngazi mbalimbali kuwataka wananchi kujitokeza kuchanja.

Alisema tangu chanjo ilipozinduliwa mwishoni mwa Julai, mwaka jana, hadi kufikia wiki iliyopita, ni watu 571,712 tu ndio ambao wamejitokeza kupata chanjo hiyo katika mkoa.

Katika kikao chake na wenyeviti wa serikali za mitaa kwa lengo la kutaka wahamasishe wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo, alisema ni muhimu kwa ajili ya usalama wa afya zao.

Mganga Mkuu huyo alisema wenyeviti wa serikali za mitaa wana mchango mkubwa katika kuhamasisha chanjo na kwamba kila mmoja katika eneo lake afanye hamasa ili wananchi wajitokeze kwa wingi.

"Sasa hivi ninavyozungumza mheshimiwa mgeni rasmi ni tumeachanja watu 5,71,712. Kama una simu unaweza kufanya hesabu hii gawanya kwa 3,800,000 bado tuko chini sana. Hatujafikia hata asilimia 20 ya lengo,” alisema Dk. Mfaume.

Dk. Mfaume alisema mkoa umejizatiti katika kupambana kwa kuenea na maambukizi ya UVIKO-19 kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na serikali kwa ujumla.

Alisema njia nyingine ya kupambana na ugonjwa huo ni kushirikisha viongozi wa serikali za mitaa kwa kuwapa majukumu ya kuhamasisha jamii kwenye maeneo yao ilijitokeze kuchanja.

Mkuu wa Wilaya ya llala, N'gwilabuzu Ludigija, ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika kikao hicho, alisema serikali imeleta chanjo za kutosha ili kila mwananchi achanjwe.

"Mtu akiugua, shughuli za uzalishaji zinasimama na hata uchumi unayumba ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan amejitahidi kuhakikisha analeta chanjo za kutosha, hivyo watu wajitokeze kuchanja,” alisema Ludigija.



Source: Nipashe
 
Back
Top Bottom