COVID19 na safari ya wana wa Israel

Baraka Sabi

Member
Mar 16, 2017
17
13
Ni wazi dunia nzima inazizima kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona (COVID -19) tangu kubainika kwake hapo disemba 2019. Ni gonjwa ambalo mpaka sasa limegharimu maisha ya maelfu ya wanadamu huku likiacha athari za kijamii na kiuchumi zisizoweza kuzibika hata kidogo miongoni mwa wanajamii.

Nakiona kipindi cha COVID-19 sawa na safari ya Wana wa Israel kuelekea nchi waliyoahidiwa na Mungu wao (Kutoka 3:7-8). Wakiwa safarini, Mungu alihakikisha anawapa maelekezo mabalimbali yatakayowafikisha salama nchi ya Kaanan. Safari yao haikuwa nyepesi hata kidogo kwani waliruhusu dhambi ya manung'uniko ikawe taa ya kuwaongoza na kuitawala safari yao (Kutoka 16:1-3). Hali hii iliwafanya kusahau kabisa maelekezo na ukuu wa Mungu wao aliyewatoa nchi ya utumwa.

Ni katika muktadha huu, dunia yote imo safarini. Tumepewa maelekezo kadha wa kadha kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) tuyazingatie kama taa ya kuyaongoza mapito yetu dhidi ya COVID-19 kama vile;

(i). Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka huku ukitumia dawa za kuua vijidudu angalau kwa sekunde 20.

(ii). Kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu mmoja na mwingine.

(iii). Kuepuka kugusa pua, macho na mdomo kwa mikono isiyo safi.

(iv). Kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya kwa kutumia kitambaa au kona ya ndani ya mkono wako.

(v). Kubaki nyumbani ikiwa hujisikii vizuri. Iwapo una mafua, homa ama kikohozi, wahi hospitalini kwa msaada zaidi.

(vi). Kuepuka sehemu yenye msongamano.

(vii). Kuvaa barakoa (Mask) inapobidi kufanya hivyo n.k.

Hiki ni kipindi cha mpito na ni kipimo cha ustahimilivu wetu. Japo kitatuacha na makovu lakini liko tumaini la kufika ng'ambo ya pili na maisha kuendelea. Si kipindi cha kulaumiana, kudharirishana au kumbeza msafiri mwenzako sababu eti ni kiongozi na hajafanya kile unachokiwaza wewe katika kipidi hiki kigumu.

Ni kipindi cha kuchukua tahadhari zote stahiki kama ambavyo zimetolewa na wataalamu wetu. Si muda wa kulalamika ama kunung'unika kwani kwa kufanya hivyo gonjwa hili litatumia udhaifu wetu kutumaliza. Kwa namna tulivyoumbwa kwa uwezo wa Mungu, lockdown ni sharti ianzie miyoni mwetu kwa faida yetu sisi wenyewe. Usisubiri uambiwe ujilock au utenganishwe na mikusanyiko inayoweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa huu ili hali ukijua ni wajibu wako kujitenga.

Nimalizie kwa kurejelea kauli iliyowahi kutolewa na Rais wa 35 wa Marekani, John F. Kennedy alisema hapa nanukuu "Ask not what your country can do for you, ask what you can do for your country" mwisho wa kunukuu. Usijiulize Serikali ikutendee nini katika kipindi cha mlipuko wa COVID-19, jiulize umeitendea nini jamii yako katika kujikinga na kuepukana na gonjwa hili baya kwani unayemuuliza naye msafiri mwenzako.

SAFARI NJEMA.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom