Jaji mstaafu awaonya wanaotaka kumshtaki aliyewaita mafisadi
Na James Magai
Mwananchi 01-10-2007
Na James Magai
WAKATI viongozi mbalimbali wa Serikali waliotuhumiwa kwa ufisadi na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Willibrod Slaa wakitishia kwenda mahakamani, Jaji Mark Bomani amewaonya viongozi hao kutokuchukua hatua hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Jaji Bomani alisema wale wote waliotuhumiwa katika kashfa ya ufisadi na rushwa wanapaswa kufikiria upya kama kuna ulazima wa kwenda mahakamani kabla ya kuchukua hatua hiyo kwani kufanya hivyo kunaweza kuibua mambo mengine mazito na kuzusha mfarakano nchini.
"Malumbano juu ya suala la rushwa na ufisadi nchini yamepamba moto na yanaweza yakafikia kiwango cha kuleta mfarakano na uhasama katika jamii. Kutokana na hali hii maombi yangu ni kwamba tuwe na uvumilivu wa kisiasa na ninawaomba ndugu zangu wanaotishana kushtakiana mahakamani wafikirie upya ulazima wa kufanya hivyo," alitahadharisha Jaji Bomani.
Alisema kabla ya kuchukua hatua ya kwenda mahakani, wote waliotuhumiwa wanapaswa kuchukua muda wa kutosha kufikiri ili kupisha joto la malumbano lipite ndipo wafikirie kuchuka hatua zaidi.
"Yawezekana wamefikia hatua hii kutokana na ughafla wa jambo lenyewe na hivyo wanaweza kutoa kauli za haraka haraka kwa sababu ya kukasirishwa, lakini pengine kuna njia nyingine ambazo wangeweza kuzitumia kumaliza suala hilo pasipo kupelekana mahakamani, " alishauri Jaji Bomani.
Alionya kuwa kupelekana mahakamani kuna athari kubwa na kwamba kunaweza kuibua mambo mengine makubwa zaidi na hivyo akatoa ushauri kuwa kabla ya kuchukua hatua hiyo, wahusika wapeleka malalamiko yao katika taasisi nyingine kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Alisema ametoa tahadhari hiyo kutokana na uzoefu wake katika mambo ya sheria na kwamba hata wateja wake ambao wanamfuata katika kazi yake ya uwakili kwa nia ya kwenda mahakamani kuhusiana na suala hilo, huwa anawashauri kwanza kutafuta suluhu kwa vile anajua suala la kwenda mahakamani kwa kukurupuka lina athari zake.
Hata hivyo, Jaji Bomani, alisema madai ya kuwepo kwa rushwa na ufisadi nchini si jambo la kushangaza, kwani vitendo hivyo vipo pamoja na kuwa havikubaliki katika nchi inayoamini katika usawa wa binadamu na utawala bora.
"Kwa hili nakubaliana na Jaji Warioba kuwa kazi kubwa mbele yetu ni kuendeleza nchi yetu ili itufikishe kwenye maisha bora kwa kila Mtanzania. Nguvu zote za taifa zinatakiwa zielekezwe kwenye jambo hili na malumbano yote yanayoweza kuyumbisha jitihada hizi hayana budi yaepukwe," alisema Jaji Bomani.
Kuhusu tuhuma zinazotolewa na vyama vya upinzani juu ya baadhi ya viongozi wa serikali kujihusisha na rushwa na ufisadi, Jaji Bomani alisema vyama hivyo vina uhuru wa kutoa maoni yao, lakini akasema shutuma zinazotolewa ni za jumla jumla mno kiasi kwamba hazibainishi ni jinsi gani viongozi hao wamehusika katika rushwa na ufisadi huo.
Mwananchi 01-10-2007