Daktari: Wapeleka watoto wanaokoroma hospitali kupata matibabu kwani kukoroma ni ugonjwa kama magonjwa mengine

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,521
9,325
DAKTARI bingwa wa magonjwa ya pua, koo na mdomo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, Perfect Godfrey, ameishauri jamii kuwapeleka watoto wanaokoroma hospitali kupata matibabu kwani kukoroma ni ugonjwa kama magonjwa mengine.

Dk. Godfrey alisema zipo jamii zinazoamini kuwa kukoroma ni kitendo cha asili au kurithi kitu ambacho sio kweli.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu jana Dar es Saalaam, Dk. Godfrey alisema ni bora mtoto akapelekwa hospitali ili kupata vipimo na kugundulika ana tatizo gani.

“Kuna jamii zinadai kuwa kukoroma ni kitendo cha asili na kwa mtoto anayekoroma wengine huamini kuwa ni tatizo la kurithi, wengine wanakwambia babu au bibi au baba yake anakoroma kwahiyo wanasema mtoto amechukua hilo kutoka kwa babu au baba, kwahiyo wanakuwa hawawaleti hospitali.

“Niwaambie tu kuwa kuja hospitali ni muhimu zaidi ili tuweze kujua tatizo ni nini kwa sababu sio wote wanaokoroma ni tatizo la nyama ya pua, yapo matatizo mengine,” alishauri Dk. Godfrey.

Alisema kuwa nyama za pua huwa watoto wanazaliwa nazo na kumsaidia kukabiliana na magonjwa ya koo na pua, lakini kuna umri ukifika zinatakiwa kusinyaa.

“Wakati watoto wakiwa wachanga pale anapotoka kwa mama na kuja duniani huwa anatakiwa atafute kinga yake, nyama hizo zinakuwepo kwa ajili ya kumsaidia katika kinga yake kutokana na magonjwa ya pua na koo.

“Na kwa kadiri anavyokua kama mwaka mmoja hivi, nyama hizo zinaanza kunyauka, kwahiyo anapoendelea kukua tunategemea kazi yake inapungua kidogo kidogo, baada muda zinasinyaa na zinakuwa hazimletei matatizo na kama hazisinyai ndo tunasema mtoto atolewe,” alisema Dk. Godfrey.

Alieleza kuwa kama nyama hizo hazisinyai mtoto anaanza kupata matatizo ikiwemo kukoroma.

“Matatizo makubwa ni kukoroma na wakati mwingine anashindwa kupumulia pua anapumulia mdomo na ndio utakuta anaacha mdomo wazi zaidi, sana pale anapokuwa amelala.

“Katika hali ya kawaida mtoto hatakiwi kukoroma na ndio maana anapokoroma tunatafuta sababu, na sio kukoroma tu hata mzio wanaweza kupata, lakini kiujumla pamoja na kupata hiyo shida sio wote wanahitaji kufanyiwa operesheni,” alisema Dk. Godfrey.

Alisema wapo wanaotibiwa kwa dawa na kupona huku ambao hawaponi kwa dawa wanafanyiwa upasuaji.

“Wito kwa jamii ni kwamba mtoto akiwa na tatizo aletwe hospitali aweze kuchunguzwa ili aweze kutibiwa kama ni kwa dawa au matibabu mengine.

“Kwa sababu zile nyama huwa zina madhara yake, endapo kama mtoto atakuwa anabanwa sana anaweza kupata matatizo mengine ya upumuaji,” alisema Dk. Godfrey.
 
kukoroma ni ugonjwa. siyo ugonjwa mpya. ulikuwepo miaka yote. pelekeni watoto Hospitali watoto wanaokoroma wakapate tiba. Hata Hospitali ya BENJAMIN MKAPA-DODOMA wanatoa huduma ya hiyo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom