Crisis leads to Chaos: Udanganyifu kozi za Ualimu

Rev. Kishoka

JF-Expert Member
Mar 7, 2006
4,526
1,529
Wengi wenu inawezekana mmeliona hili au hamkuliona na kulipa umaana na umakini.

Lakini nimeguswa sana na kuhuzunika kuona jinsi Mtanzania anavyoendelea kuhangaika na kutafuta kila mbinu kujipatia kipato.

Mtakayosoma hapa chini, si ya kupuuza au kufikiria kuwa ni suala la "ukihiyo" au elimu feki, mlipokee kama kiu ya wananchi kujiendeleza na wanashindwa kuona tumaini kutokana na mfumo mbovu wa elimu, mfumo uliozorota wa uchumi na uongozi.

Ikiwa karibu nusu ya wanachuo hiki walikuwa wamefoji vyeti, wametumia majina bandia ili wapate nafasi kwenda shule, je tunajiambia nini kama Taifa? je tumekaa chini na kujihoji kujua tatizo letu ni nini?

Je serikali ilipobaini yaliyotokea kupitia Baraza la Mitihani, imechukua hatua gani kutafuta ufumbuzi wa kudumu?

Nukuu kutoka gazeti la Majira:
Udanganyifu kozi za ualimu waongezeka


Na Reuben Kagaruki

BARAZA la Mitihani la Taifa limetangaza matokeo ya Taifa ya mitihani ya vyuo vya ualimu iliyofanyika Mei mwaka huu na kubaini ongezeko la idadi ya watahiniwa wanaofanya udanganyifu ili kujipatia sifa za kujiunga na vyuo, ikiwa ni pamoja na kutumia vyeti vya waliokufa na wasioona.

Kutokana na hali hiyo, Baraza limekiri kukithiri kwa udanganyifu kwa kasi kubwa na limetangaza mkakati madhubuti wa kupambana na watu hao.

Mkakati huo ni pamoja na kuhakiki watahiniwa, vyeti kuwa na picha na wale ambao watabainika walidanganya, vyeti vyao vitabatilishwa hata kama watakuwa wameanza kazi na hiyo haitahusu walimu tu.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Joyce Ndalichako, wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa vyuo vya ualimu daraja A, ualimu daraja A-kozi maalumu, Stashahada ya ualimu, Cheti cha Ufundi na Stashahada ya Juu ya Uhandisi.

Alitaja chuo ambacho kimevunja rekodi kwa kuwa na watahiniwa waliovunja rekodi kwa udanganyifu ni Kange cha Tanga ambapo kati ya wahitimu wote 1,066, watahiniwa 405 walibainika kufanya udanganyifu na wengine wanachunguzwa.

Dkt. Ndalichako alisema watahiniwa wa chuo hicho baadhi yao walipoulizwa majina yao, walikosea wengine wakawa hawajui zilipo shule walizosoma.

Alisema Baraza lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa katika chuo hicho kulikuwa na watahiniwa waliosajiliwa kufanya mitihani bila sifa zinazotakiwa.

Alisema Baraza liliamua kufanya ufuatiliaji zaidi wakati watahiniwa hao walipokuwa wakifanya mtihani. "Uchunguzi wa awali ulionesha dalili za kuwapo watahiniwa wasiokuwa na sifa," alisisitiza Dkt. Ndalichako na kuongeza kuwa dalili hizo zilijitokeza wakati wa mahojiano baina yao na maofisa wa Baraza.

Alitoa mfano akisema watahiniwa 18 walipoulizwa majina yao na shule walizosoma, walitaja majina tofauti na waliyokuwa wameyatumia katika usajili wa mtihani.

Aliongeza kuwa watahiniwa 40 walikosea kutaja mahali zilipo shule walizosomea. Alisema yupo mtahiniwa aliyedai amehitimu katika Sekondari Jangwani, lakini alipoulizwa iko wapi, alijibu iko Dar es Salaam maeneo ya Posta Mpya kushoto.

"Msichana mmoja alipoulizwa amesoma shule gani alijibu Sengerema wakati hiyo ni ya wavulana," alisema Dkt. Ndalichako kwa mshangao.

Watahiniwa 17 waligoma kujibu maswali na baadhi yao walionekana kukerwa na kitendo cha kuulizwa maswali.

Dkt. Ndalichako alisema Baraza liliamua kuwapiga picha na kutakiwa kuandika maelezo yao nyuma ikiwa ni pamoja na majina yao na shule walizosoma.

Baada ya hapo alisema Baraza liliwaandikia wakuu wa shule barua za kuwaomba kutuma nyaraka za wanafunzi hao, ikiwa ni pamoja na kadi za maendeleo na picha za watahiniwa waliomaliza kidato cha nne katika shule zao.

Alisema hadi Julai 28 mwaka huu, Baraza lilikuwa limepokea taarifa za wanafunzi 658 kati ya watahiniwa 1,066 waliofanya mtihani katika chuo cha Kange.

Katika uchunguzi huo ilibainika kuwa picha za watahiniwa 405 zilizowasilishwa na wakuu wa shule hazifanani na picha walizopigwa wakati wa kufanya mtihani.

Alisema watahiniwa 83 walichaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na kati yao, tisa walishafuzu mafunzo na kuajiriwa katika taasisi mbalimbali.

Ilibainika kuwa watahiniwa wawili walishafariki dunia na wengine idadi kama hiyo walikuwa wanaona lakini walitumia matokeo ya watahiniwa wasioona.

"Kwa mantiki hiyo uchunguzi umethibitisha kuwa watahiniwa 405 katika chuo cha Kange waliofanya mtihani wa Daraja 'A' hawakuwa watahiniwa halali na walitumia matokeo ya watu wengine," alisema Dkt. Ndalichako na kuongeza:

"Idadi hiyo ni kubwa na inaonesha jinsi ambavyo vitendo vya udanganyifu katika sifa za elimu vinavyozidi kukithiri," Dkt. Ndalichako aliahidi kuwa Baraza linaendelea na uchunguzi wa wanafunzi waliobaki.

Mbali na wanafunzi hao, alisema Baraza limefuta matokeo ya wanafunzi wanane waliofanya udanganyifu. Kati ya wanafunzo hao watatu ni wa Taasisi ya Ufundi Dar es Salaam (DIT) ambao walifanyiwa mtihani na watu wengine.

Alisema watahiniwa 124 kutoka vyuo 11 vya ualimu walisajiliwa kujiunga na vyuo hivyo kinyume na taratibu kwa vile walimaliza masomo ya sekondari Oktoba mwaka juzi.

Watahiniwa wawili katika chuo cha Tarime walibainika kuongezwa katika orodha ya mahudhurio na wasimamizi wa mitihani bila idhini.

Ili kukabiliana na udanganyifu huo, Dkt. Ndalichako alisema Baraza limeweka mkakati wa kukabiliana na vitendo hivyo ambapo vyeti vyote vitakuwa na picha na uhakiki mwingine utakuwa ukifanyika.


Alisema ana imani Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itachukua hatua dhidi ya vyuo vinavyojihusisha na udanganyifu. Adhabu ambazo zinaweza kutolewa ni pamoja na kituo cha mtihani kufutwa.

Ukiondoa dosari hiyo, Dkt. Ndalichako alisema kati ya matokeo ya watahiniwa 7,257 aliyoyatangaza rasmi jana 7,164 sawa na asilimia 98.7 wamefaulu mtihani huo.
Walioshindwa ni watahiniwa 95, kati yao wasichana ni 50.

Alisema Baraza hilo limesitisha kutoa matokeo ya mitihani ya watahiniwa 33 ambao hawajalipa ada na yatatangazwa baada ya kulipa ada na faini. Aliongeza kuwa iwapo malipo hayo hayatafanyika ndani ya kipindi cha miezi sita, yatafutwa.

Pia Baraza hilo limesitisha kutangaza matokeo ya watahiniwa wasiokuwa na alama za maendeleo wapatao 35 na kama wakuu wao wa vyuo hawataziwasilisha ndani ya miezi sita yatafutwa kwa kufuata kifungu 52 cha kanuni za mtihani.
 
...yaani, mtu unakosa hata pakuanzia. ingelikuwa nyumba, yaani mtu unabomoa yote na kuanza kujenga tofali moja baada ya jingine mpaka ujenzi unakamilika.

...kila kitu shaghalabagala tu, please bring on some good news for once! Grrrrrrrr :(
 
Kila kona uozo. Hii inatuonyesha kwa mara ingine tena umuhimu wa uongozi makini. Watanzania tunacheza na maisha yetu na uhai wa nchi yetu tunapoendelea kucheza na uongozi wa nchi kwa kuwachekea hawa CCM, ni hatari tena sio kidogo
 
...yaani, mtu unakosa hata pakuanzia. ingelikuwa nyumba, yaani mtu unabomoa yote na kuanza kujenga tofali moja baada ya jingine mpaka ujenzi unakamilika.

...kila kitu shaghalabagala tu, please bring on some good news for once! Grrrrrrrr :(

Inawezekana kuanza upya hata katika siasa; ni kubadilisha mfumo kwa maana ya kuanza upya na chama kingine kabisa. CCM wafanyeje ndio tujue kwamba ni waharibifu?
 
Truth of matter is that BAMITA na Serikali watachukulia hatua makosa yaliyotokea, lakini si chimbuko au mzizi wa makosa kutokoea.

Wanasema kinga ni bora kuliko matibabu, wao wanatafuta kinga kuzuia kufoji vyeti na si kujiuliza kwa nini watu wanafoji vyeti au kughushi nyaraka ili wapate kwenda vyuoni!
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom