CPC na CCM vyaboresha uhusiano wao kutoka wa kirafiki na kindugu hadi kuwa msingi imara wa kukuza fursa za kiuchumi na uwekezaji

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,063
1,072
1720423095271.png


Tangu ufanyike mkutano wa 18 wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti ikiongozwa na Xi Jinping, imekuwa ikitoa mawazo mapya, mitazamo mipya na hatua mpya za kuongoza kazi ya kimataifa ya Chama.

Chama cha CPC pia kimefanya ujenzi wa Pendekezo la ‘Ukanda Mmoja Njia Moja’ kuwa kituo cha kuanzia, na ujenzi wa ‘Jumuiya ya Binadamu yenye Mustakabali wa Pamoja’ kuwa lengo lake la mkakati wa kutekeleza diplomasia ya chama chake. Wakati huo huo, pendekezo la ‘Jumuiya ya China na Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja’ pia linatoa mahitaji mapya kwa ajili ya mawasiliano ya vyama vya siasa vya China na Afrika.

Kikiwa chama cha siasa kilichoongoza kwa muda mrefu zaidi nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina historia ndefu ya mawasiliano ya kirafiki na chama cha CPC. Wakati uhusiano wa CPC na CCM ukifikia miongo sita sasa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, hivi majuzi alipokutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPC, Tang Dengjie aliyewasili Tanzania kwa ziara ya siku tatu na kukutana na viongozi wa CCM, ameitaka China kuunga mkono uwekezaji katika sekta zinazoendelea nchini humo, zikiwemo sekta za afya, ujenzi, utalii, kilimo, dawa, biashara na uchumi, akisema urafiki huo unapaswa kuendelea katika sekta za maendeleo.

Siri kubwa ya uhusiano huu wa muda mrefu kati ya CPC na CCM ambao ulianzishwa na waasisi wa vyama hivyo yaani Mao Zedong wa China na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, ni kwamba unaendana sana na kanuni zake za kiitikadi, kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwa sasa umekuwa mfano wa kuigwa katika Afrika na hata dunia nzima.

Ikumbukwe kuwa awali ushirikiano huu wa tangu enzi na dahari ulikuwa ni wa kirafiki na kindugu lakini sasa umebadilika na kuwa msingi imara wa kukuza fursa za kiuchumi na uwekezaji, huku ukilenga kuimarisha ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.

Kabla ya CCM kuanzishwa, CPC ilianza mawasiliano yake na chama cha TANU. Baada ya hapo, mahusiano kati ya CPC na CCM yakapitia hatua tofauti. Kutoka “Nadharia ya Dunia Tatu” ya Mao Zedong, ambayo iligawa dunia katika sehemu tatu tofauti kwa kuzingatia ushawishi wa kisiasa na kiuchumi, hadi “Kanuni Tano za Kuishi pamoja kwa Amani” zilizotolewa na Zhou Enlai na hadi sasa “Jumuiya ya Binadamu yenye Mustakabali wa Pamoja” ya Xi Jinping, mambo mengi mapya yameonekana katika kila hatua.

Mwaka 2017, rais Xi Jinping alitangaza katika Mkutano wa 19 wa CPC kwamba Ujamaa wenye sifa ya Kichina umeingia katika zama mpya, na mawasiliano kati ya CPC na nchi za kigeni pia yameingia katika zama mpya, na hata mawasiliano ya vyama vya CPC na CCM pia yameingia katika zama mpya. Kwa kuzingatia kauli hiyo ya rais Xi, Tang Dengjie amesema dhamira ya China ni kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kuunga mkono mipango inayowanufaisha wananchi wa pande zote.

“Miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania ni ushahidi wa urafiki wetu wa kudumu na kuheshimiana, tumejitolea kuimarisha zaidi uhusiano huu kwa manufaa ya watu wetu,” amesema Tang Dengjie.

Kwa sasa China ndiyo mshirika mkuu wa biashara wa Tanzania, hali iliyodumu kwa miaka minane mfululizo. Mwaka 2023, urari wa biashara kati ya nchi hizi mbili ulifikia Dola 8.78 bilioni za Marekani, ikionesha ongezeko la asilimia 5.66 kutoka mwaka uliopita. China pia imewekeza miradi 260 katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, na kuweza kuimarisha nafasi yake ya kuwa mwekezaji mkubwa wa kigeni wa nchi hiyo.

Kwa upande wa diplomasia ya kisiasa, CPC kupitia wataalamu wake wa vyuo vikuu imejitahidi kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watendaji na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kulingana na mahitaji yao ya kitaaluma na kisiasa. Na kwa kuwa China ina uzoefu na maarifa mengi katika nyanja tofauti ikiwemo teknolojia, wakati huohuo ikiwa tayari kushirikiana na nchi nyingine, ni matarajio ya kila mtu kwamba uhusiano huu wa vyama vya siasa utazidi kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote.
 
Back
Top Bottom