CTV: Mdahalo wa wagombea Ubunge Igunga

Donyongijape

JF-Expert Member
May 28, 2010
1,497
811
Mgombea wa CHADEMA katika Uchaguzi mdogo wa Igunga Mwalimu Kashindye usiku wa Sept 25 alimuumbua Dk. Dalaly Kafumu katika Mdahalo uliofanyika Ukumbi wa Sakao Igunga baada ya Kafumu kuudanganya mdahalo kuhusu ujenzi wa daraja la Mbutu. Alichoambulia baada ya hapo ni kelele za kuzomewa na kejeli, boooooo!. Mdahalo uliandaliwa na VoX Media. Mada ilikuwa Ni The Tanzania we Want.

Jionee habari ambayo huwezi kupata popote katika TBCCM au CCM-ITV...Ni kupitia CTV pekee.

Dk.Kafumu aumbuliwa na Mgombea wa CHADEMA kwenye Mdahalo - YouTube

Embedded video:

 
Last edited by a moderator:
Mratibu wa Kampeni wa chama cha Mapinduzi, Mwigulu Nchemba alijikuta katika wakati mgumu na kulazimika kunyang'anya kipaza sauti na kuzomewa.

Hatua hiyo ilisababishwa na kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro kukituhumu CCM kuwa ndicho chama kinachoanzisha vurugu katika uchaguzi mdogo wa Igunga licha ya viongozi wake kuhubiri amani.

Mtatiro alitoa kauli hiyo wakati viongozi wa vyama vya siasa walipokaribishwa jukwaani baada ya kumalizika kwa mdahalo wa wagombea.

Alikishambulia CCM na kujibu hoja za Mratibu wa Kampeni wa chama hicho,“Mwigulu ameongea amani ya kudumu huku akiwa ameandaa makambi ya vijana katika Wilaya ya Nzega, Uyui na Iramba mkoani Singida, vijana hao wanajiandaa kufanya nini?” alihoji Mtatiro.

Kauli ya Mtatiro ilimfanya Nchemba kusimama na kuchukua kipaza sauti kwa lengo la kutaka kujibu hoja hizo lakini kundi la watu waliohudhuria mkutano lilipinga kitendo hicho.

Huku Nchemba akiwa ameshika kipaza sauti mkononi, hali ilibadilika ukumbini hapo, kundi hilo lilipiga kelele na kuanza kusogea eneo lilikokuwa jukwaa kuu kupinga kitendo hicho.

“Hapana, hapana hii haikubaliki hatutaki azungumze huyo,” zilisika kauli kutoka kwa washiriki wa mdahalo huo.

Hali hiyo iliwafanya wanachama na wafuasi wa CCM waliomsindikiza mgombea huyo ukumbini kutoka wakiwa hawana furaha ya kutosha kama ilivyokuwa wa wafuasi wa vyama vya CUF na Chadema.

:::Mwananchi:::
 
Mgombea wa ccm wakati akijibu swali kuhusu ujenzi wa daraja la mbutu alisema kuwa mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo ameshapatikana
na ujenzi utaanza hivi karibuni hapo ndipo mgombea wa chadema aliposimama na kuueleza ukumbi huo uliojaa kuwa hakuna kitu kama hicho kwani tenda ndio kwanza zimetangazwa mwezi wa tisa mwanzoni na mkandarasi atapatikana mwezi wa kumi je mgombea wa ccm atueleze huyo mkandarasi wake amempata wapi ??

DR.Kafumu akasimama akadai samahani ULIMI UMETELEZA watu ukumbi mzima wakaanza kumzomea na hata alivyoendelea kuongea hakuna aliyekuwa anamsikiliza na baada ya hapo akanyanyuka mgombea wa CUF akamshindilia ngumi nyingine kwa
kumuita DR. MZIMA UNAKUWA MUONGO na watu ukumbi mzima wakaendelea kumzomea kafumu . kafumu mdahalo huu unaweza kuwa umemmaliza.
 
Mimi nafikiri Dr. Kafumu hakukosea ila ametoa siri ya serikali maana kwa CCM tenda huwa ni kiini macho tu mkandarasi tayari wanamjua mmesahau walivyomfanya mzee Mengi kwenye tenda ya Hotel ya Kilimanjaro.
 
Mratibu wa Kampeni wa chama cha Mapinduzi, Mwigulu Nchemba alijikuta katika wakati mgumu na kulazimika kunyang'anya kipaza sauti na kuzomewa.

Hatua hiyo ilisababishwa na kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro kukituhumu CCM kuwa ndicho chama kinachoanzisha vurugu katika uchaguzi mdogo wa Igunga licha ya viongozi wake kuhubiri amani.

Mtatiro alitoa kauli hiyo wakati viongozi wa vyama vya siasa walipokaribishwa jukwaani baada ya kumalizika kwa mdahalo wa wagombea.

Alikishambulia CCM na kujibu hoja za Mratibu wa Kampeni wa chama hicho,“Mwigulu ameongea amani ya kudumu huku akiwa ameandaa makambi ya vijana katika Wilaya ya Nzega, Uyui na Iramba mkoani Singida, vijana hao wanajiandaa kufanya nini?” alihoji Mtatiro.

Kauli ya Mtatiro ilimfanya Nchemba kusimama na kuchukua kipaza sauti kwa lengo la kutaka kujibu hoja hizo lakini kundi la watu waliohudhuria mkutano lilipinga kitendo hicho.

Huku Nchemba akiwa ameshika kipaza sauti mkononi, hali ilibadilika ukumbini hapo, kundi hilo lilipiga kelele na kuanza kusogea eneo lilikokuwa jukwaa kuu kupinga kitendo hicho.

“Hapana, hapana hii haikubaliki hatutaki azungumze huyo,” zilisika kauli kutoka kwa washiriki wa mdahalo huo.

Hali hiyo iliwafanya wanachama na wafuasi wa CCM waliomsindikiza mgombea huyo ukumbini kutoka wakiwa hawana furaha ya kutosha kama ilivyokuwa wa wafuasi wa vyama vya CUF na Chadema.

:::Mwananchi:::
Hapo kwenye red pamenifurahisha.Pigo moja tu watu wazima wamesononeka moyoni na kushindwa kuzuia hisia zao za uchungu walizozipata kutokana na aibu alioifanya kafumu mbele ya wapiga kura wa igunga.
 
MGOMBEA WA CCM AMEDANGANYA TENA KWENYE ISSUE YA VYAMA HUKO USA.

inaelekea mgombea wa ccm dr.kafumu is a serial liar kwa sababu siyo kweli marekani kila mgombea ana sera zake
huo ni uongo wa wazi kwani vyama vikuu vya marekani vya democratic party na republican vina sera tofauti kabisa
republican ikiwa ni chama kinachotetea mabepari na democratic kikitetea wanyonge. wagombea wote wa democratic
wanatetea sera za chama hicho ingawaje sometimes mgombea anaweza akatofauti kwenye issue hii na ile lakini asilimia
90% atakuwa na sera za chama chake kwahiyo hata na hili Dr. kafumu amewadanganya tena wana igunga labda CDM
kuanzia kesho waanze kumpachika jina la mgombea muongo hatufai igunga. kama anadanganya kwa hili ili achaguliwe
basi ameshawandanya watu kwa mangapi anayoongea kila kukicha na kama amekubali kandanganya ktk hili tutaamini vipi km
atakoyasema kesho yana ukweli wowote.
 
Alipotakiwa kueleza atafanya nini kujenga daraja la Mbutu, linalozungumzwa kama moja ya vigezo vya kuinyima CCM kura, Dk. Kafumu alisema lipo katika Ilani ya Uchaguzi na tayari limetengewa fedha katika Bajeti ya mwaka huu na mkandarasi wa kulijenga ameshatangazwa.

Hata hivyo, Kashindye aliema Dk. Kafumu amedanganya, kwa kuwa zabuni ya ujenzi wa daraja hilo ndiyo imetangazwa na anashangaa kusikia mkandarasi amepatikana.

Lakini Dk. Kafumu aliomba radhi kuwa ulimi uliteleza.

Source: Gazeti la HabariLeo
Siamini kama gazeti la CCM limeshindwa kumtetea hata kufichaficha kwa kuremba alivyoumbuka au wao pia wameshajua jimbo limeshakwenda?
 
du! jamaa kaumbuka kwelikweli, huu mdahalo wadau umefanyika lini na je haukulushwa live? maana ulikuwa ni uhondo kwelikweli
 
CUF 'kidedea' mdahalo Igunga
CHAMA cha Wananchi (CUF) juzi usiku kiliibuka 'kidedea' katika mdahalo wa wagombea wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda ubunge wa Igunga, huku CCM na Chadema wakijikuta katika wakati mgumu wa kujibu tuhuma zinazowakabili wagombea wao.

Hata hivyo, katika mdahalo huo uliotawaliwa na vurugu za mashabiki wa vyama hivyo tangu mwanzo hadi mwisho, mgombea wa CCM, Dk. Dalaly Kafumu, aliwashangaza wana CCM kwa utulivu na uwezo wake wa kutumia Ilani ya CCM, usomi na ufahamu wake wa jimbo hilo kujibu tuhuma zilizomwandama kuhusu mikataba mibovu ya madini.

Mgombea wa Chadema, Peter Kashindye, aliyetarajiwa kung'ara kutokana na mtindo wa siasa za chama hicho wa kutumia tuhuma kupata mashabiki, alijikuta katika wakati mgumu wa kunyong'onyesha mashabiki wake, baada ya siasa hizo kumgeuka.

Mgombea wa CUF, Leopold Mahona, ambaye hakuwa na tuhuma, ndiye aliyegeuzia kibao cha ufisadi kwa mgombea wa Chadema pale alipomtaka Kashindye aeleze alivyoshiriki kula fedha za mradi wa majengo ya kituo cha elimu katika tarafa ya Simbo akiwa Mratibu wa Elimu, huku akishangaa ilikuwaje akapandishwa cheo kuwa Mkaguzi wa Shule.

Mahona alisema wagombea wa Chadema na CCM wanajuana, kwa kuwa wametoka nyumba moja; serikalini huku akihoji iweje mgombea wa Chadema, Kashindye 'avute' mshahara wa Serikali ya CCM mwisho wa mwezi na baada ya hapo tarehe moja mwezi uliofuata ajiite mpinzani.

Siasa za ufisadi, vurugu Chadema
Kashindye aliingia ukumbini na kitabu cha madini kumtuhumu Dk. Kafumu kwa kutangaza kwa lengo la kuuza maeneo ya madini ya Igunga nje ya nchi na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka uliopita, ikieleza Sh milioni 800 zilivyopotea katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.

Hata hivyo, hakutarajia pale Dk. Kafumu kwa utaratibu aliposema “nimetupiwa madongo mengi, ngoja nami ingawa si kilichotuleta hapa, nirushe kidogo madongo kwa Kashindye, kwa kushiriki kutafuna Sh milioni 800 alizozisoma katika taarifa ya CAG.”

Katika majibu kuhusu alivyokula fedha za mradi wa tarafa ya Simbo, Kashindye alisema anamwona Mahona aliyekuwa mwanafunzi wake, anajaribu kumrushia madongo na kuongeza kuwa mgombea huyo wa CUF hajui kitu, kwa kuwa wakati yeye akiwa msimamizi wa mradi huo, Mahona alikuwa mwanafunzi asiyejua kitu.

Kuhusu kushiriki kula Sh milioni 800 za Halmashauri akiwa Mkaguzi wa Elimu na mmoja wa maofisa wa halmashauri hiyo, Kashindye alijikuta akikana kuwa ofisa wa halmashauri hiyo na kujiita kuwa ofisa wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye akasahau na kujiita ofisa wa Wizara ya Elimu.

Alipoulizwa kwa nini hakusema kuwa kuna wizi wa fedha mpaka akasubiri wakati wa kampeni, alijibu kuwa yeye amesomea lugha na anajua anavyopaswa kusema kitu sahihi kwa wakati sahihi na mahali sahihi.

Huku akiwa amesahau kuwa alikana kuwa ofisa wa Halmashauri, alijikuta akikubali akisema asingeweza kusema kuwa kuna wizi wa fedha katika halmashauri, kwa kuwa alihofia kuharibu uhusiano ofisini.

Alipotuhumiwa kuhusika kuporomosha kiwango cha elimu Igunga ili CCM izidi kulaumiwa, Kashindye alisema yeye ni kama mpimaji wa maabara, anapima ugonjwa na kutoa ushauri, watekelezaji ambao ni halmashauri ndio wa kulaumiwa.

Kuhusu Chadema kutumia alama ya V, inayotumiwa na makundi ya kigaidi duniani kikiwamo cha Al-Qaeda, Al-Shabaab na vingine, Kashindye alisema alama hiyo si ya kigaidi bali ya ushindi.

Alifafanua, kuwa alama hiyo imetumika Libya, Tunisia na Misri kukomboa wananchi kutoka serikali kandamizi na kwa Tanzania Serikali ya CCM ni kandamizi na iko mbioni kuondolewa.

Kuhusu vipi atatetea wanawake wasionewe, wakati Chadema ilimshambulia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, Kashindye alisema Mkuu huyo hakushambuliwa, bali alihujumu uchaguzi na alitolewa tu katika jengo alimokuwa akifanyia mkutano wa kuihujumu Chadema.

Kafumu awashangaza CCM
Wakati mpaka saa 10 jioni kulikuwa na taarifa kuwa Dk. Kafumu asingeshiriki mdahalo huo,
baadaye aliingia ukumbini na wagombea wengine wa Chadema na CUF, na kuonesha umahiri wa kutumia ilani ya CCM kwa utulivu kujibu tuhuma dhidi yake na hoja mbalimbali na kuwaamsha wana CCM vitini kwa shangwe.

Kuhusu hoja kuwa alihusika kusaini mikataba ya madini inayoinyima nchi mapato, Dk. Kafumu alisema yeye alikuwa Kamishna wa Madini kwa miaka mitano na kazi yake ilikuwa ni
kushauri na kusimamia sheria na anayesaini mikataba ni Waziri na anayetunga sheria ni Bunge, ambamo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto alishiriki.

Alipotakiwa aeleze alishindwa nini kusaidia wachimbaji wadogo wa Igunga wakati akiwa jikoni kama Kamishna wa Madini na sasa atafanya nini akiwa Mbunge, Dk Kafumu alisema hakushindwa bali kuna mambo alifanya.

Alisema alitoa vibali vya uchimbaji mdogo maeneo ya Igunga na kuwaanzishia soko la kuongeza thamani madini yao Nzega. Alifafanua kuwa katika nafasi ya

ukamishna, alikuwa akishughulikia nchi nzima na ilikuwa vigumu kusaidia Igunga peke yake, lakini akiwa Mbunge, atashughulikia Igunga pekee na kutumia utaalamu wake kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo zaidi.

Alipotakiwa kueleza atafanya nini kujenga daraja la Mbutu, linalozungumzwa kama moja ya vigezo vya kuinyima CCM kura, Dk. Kafumu alisema lipo katika Ilani ya Uchaguzi na tayari
limetengewa fedha katika Bajeti ya mwaka huu na mkandarasi wa kulijenga ameshatangazwa.

Hata hivyo, Kashindye aliema Dk. Kafumu amedanganya, kwa kuwa zabuni ya ujenzi wa daraja hilo ndiyo imetangazwa na anashangaa kusikia mkandarasi amepatikana.

Lakini Dk. Kafumu aliomba radhi kuwa ulimi uliteleza.

Kwa upande wa Mahona, alisema ataanza ujenzi wa daraja hilo bila kutegemea bajeti ya Serikali siku 100 baada ya kuchaguliwa kwa kutumia rasilimali za Igunga, lakini Dk. Kafumu alimwambia hajui utaratibu wa uwekezaji, ndiyo maana anazungumzia nadharia ambayo ni tofauti na utekelezaji.

Vurugu na ushindi wa CUF
Awali kabla ya kuanza kwa mdahalo huo wenye jina la ‘Uchaguzi Mdogo wa Igunga na Tanzania Tunayoitaka’, mashabiki wengi wa CUF walifika mapema ukumbini na kuchukua nafasi zote za mbele kabla ya mashabiki wa CCM na Chadema.

Baada ya kuchukua nafasi hizo, mabango mengi ya mgombea wa CUF na bendera za chama hicho, viligawiwa kabla Chadema na CCM hawajafika na wachache waliokuwapo, walikuwa mikono mitupu bila mabango wala sare za vyama vyao.

Mbinu hiyo ya CUF, ilisababisha mashabiki wengi wa CCM na Chadema wakiwamo wabunge wao, kulazimika kukaa viti vya nyuma, huku wakituma magari yao kwenda kutafuta mabango ya wagombea wao na kuchangia kutokea kwa vurugu za mara kwa mara kati ya CCM na Chadema waliokuwa wamekaa pamoja.

Wagombea walipoingia ukumbini, mashabiki wa CUF walisimama na mabango ya Mahona na kumsifu, jambo lililosababisha mashabiki wa Chadema na CCM kutoka nyuma ya ukumbi nao kuja mbele kushangilia wagombea wao.

Mratibu wa Mdahalo huo, Rosemary Mwakitwange, alilazimika kusitisha matangazo na kuomba viongozi wa kitaifa wa vyama hivyo, Mwigulu Nchemba wa CCM, Zitto wa Chadema na Julius Mtatiro wa CUF kuzungumza kutuliza mashabiki wao.

Mdahalo ulipoanza, ghafla kuliibuka mzozo kati ya mashabiki wa Chadema na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage na kusababisha mdahalo usitishwe tena, ambapo Zitto alilazimika kwenda kumchukua Rage na kumhamishia viti vya mbele na kumtoa nje mmoja wa mabaunsa wa Chadema.

Baada ya kumalizika kwa mdahalo, viongozi hao wa kitaifa walipewa nafasi ya kusema neno la kufunga, akaanza Nchemba, akafuatia Zitto lakini alipoanza kuzungumza Mtatiro, alimtuhumu Nchemba kwa kuweka kambi za vijana kwa ajili ya vurugu na kutishia kuwa CUF, ndio wanaoziweza na kila mtu anajua.

Tuhuma hizo zilimwamsha Nchemba akitaka kujibu mapigo na alipopewa kipaza sauti, mashabiki wa CUF walisimama na kupiga kelele, huku wakivamia eneo rasmi la kuzungumzia na kumzuia, ikabidi mdahalo ufungwe kuepuka vurugu zaidi huku nje ya ukumbi polisi wakiwa na mabomu ya kutoa machozi wakijiweka sawa.

NEC yalaani uhuni
Naye Halima Mlacha anaripoti kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imelaani vitendo vya kihuni na visivyo vya kistaarabu vinavyofanywa na baadhi ya vyama katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Mwenyekiti wa Muda wa Tume hiyo, Profesa Amon Chaligha, alisema vitendo hivyo ambavyo ni pamoja na kumwagiana tindikali,
kurushiana matusi na risasi na kuvuliwa nguo kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, vinakwenda kinyume na Sheria na Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

“Vitendo hivi pia ni kinyume na utamaduni wa Mtanzania wa kuheshimiana na kujenga umoja uliodumu kwa miaka 50 ya uhuru wa Taifa letu,” alisema Profesa Chaligha.

Alisema tangu kampeni za uchaguzi huo zianze mapema mwezi huu, Msimamizi wa Uchaguzi wa Igunga, amepokea malalamiko matatu ambayo ni kumwagiwa tindikali, kudhalilishwa kwa DC na kujeruhiwa kwa mapanga aliyoyawasilisha katika Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ngazi ya jimbo.

“Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka kila chama cha siasa nchini, iliyapitia malalamiko hayo na kuyatolea uamuzi ili kuipa uhuru Mahakama iyashughulikie bila kuingiliwa,” alisema.

Hata hivyo, baada ya Kamati hiyo kumaliza kujadili malalamiko hayo, muda mfupi baadaye, matukio mengine ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi yaliripotiwa; ambayo ni kurushiana risasi za moto, kuwa na silaha katika mikutano ya kampeni, kuharibu mali na kutumia lugha ya
matusi na ukabila badala ya Kiswahili katika kampeni.

Profesa Chaligha alisema baadhi ya matukio hayo yameshawasilishwa katika Kamati ili yajadiliwe na kutolewa uamuzi, lakini pia alisisitiza kuwa timu ya makamishna wa Tume hiyo inajiandaa kwenda Igunga kukutana na vyama vya siasa vinavyofanya kampeni jimboni humo, ili kuvikumbusha umuhimu wa kufuata maadili ya uchaguzi.
HabariLeo | CUF 'kidedea' mdahalo Igunga

MY TAKE
Huu upupu unalenga kuzigawa kura za wale wasioitaka CCM! Hizi mbinu zinajulikana na CCM imekula kwao naona habarileo limekuwa la mipasho sasa
 
ukisikia upupu kama hujui ndio huu...........wewe ndugu huna hoja au njaa inakusumbua? Acha kutumia masaburi wewe tumia kichwa katika kufikiri.
 
MY TAKE
Huu upupu unalenga kuzigawa kura za wale wasioitaka CCM! Hizi mbinu zinajulikana na CCM imekula kwao naona habarileo limekuwa la mipasho sasa

Mkuu Gezaulole - Hawa Habarileo ni jana tu nilianzisha thread juu yao kuhusu kama wao ni mali ya CCM, all of a sudden the diehard supportes of CCM wanashabikia CUF!!!!!!!! Yaani ni siasa za kizamani mno! But this is another proof kwamba CCM imebanwa mbavu Igunga na hawana pa kutokea!!!!!
 
Ccm hawana hoja jazba tu.kizazi kinacho kuja z even worse hakitasikiliza uchwara na ngonjera za gamba inayoimbwa na ccm na kwa master wao nape na chiligati hawa lazima siasa iwa costi
 
Monday, 26 September 2011 21:12

Geofrey Nyang'oro, Igunga

WAGOMBEA ubunge katika Jimbo la Igunga, Leopold Mahona wa CUF na Mwalimu Joseph Kashindye wa Chadema, jana walimkaba koo mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu katika mdahalo uliofanyika jana mjini hapa kuwa amehusika na mikataba mibovu ya madini.Walitoa maneno hayo kwenye mdahalo wa uchaguzi mdogo wa Igunga na Tanzania tunayoitaka ambao uliwahusisha wagombea hao watatu uliofanyika katika ukumbi wa Sakawa.

Mahona alimtuhumu Dk Kafumu kuwa ndiye aliyesaini mikataba mibovu ya madini inayoligharimu taifa hadi sasa akidai kwamba katika kila Sh100 ya Tanzania, nchi inapata Sh3.“Hakuna wilaya ambayo mtu anaweza kutembea na kuokota almasi, isipokuwa Igunga. Lakini sekta hiyo iko chini na chanzo ni huyu bwana, nani asiyejua kuwa ndiye aliyesaini mikataba mibovu ya madini?” alihoji Mahona.

“Mikataba ambayo katika kila Sh100, Serikali ya Tanzania na watu wake inaambulia Sh3!”alisema Mahona huku akishangiliwa na watu waliohudhuria madahalo huo.Akijibu hoja hiyo, Dk Kafumu alisema hakuwahi kuingia mikataba ya madini, bali alikuwa msimamizi wa sheria iliyotungwa bungeni.

“Mimi kazi yangu ni kusimamia sheria na si kusaini mikataba. Kazi ya kusaini mikataba inafanywa na waziri na sheria inatungwa bungeni kina Zitto (Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Chadema) wanafahamu,” alisema Dk Kafumu.

Hata hivyo, baada ya majibu hayo mgombea wa Chadema Kashindye, alisimama na kitabu kinachoelezea utafiti wa madini nchini alichoeleza kuwa hakijulikani kwa wananchi wa kawaida na badala yake, kimeuzwa Ulaya kutafuta wawekezaji.

“Katika kitabu cha mgombea wa CCM kinaeleza kuwa Igunga kuna madini ya aina 11, kitabu hiki amekiuza na kukitangaza Ulaya kuvutia wawekezaji, woga wangu ni kuwa ule mpango wa kufukia wananchi katika Mgodi wa Bulyanhulu, unaweza kufanyika hapa Igunga,” alisema Kashindye.

Maswali kwa mgombea wa Chadema
Moja ya matukio yaliyopamba mjadala huo ni maswali ya papo kwa papo yaliyoelekezwa kwa wagombea na mengi yaliyoonekana kuwa magumu yalielekezwa kwa Kashindye.

Miongoni mwa maswali yaliyompa mgombea huyo wakati mgumu kujibu ni kueleza endapo chama hicho si chama cha fujo kutokana na matukio kadhaa yaliyotokea wakati wa kampeni ikiwamo kupigwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

Akijibu swali hilo Kashindye alisema kwa kuwa kesi iko mahakamani ushahidi wa wazi kuhusu tuhuma hizo utafafanuliwa mahakamani na watu wote watajua ukweli.

Swali jingine lilihusu yeye kuwa mtumishi wa halmashauri na moja ya matatizo katika wilaya hiyo ni ubadhirifu wa mali za umma na elimu duni.

Alisema: “Mimi sikuwa mtumishi wa halmashauri ya wilaya kama ambavyo inapotoshwa hapa. Mimi ni Mkaguzi wa Elimu na bosi wangu ni Wizara ya Elimu na wala si halmashauri ya wilaya,” alisema.

Alitaja kazi ya mkaguzi wa elimu kuwa ni kuangalia matatizo katika shule mbalimbali na kutoa ushauri wa kitaalamu unaopaswa kutekelezwa na watendaji wa halmashauri iliyoko chini ya DC, mkurugenzi na ofisa elimu.

“Nilifanya kazi yangu na kukabidhi ushauri wangu lakini watendaji serikalini hawakuufanyia kazi, mkaguzi ni kama mtu wa maabara anayepima na kueleza ugonjwa lakini wa kuandika dawa ni daktari,” alisema.

Kuhusu alama ya vidole viwili kama alama ya fujo alisema alama hiyo huashiria ukombozi na imekuwa ikitumiwa na wananchi wanaotafuta ukombozi wanapokuwa wamechoshwa na Serikali zao.

“Nchi kama Libya, Tunisia, Misri wale siyo waasi, bali ni wananchi wanaopigania ukombozi wa nchi zao baada ya kuchoshwa na Serikali dhalimu na sisi Chadema, tunasema tutawakomboa wananchi wa Tanzania tukianzia na Igunga kwa njia ya kura,” alisema.

CUF yaahidi mabadiliko ndani ya siku 100

Kwa upande wake, Mahona aliahidi mabadiliko ndani ya siku 100 endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Alisema endapo atachaguliwa, atahakikisha ndani ya siku 600 anajenga Daraja la Mbutu na kuwafikishia neema wakazi wa Jimbo hilo.Alisema ataanzisha Saccos katika kila tarafa, atachimba visima vya maji katika kila kijiji na atahakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha wakazi wa Igunga

CCM yajivunia Ilani ya Uchaguzi ya 2010

Dk Kafumu alisema endapo atachaguliwa atahakikisha anatekeleza ahadi zote zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.Alisema katika ilani hiyo kuna ujenzi wa Daraja la Mbutu ambalo limekuwa likiisumbua Igunga, kukamilisha ujenzi wa zahanati na shule za kata.

Kuhusu maji, alisema atachimba bwawa kubwa litakalolingana na lile la Kata ya Mwanzugi katika kila kata ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wote wa Igunga. Aidha, alisema atahakikisha anatekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.

Mtatiro aisukumia CCM zigo la vurugu
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro amekituhumu CCM kuwa ndicho chama kinachoanzisha vurugu katika uchaguzi mdogo wa Igunga licha ya viongozi wake kuhubiri amani.

Mtatiro alitoa kauli hiyo wakati viongozi wa vyama vya siasa walipokaribishwa jukwaani baada ya kumalizika kwa mdahalo wa wagombea.

Alikishambulia CCM na kujibu hoja za Mratibu wa Kampeni wa chama hicho, Mwigulu Nchemba.“Mwigulu ameongea amani ya kudumu huku akiwa ameandaa makambi ya vijana katika Wilaya ya Nzega, Uyui na Iramba mkoani Singida, vijana hao wanajiandaa kufanya nini?” alihoji Mtatiro.

Aliwataka wakazi wa Igunga kumchagua Mahona akidai kuwa ndiye kijana pekee aliyeonyesha kuwa anaweza kuwatumikia wakazi wake na kwamba ana mtaji wa kura zaidi ya 11,000.

Nchemba azomewa jukwaani
Kauli ya Mtatiro ilimfanya Nchemba kusimama na kuchukua kipaza sauti kwa lengo la kutaka kujibu hoja hizo lakini kundi la watu waliohudhuria mkutano lilipinga kitendo hicho.

Washiriki wa mdahalo huo hasa waliodaiwa kutoka vyama vya CUF na Chadema walisimama na kupinga mratibu huyo kupewa kipaza sauti kwa kile walichoeleza kuwa Mtatiro alikuwa mzungumzaji wa mwisho.

Huku Nchemba akiwa ameshika kipaza sauti mkononi, hali ilibadilika ukumbini hapo, kundi hilo lilipiga kelele na kuanza kusogea eneo lilikokuwa jukwaa kuu kupinga kitendo hicho.

“Hapana, hapana hii haikubaliki hatutaki azungumze huyo,” zilisika kauli kutoka kwa washiriki wa mdahalo huo.

Hali hiyo iliwafanya wanachama na wafuasi wa CCM waliomsindikiza mgombea huyo ukumbini kutoka wakiwa hawana furaha ya kutosha kama ilivyokuwa wa wafuasi wa vyama vya CUF na Chadema.

Zitto aahidi utumishi uliotukuka
Kwa upande wake, Zitto aliwaasa wakazi wa Igunga kuchagua mbunge atakayeweza kuwasemea kero zao ili zifanyiwe kazi.“Nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wagombea wote, wameonyesha namna walivyojiandaa kuwatumikia wananchi,” alisema Zito na kuongeza:

“Kumbukeni kuwa uchaguzi huu si wa kuamua nani anajua kutukana, nani kavuliwa hijabu ni uchaguzi uliolenga kumpata Mbunge wa Igunga atakayeshughulika na matatizo ya watu.”

“Uchaguzi huu unaohusu kero za maji, ajira kwa vijana na hatima ya maendeleo ya watu wa Igunga na Chadema tumeshaonyesha mfano bungeni tupatieni mbunge wa 49 ili kutuongezea nguvu,” alisema.

Aliwahimiza wakazi wa Igunga kwenda kupiga kura kumchagua mbunge atakayeweza kuwasemea bungeni na si bora kiongozi.Alisema watu wanakumbuka katika Bunge la Tisa ambalo wabunge wa Chadema walikuwa 11, lakini kazi zao zilionekana na sasa wamefikia 48.

“Chadema hatuahidi maziwa na asali kwa wakazi wa Igunga, kazi zetu Watanzania mmeziona na mkatuongeza hadi kufikia 48 na sasa tunataka Igunga mtuongezee mtu wa 49 ili kutuongezea nguvu ya kufanya kazi.”

Kabla ya mdahalo

Mdahalo huo ulitanguliwa na vurugu za hapa na pale. Watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM na CUF walishambuliana kwa maneno.Hali hiyo ilimlazimu Polisi aliyekuwapo ukumbini kusimama na kutoa maelezo juu ya malengo ya mdahalo huo kwamba ni kuwapima wagombea wao na kutishia kwamba endapo hali ingeendelea kuwa hivyo kungeahirishwa.

“Mdahalo unawapa nafasi ninyi wakazi wa Igunga kupima wagombea, lakini kama hali itaendelea hivi tuna uwezo kusitisha,” alisema.

 
Source ya habari yako? Halafu mgombea wa cuf anasema atahakikisha baada ya siku 600 daraja linajengwa..! Hapo vp?
 
Nilikuwa nasubiri kwa hamu sana kupata yaliyojiri kwenye mdahalo wa wagombea huko igunga. Nashukuru nimepata kutoka mwananchi na habarileo. Angalau nimepata picha ya yaliyojiri.

Kuhusu mgombea wa ccm kupatwa na hicho alichokiita "ulimi kuteleza" aka "kudanganya" sidhani kama ilikuwa ni sahihi sana! Alitakiwa atuambie hizo data za uongo alizitoa wapi na kama ametunga, aseme alikuwa na lengo gani. Maana ndio umekuwa mtindo wa wagombea kutudanganya tunawapa kura halafu wanahamia dar na kuonekana ni hadi tbc wakionesha bunge. Kusema tu ulimi umeteleza is very cheap hivyo alitakiwa kwenda deep zaidi!
 
mgombea wa CUF, Leopold Mahona ameibuka kidedea katika mdahalo wa wagombea ubunge katika jimbo la igunga akiongea kwa kujiamini na kueleza nini atakacho wafanyia wakazi wa jimbo la igunga huku akiwatuhumu wagombea wenzake kukabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wakati wakiwa kazini, ambapo alisema kashindye alipokuwa mratibu alikabiliwa na ubadhirifu wa sh 14,000,000. ambapo kashindye alishindwa kukanusha, akijibu maswali kwa ufasaha huku akipigiwa makofi mengi na waliohudhuria.
 
mgombea wa CUF, Leopold Mahona ameibuka kidedea katika mdahalo wa wagombea ubunge katika jimbo la igunga akiongea kwa kujiamini na kueleza nini atakacho wafanyia wakazi wa jimbo la igunga huku akiwatuhumu wagombea wenzake kukabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wakati wakiwa kazini, ambapo alisema kashindye alipokuwa mratibu alikabiliwa na ubadhirifu wa sh 14,000,000. ambapo kashindye alishindwa kukanusha, akijibu maswali kwa ufasaha huku akipigiwa makofi mengi na waliohudhuria.

Kumbe mgombea wa Chadema ana kashfa ya ubadhirifu. Sasa mbona anaendelea na kampeni?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom