ARUSHA PRESS CLUB (APC)
P.O BOX 6011
ARUSHA, TANZANIA
TEL; 0713-231752 / 0754-299861
Email;arushapressclub@gmail.com
TAMKO LA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA ARUSHA (APC) JUU YA TUHUMA ZA WIZI WA LAPTOP KWA MWANDISHI MAGESA H. MAGESA.
CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), kinawajulisha waandishi wa habari mkoa wa Arusha, wadau na jamii kwa ujumla kuwa kina laani vikali kitendo kilichofanywa na mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti la Majira Magesa H Magesa kujaribu kwa nia ovu iliyo kinyume na misingi ya taaluna ya habari na sheria za nchi kuchukua LAPTOP isiyokuwa mali ya kwake kwenye semina ya Tanzania Public Health Association TPHA iliytofanyika Corridor Spring Hoteli mjini Arusha,Novemba 29,mwaka huu.
Kitendo hicho kimeidhalilisha, kimesikitisha na kimeiabisha tasnia nzima ya habari si mkoani Arusha tu bali nchi nzima kwa ujumla wake. Hivyo basi APC kinapenda kuomba radhi kwa wadau wote walioguswa na tukio hilo kwa namna moja au nyingine.
Ieleweke kwamba APC haihusiki kwa namna yoyote ile na uovu uliokithiri wa baadhi ya waandishi wa habari na kamwe haitafumbia macho masuala kama hayo.
Kwa mujibu wa Katiba yake, APC itawatetea, kuwalinda na kuwapigania wanachama wake watakao nyanyaswa, kuonewa na kubugudhiwa wakati wa utendaji wa shughuli halali za kitaaluma na nyingine za kijamii na si vinginevyo.
Kwa misingi hiyo basi, na kwa kufuata Katiba ya APC, Kamati Kuu ya APC baada ya kupokea taarifa hizo na kujadili kwa kina tukio hilo ovu,na kwa kutumia kipengele cha 3 (c) cha Mamlaka na mipaka ya Kamati ya Haki,meamua kusitisha uanachama wa Magesa H. Magesa kwa muda hadi hapo uchunguzi wa tukio hilo, unaohusisha vyombo vya dola, utakapokamilika.
Katika kipindi hicho Magesa H. Magesa amevuliwa uanachama wa APC kwa mujibu wa Katiba ya Chama, na hata ruhusiwa kujihusisha na jambo lolote linalohusiana na APC.
APC inapenda kuchukua nafasi hii kuwaonya wanachama wake wenye tabia zinazokinzana na uandishi wa habari,na zenye dalili za makosa ya jinai kuwa haitasita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watakaothibitika kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na kuwafukuza uanachama kwa mujibu wa Katiba.
Aidha, APC inawaomba wadau wote wa sekta ya habari mkoani Arusha kutoa ushirikiano wa dhati kwa APC ikiwa ni pamoja na kuwaripoti chamani mara moja waandishi wote watakao kuwa na tabia hizo ikiwa ni pamoja na wale wanaovamia mikutano, semina na shughuli nyinginezo bila ya kualikwa.
Daima tutashirikiana na wadau wote wa habari katika kuhakikisha kuwa fani ya uandishi wa habari mkoani Arusha inaboreshwa kwa manufaa ya jamii nzima
Eliya Mbonea
Katibu Mkuu-APC
December 2, 2010
Nakala .
UTPC
RPC -Arusha
RC -Arusha
DC -Arusha
MCT
Gazerti la Majira
Jukwaa la Wahariri