Daktari - si sahihi kuendesha gari za wagonjwa (ambulance) kwa mwendo kasi

Tang Zhou

JF-Expert Member
Mar 14, 2018
1,206
2,587
Nimemwelewa huyu daktari, unakuta mgonjwa amapata ajali kichwa kimepondeka lkn huo mwendo anaopitishwa nao barabarani ni hatari - na 'ambulance' zenyewe za Bongo ndo vile unakuta haina hata kitanda!

SEHEMU ya pili ya ripoti hii maalumu, tuliishia pale ambapo Mratibu wa Huduma za Kwanza wa Chama cha Msalaba Mwekundu (TRCS), Kheri Issa, akielezea namna ambavyo wamekuwa wakitoa huduma ya uokoaji kwa majeruhi nchini.

Alisema namna wanavyoshirikiana kwa ukaribu na Jeshi la Polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama wa watoa huduma wetu na majeruhi wenyewe katika maeneo husika.

“Hivi sasa tuna mkataba wa miaka minne na Belgian Red Cross, wao wana uzoefu mkubwa, wamewekeza katika sekta ya utafiti na mafunzo na wamesaidia nchi nyingi, hivyo tunajifunza mengi kutokana na ushirikiano tulionao,” alisema. Endelea….

“Katika utekelezaji wa mkataba huu tayari tumeshamaliza mwaka mmoja wa mkataba wetu, tulianza kununua vifaa, kutoa mafunzo katika mikoa minne sasa tunapanua wigo tunataka twende mikoa zaidi ya 13 kuwapa mafunzo wanachama wetu na wale wanaotoa huduma kwa kujitolea.

“Tunawapa mafunzo katika vitu muhimu ili kutoa huduma sahihi kwa zana za kisasa na hata ikibidi kufaragua (improvise) yaani kwa mfano anaweza kwenda mahala akakosa machela ataangalia nyenzo zingine kwa mfano kanga safi na milunda ili kumsaidia mgonjwa bila kuleta madhara.

“Tuna changamoto kadhaa ikiwamo rasilimali watu, rasilimali fedha na vifaa vya kutosha vya kutolea huduma za dharura, uwiano wa watoa huduma na bajeti ni kikwazo cha kufikia maeneo mengi,” anasema.

Anaongeza: “Tuna uhaba wa vifaa, kwa mfano kwa makao makuu tuna ‘ambulance’ mbili pekee ambazo huwa tunazitumia pale yanapotokea majanga makubwa ambako huwa kuna kundi kubwa la watu kuhitaji huduma.

“Pia tunazo gari za kubebea wagonjwa mkoa wa Kigoma katika kambi ya wakimbizi ambapo tunashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kusaidia Wakimbizi (UNHCR).

“Kwa hiyo tunalazimika kutumia fedha chache tunazopata kutoka kwa wahisani na michango ya wanachama huwa tunazitumia kuwezesha kufika katika maeneo ya kutoa huduma, lakini wakati mwingine mahitaji yanakuwa makubwa kuliko uwezo wetu.

“Uzuri tuna wadau wengi ambao huwa tunashirikiana nao, ukienda kwenye eneo la dharura utakuta kuna askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Polisi, madaktari kutoa hospitali za umma na binafsi hivyo kwa pamoja tunashirikiana kutoa huduma,” anabainisha.

Kheri anasema ni muhimu kila mmoja akaelewa umuhimu wa kupata mafunzo ya huduma ya kwanza na kwamba mamlaka zinazohusika na sekta ya elimu ni vema zikaangalia upya mitaala yake na kujumuisha somo hili, hasa walimu wa afya shuleni ni muhimu pia kupatiwa mafunzo jinsi ya kutoa huduma ya kwanza na wapatiwe vifaa vya kutosha, ili wawasaidie wanafunzi pale inapotokea dharura tofauti na sasa wanachofanya kwa mfano mtoto akiugua wanamchukua tu na kumpeleka hospitalini.

“Lakini pia mamlaka zinazosimamia sekta ya usafiri wa mijini na masafa marefu ni vema kusimamia kuhakikisha madereva na makondakta wao hadi maofisa usalama barabarani nao wapate mafunzo haya,” anasema.

Anasema hatua hiyo itasaidia kukabili changamoto ya rasilimali watu inayokabili taasisi hiyo na itarahishia huduma kutolewa kwa wakati katika eneo lolote nchini.

“Kwa mfano sasa hivi ikitokea ajali huko Kitonga mkoani Iringa inaweza kuwa si rahisi kwetu kufika kwa wakati katika eneo la tukio, lakini kama watu wamepewa mafunzo (madereva, makondakta, askari wa usalama barabarani na wananchi kwa ujumla) wanaweza kuwa wa kwanza kufika eneo la tukio na wakaokoa majeruhi,” anabainisha.

Anasema pamoja na hayo, ni muhimu pia serikali ikatunga sheria itakayomlinda msamaria mwema (Good Samaritan Law) kwani sasa hakuna kinga yoyote anayoipata mtoa huduma hii kwa kujitolea,” anasema.

Inavyopaswa kuwa

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Upendo George, anaeleza kwa kina huduma anazotakiwa kupatiwa majeruhi kabla ya kufikishwa hospitalini.

Anasema inapotokea mtu amepata ajali, huduma ya kwanza anayopaswa kupewa ni ile ambayo itamsaidia kuendelea kupokea hewa ya oksijeni ili aendelee kupumua.

“Mara nyingi kama mtu ameumia kichwani na kupelekea ufahamu wake kupungua kidogo, ulimi wake huwa unashuka kwa nyuma (mdomoni) na kuziba njia ya hewa.

“Kwa hiyo, kitu cha kwanza ni namna ya kumsaidia kuweka vizuri kichwa chake, ili huduma zingine ziweze kuendelea, hapo ataangaliwa iwapo hewa ya kutosha inaingia mwilini mwake au bado kuna tatizo jingine lolote ambalo linazuia hewa kuingia.

“Kama hilo halikuzingatia inaweza kuwa sababu itakayopelekea majeruhi husika kufariki dunia haraka punde tu baada ya kutokea kwa ajali,” anabainisha.

Jambo la kuzingatia

Anasema: “Wakati akipatiwa huduma katika eneo la ajali, kuna mfumo mwingine ambao ni muhimu mtoa huduma kuuzingatia, ni pale katika eneo la mishipa ya fahamu ya kwenye shingo.

“Hii yenyewe huwa inasaidia mwili kupumua, lakini kile kitendo tunaona watu (wasamaria wema) wanafika eneo la ajali na kumnyanyua mtu kama alivyo bila kuzingatia mambo haya ya msingi na kumuweka kwenye gari hivyo hivyo.

“Mara nyingi wanakuwa wanawaumiza zaidi majeruhi hasa katika mfumo wa fahamu unaopita kwenye mgongo.”

Anasema kuwa inapotokea hivyo, majeruhi anaweza akapooza mwili kabisa au asipumue kabisa tangu aliponyanyuliwa na hivyo kupoteza maisha.

Dakika muhimu

Daktari huyo anasisitiza wagonjwa wa ajali huhitaji kupatiwa huduma ya dharura mapema ili kuweza kuokoa maisha yao.

“Siwezi kutaja hasa ni kwa muda gani kwa sababu hapo itabidi tuangalie ni muda gani ajali hiyo imetokea na ni katika eneo gani na amepatiwa huduma saa ngapi.

“Lakini inasisitizwa kwamba ikiwa inawezekana inatakiwa ajali inapotokea isipite hata zaidi ya dakika 15 lazima awepo mtu wa kumsaidia na kujua huduma ipi inatakiwa kuanza kutolewa ili kumsaidia,” anabainisha.

Hali halisi

Anasema hata hivyo changamoto ni kwamba wagonjwa wengi wa ajali hufikishwa hospitalini muda ukiwa umekwenda mno tangu ajali ilipotokea na hivyo kuwaweka katika hatari zaidi ya kupoteza maisha.

“Ikiwa majeruhi alivuja damu nyingi ndipo pale utaona wengi wanapoteza maisha pale pale katika eneo la ajali au kama atafikishwa wapo ambao hufariki katika mlango wa hospitali ama wodini wakiendelea kupatiwa msaada,” anasema.

Je! ‘ambulance’ zinapaswa kuendeshwa kasi?

Dk. Upendo anasema: “Gari la kubeba wagonjwa halipaswi kuendeshwa kwa mwendo kasi, lakini inatokea hivyo nadhani

huenda ni kutokana na kuchelewa kuwapo kwa huduma hiyo ya magari ya wagonjwa wa dharura nchini.

“Kawaida kabla dereva hajakabidhiwa kuanza kuiendesha kuna vitu anatakiwa afundishwe kabla, jinsi gani ya kuendesha na muda gani anatakiwa awashe kile king’ora.”

Anasema dereva anafundishwa pia muda gani awashe zile taa maalum zilizopo katika mfumo wa gari hilo, muda gani aendeshe taratibu na muda gani anapaswa kusimama kwanza mgonjwa apatiwe huduma ndipo naye aendelee kuendesha.

“Lakini inakuwa shida kwetu (Tanzania) kwa sababu madereva wa magari ya kawaida baadhi yao huwa hawaheshimu magari ya wagonjwa wa dharura.

“Kwa upande wetu pia kuna changamoto, baadhi ya madereva hawajui jinsi gani wanapaswa kuendesha magari haya kulingana na utaratibu unaotakiwa,” anasema.

Chuo cha Usafirishaji Tanzania

Kuhusu kuwapo kwa kozi ya madereza wa kuendesha magari ya wagonjwa, Msemaji wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), David Ngusekela, anasema kwa sasa hakuna mafunzo kwa ajili ya kuwapima madereva wanaotaka kuendesha gari hizo.

“Madereva wote wanaokuja hapa huwa wametokea kwenye vyuo mbalimbali, huwa tunawapima uwezo wao ili waweze kupatiwa rasmi leseni.

“Kwa sasa hatuna mafunzo maalum ya kuwapima wale wanaotaka kuendesha ambulance pekee, lakini tupo kwenye mchakato wa kuingiza mafunzo hayo kwenye mfumo wetu,” anasema.

Dk. Upendo anasema: “Kimsingi kuna vitu havitakiwi kufanyika, nadhani labda hawajui au ni mazoea kwamba tangu zamani tunajua magari ya dharura ni maalum kwa ajili ya kuhamisha mgonjwa kutoka hospitali moja kwenda nyingine.

Magari hayana vifaa

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA umebaini kwamba magari mengi ya kubebea wagonjwa nchini hayana vifaa vya kutosha na mengine hayana kabisa vifaa zaidi ya kitanda cha mgonjwa.

Dk. Upendo anasema hiyo ni changamoto nyingine iliyopo nchini katika utoaji wa huduma ya dharura na kusisitiza hata magari yaliyopo ni machache na mengi hayakidhi vigezo.

“Unakuta nyingi hazina vifaa tiba, kuna mengine yapo tu kama magari ya kawaida, kwa hiyo unakuta mtaalamu anajiuliza hata nikikaa hapa na huyu mgonjwa akiendelea kuzidiwa sitakuwa na jinsi ya kumsaidia.

Daktari huyo anasema bado pia kuna safari ndefu ya kuwafundisha wataalamu wa afya jinsi gani ya kumsaidia mgonjwa aliye mahututi.

Njia mbadala

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, anasema pamoja na hayo bado wataalamu na jamii kwa ujumla inapaswa kujifunza pia njia mbadala za kuwasaidia majeruhi wa ajali.

Mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa waandishi waliochaguliwa kushiriki mafunzo ya uandishi wa habari za usalama barabarani yanayotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kupitia mradi wa Bloomberg (BIGRS).
 
Back
Top Bottom