Colonel Dr. Hassy Kitine afichua siri yake na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere

JokaKuu

Platinum Member
Jul 31, 2006
30,441
55,018
HIVI karibuni Livingstone Ruhere alifanya mahojiano na Dk. Hassy Kitine, ili kufahamu kilichojiri endelea kusoma mahojiano haya.
…………………….

Raia Mwema: Historia yako kwa kifupi, tafadhali.


Dk. Hassy Kitine
Dk. Kitine: Rasmi naitwa Dk. Hassy Kitine, si Hansy, kama magazeti mengi yanavyoandika. Hakuna n, Hansy ni jina la Kijerumani.

Vile vile Hassy halitokani na jina Hassan, Hassy ndilo jina langu nililopewa na bibi yangu. Nilizaliwa mwaka 1943 Kijiji cha Kisinga, Kata ya Lupalilo, Tarafa ya Lupalilo, Wilaya ya Makete.

Mwaka 1950 nilianza Shule ya Msingi Rungwe, Tukuyu niliondoka Makete nikiwa na miaka minne kwenda kumfuata shangazi yangu, bibi yangu amenibeba kutoka Makete kwenda Tukuyu baada ya baba yangu kufariki mwaka 1948.

Sijui kwa nini alinipa jina la Hassy. Lakini hilo ni jina lenye asili ya huko Makete, la ki-Kinga.
Mwaka 1954 nikafaulu kwenda Middle School Ndembela, sasa hivi ni shule ya sekondari hapo hapo mji wa Tukuyu. Halafu mwaka 1958 nikafaulu kutoka Ndembela kwenda Shule ya Sekondari Malangali kuanzia mwaka 1958 darasa la tisa hadi mwaka 1961.

Mwaka wa Uhuru nikamaliza darasa la 12, nikafanya mtihani wa Cambridge School Certificate mwanzoni mwa mwaka 1962 nikafaulu kwenda Tabora Boys. Nikakaa pale darasa la 13 hadi la 14 mwaka 1963, mwaka 1964 nikafaulu kuja Chuo Kikuu Dar es Salaam, kusoma shahada ya uchumi.

Nikiwa Chuo Kikuu, nilikuwa na Samuel Sitta. Nimesoma naye darasa moja tangu Tabora School hadi Chuo Kikuu Dar es Salam. Tukiwa hapo Chuo Kikuu tulifanya maandamano yale ya JKT lakini si yale ya kuchapwa viboko, haya yalikuwa ya awali kabisa. Ya viboko ilikuwa ya akina marehemu Wilfred Mwabulambo.

Tulifukuzwa na kukaa nje mwaka mmoja na katika taaluma tulipoteza miaka miwili, tukarudi mwaka 1968 badala ya 1967.

Nilipotoka Chuo Kikuu nikafundisha Shule ya Ihungo, iko Bukoba, darasa la 13 na 14. Nilikuwa nafundisha somo la uchumi kwa muda wa miezi minne, mwaka wa kwanza Januari mpaka Aprili, 1969 halafu ndiyo nikaitwa kwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu, kwa mujibu wa sheria.
Kwa sababu nilikuwa msomi, nilienda Ruvu miezi mitatu nikaja kufanya kazi ya ukarani Makao Makuu ya JKT. Mkuu wa JKT wakati huo alikuwa Robert Kaswende (marehemu).

Nilikaa JKT chini ya miezi 18 kwa sababu kiserikali walikuwa wanateuliwa vijana kwa mujibu wa sheria, mkitoka pale JKT mnakwenda sehemu mbalimbali. Sasa mimi ulitolewa uamuzi kwamba vijana 10 waliomaliza kwa mujibu wa sheria wabakizwe JKT baada ya miezi 18, mimi nikawa mmojawapo.

Nilivyoambiwa hivyo wakati huo tulikuwa tunaichukia sana JKT. Jamaa zangu fulani walikuwa wako jeshini, (marehemu) Meja Jenerali Godfrey Mang’enya tulisoma naye tokea Tabora School na Chuo Kikuu na mwingine ni Brigedia Jenerali Peter Ligate kwa sasa amestaafu.

Ligate nilisoma naye Malangali, kwa hiyo waliniuliza kwa nini huwezi kuja jeshini kama wamekwambia uwe JKT. Nikawaambia sawa nadhani naweza kuja. Wakamwambia Mkuu wa Jeshi, Jenerali Sarakikya, kuna kijana anataka kuja jeshini, nikaitwa ofisini kwake akanikubaliana kwenda jeshini.

Nikaondolewa JKT ikabidi nikasomee recruit training Mgulani, kozi ya kwanza ya uaskari nikakaa pale miezi miwili au mitatu nikaenda Uingereza kama Officer Cadet kwenda kusomea uofisa. Nikakaa mwaka mmoja. Kule tulikuwa Watanzania wawili, mimi na Jenerali Mbita, yeye alikuwa nadhani Press Secretary wa Rais. Alikuwa mkubwa kwangu wala Tabora School sikumkuta.

Tukasoma programu ngumu ya masomo ya kijeshi, mwaka 1971 katikati tukarudi. Baada ya hapo nikapelekwa kufanya kazi Nachingwea, nilikuwa Luteni. Nikaenda kule kuwa platoon commander, nilikuwa na kikosi changu yaani platoon yangu.

Nikawa nalinda mpaka kutoka Mtwara hadi Nachingwea kwa hiyo mimi literary nimepigana kwa kusaidiana na Freelimo. Najivunia kusema nimeipigania nchi yangu na nimesaidia kupata uhuru wa Waafrika wenzetu.

Kwa muda wa mwaka mmoja hivi tulikuwa tunapigana na Wareno, Freelimo wanakwenda ndani sisi tunalinda mpaka.

Baada ya pale nikahamishwa kurudi Dar es Salaam. Serikali ikaamua kwamba tufundishe maofisa wetu sisi wenyewe, yaani Jeshi la Wananchi wa Tanzania lilikuwa linapeleka vijana kwenda kwenye mafunzo, katika nchi za India, Pakistan, Urusi, China, Canada na Uingereza.

Kwa hiyo, mwaka 1971, tukaanzisha chuo cha kufundisha maofisa wetu hapa hapa. Mwanzo wa Chuo cha Monduli unatokana na chuo kilichoitwa OCS, Officer Cadet School, ambacho tulianza pale Kurasini kwenye Chuo cha Mafunzo cha Polisi.

Tulianza mwaka 1971 maofisa watano kufundisha maofisa wetu wa JWTZ, mkubwa wetu alikuwa akiitwa OCS Jenerali Tumainieli Kiwelu, maana yake Office Command School, ma-platoon kamanda walikuwa wawili, marehemu Meja Jenerali Sam Tareku Laiser halafu Meja Paul Mungai, mimi nilikuwa assistant training officer.

Kazi yangu ilikuwa kutengeneza programu za mafunzo darasani na nje ya darasa. Lakini kazi yangu nyingine ilikuwa ni political education officer, nilikuwa officer wa nne, nikiwa Luteni na baadaye Kapteni, halafu tulikuwa na Godfrey Mwambapa.

Halafu mwaka 1972 nikapelekwa Kivukoni kufundisha. Kupata ufundi wa juu wa mbinu za kufundisha siasa jeshini.

Palikuwa na Mzungu alikuwa anaitwa Canning, baadaye akachukua marehemu Elinawinga, akiwa mkuu wa chuo.

Mwezi wa 11 na 12, mwaka 1972 nikarudishwa jeshini, lakini tukawa tumehamia Monduli. Niliendelea na shughuli zangu hizo hizo. Tulikuwa na Jenerali Kiwelu bado, tukakaa kule baadaye alikuja marehemu Jenerali Anatoly Kamazima.

Nikakaa mwaka 1972 Desemba hadi 1973 mwisho hadi Aprili 1974, Rais akafanya mabadiliko ya uongozi serikalini. Akamwondoa Jenerali Sarakikya kuwa Waziri wa Habari na Michezo halafu Jenerali Abdallah Twalipo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera akamwondoa huko akaja kuwa Mkuu wa Majeshi.

Na mimi wakaniondoa Aprili 1974 Monduli wakanileta hapa kama msaidizi wa Mkuu wa Majeshi, kama Katibu wa Mkuu wa Majeshi.

Aprili hadi Julai, nikahamishiwa Morogoro kwenda kiwanda cha kutengeneza silaha ndogo, Mzinga, kuwa Naibu Meneja Mkuu chini ya Marehemu Brigedia Jenerali Nyoka na tukakaa wote pale halafu Mwezi wa Sita, tulikaa pale miezi mitatu, mwezi wa Nane nikarudishwa pale pale kwa maagizo ya CDF kulitokea matatizo.

Halafu nikakaa pale hadi miezi kama sita, baada ya hapo nikateuliwa na Baba wa Taifa kuwa Mkuu wa Chuo cha Monduli (Commandant).

Kile cheo ni kikubwa. Ni cheo cha Jenerali, lakini mimi nilikuwa meja ambacho ni cheo kidogo. Nilitoka kapteni kwenda kule lakini nikawa mkuu wa chuo sijui kwa nini walifanya hivyo kwa sababu hicho ni cheo kidogo, lakini wanasema ni uwezo wa ofisa bila kujali sana cheo.

Nikakaa pale mwaka 1974 mwishoni na mwaka wote wa 1975 nikiwa Commandant. Mwaka 1976 Februari, Rais akaniteua kuniondoa jeshini kunipeleka Usalama, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa.

Lakini si kwamba alinifahamu sana. Ninaposema sana ni kwa sababu mimi nilikuwa responsible kuwa trainging officer na siasa kwa muda wote na Rais anakuja pale kila mwaka kukamisheni vijana.
Na wakati huo muda wote akija nilikuwa nipo pale na nilikuwa nimefundisha maofisa.

Kulikuwa na awamu mbili, ya kwanza maofisa wa infantry (askari wa miguu) na ya pili ilikuwa ile ya mkondo wa CMS, mafunzo ya kijeshi ambayo ni maofisa ambao wanatoka kuwa wanasiasa, wakuu wa mikoa na wilaya. Nilikuwa nawafundisha siasa akina marehemu Nnauye, Andrew Shija, Meja Joseph Butiku. Nilikuwa nawafundisha political science na military training.

Tarehe tano mwezi wa pili mwaka 1976 nilikuwa kwenye mafunzo porini. Wakati huo ananiteua ananifahamu moja ya sababu ni hiyo. Hawa maofisa wakuu wa mikoa, alikuwa ananiita kuja kuniuliza maswali.

Nataka kumteua mwanafunzi wako fulani kuwa mkuu wa mkoa au wakuu wa mikoa unaona vipi, unaonaje? Namwambia huyu atakusaidia. Huyu si sana, ngoja kidogo, kwa hiyo nilianza kufanya kazi ya usalama mapema zaidi.

Jeshini kuna vionjo vya mafunzo ya usalama pia. Lakini mimi baada ya kuteuliwa nilifanya mafunzo maeneo mengi na makubwa sana duniani, Cuba, Chekslovakia, Yugoslavia, Uingereza na nchi nyingine.

Raia Mwema: Nasikia kuna wakati fulani taifa lilifanya mabadiliko ndani ya Jeshi la Polisi, wewe na Joseph Butiku naambiwa ndiyo mliopewa kazi hiyo. Hili lilikuwaje?

Dk. Kitine: Kwanza hizo ndizo kazi za kiusalama za ndani. Siwezi kuzisema. Hata kama kuna ukweli.

Raia Mwema: Inaonekana kuna tofauti ya kiutendaji kwa upande wa usalama kwa sasa na wakati wako, tatizo ni nini?

Dk. Kitine: Kuna tofauti. Huwezi kusema tatizo ni nini, lakini kuna mabadiliko. Hali imekuwa nzuri zaidi kuliko ilivyokuwa zamani. Kuna mambo mengi sana yamebadilika.

Unajua ukishakuwa nje ya idara ya usalama kwa sababu kama mku wa usalama unaapishwa kila mtu anajua nchi nzima, unafanya kazi nchi inaendelea, ukishaondoka kwenye idara ya usalama kama mimi nilivyoondoka miaka mingi, huwezi kuwa na uwezo wa kutoa maoni juu ya hali ya usalama wakati huu.

Wakati wetu rushwa haikuwapo kwa kiwango hiki. Hili la escrow sijui limetokea vipi, lakini suala la rushwa wakati wetu ilidhibitiwa sana. Mambo kama Escrow yasingeweza kutokea kwa sababu rushwa ya namna hiyo haikuwapo.

Raia Mwema: Huoni nchi kwa sasa imeaibika kwa wizi kama wa Escrow, ukiwa kama mtaalamu wa masuala ya usalama.

Dk. Kitine: Mambo kama hayo katika Afrika, wakati mwingine tusijilaumu sana, nchi kama Nigeria, kiwango cha fedha ambayo imeibiwa nchini humo na viongozi, hii Escrow ni nini?

Hakuna kitu. Kuna rushwa katika Bara hili mbaya zaidi mara 600 au zaidi. Kilichotokea ni kibaya, ni kashfa lakini angalau tujiridhishe kwamba hii ni child’s play (cha mtoto).

Kuna viongozi Afrika wanasema haijulikani viwango vya utajiri wao.

Matatizo ya rushwa yanashughulikiwa na Takukuru, usalama ni idara inayoshughulika na masuala yote ya nchi.

Hatujui, inawezekana waliwasiliana na Takukuru, wakaamua namna ya kushauri viongozi wa serikali. Sasa mimi ningetaraji Takukuru walipewa taarifa na hata kwa viongozi wa serikali, inawezekana walishauriwa na wakaamua namna ya kushughulikia tatizo.

Mimi simlaumu mtu wala idara yoyote. Naamini kila mmoja alifanya kazi yake. Mimi niko nje sijui. Tukianza kusema Escrow itabidi tujiulize ni sehemu gani ya kambi kumetokea udhaifu? Nadhani serikali imechukua hatua.

Raia Mwema: Umeeleza ulikuwa Nachingwea, ilikuwaje zaidi.

Dk. Kitine: Mimi nimepigania nchi maeneo mengi si Msumbiji tu. Tulisaidia ukombozi bila kuathiri usalama wetu wa ndani.

Vyama vya ukombozi vilifanya shughuli zake ndani ya nchi bila kuathiri usalama wa nchi yetu hata siku moja. Vyama kama Swapo, Zanu, Freelimo, ANC, Liberation Organization Seychelles, Comoro, Uganda, Guinne Bissau.

Tulifanikiwa hivyo kutokana na msimamo wa uongozi wetu wa nchi. Kwamba haikuwa na maana Tanzania kuwa huru kama Afrika yote haipo huru. Ilikuwa kazi ngumu lakini ilifanyika.

Amani ilikuwapo nchini na kazi ya ukombozi ilikiwa ukiendelea nchi mbalimbali. Kwa wakati wangu nilikuwa nakutana na viongozi mbalimbali wakuu wa mapambano, wale vinara.

Kwa mfano, Yoweri Museveni alikuja nyumbani kwangu zaidi ya mara 20. Milton Obote zaidi ya mara 100, Sam Nujoma, Samora Machel, Chisano, Chipande, Guebuza, Mzee Kaunda, Dos Santos, wote hawa nilifanya nao kazi. Na mimi nashukuru hawa ni watu wakubwa sana lakini Baba wa Taifa alinitambulisha kwa wote hao, ni fursa kubwa sana.

Ukizungumza habari ya Farm 17 unazungumza habari ya Msumbiji. Ukizungumza habari ya Kongwa unazungumzia habari ya Namibia, Mazimbu- ANC, Handeni – wapigania uhuru wengine.

Raia Mwema: Tueleze kuhusu Seychelles

Dk. Kitine: Huko nimekwenda na nchi nyingine nyingi Afrika. Mimi ni mpigania uhuru. Nimekwenda Comoro, Madagascar, Msumbiji, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini kote huko.

Raia Mwema: Inasemekana ulipata gari aina ya benz kule Seychelles, uliletewa hapa ndani ya ndege.
Dk. Kitine: Si kweli. Hakuna kitu kama hicho. Sijawahi kuwa na benz. Ni uzushi. Nilinunua gari mimi kule Peugeot, 405, na nilinunua ile gari kwa dola hata 1,000 hazikufika. Sijui 500 au 600, na hiyo pesa niliyotumia alinipa Hassan Ngwilizi.


Halafu yeye alikuwa na mjomba wake hapa (nchini), alikuwa anajenga nyumba yake kule Lushoto akaniambia tafadhali kampe mjomba wangu hiyo, ilikuwa sawa na shilingi laki sita au saba.

Alinunua ile gari kwa niaba yangu, baadaye akafanya utaratibu wa kuileta huku, sasa alitumia hela yake hata dola 1,000 haikufika. Akaniambia tafadhali najenga nyumba kule kampe mjomba wangu.
Nimefika hapa nikampa hiyo pesa. Gari yenyewe nimenunua ya zamani ilikuwa ya hela ndogo, akanipa niilete. Lakini watu wakapiga kelele. Nimenunua gari, Mwalimu (Rais Nyerere) amenifukuza kazi.

Raia Mwema: Kuna wanaosema hiyo ndiyo sababu Mwalimu Nyerere alikufukuza kazi Usalama wa Taifa?

Dk. Kitine: Kwanza Mwalimu hakunifukuza kazi. Mimi kabla ya hapo nilikwishakuwa nimefanya kazi miaka mingi, nimechoka sana.

Nilimwomba Mwalimu ukipata mtu mwingine naomba unisaidie nipumzike. Nimeanza kazi nikiwa na miaka 33 ya usalama wa taifa hadi miaka 40. Ile kazi ukifanya mwaka mmoja tu ni kazi kubwa sana.

Kwa hiyo nikwambia Mwalimu, akasema sasa wewe nikikuruhusu upumzike unataka kufanya nini?
Akaniambia nitakuteua mkuu wa mkoa, nikasema hapana. Naomba unisaidie nikasome na nikishasoma nikafundishe chuo kikuu. Akakubali akanitafutia scholarship.

Akamwita Balozi wa Canada ofisini kwake na kumwambia kijana wangu amenisaidia sana katika kazi ngumu sana, naomba uwaambie Canada angependa aje kusoma huko ama Sweden. Waambie wakubwa zako wamtafutie scholarship, nikapata nafasi hiyo siku hiyo hiyo moja.

Kuhusu suala la gari, ile gari ilikuja hapa, kabla haijafika nikazungumza na Gavana wa Benki Kuu, Charles Nyirabu. Nikazungumza na waziri mkuu Edward Sokoine, kuwaambia iko gari inakuja huko nilishafanya utaratibu zaidi ya miezi miwili iliyopita.

Unajua walikuwa wanakamata magari kupeleka Kampuni ya Taifa ya Magari. Lakini nataka kusema kwamba hakuna hata senti moja ya kwetu kwenye dola ambayo imetumika.

Unajua, ngoja nikwambie, Baba wa Taifa wamemwambia watu wa ndani kwamba Kitine naye ameagiza gari. Baba wa Taifa akachukia sana akaniita …. akaniuliza nikamweleza.

Tatizo ni foreign exchange, na mimi najua, na hii gari hakuna hata senti moja ya dola ya Tanzania ilitumika. Nimezungumza na Jenerali Ngwilizi akanunua na ile gari ikaja hapa.

Sasa akasema sawa, waliompiga pampu wakawamshawishi akafanya uamuzi, akasema lakini jina lako limechafuka.

Raia Mwema: Hebu eleza vizuri namna Baba wa Taifa alivyokuuliza swali kuhusu suala hili.

Dk. Kitine: Kwa nini wewe umeleta gari na mimi hujaniambia? Hiyo ndiyo iliyokuwa kauli yake. Nikamwambia Mwalimu ni kweli nimeleta gari sikudhani kwamba ni jambo la kukwambia.

Nimemwambia Gavana unaweza kumwita hapa na nimezungumza na Waziri Mkuu, wote wameniambia hakuna uhalifu wowote. Unaweza kuwaita kabla mimi pengine sijawasiliana nao.

Akaniambia lete funguo. Nikamwachia. Basi, baadaye wakampa kukaimu cheo Augustine Mahiga. Mahiga alikuwa mmoja wa wakurugenzi.

Nilikuwa na wakurugenzi wanne, alikuwa yeye, Adam Marwa, Emmanuel Mwambulukutu na Nimrod Lugoye. Akamteua Mahiga.

Baadaye nilimwambia Sokoine. Yule mtu alikuwa kiongozi sana. Sokoine akaniambia nenda nyumbani mwandikie barua Mwalimu. Mwambie kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutumikia nchi yangu.

Ni matumaini yangu nimefanya kazi kwa uadilifu kwa kadiri nilivyoweza. Lakini pia naomba ufanye uchunguzi ili kusudi kama nimefanya kosa niadhibiwe kwa kupelekwa mahakamani. Lakini kama hakuna kosa naomba unisafishe kwa sababu hii inachafua rekodi yangu.

Alivyoisoma ile barua, niliipeleka mwenyewe. Alivyosoma ikamuuma sana. Kwa sabbu akajua kwamba mambo aliyoambiwa ilikuwa ni uongo mtupu.

Kwa hiyo, ameisoma ile barua akawaambia vijana hebu niitieni bosi wenu (mimi) kwa sababu ilikuwa bado haijatangazwa.

Akaniambia nimesoma barua yako vizuri sana nataka nikuhakikishie bado nakuamini. Sasa hapo maana yake anakubali ameambiwa uongo.

Raia Mwema: Je, alikusafisha kama ulivyoomba katika barua yako kwake.

Dk. Kitine: Kunisafisha? Mwalimu alikuwa hakuandikii barua. Lakini vitendo vyake vilionyesha. Muda mfupi tu alimwita balozi akasema umenithibitishia kwamba unataka kitu kimoja kwenda kusoma basi ili ufundishe chuo kikuu.

Akanitafutia hiyo scholarship. Balozi akaondoka mchana ule siku ya pili asubuhi anapiga simu kwa Mwalimu kuomba mihadi kuripoti. Akaenda kwa Mwalimu akafika akamwambia nimepata scholarship tangu jana na ni nzuri sana na kwa hiyo nitaomba tu Hassy aje tupange utaratibu.

Kwa sababu ilikuwa mwezi Julai akasema anaweza kwenda Septemba. Mwalimu akawaambia vijana mwiteni Hassy, akasema kamwone Balozi. Sasa wakati huo yakaanza mambo ya kampeni ilikuwa mwaka 1980. Nikaenda kusoma.

Raia Mwema: Kuna taarifa kwamba mmoja wa maofisa wako alikusainisha hundi au nyaraka ya malipo.

Dk. Kitine: Hakuna kitu kama hicho. Alikuwa ofisa mmoja ndiye aliyezusha hayo mambo na walimwita alete hizo karatasi.

Ni muongo muhuni kabisa. Alishindwa kuthibitisha ile nafasi ni kubwa sana. Unajua watu wanaitaka.
Baaaye naambiwa alikufa baada ya kushindwa kuthibitisha madai yale.

Maana aliulizwa kweli amenunua gari kihuni? Amenunua kwa hela za serikali? Anaulizwa ulimwambia mkubwa wako? Akasema nimesaini, na mimi sikusaini. Alidanganya. Kama ilikuwa saini basi aliiga.

Raia Mwema: Kwa nini wewe ulipokuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa hukushiriki vita ya Uganda?

Dk. Kitine: Hapana. Nimekwenda Uganda. Nimekwenda Kagera. Mimi ndiye nakwenda, narudi. Sipigani nafanya tathmini. Nakuja kutoa taarifa kwa Mwalimu, mpaka tumefika. Nimekwenda zaidi ya mara 10 au 15 nampa taarifa Mwalimu mpaka tunaingia ndani na baada ya siku kadhaa tutaingia Kampala na itakuwa aibu kwa sababu Amin amekimbia na hakuna serikali.

Nikamwambia tuna orodha ya Waganda wote dunia nzima. Wengine wako New York, wengine San Francisco, wengine London, Zimbabwe, kila mahali.

Mwalimu akasema fanyeni utaratibu muwaandikie wote waje ili wajadili juu ya kuunda serikali yao. Kwa sababu sisi vijana wetu wapo pale, lakini hakuna serikali.

Ule mkutano wa Moshi uligharimiwa na Idara yetu ya Usalama. Walikuwa Waganda zaidi ya 100, tumewalipia tiketi. Wamekuja wamekaa tukawaweka kwenye hoteli.

Wamekaa pale siku tatu wanabishana. Tukawaambia ajenda yetu mtoke hapa mmependekeza rais na baraza la mawaziri. Mimi nakwenda kumwambia Nyerere naye anaweza kurekebisha hapa na pale.
Na kweli wakapanga orodha yao. Nikaipeleka kwa Mwalimu Nyerere naye akapangua kidogo. Alikuwapo Dk. Kisasi akasema huyu hawezi kuwa Foreign, huyu hawezi kuwa wa Ulinzi, Museveni alikuwa Naibu kwenye moja ya wizara.

Raia Mwema: Nchi nyingi tulizozisaidia kuzikomboa idara zao pia za usalama zimeandaliwa kwa ushauri wa Tanzania, ni kweli hili?

Dk. Kitine: Ni Kweli. Na kwa kweli mimi nakusudia kuandika Kitabu. Nelson Mandela amekua kama kiongozi wa kwanza duniani, hasa alipofariki.

Hapana. Si sahihi. Mandela asingeweza kuinukia kama si Mwalimu Nyerere. Kilichomsaidia kwa namna tofauti Mandela ni kukaa jela miaka 20.

Nasema hivyo kwa sababu hakuna nchi yoyote katika Afrika na dunia na kiongozi yeyote aliyekuwa amejitolea kuleta uhuru wa nchi zote hizi kama si Mwalimu.

Ni Mwalimu ndiye aliyemwinua Mandela. Lakini Mwalimu alikuwa hajikwezi. Ni Robert Mugabe tu ndiye anaweka wazi haya.

Mimi nilikuwa bosi Jeshini na Usalama, najua. Idara ya Usalama wakati wa Ukombozi imeongozwa na watu wengi, alikuwapo Mzena, akaja Gama, halafu nikaja mimi kwa hiyo unatambua mafaniko ya Idara na sisi tuliokuwa kwenye Idara tunajua nguvu ya Mwalimu katika ukombozi. Natafakari kuandika kitabu.

Raia Mwema: Je, ulirudi kufundisha chuoni?

Dk. Kitine: Nilifundisha na wakati nafundisha mimi nilikulia Tukuyu, Mbeya, Iringa nilizaliwa Makete.

Kwa hiyo, nilivyorudi hapa nafundisha chuo kikuu nilifundisha miaka miwili, wanafunzi walinipenda sana, kuna wanafunzi wengi sana nimesahau majina.

Wakati nafundisha wakaja watu wa Iringa wakaniambia wewe ni mtu ambaye umekuwa kiongozi. Nchi inakufahamu kwenu ni Makete umekulia Tukuyu.

Kwa hiyo wewe ni southern highlander, hiyo ni 1995. Nikawaambia mimi mambo ya siasa sijui. Mimi ni mtaalamu wa uchumi. Nilikataa lakini nikashindwa. Wakasema kama unakataa una dharau. Wakasema tutajaza fomu na kulipia.

Nikawaambia fanyeni lakini mimi sihitaji. Nikaenda kura za maoni nikashinda. Tulikuwa 13 nikawa wa kwanza. Katika zile kura wote waliobaki 12 kura zao zote zikawa nusu ya kura zangu.

Tukaanza uchaguzi wa mwaka 1995. Nikashinda. Lakini kule wana tatizo kubwa la ukabila na udini. Wengi ni Wakatoliki, sasa wale hawakutaka Mwislamu awe mbunge. Kura zikaibwa. Zikakutwa chooni. Basi CCM tukashindwa. Wakasema afadhali tuwape wapinzani, na walisikia Benjamin Mkapa atanipa uwaziri nyeti.

Kwa hiyo Mkapa akachukia sana. Akaniteua kuwa Mkuu wa Mkoa Tanga. Nikamwambia hii si vizuri kwa sababu nimeshindwa uchaguzi halafu nakuwa Mkuu wa Mkoa si sahihi, akasema achana na hayo.

Akasema njoo nikuapishe, nikaapishwa nikaenda Tanga miaka miwili. Mwaka 1996 mwezi wa nane Tuntemeke Sanga akafariki dunia. Wakanifuata Tanga kuniomba nikagombee. Wakaniambia hivyo hivyo kama mwanzo, wakanishawishi na kunishinikiza.

Nikaenda Makete nikashinda kama ilivyokuwa Iringa, nikaitwa Dar es Salaam Ikulu, nikaonana na Rais akanipa hongera akaniambia nataka uwe waziri wa utawala bora.

Kwamba ripoti ya mzee Joseph Warioba alipendekeza niteue waziri atakayekuwa ofisini kwangu. Ndipo nikawa waziri wa mwanzo wa utawala bora.

Nikamwambia unanitilia uadui. Wabunge wengi wamekaa muda mwingi hawajawa wabunge mimi nimeshinda juzi juzi tu nakuwa waziri?

Raia Mwema: Mwaka huu kuna uchaghuzi na Katiba Inayopendekezwa, unazungumziaje masuala haya?

Dk. Kitine: Nasema wananchi wachague viongozi waadilifu. Uadilifu ndiyo namba moja. Kiongozi mwadilifu atakayekemea mambo mabaya na atasaidiana na viongozi wengine waadilifu wazuri kupunguza uchafu. Uchafu tulionao ni mwingi sana.

Kunahitajika kiongozi ambaye ana uadilifu. Anajua matatizo ya usalama ya nchi yetu, matatizo ya ulinzi ya nchi yetu. Tunahitaji uongozi unaojua nchi yenyewe, kila wilaya, kila tarafa, uongozi unaojua nchi yetu ina mipaka nane na si wote marafiki zetu kwa kiwango cha kuridhisha.

Tunahitaji kiongozi makini mwenye kazi ya kuvusha hii nchi ivuke. huwezi kuwa na kiongozi lelemama.

Raia Mwema: Je, utachukua fomu kugombea urais mwaka huu?

Dk. Kitine: Kuchukua fomu mwaka huu itategemea. Watu wanaotaka kunishawishi itabidi wanipe sababu kwa nini wanataka iwe hivyo.

Mimi nina vigezo vyote hivyo na zaidi ya hivyo. lakini kugombea urais itategemea. Siogopi, na Watanzania wote pamoja na viongozi wanajua kwamba mimi si mwoga kuhusu nchi hii.

Kama wanaona naweza shauri yao. Lakini mimi sina pesa. Uongozi wa sasa ni pesa. Lakini naweza kuwa rais bora zaidi. Nitakuwa rais bora zaidi kama nikipewa nafasi.

Katika watu waliojitokeza kutaka urais hakuna hata mmoja anayeifahamu hii nchi kuliko mimi. Naijua nchi hii, pia ni msomi niliyebobea nina digrii nne.

Mimi ni mchumi. Naujua uchumi wa nchi. Najua usalama. Hakuna hata mmoja anayejua usalama kama mimi. Hakuna mtu anayejua matatizo ya ulinzi kama mimi. Hakuna mtu anayejua usalama wa nchi kama mimi.

Hatutaki mambo kama ya Tanga (ugaidi) lazima kuwe na wa kukemea. Simtishi mtu, nazungumza habari ya nchi. Sina cha kulipiza kisasi.

Ujumbe wangu kwa Watanzania hawa ni kwamba, kuna mambo mawili makubwa, kwanza uchaguzi hasa wa mwaka huu, zipo pesa zimekuwa zikipita nchi nzima.

Nimekuwa nikiongea na Watanzania pamoja na viongozi. Nimepita mikoa fulani nawaambia viongozi wa CCM kwamba ninyi ndio mnaowapeleka wanaCCM kwenda kwenye mikutano wa kupiga kura.

Kuna wagombea watawapa pesa. Kuleni hizo pesa. Msikatae. Pesa ni pesa. Aliyekuwa anazikataa labda Baba wa Taifa tu. Kuleni, lakini kura yako ya kumchagua kiongozi wa kukuongoza haina thamani sawa na hizo pesa. Kura yako ni zaidi ya mamilioni ya fedha. Kura yako isilinganishwe na pesa.

Hawa wagombea (baadhi) wanazo pesa ambazo ni za wizi. Wametuibia hapa. Wanayo mapesa mengi, kuleni pesa zao, lakini kura yako ni zaidi ya thamani ya pesa hizo.

Pili, fika kwenye mkutano mkuu halafu kituo cha kura mpigie mtu unayemuona ni mtu safi. Na usafi huo unatokana na uwezo wa kukataa rushwa.

Kwa upande wangu nasema mimi sijajaza fomu. Lakini kama nisingekuwa mwadilifu, ningetaka kuwa na mapesa mengi, ningekuwa na mepesa hayo, mengi kuliko wote hawa wanaotaka urais.

Ningekwa nachota kule Usalama wa Taifa wakati niko mkubwa na kisha leo ningetoa rushwa. Lakini siwezi kuchanganya pesa na uongozi wa nchi.
cc ,misasa, BAK, ChamaDola, MTAZAMO
 
..ameeleza vitu vingi sana.

..jina lake ni HASSY Kitine.

..Ingawa Kitine ni Muislamu, lakini jina lake siyo kufupisho cha Hassan

..humo utapata historia ya chuo cha kijeshi cha Monduli.

..pia kuna vidokezo vya Tz kuwa na kikosi cha Wanajeshi nchini Seychelles kilichokuwa chini ya kamanda Brig.Hassan Ngwilizi.

..vipo vidokezo vya vita ya ukombozi Kusini mwa Afrika.

..Pamoja na kwamba aliondoka serikalini kwa kashfa, nadhani Col.Dr.Kitine anapaswa kuandika kitabu na kueleza mambo aliyokutana nayo ktk utumishi wake serikalini.
 
Historia murua kabisa.

Somo nililopata:

Nchi yetu ina mipaka mikubwa 8.

Na wote wa majirani wetu katika hiyo mipaka sio marafiki wazuri.

Mungu uilinde nchi yetu Tanzania dhidi ya wote wasioitakia mema nchi yetu.
 
Ameficha mengi sana ana siri nyingi sana hasa za ukombozi na jinsi JKN alivyokuwa anaendesha nchi wakati ule.....nadhani akiandika kitabu atatupa historia nzuri sana.....na nzuri kwa faida ya kizazi cha sasa.....!! Pole Mzee Kitine kwa msukosuko uliokutoa DG wa Kitengo
 
Aisee hii ni Historia Nzuri na Ya Kuigwa. Nitaendelea kuisoma nikipata muda. Maana naona nachelewa kupost maoni yangu.
 
safi sana lakini ni ya lini? mbona ina mambo ya uchaguzi, mshauri siku zinaenda, ndiye anayeteegemewa aandike historia safi ya nyerere na mstakabari wa ukombozi wa africa na udhubut wake
 
Back
Top Bottom