CUF sasa yameguka; Hamad yuko hatarini kung’olewa kwenye uongozi wa juu wa chama hicho

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797

maalum.jpg

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 10 December 2011

SEIF Shariff Hamad, katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), yuko hatarini kung'olewa kwenye uongozi wa juu wa chama hicho, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema mkakati wa kumng'oa kiongozi huyo maarufu kwa jina la "Maalim Seif," unasukwa kwa ustadi mkubwa na unaweza kutekelezwa wakati wowote kuanzia sasa.

Viongozi 19 waandamizi ndani ya CUF, wakiongozwa na mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohammed, wametajwa kuwa vinara wa mkakati unaoweza kumwangamiza Maalim Seif kisiasa.

Mtoa taarifa anasema Hamad Rashid ndiye anataka nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho maarufu zaidi visiwani Unguja na Pemba.

Uamuzi wa Hamad na wenzake kutaka kumg'oa Maalim Seif kwenye uongozi, unatokana na kile wanachoita, "Kutoridhishwa na hatua yake ya kukabidhi chama kwa Ismail Jussa Ladhu," naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar.

Jussa anadaiwa kukitumia chama cha CUF "kwa maslahi binafsi."

Alipoulizwa Hamad Rashid juu ya taarifa ya kutaka kumng'oa Maalim Seif kwenye nafasi yake alisema, "Ni kweli, nimemwandikia barua mwenyekiti wangu, Profesa Ibrahim Lipumba. Nimemueleza mengi kuhusu chama chetu."

Hamad amesema hadi juzi Jumatatu, Profesa Lipumba alikuwa hajajibu barua yake hiyo.

Alipoulizwa iwapo ni kweli kwamba anakusudia kunyakua ukatibu mkuu, Hamad alisema, "Ndiyo. Mimi ni mwana-CUF na nina sifa za kushika wadhifa huo."

Alisema, "Nataka kugombea nafasi hii ili kuondokana na utamaduni wa kuufanya ukatibu mkuu kama utume kwenye chama chetu. Ifike wakati ukatibu mkuu uwe utumishi, badala ya kuwa utume ndani ya chama."

Kauli ya Hamad inaendana na madai ya baadhi ya vijana na viongozi wengine, kwa zaidi ya miezi sita sasa, kuwa Maalim Seif amekaa sana kwenye nafasi hiyo "kama kiongozi wa kiroho."

Kwa upande wake, Jussa aliliambia gazeti hili, "Hatufanyi kazi kupitia magazetini."

Jussa alikuwa ameulizwa kuhusu mwenendo wake ambao inadaiwa umefanya baadhi ya waasisi na viongozi wengine wa chama kuamua kupambana na Maalim Seif.

Akionesha kuongea kwa tahadhari, Jussa ambaye pia ni mwakilishi wa Mji Mkongwe, Unguja alisema, "Tunawashangaa sana watu wanaotumia magazeti. Kama kuna tofauti tutakwenda kuzimalizia kwenye vikao."

Kwa mujibu wa mawasiliano miongoni mwa viongozi, ambayo gazeti hili limenasa, kuenguliwa kwa Maalim Seif "kunalenga kunusuru CUF na kukiwezesha chama hicho kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Visiwani."

Mawasiliano muhimu juu ya mkakati huo ni miongoni mwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba, naibu katibu mkuu wa CUF – Tanzania Bara, Julius Mtatiro, Hamad Rashid, Jussa Ladhu na Jubeir Shamte, mwanachama wa chama hicho anayeishi Dubai.

"Jussa ndiye anavuruga CUF. Hili tumelifahamu muda mrefu, lakini tumeshindwa
kulieleza kutokana na kulindwa na Maalim Seif. Hivyo, ili kukinusuru chama chetu, tumeamua kumuondoa Maalim ili kumdhibiti Jussa," ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa CUF kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Anatoa mfano wa matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani, ambapo inadaiwa kuwa chama hicho "kimeshindwa" hadi sasa, kukusanya baadhi ya fomu za matokeo ya uchaguzi kwenye majimbo matano ya Unguja.

Amesema, "Huyu bwana ndiye alikuwa msaidizi maalum wa katibu mkuu. Katika uchaguzi ule, CUF ilishindwa kukusanya matokeo ya uchaguzi katika majimbo matano ya Unguja, huku Jussa akiharakisha kushawishi Maalim akubali kushika nafasi ya pili katika serikali. Haya mambo hayakufanyika kwa bahati mbaya."

Haijafahamika iwapo matokeo hayo yalitumika kusaidia CCM "kushinda."

Kuibuka kwa taarifa za kumwengua Maalim Seif kumekuja mwaka mmoja baada ya gazeti hili kuripoti kuwapo kwa mawasiliano ya shaka kati ya Jussa Ladhu na January Makamba (Mbunge wa Bumbuli – CCM).

Katika mawasiliano maalum, Makamba anadaiwa kumwandikia i-meili Jussa na kusema, "Utakumbuka yale makubaliano yetu; imekuwaje mwafaka wa kutoenda personal (kushambulia mtu binafsi)?

Naye Jussa akijibu Makamba alisema, "January, maelewano yetu yako palepale. Kosa lilikuwa langu kumsubiri (Lipumba) hadi tuonane uso kwa uso ili nimpe briefing (taarifa). Bahati leo amekuja Zanzibar na tumeelewana…"

Hatua ya Makamba kulalamikia Jussa ilitokana na taarifa zilizochapishwa na gazeti la Tanzania Daima zikimkalili Profesa Lipumba akimtuhumu Rais Jakaya Kikwete, mkewe Salma na mwanae Ridhiwani kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Katika barua pepe iliyotumwa na Hamad Rashid kwa Profesa Lipumba na kunakiriwa kwa Shamte, tarehe 12 Novemba 2011, mbunge huyo wa Wawi anaeleza dhamira yake ya kumng'oa Maalim Seif kwenye wadhifa wa ukatibu mkuu kwenye uchaguzi mkuu wa chama mwaka kesho.

Hamad ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa upinzani bungeni anasema, "…Kwa kuzingatia nililokuandikia, naomba kukuarifu rasmi kuwa Mwenyezi Mungu akinijalia uhai na uzima; natia nia ya kugombea ukatibu mkuu wa chama wakati wa uchaguzi ndani ya chama utakapowadia."

Awali akiandika kwa Profesa Lipumba, Hamad anamtaka arejee kikao chao chini ya uenyekiti wake (Lipumba) kilichofanyika Zanzibar, Masons Hotel, baina ya (Hamad Rashid), Makamo Mwenyekiti (Khamis Machano Alli) na katibu mkuu na makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar (Maalim Seif).

Kikao kilizungumzia, pamoja na mambo mengine, sababu "zilizonifanya kuandika kijitabu nilichokiita ‘Yaliyojiri' baada ya kubaini njama zilizopangwa za kutaka kuniua kisiasa."

Hamad Rashid anasema katika mazungumzo hayo, wote wanne walikubaliana kwenda kwa wanachama wa CUF kuwaambia kuwa wamemaliza tofauti zao; (na kwamba) wamekubaliana pia kuitishwa kwa mkutano wa pamoja utakaowashirikisha wabunge, wawakilishi na viongozi wa juu wa chama hicho.

Hata hivyo, Hamad Rashid anasema hakuna hata moja lililotekelezwa miongoni mwa waliyokubaliana. Anasema alikuwa anamwandikia kumtaarifu juu ya vitendo vinavyofanywa na katibu mkuu na wasaidizi wake, vya kumtangaza yeye na wanachama wenzake 18 kuwa ni waasi ndani ya chama.

Hamad Rashid anasema kuwa ameambiwa kwamba kugombea ukatibu mkuu "…kwa chama chetu ni utume…na eti Mhe. Salum Khalfan Barwany (Mbunge wa Lindi Mjini,) anataka kugombea uenyekiti ambao nao pia ni utume ndani ya chama chetu."

Katika kudhihirisha kupamba moto kwa mgogoro hatari ndani ya CUF, Hamad Rashid anasema baada ya Maalim Seif kukutana na wenyeviti na makatibu wa wilaya mjini Wete, kisiwani Pemba siku ya Baraza la Eid El Hajj, maagizo yalitolewa kuandaa vikao vya Kamati ya Utendaji na mikutano mikuu ya Wilaya ili kuwajulisha viongozi hao juu ya uasi uliomo ndani ya chama.

Anasema baadhi ya viongozi hasa wabunge na wajumbe wa baraza kuu la uongozi la taifa waliotoa hoja ya udhaifu wa utendaji, matumizi mabaya ya fedha na kudhoofika kwa chama hasa Tanzania Bara, kwenye kikao halali cha baraza kuu, walituhumiwa kuwa ni vibaraka wake.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa mgogoro huo umezidi kupamba moto baada ya CUF kufanya vibaya kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga.

Waraka wa Hamad Rashid unadai, "Pamoja na chama kutumia zaidi ya Sh. 300 milioni kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga, baadhi ya wajumbe wa baraza kuu waliochangia ajenda ya hali ya kisiasa, ‘wote waliitwa vibaraka wangu,' na kwamba eti mimi ‘napewa pesa na Mhe. Pinda kuiua CUF."

Wanaotajwa kuwa vibaraka wa Hamad Rashid, ni pamoja na mbunge wa Gando, kisiwani Pemba, Khalifa Suleiman Khalifa, mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa, mbunge wa Mtambile, Masoud Abdulla Salim, mbunge wa Chambani, Salim Hemed na mbunge wa Lindi Mjini, Barwany.

Wengine wanaotajwa kuwa vibaraka wa Hamad na hivyo kupachikwa tuhuma za uasi ndani ya chama, ni wajumbe wa baraza kuu, Hassan Doyo, Masoud Kirungi, Rakesh na Masoud Abdallah Masoud, mbunge wa zamani wa Micheweni kisiwani Pemba.

Gazeti hili lilipomuuliza Hamad Rashid kwa njia ya simu, kwa nini mpango wake wa kutaka kugombea ukatibu mkuu uhusishwe na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alijibu haraka, "Akutukanaye hakuchagulii tusi. Sijatumwa na Pinda kuvuruga chama na wala situmiki bali naeleza ukweli wa yaliyomo ndani ya CUF."

Profesa Lipumba akimuandikia Maalim Seif kuhusu madai ya Hamad, Jumatatu ya 14 Novemba 2011, saa 12 asubuhi anasema, "…Nimepata barua pepe toka kwa Jubeir Shamte. Sidhani kama nimekutana naye. Hamad Rashid alimpelekea nakala ya barua aliyoniletea. Sijamjibu Hamad wala sijui la kumjibu. Lakini suala linakuzwa.

Mwenyekiti."
Waraka wa Lipumba uliotumwa kwa Maalim Seif ulinukuliwa kwa Jussa na Mtatiro.
Hatua ya Profesa Lipumba kumuandikia Maalim Seif ilifuatia Shamte kumtaka kiongozi huyo wa CUF kuchukua hatua "kukinusuru chama."

Akiandika kwa uchungu, siku hiyohiyo ya 14 Novemba 2011, Shamte anasema, "… Natumai hali yako nzuri na nimearifiwa kuwa uko USA kwa muda wa miezi sita… Nimesikitishwa sana na hali inayoendelea kwenye chama chetu. Japokuwa mie niko mbali (Dubai), lakini naona huzuni kubwa kuona mambo haya ambayo yanaweza kutuweka pabaya kama hayajatuweka bado."

Anasema, "Sisi tuliochangia kwa hali na mali kuanzisha chama hiki… hatutafurahi kuona mbuyu unaanguka. Tutakuwa na fakhari kuona mti unazaa matunda na watu wanafaidika…"

Awali Hamad akiandika kwa Profesa Lipumba kwa njia ya kulalama anasema, "…Tarehe 10 Novemba 2011, kamati tendaji ya wilaya Chake Chake ilikutana bila mimi kujulishwa jinsi ya kutekeleza maagizo ya katibu mkuu, ambapo pamoja na mambo mengine, yanataka kufukuzwa kutoka ndani ya chama viongozi 19 kwa madai ya uasi ndani ya chama."

Hamad Rashid anaeleza katika andishi lake kwa Profesa Lipumba, "Pamoja na mvutano mkali uliotokea katika kikao hicho, hasa kutoka kwa wajumbe wa jimbo langu la Wawi ambao wanaelewa kiini na ukweli wa mipango ya Jussa na wenzake; wakipewa nguvu na katibu mkuu, lakini viongozi wa wilaya wameamua kuitisha mkutano mkuu wa wilaya 14 Novemba 2011 ili kutimiza agizo" hilo.

Katika barua yake kwa Profesa Lipumba anasema "…nataka kukuthibitishia kuwa mpango huu ulioandaliwa kijasusi, kuzidi kukiua chama chetu unavyoendelea; Jussa ambaye kinyume cha katiba ya CUF amepewa wadhifa wa katibu wa kamati ya ulinzi na usalama, leo 12 Novemba 2011 kwa kutumia viongozi wa Blue Guard (kikosi cha ulinzi cha chama), ameitisha kikao cha Blue Guard na kuwapa kazi ya kuzunguka nchi nzima, kuchafua majina yetu na kupandikiza maneno ya uwongo."

Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwekwa kizuizini Zanzibar kwa miaka mitatu kwa madai ya kutaka kuipindua serikali ya Dk. Salmin Amour, analalamika kuwa "…fedha za walipa kodi na michango ya wabunge na wawakilishi inatumika kuua chama badala ya kukiendeleza."

Akiandika kwa uchungu Hamad Rashid anasema, "Chama kinatumia fedha zote hizi ili kufanikisha mradi binafsi na kwa maslahi binafsi."

Anasema chama chake kimeshindwa kupeleka ruzuku wilayani, hasa Tanzania Bara kwa zaidi ya miezi sita sasa; wajumbe wakihoji wanaitwa wasaliti wa chama.
"Mhe. Mwenyekiti, nakuandika taarifa hii fupi kwa madhumuni ya kukupa fursa,

angalau ya kupata muhtasari wa yanayojiri huku katika chama unachokiongoza; wala si kwa madumuni ya kuomba shufaa, kwani haya nilikwishayaeleza katika kijitabu changu cha ‘Yaliojiri,' ambacho uliniomba nisiendelee kukisambaza, lakini huenda nikavisambaza zaidi ili Watanzania waujue upande wa pili wa shilingi," anaeleza Hamad Rashid.

Kuhusu Maalim Seif kung'atuliwa, Hamad anasema, "…hakuna asiyejua na kutambua mchango wa Maalim Seif katika mustakbali wa kisiasa Zanzibar na Tanzania kwa jumla. Ametoa mchango mkubwa wa kuhakiksha nchi inabaki katika amani, ameshirikiana na viongozi wenzake katika kuanzisha chama na akakisimamia hasa Zanzibar ambako leo tuko katika serikali ya umoja wa kitaifa."

Anasema mchango wa Maalim Seif hauwezi kupita hivihivi. Anaeleza, "Nidhahiri Maalim anafaa kuheshimiwa na kuenziwa, ili mradi mwenyewe aamue kupewa heshima hiyo, kama ambavyo aliamua rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Andishi la Hamad Rashid juu ya Maalim Seif linafanana na kauli iliyotolewa na Doyo kwenye mazungumzo yake kwa njia ya simu na mmoja wa washirika wake.

Katika mazungumzo hayo, Hassan Doyo anasema wakati wa Maalim Seif kung'atuka kwenye chama umefika. Anataja sababu kadhaa ikiwamo kutingwa na shughuli za umakamu wa rais. Vilevile anaunga mkono mpango wa Hamad Rashid kugombea nafasi ya katibu mkuu.

Anasema, "Tunataka mabadiliko makubwa ya uongozi. Tunataka katibu mkuu apumzike. Umakamu umemzidi mpaka chama hakitaki. Hana ziara popote, yeye ni umakamu na ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za chama."

Anasema, "Kwa hiyo, tunafanya harakati za mabadiliko ya uongozi kwa kuanzia na yeye. Tunataka abaki kwenye umakamu ili tupate katibu mkuu atakayekuwa katibu mtendaji."

Kuhusu Lipumba, Doyo anasema, bado anaweza kuendelea kubaki kukiongoza chama hicho kutokana na umri wake kuwa mdogo na kwa elimu yake pana; akiongeza kuwa huyo hajawahi kufanya mabaya kwa chama chake.

Anasema, "Lakini katibu mkuu tunataka aondoke, siyo kwa sababu amekifanyia chama mabaya, hapana. Bali, muda wake wa kufanya shughuli za kisiasa ni mdogo; " jambo ambalo anasema linakifanya chama hicho kuonekana kama hakina katibu mkuu.

Doyo anasema, "Leo nani utamueleza CUF akakuelewa? Mara tunaitwa CCM B… Badala ya watu kufanya kazi za kisiasa wilayani, wanaishia kuitisha "press" (mikutano ya waandishi wa habari) Dar es Salaam. Hizi ndizo harakati ambazo tunazungumza na wala siyo mbaya."

"…hayo mabadiliko yanayotajwa ni ya kweli. Na sisi tunayaongoza bila woga kwa sababu ni sehemu ya demokrasia. Naamini katika ninachokifanya na Hamad Rashid ametangaza kugombea nafasi ya katibu mkuu; nami namuunga mkono," anaeleza Doyo.

Mwanasiasa huyo machachari anasema, muda si mrefu watasambaza alioita
"washikadau" nchi mzima ili kufanya mikutano ya kuelemisha wanachama na wananchi kwa jumla juu ya umuhimu wa kufanyika mabadiliko.

Anasema, "Tutakwenda nchi mzima kusambaza jambo hilo. Kwanza, katibu mkuu wetu
hatutaki atukanwe. Pili, hatutaki akashifiwe na hatutaki adhalilishwe. Ila tunataka kuwaambia wanachama wa CUF kuwa tunataka mabadiliko. Miaka ya katibu mkuu ni mingi; amekitumikia chama kwa zaidi ya miaka 20, lakini chama kinarudi nyuma. Tunataka mawazo mengine ya kuweza kusogeza chama chetu mbele."

Doyo anasema, hiyo ndiyo ajenda ambayo wanakwenda nayo kwa wananchi. Gazeti hili halikufanikiwa kumpata kueleza mipango ya kumwengua Maalim Seif imefikia hatua gani.

Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, hakupatika kujibu iwapo anajua kinachotendeka ndani ya chama chake na hatua ambazo anachukua kukiokoa kisigawanyike kati ya Pemba na Unguja. Imeelezwa yuko nchini Marekani kikazi kwa miezi sita.

Gazeti lilituma ujumbe kupitia i-meili uliotaka kufahamu kwa nini hakutuma majibu ya barua ya Hamad kwake mwenyewe. Hadi tunakwenda mtamboni juzi Jumatatu, Profesa Lipumba alikuwa hajajibu ujumbe huo.

Naye, makamu wake wa CUF, Machano Khamis Ali hakupatikana. Imeelezwa yuko nje ya nchi kikazi. Haikuweza kufahamika yuko nchi gani na amekwenda kwa kazi gani.

Lakini Julius Mtatiro, alipoulizwa alisema, "Binafsi sielewi. Nimeona tu kwenye vyombo vya habari, Mhe. Hamad Rashid wakim-quote (wakimnukuu) juu ya mvutano ndani ya CUF. Tatizo ni nini; sielewe kinachoendelea…"

Alisema, "…ninavyofahamu mimi ni kwamba kuna vikao vya kamati tendaji, baraza kuu na mkutano mkuu wa chama. Masuala yote yanajadiliwa kwenye vikao na niseme ukweli tu kwamba; si vema masuala yetu yakaendeshwa kwa njia ya magazeti.

Inaleta picha mbaya mbele ya jamii."

Alipoelezwa gazeti halikuletewa habari na Hamad bali limepata mawasiliano kati ya Lipumba, Jussa na yeye; Mtatiro alisema, "Sawa. Lakini si vizuri mambo ya siasa yakaendeshwa na magazeti."

Wengine wanaodaiwa kuwa ni watu wa Hamad Rashid, ni Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi kwenye serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Masoud, Waziri wa Sheria na Katiba, Abubakari Khamis Bakari na aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho, Nassoro Seif Amour.

Msemaji wa chama hicho, Salim Bimani amesema, "Sisi tunapokea taarifa kwenye vikao na kufanya kazi kwa maagizo ya vikao. Tuna ngazi za kuzungumza mambo yetu." Alisema vikao hivyo vinatarajiwa kufanyika hivi karibuni.


 
Uroho wa madaraka utamuua Rashid Hamadi utadhani alizaliwa awe kiongozi.
 
Kwa wenye uelewa wa Katiba ya CUF na siasa za CUF, ninaomba kuelimishwa [kuuliza si ujinga]

1. Utaratibu wa kumpata Katibu Mkuu wa CUF ukoje?

2. Utaratibu wa kumpata mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia CUF ukoje?
 
Ukali na hasira waliyokuwa nayo kwa Tundu Lissu kumbe ilitokana na migogoro ndani ya chama chao. Wamenikumbusha mbali sana. Kuna mwl mmoja alikuwa na tabia kama hiyo. Ukiona anatandika wanafunzi asubuhi asubuhi ujue tu amegombana na mume wake nyumbani.
 
Mbona hawa wataikomboa CUF. Maana tangu jamaa awekwe nyumba ndogo na CCM ametupa jongoo na mti wake. Walichelewa kuliona hili. Amewasaliti hasa wale waliopoteza ndugu zao kwenye harakati zake za kuutafuta umakamu wa rais wa nyumba ndogo.
 
Ndio uhai wa chama, kuliko kukaa kimya kudumisha fikra za mwenyekiti, katibu na wagombea
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom