CUF waisakama serikali kuhusu Richmond, EPA, rada, ufisadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CUF waisakama serikali kuhusu Richmond, EPA, rada, ufisadi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Aug 28, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 28, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,461
  Likes Received: 81,711
  Trophy Points: 280
  Date::8/28/2008
  CUF waisakama serikali kuhusu Richmond, EPA, rada, ufisadi .....
  Kizitto Noya na Saa Mohamed
  Mwananchi

  MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekosa maadili ya uongozi kutokana na kutowachukulia hatua za kisheria mafisadi.

  Profesa Lipumba alisema hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye Kongamano Maalum la Kujadili Ukosefu wa Uongozi na Hatima ya Tanzania lililoandaliwa na chama hicho na kufanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

  Alisema serikali ya Kikwete imejaa mafisadi na ndio maana imeshindwa kuwashughulikia watuhumiwa wa ufisadi wa EPA, Richmond, rada na ndege ya rais.

  "Ndugu zangu hatuna viongozi makni. CCM imechoka na haina uwezo wa kufikiri mawazo mapya na ndio maana wako katika makundi. Unapokuwa na kundi dogo linanufaika na rasilimali za umma huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa umaskini, ni ishara kwamba uongozi umekushinda," alisema Profesa Lipumba.

  Profesa Lipumba alisema CCM imechoka mpaka imeshindwa kuendeleza sifa za kuongoza ambazo ni uadilifu, umoja, kujenga misingi ya demokrasia, kuwajibika kwa jamii, upendo kwa wanaowaongoza na kuheshimu misingi ya maamuzi ya pamoja.

  Alisema kwa kukosa sifa hizo, CCM imeifikisha nchi pabaya na imepoteza sifa za kuendelea kuwaongoza Watanzania na kuonya kuwa endapo mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete hatakuwa makini, itasambaratika mikononi mwake.

  Kwa mujibu wa Profesa Lipumba rais anatakiwa kuvunja makundi ndani ya CCM na kuanza kuwashughulikia mafisadi kwa mujibu wa sheria za nchi, badala ya kuendelea kuwakumbatia ili haki itendeke na nchi isigawanyike katika makundi ya walalahoi na matajiri.

  "Huwezi ukasema wewe ni kiongozi kama unashindwa kuvunja makundi na kutenda haki pia huwezi kusema unapambana na rushwa na mwenyewe ukiwa ama mla rushwa au unakumbatia walarushwa," alisema Profesa Lupimba na kuongeza:

  "Kiongozi mwadilifu anajali umoja na sio kutengeneza makundi, huwezi ukawa kiongozi bora kama unawajali wanamtandao na kuwakandamiza wananchi walio wengi. Kiongozi awajibike na kuwapenda wananchi kwa kuguswa na matatizo yao".

  Alisema CCM imeligawa taifa kwa kupindisha sheria za nchi kutokana na uamuzi wake wa kuwalinda mafisadi kwa kuwabembeleza warudishe fedha badala ya kuwafikisha mahakamani.

  Profesa Lipumba alisema matatizo ya uongozi katika Serikali ya CCM yalianza kujitokeza tangu serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani mwaka 2005 ambapo iliunda serikali yenye mawaziri wengi kuliko nchi yoyote duniani kwa lengo la kuwafurahisha wanamtandao.

  Profesa Lipumba alisema CCM iliudanganya umma katika Ilani yake ya uchaguzi kwamba kingeshughulikia masuala ya umaskini kwa kuongeza ajira, elimu na afya ya msingi, kwani leo ikiwa ni zaidi ya miaka miwili tangu ilipoingia madarakani utekelezaji wake umekuwa hafifu na mahali pengine hakuna kinachoendelea.

  "Katika sekta za afya na uchumi hakuna mabadiliko ya maana na rais badala ya kuwaomba radhi wananchi alipokuwa akilihutubia Bunge, alisema hali ni nzuri na amefanikiwa kuongeza ajira," alisema.

  Aliongeza kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha kwani bei za vyakula zinazidi kupaa badala ya kupungua ili kuwaletea maisha bora kama ilivyoahidi katika uchaguzi mkuu.

  "Bei ya sembe imepanda kutoka 250 hadi 750 kwa kilo, mchele Sh500 hadi Sh1300, maharage kutoka Sh400 mpaka 1200, sukari Sh600 hadi 1200 na dagaa kutoka Sh2500 hadi 8000," alibainisha Profesa Lipumba.

  Akizungumzia tuhuma hizo jana, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba alisema CCM bado ni thabiti kwa kuwa bado ndicho chama chenye sifa ya kuongoza nchi.

  Alisema wapinzani wanapoteza muda kuinenea mabaya CCM kwani hawatafanikiwa kuing'oa madarakani katika uchaguzi wowote utakaofanyika nchini kwa sababu sera zake bado zinakubalika.

  "CCM ina sifa za kuiongoza nchi na ndio maana ilishinda uchaguzi wa 2005 Bara na Visiwani, wapinzani wanapoteza muda kuizungumzia mabaya," alisema Makamba.
   
Loading...