figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,658
- 55,484
Watu sita wamejeruhiwa baada ya chui kuvamia shule moja iitwayo Vibgyo nchini India na kuwajeruhi vibaya watu hao waliojaribu kumdhibiti.
Tukio hilo limetokea katika jiji la Bangalore nchini humo ambalo hivi karibuni liliwekwa kwenye vichwa vya habari duniani baada ya baadhi ya wakazi wa jiji hilo kumvamia na kumdhalilisha mwanafunzi wa kike Mtanzania anayesoma nchini humo.
Vipande vya video vilivyonaswa na kamera za usalama katika shule hiyo zimemuonesha chui huyo akipambana vikali na mtu mmoja aliyejaribu kumdhibiti ili asimdhuru akijaribu kupanda uzio wa shule hiyo bila mafanikio.
Mtu huyo ambaye alionekana kuyapigania maisha yake kwa kila namna aliokolewa baadae akiwa na majeraha ya kung’atwa na chui huyo mikononi. Chui huyo alitembeza meno yake kwa kila aliyekutana naye katika eneo la shule hiyo.
Kwa bahati nzuri, alidhibitiwa baadaye na maafisa wanyama pori waliofika katika eneo hilo na kumrudisha porini.
Afisa wa wanyama pori, Ravi Ralph aliiambia BBC kuwa chui huyo huenda alitoka kwenye msitu ulio karibu.
Sensa ya wanyama pori iliyofanywa hivi karibuni nchini India, inaonesha kuwa nchi hiyo ina idadi ya chui kati ya 12,000 na 14,000.