Chukua tahadhari unapopokea simu za watu usiowajua/kutoka namba ngeni

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,799
Kuwa makini unapopokea simu za watu usiowajua.jpg


Ulaghai wa simu ni jambo ambalo hadithi zake tunazisikia kila siku toka kwa watu wanaotuzunguka. Mara nyingine, sisi wenyewe tunajikuta tukiwa waathirika. Ulaghai huu unaweza kumgharimu mlengwa kwa kiasi kikubwa, wakati mwingine hata akiba ya maisha.

Kwakuwa sote tunatumia vifaa hivi kama sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku, ni vema kujua aina za ulaghai wa simu na jinsi ya kuepuka.

Unahitaji kuwa mwangalifu unapopokea simu kutoka namba usizozijua. Ukipokea simu au SMS kutoka kwa namba usiyoijua, jambo bora zaidi unaloweza kufanya ni kutofuata maelekezo yoyote, hasa ikiwa unatakiwa kutoa taarifa binafsi na/au za kifedha.

Mojawapo ya ishara za kukujuza unazungumza na mtu anayedhamiria kukulaghai ni pale anapokushinikiza kufuata maelekezo yake haraka na kutomshirikisha mtu mwingine mazungumzo hayo.

Mbinu nyingine wanayotumia walaghai hujifanya kuwa maafisa kutoka serikalini, watoa huduma fulani wanaokupa taarifa muhimu ya zawadi (bonus), maafisa kutoka vyombo vya usalama n.k. Wengine hudai kuwa wanatoka kampuni fulani ya simu au benki na wanahitaji taarifa au kufikia akaunti yako kama sehemu ya huduma kwako.

Wakati mwingine huenda wakajifanya wanakufikishia taarifa mbaya kama vile kudaiwa kodi, tatizo kwenye akaunti yako au mkopo. Na mara nyingi hata iwe ni suala gani, huwa wanasisitiza kuwa tatizo linaweza kutatuliwa ikiwa tu, utatoa taarifa zako au utafanya malipo ya haraka.

Bila ufahamu kidogo wa usalama katika zama za teknolojia, inaweza kuwa changamoto kutambua ulaghai huu.

Hata hivyo, muhimu ni kuthibitisha kwanza utambulisho wa mtu unayezungumza naye kabla ya kujibu maswali yake. Walaghai kwa kawaida hukwepa ikiwa utajaribu kuwauliza uthibitisho.

Katika hali hiyo, jaribu kuomba nambari ya kampuni anayodai anatokea na kisha fanya utafiti kujiridhisha uhalali wake. Kwa mfano, umepigiwa simu kuwa mwanao aliye shule fulani ni mgonjwa na anahitaji matibabu ya haraka hivyo utume pesa chap chap. Ni vema kuhakikisha unawasiliana na shule husika ili kuthibitisha ukweli wa taarifa hiyo.

Utajua ikiwa aliyekupigia simu hatokasirika kwakuwa umemuuliza maswali na kumtilia shaka. Lakini pia, ikiwa ana dhamira njema hatoonesha kukasirika unapoamua kutotoa taarifa zako.

Jambo la msingi ni kwamba sote tunapaswa kuwa makini na simu tunazopokea kutoka kwa watu tusiowajua. Haiwezekani kabisa kwamba mtu fulani “mwenye upendo sana” atakupigia simu na kukupa mamilioni ya pesa bila sababu.

Ulaghai wa simu mara nyingi hutegemea watu kutoa taarifa zao kwa urahisi. Hivyo basi, kwa kubadilisha tu tabia zako za kawaida unaweza kuzuia kuwa mwathirika wa matukio hayo.

Kufahamu udhaifu wa kiusalama na aina ya ulaghai unaoendelea kunaweza kupunguza uwezekano wa kutapeliwa.

Tujihadhari na utapeli. Upo kila mahali, na kuna uwezekano kwamba unaweza kupata simu kadhaa kila siku ambazo zinalenga kukulaghai. Usiruhusu kupoteza jasho lako kiulaini. Ni haki yako kulinda taarifa zako endapo hujajiridhisha kuhusu usalama wako na mali zako.
 
Asante kwa elimu hii kiongozi kwa kweli umakini unahitajika sana kwenye jambo hili
 
Siogopi simu yoyote, maongezi yataniongoza kujua nadili na nani…. siwezi kupigwa.
Mkuu tapeli ni sawa na shetani hana rangi.

Ukiwa mjanja mjanja sana, wakikuamria hauwakwepi.

Siyo kwa simu tu, hata katika angle zingine tena kwenye udhaifu wako ndipo utaponasika.

Zamani nilijiamini kama wewe,lakini nilipokuja kutapeliwa kitu chenye thamani ndogo sana, toka kwa mtu nisiyemtegemea, tena kwa mtego unaotengulia kirahisi, nikaja kukubali kuwa nimetapeliwa kwa haki!
 
Lkn hili swala mm binafsi nawatupia polic , mitandao ya cm na tcra hivi kweli hawa wameshindwa kutatua tatizo, nn maaana ya kutumia kitambulisho cha taifa? Ina kupitia hivyo kila mteja taarufa zao wananzo kwnnn wasiwamate?

Sent from my SM-A032F using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom