CUF- Chama Cha Wananchi kinapokea kwa mstuko Mkubwa Taarifa za kuenea kwa kasi kwa Maambukizi ya CORONA katika maeneo mbalimbali ya Dunia

CUF Habari

Verified Member
Dec 12, 2019
239
250
TAARIFA KWA UMMA

CUF- Chama Cha Wananchi
kinapokea kwa mstuko Mkubwa Taarifa za kuenea kwa kasi kwa Maambizi ya CORONA katika maeneo mbalimbali ya Dunia ikiwa ni pamoja na nchi jirani na Tanzania.

Japokuwa takwimu halisi za Maambukizi kwa Tanzania haziko bayana, wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Dini wamedhihirisha hofu kubwa juu ya kurudi upya kwa maradhi haya.

CUF- Chama Cha Wananchi kinaunga mkono msimamo aliousisitiza Rais Magufuli wakati anazindua Shamba la miti huko CHATO, wa kutoifungia nchi ( Lockdown) katika kupambana na Maambukizi ya COVID-19.

Hata hivyo pamoja na kuunga mkono matumizi ya njia sahihi za asili za kupambana na CORONA, CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa wito kwa Serikali kufuata njia za Kisayansi katika Masuala ya CORONA ikiwa ni pamoja na kutafakari upya juu ya Msimamo uliotolewa kuhusu chanjo.

Pamoja na maelezo yaliyotolewa na Rais dhidi ya Chanjo, ni vema tukakumbuka kwamba Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa Tanzania, aliruhusu na kusimamia chanjo za maradhi mbalimbali yaliyosumbua kama vile ndui na polio. Kuhusu hofu kwamba Chanjo zinaweza kuwa na madhara yaliyokusudiwa kwa Waafrika, ni vema tukakumbushana kwamba kwa sasa Shirika la Afya Duniani linaongozwa na mwafrika, Waziri wa Afya wa zamani wa ETHIOPIA na lina Mahusiano mema na nchi za Afrika.

Tunashauri Wataalam wetu wajipange kutathmini Ubora wa chanjo tunazoweza kutumia Tanzania dhidi ya CORONA, badala ya kuzikataa kienyeji. Aidha Serikali iweke Utaratibu mwepesi na usio ghali wa kupima CORONA.

Aidha CUF- Chama Cha Wananchi kimesikitishwa na Maamuzi ya Meya wa Moshi ya kuwavua watu barakoa, tena wakiwa kwenye mkusanyiko. Bado uvaaji barakoa katika maeneo hatarishi unastahili kuhamasishwa na pia ni muhimu sana kushirikiana na Shirika la Afya Duniani ( WHO) katika mapambano haya.

Aidha CUF - Chama Cha Wananchi kinampongeza Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ( TEC), Askofu Gervas Nyaisonga kwa ujasiri wake alipoamua kupaza sauti kwa maaskofu wenzake kwa kuwahimiza wawaongoze waumini wao katika Mapambano dhidi ya CORONA kwa kuzingatia maelekezo ya Kisayansi ya kupambana na maradhi haya, pamoja na sala. Ni wakati muafaka sasa kwa Viongozi wa Madhehebu yote ya Dini nchini kuunganisha nguvu katika hili.

Kuhusu Mapambano ya kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, CUF- Chama cha Wananchi kinawapongeza wanachama wake na wadau wote walioamua kuibeba mada hii muhimu.

Kwa hakika Mahafidhina wameanza kuhaha kujaribu kuyazima Mapambano haya. Kwa mfano maamuzi ya Mwandishi wa gazeti la Mwananchi Na. 7480 la Januari 28, 2021 alipoamua kwa makusudi kupotosha maana ya kile alichokiongea Mwenyekiti wa Chama Prof. Ibrahim Lipumba Januari 27 wakati wa Kuwakumbuka Mashujaa waliouawa kinyama 2001 kunaweza kutafsirika kwamba ni Mpango Maalum wa kutaka kuwahamisha Watanzania kutoka kwenye Agenda ya msingi ya Kudai Katiba Mpya na Tume Huru. Tunaamini hata Mwandishi mwenyewe hauamini huo uzushi wake aloamua kuusambaza kwa Umma na kila mtanzania anajua kwamba Prof. Lipumba hawezi kumwangukia mtu ambaye kwa sasa ameshadhihirisha Usaliti wake kwa Wazanzibar na kwa Siasa za Upinzani kwa ujumla.

Tunatoa wito kwa wanachama wa CUF-Chama Cha Wananchi na wale wote wanaopambana kuidai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi wasikubali kuingia kwenye Mtego huo wa hovyo unaoratibiwa na wale wasiopenda Katiba Mpya na Tume Huru vipatikane.

Tukumbuke kwamba tayari wapinzani wenzetu wa NCCR- Mageuzi, CHADEMA na Vyama vingine pamoja na Viongozi Jasiri wa Dini kama Askofu Mwamakula wameonesha nia ya dhati ya Kuunganisha nguvu zetu katika Madai haya muhimu kwa Taifa. Kwa vyovyote vile, Mapambano yetu hayawafurahishi watawala wasiopenda Haki ikiwa ni pamoja na CCM na wenzao walioshirikiana kuunda Serikali isiyotokana na Uchaguzi Halali.

Tusikubali kutolewa kwenye Jambo letu na waandishi wanaoshindwa KUHESHIMU Maadili na Miiko ya Taaluma yao, tuwapuuze. Tusipoteze muda wetu muhimu kujibizana na waliopo nyuma ya Mwandishi yeyote wa aina hii bali tuutumie muda wetu kuendeleza Mapambano yetu haya muhimu. CUF- Chama Cha Wananchi kitaendelea kushirikiana na waandishi wote wanaofanya kazi kwa weledi na kuheshimu Maadili ya Taaluma yao, ambao hawako tayari kutumika.

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Januari 29, 2021
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom