CUF yataka Katiba mpya

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kinaungana na Watanzania wapenda demokrasia na mabadiliko kudai Katiba mpya ya Tanzania itakayokuwa na misingi ya kidemokrasia ya kweli na itakayoweka dira ya maendeleo ya Taifa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, chama hicho kimempongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuonesha msimamo thabiti katika kusimamia maridhiano ya kisiasa na kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuweka uwiano mzuri wakati wa kugawa Wizara kwa vyama vinavyoshiriki katika serikali hiyo.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lililokutana Desemba 10 hadi 11, mwaka huu kwa ajili ya kufanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu.

“CUF inaungana na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama au nafasi walizonazo katika jamii kwa kutumia njia za kidemokrasia kudai mabadiliko ya Katiba ya nchi yetu ili ikidhi matakwa ya hali ya wakati tulionao,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema pamoja na madai ya Katiba mpya, Baraza Kuu liliagiza wadau mbalimbali na Watanzania kuendeleza madai ya mabadiliko ya sheria za uchaguzi na haja ya kuwepo kwa Tume huru ya uchaguzi ya haki ambayo itaheshimika na kila Mtanzania kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Profesa Lipumba alisema kutokana na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Lewis Makame, imedhihirika wazi kuwa Tume iliyopo haina sifa za kuaminika mbele ya macho ya Watanzania hasa kwa kasoro, udanganyifu na mfumo wa uchakachuaji wa idadi ya wapiga kura kuwa waliojitokeza ni 8,626,283 kati ya waliojiandikisha 20,137,303.

“Waliopiga kura kwa mwaka 2010 ni sawa na asilimia 42.8 ya wale waliojiandikisha, hii ni tofauti kubwa sana ikilinganishwa na waliojitokeza kupiga kura 1995 kwa asilimia 76.7, mwaka 2000 asilimia 84.4 na mwaka 2005 waliokuwa asilimia 72.4, Watanzania wengi wamepoteza imani na Tume kama inaweza kusimamia uchaguzi ulio huru na haki,” alisema Profesa Lipumba.

Aidha, Profesa Lipumba alisema chama hicho kinapongeza hatua iliyofikiwa ya uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar, ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho kutokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa mwaka jana.

“CUF inampongeza Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na pia kwa wanachama wengine wanane walioteuliwa kuwa mawaziri na wawili, naibu mawaziri,” alisema.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom