Chonde chonde madaktari, serikali tuepusheni na hili

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,314
33,108
KATUNI(648).jpg

Maoni ya katuni


Kuna kila dalili kwamba madaktari wa hospitali za umma wataanzisha mgomo mwingine kesho kama hatua za haraka hazitachukuliwa kuzuia hali hiyo kutokea. Uwezekano huo unatokana na ukweli kwamba tarehe ya mwisho ya kutimizwa kwa madai iliyowekwa imepita na wenyewe wametangaza kuwa wataanza mgomo mkubwa kesho.

Ni jambo la kusikitisha kwamba baada ya madhara ya mgomo uliodumu kwa takribani mwezi mzima kati ya Januari na Februari mwaka huu, idadi ya vifo na madhara mengine ya kisaikolojia kwa wagonjwa na ndugu zao, kesho wananchi wanaopata huduma katika hospitali za umma watajikuta katika hofu ya kukumbwa tena na masahibu yale yale, kisa, kutokukamilika kwa makubaliano ya serikali na madaktari.
Tunasema kwa uwazi kabisa, si haki na kwa kweli haionyesha uwajibikaji wa kweli kwa upande wa serikali katika kushughulikia madai ya madaktari kama ambavyo walikubaliana wakati wamekutana na Waziri Mkuu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kukubaliana kusitisha mgomo na hivyo kuafikiana kushughulikia madai yao hadi ifikapo Machi 3, mwaka huu.
Kamati iliyokuwa imeundwa ilijua wazi kwamba ilitakiwa kufanya kazi kwa kipindi husika ili ifikapo tarehe ya mwisho kila kitu kiwe tayari.
Ukitafakari kwa kina wanaoathirika na mgomo wa madaktari katika hopitali za umma, ni wananchi wa kawaida sana ambao aghalab hawana uwezo kulipia huduma hizo kwenye hospitali kubwa za binafsi; hawa ndiyo wapiga kura hasa, hawa ndiyo wenye nchi na kimsingi ni walengwa namba moja wa huduma za afya zinazotolewa na hospitali ya umma.
Kama ambavyo kwenye mgomo wa awali walioathirika baada ya hopsitali kubwa za umma kama Muhimbili, MOI, Ocean Road, KCMC, hospitali za manispaa za jiji la Dar es Salaam za Amana, Temeke Mwananyamala; Bugando, hospitali za mikoa za Dodoma na Mbeya, kusitisha huduma au kusuasua kutokana na uhaba wa madaktari, na safari hii ni wananchi wa kawaida kabisa.

Ni kwa maana hiyo tunasema si sawa hata kidogo mchezo huu baina ya madaktari na serikali kuachwa uendelee tu hivi hivi bila hatua za haraka kuchukuliwa. Tunasema ni mchezo kati ya serikali na madaktari kwa sababu ndio wahusika wakuu katika mgogoro huu wa kitabibu nchini.

Serikali inatambua kuwa ina wajibu wa kutekeleza madai ya madaktari kama walivyokubaliana, kwanza kwa kutazama ni mambo gani katika madai yao yanaweza kutekelezwa katika kipindi cha muda mfupi na kwa haraka bila kuathiri kwa kiwango kikubwa mahitaji mengine ya serikali katika maeneo mengine.
Inavyoonekana, serikali imeshughulikia suala la nyongeza ya posho tu, lakini madai mengine ya mazingira ya kazi kwa madaktari kwa maana ya kuwapo kwa vifaa vya kitabibu bado hatua za maana na za kuridhisha hazijachukuliwa kabisa.
Madaktari wangali wanalalamika kuwa wagonjwa wanawafia si kwa sababu hawana uwezo wa kuwasaidia, ila kwa sababu hakuna vifaa vya kitabibu vya kukabiliana na shida mbalimbali za wagonjwa. Tunaamini huu ni udhaifu wa hali ya juu kwa upande wa serikali.
Tunafikiri kuendelea kuvuta miguu kwa upande wa serikali katika kutekeleza madai ya madaktari kama vile kuondoa viongozi wanaodhaniwa kuwa ni vikwazo kwenye wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, hatua ambayo pengine ingejenga moyo wa kuaminiana na kuvumiliana baina ya madaktari na serikali kwani ikionekana kuwa tangu mwanzo kushindwa kwao kuwajibika vilivyo ndiko kulikoumua mgomo huo hadi kufikia hatua iliyoshuhudiwa mwezi uliopita, ni kutafuta janga.
Tunafahamu madaktari wana machungu mengi, kubwa kwa kushindwa kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao kwa maana ya kukosekana kwa vifaa na dawa katika kuwahudumia wagonjwa, lakini pia kwa kuamini kwamba serikali imekataa au inachelea kuwaondoa viongozi wakuu wa wizara ambao wanafungamanishwa na uzembe unaotokea katika sekta ya afya, pamoja na machungu hayo, sisi tunaamini kuwa bado wana nafasi ya kutoa muda zaidi kwa madai yao kuendelea kushughulikiwa.

Tunaposema madaktari wawe na subira hatumaanishi kwamba madai yao hayana msingi, au hatusemi hivyo kuinga serikali mkono kwa kuendelea kuvuta miguu, ila ni katika kutafakari na kutambua kuwa hakika wanaoumia hapa wala si viongozi wa serikali bali ni wananchi wa kawaida kabisa kwa kukosa huduma za afya.
Ni kwa maana hiyo tunawaomba madaktari wawe na uvumilivu kidogo katika mchakato mzima wa kushughulikiwa kwa madai yao, nia ikiwa ni kuwasaidia wananchi. Wakifanya hivyo wataokoa roho za wananchi zaidi.
Tunaomba haya kwa kuwa uzoefu wa mgomo uliopita ulionyesha jinsi serikali kwa maana ya viongozi wakuu walivyoepuka madhara ya mgomo huo kwa kuwa wengi hawatibiwi katika hospitali za umma na wana nguvu ya kufuata huduma hizo hospitali binafsi.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom