Clubhouse yakabiliwa na ukosoaji kuhusu usalama wa taarifa za watumiaji

Sam Gidori

Verified Member
Sep 7, 2020
94
150
Baada ya kushuhudia miezi kadhaa ya ukuaji wa idadi ya watumiaji, mtandao wa kijamii unaotumia zaidi sauti wa Clubhouse umeanza kukabiliwa na ukosoaji mkubwa hasa kuhusu usalama wa taarifa za watumiaji, na kuifanya kampuni hiyo kuhaha kutengeneza suluhu ya changamoto zake kurejesha imani ya watumiaji.

Licha ya kuwa katika hatua za awali za utengenezaji (beta), mtandao huo umejizolea zaidi ya watumiaji milioni 10 duniani, ukitajwa kuwa na thamani ya dola bilioni 1 za Marekani. Watumiaji wa mtandao huo wanahoji kuhusu kiasi cha taarifa zao binafsi kinachonyonywa na mtandao huo na usalama wa jinsi taarifa hizo zinavyohifadhiwa.

Mtandao huo unapatikana kwa watumiaji wa iOS tu (iPhone), na unaweza kujiunga kwa kualikwa na mtumiaji mwingine na huwawezesha watumiaji kujiunga na 'majukwaa' (rooms) ambayo ni mahsusi kwa majadiliano kwa njia ya sauti tu. Majukwaa hayo huweza kuwa ya umma ambapo baadhi ya wazungumzaji huongoza mjadala na wengine kuwa wasikilizaji, huku ikitoa fursa ya kuwa na majukwaa ya kijamii ambayo huruhusu kuwaunganisha wale unaowafuatilia tu na majukwaa binafsi ambayo utaruhusiwa kujiunga baada ya kupewa mwaliko.

Changamoto ya usalama ya Clubhouse ilianza kuanikwa na watafiti wa usalama wa kimtandao kutoka Taasisi ya Uchunguzi wa Intaneti ya Stanford baada ya kubaini kuwa taarifa za utambulisho wa watumiaji na majukwaa yao zilikuwa zikipatikana bila kuwekwa katika mfumo wa msimbo fiche (encryption), hii ikimaanisha kuwa mtu mwingine anaweza kufuatilia na kuwatambua watumiaji wa mtandao huo kwa urahisi.

Watafiti hao walibainisha kuwa baadhi ya miundombinu ya Mtandao huo, ikiwamo seva, zilikuwa zikiendeshwa na kampuni moja yenye makao yake katika Jiji la Shanghai nchini China, ikimaanisha kuwa baadhi ya taarifa za watumiaji zililazimika kuhifadhiwa nchini China, na kuongeza wasiwasi wa ufuatiliaji wa taarifa za watumiaji kutoka kwa hasimu wa Marekani kibiashara: Serikali ya China.

Kuongeza pilipili juu ya kidonda, siku ya Jumapili, mtandao wa Bloomberg ulithibitisha kuwa tovuti isiyokuwa rasmi ilikuwa ikikomba na kuunganisha sauti kutoka katika mtandao wa Clubhouse na kuzipeleka katika programu tumishi ya Android isiyokuwa imerasmishwa kutumiwa na Clubhouse, hivyo kuwawezesha watumiaji wa Android kusikiliza majadiliano ya mtandao huo kama watumiaji wa iOS. Tovuti hiyo, ilibainika, haikuwa na nia mbaya, ilikuwa tu na lengo la kutaka mtandao huo upatikane kwa watumiaji wengi zaidi!

Matukio kama hayo yanauweka mtandao huo katika utata kuhusu usalama wake. Mitandao kongwe kama Facebook, licha ya kuwa na changamoto za mara kwa mara za kiusalama, imeboresha jinsi inavyolinda taarifa za watumiaji wake inazomiliki.

Mtandao wa Clubhouse umekumbana pia na ukosoaji wa kiwango cha taarifa kinachokusanywa kutoka kwa watumiaji. Mtandao huo unapendekeza kuruhusu kukusanya taarifa za namba za watu zilizohifadhiwa kwenye simu yako (contact list) ili kuweza kukusaidia kupendekeza watu unaoweza kuwafahamu waliopo katika mtandao huo au kuwaalika watu wengine. Baadhi ya watumiaji wameonesha wasiwasi wao kuhusu utoaji wa taarifa hizo kutokana na kuwa programu hiyo inakupa mapendekezo ya watu wa kuwaalika kutokana na watumiaji waliopo kwenye simu yako ambao wapo pia katika simu za watumiaji wengine wa mtandao huo. Kwa lugha rahisi ni kuwa kama wewe na rafiki zako mnaenda kwa kinyozi mmoja, au daktari mmoja, au mfanyabiashara mmoja wa mihadarati, wote wanaweza kujitokeza kama watu ambao wanapendekezwa uwaalike.

Licha ya kukabiliana na changamoto hizi za kiusalama, Clubhouse inaendelea kuboresha kiwango chake cha usalama. Baada ya kuibuliwa kwa tuhuma za kuhifadhi taarifa nchini China, mtandao huo umetangaza kubadili njia za uhifadhi wake na kusema unaacha kupitisha taarifa zake nchini China na kuwa utaongeza kiwango cha usalama. Kuhusu tovuti iliyokuwa ikitumia taarifa za mtandao huo kwa watumiaji wa Android, Clubhouse imesema imeifungia moja kwa moja tovuti hiyo na itaongeza njia za kuzuia tukio kama hilo kutokea tena.

Watafiti wanasema Mtandao huo bado una safari ndefu ya kiusalama na kuwaridhisha watumiaji wake kuhusu taarifa zinazokusanywa na jinsi zinavyohifadhiwa. Changamoto za kiusalama za mtandao huo bado zinazidi kuibuliwa ikiwamo kukosekana kwa mfumo wa usimbaji fiche wa mwisho hadi mwisho (end-to-end encryption) kulinda mawasiliano ya watumiaji, na uwezekano wa kurekodiwa kwa mazungumzo katika majukwaa ya mawasiliano. Zaidi, mtandao huo hauna njia za wazi za kukabiliana na mijadala yenye ubaguzi au chuki, licha ya kuweka sera kupinga mijadala ya aina hiyo. Wataalamu wa usalama wanapendekeza kutumia mtandao huo kwa tahadhari ukiwa unaelewa madhara yanayoweza kukupata kutokana na kutumia mtandao huo!

- Wired
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom