Daktari aeleza athari za sigara, pombe kwa watoto, wajawazito

Status
Not open for further replies.

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
625
938
photo_2020-10-07_19-54-41.jpg


Daktari bingwa wa watoto kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Fransis Furia, amesema watoto wanaokaa na watu wanaotumia bidhaa za tumbaku kama sigara wako hatarini kupata saratani.

Dk. Furia pia alisema kuna madhara makubwa kwa mtoto aliyeko tumboni endapo mama mjamzito atatumia tumbaku au kukaa karibu na watu wanaotumia bidhaa hizo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu Dar es Salaam jana, alisema madhara yanayotokea ni mtoto kuzaliwa akiwa njiti na pia kuna uwezekano mkubwa wa mimba kuharibika.

“Naweza kusema kuwa hata mimi navuta sigara kwa sababu sio lazima uvute moja kwa moja, ila ukikaa na mtu anayevuta na wewe pia unavuta, katika uvutaji sigara sio mtu mmoja tu anaathirika, lakini pia wale watu ambao wako karibu na mvutaji.

“Mtu anaweza akavuta sigara sehemu mfano kochi au gari, anaweza kuacha madhara pale, kwahiyo akija mtu mwingine anaweza kuvuta. “Kwahiyo wako watu wengi wanavuta sigara bila kujua, ukipata harufu ya sigara ina maana moshi huo umeingia ndani yako.

“Hayo matatizo pia yanaweza kumwathiri mama mjamzito, akivuta sigara au kukaa na watu wanaovuta sigara, inaleta madhara kwa mtoto kwani huathiri ukuaji na kufanya watoto kuzaliwa wakiwa njiti,” alibainisha Dk. Furia.

Alisema madhara mengine ni mama kupata shinikizo la damu hali ambayo inaweza kusababisha mimba kuharibika. “Tumeshasikia kinamama wakipoteza maisha na nilishawahi kupata kesi ya mama mmoja mimba ilitoka mara saba, lakini yeye hatumii sigara kwa sababu tu anakaa na mtu anayetumia.

“Tafiti zinaonyesha kuwa mtoto akizaliwa njiti wakati wa ukubwani anaweza kupata magonjwa yasiyo ya kuambukizwa baadae kama matatizo ya figo, kisukari, shinikizo la damu, pia anaweza kupata shida ya kifua kama pumu.

“Mtoto anayekaa nyumbani na baba yake anavuta sigara, ina maana mfano mpaka anamaliza kidato cha nne amevuta sigara kwa miaka 14,” alieleza Dk. Furia. Alisema madhara ya bidhaa za tumbaku kwa watu wazima ni saratani za aina nyingi, matatizo ya shinikizo la damu, matatizo ya mfumo wa fahamu na magonjwa ya moyo.

Dk. Furia alisema uelewa ni mdogo kwa jamii kuhusu madhara ya sigara kutokana na watu wengi kutokujua sheria kwamba inakataza kuvuta sigara eneo lenye watu. “Elimu hii inatakiwa itolewe kwenye jamii ambako wanavuta sigara, watu wajue kuwa sigara ina madhara na wanaovuta waelewe kuwa wanawaathiri watu wengi, kuna vijana wengi wanapata saratani kama ya koo, hata matiti kutokana na sigara,” alisema Dk. Furia.

Akizungumza kuhusu madhara ya vilevi, alisema unywaji pombe kwa wajawazito huweza kumwathiri mtoto aliyekuwa tumboni.

“Mtoto anaweza akazaliwa na tatizo la mdomo sungu, shida katika ubongo, nikimaanisha ukuaji na kiwango cha kufikiri kinaweza kuathirika. “Kinamama wasitumie vilevi wakati wa ujauzito kwa sababu wanapokunywa wanawaywesha na watoto wao kwani mtoto anatumia chakula anachokula mama yake akiwa tumboni,” alisema Dk. Furia.

Mtanzania
 
Sigara yangu ya mwisho nilivuta zaidi ya siku 670 zilizopita. Namshukuru Mungu kwa kunipa moyo wa kuacha kuvuta sigara. ila kilichonipa msukumo wa kuacha ni mtoto wangu sikutaka akuwe huku akiniona navuta sigara na kumuathiri na yeye, naamini nita-mark siku nyingi zaidi ya hizo na Mungu atanisaidia kwa hili.
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom