Na Caroline Nassoro
Mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC utafanyika tarehe 16 Oktoba hapa Beijing. Lakini kabla ya kufanyika kwa Mkutano huo, ikiwa sasa watu wa China wanakuwa katika mapumziko ya siku saba ya kusherehekea miaka 73 ya kuzaliwa kwa taifa la China, siku ya taifa inayoangukia tarehe mosi, Oktoba, tuangazie mafanikio ambayo China imeyapata katika miaka hii 10 tangu Xi Jinping achaguliwe kuwa katibu mkuu wa Kamati Kuu ya CPC, leo hii tukiangazia suala la ujenzi wa miundombinu.
China ni nchi iliyopata maendeleo makubwa katika sekta ya ujenzi wa miundombinu, si tu ya barabara, bali pia reli, bandari, viwanja vya ndege na madaraja. Tukitolea mfano wa daraja linalounganisha mikoa ya Hong Kong na Macau na jiji la China bara la Zhuhai, ambalo lilizinduliwa Oktoba mwaka 2018 na rais wa China, Xi Jinping. Daraja hilo lina urefu wa kilomita 55 na ujenzi wake uligharimu dola za kimarekani bilioni 20. Takriban kilomita 30 za daraja hilo zimepitia baharini kwenye mlango wa Mto Pearl.
Mwaka uliofuata mwezi Septemba, uwanja mpya wa kimataifa wa ndege ulifunguliwa mjini Beijing. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Daxing una ukubwa wa mita 700,000 za mraba, ambazo ni sawa na ukubwa wa viwanja 98 vya soka.
Si hayo tu, China pia imepata maendeleo makubwa katika miundombinu ya mawasiliano, ambapo teknolojia ya mtandao wa 5G inaongoza kwa kutumiwa na wananchi wengi. Idadi ya vifaa vilivyounganishwa kwenye mtandao wa 5G nchini China pia imezidi milioni 310, na kuchukua zaidi ya asilimia 80 ya jumla ya dunia nzima.
Mapema mwezi Machi mwaka huu, gazeti la The Wall Street la Marekani lilisema kuwa, China inaongoza duniani katika kujenga miundombinu ya mtandao wa 5G, hasa kutumia teknolojia hiyo katika viwanda, migodi ya makaa ya mawe, viwanda vya meli na maghala.
Gazeti hilo lilisema, China inaonekana kuongoza katika kutumia mtandao wa 5G wenye uwezo mkubwa katika maeneo mengi ya viwanda, ambao unalenga kutumia teknolojia hiyo kusaidia kujiendesha katika viwanda vinavyohitaji watu wengi na michakato ya hatari ya viwanda, na kutarajia kuongeza uwezo wa uzalishaji.
Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China imesema, mpaka kufikia mwezi Julai mwaka huu, idadi ya watumiaji wa simu za 5G nchini China ilifikia milioni 475. Pia Wizara hiyo imesema, hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai, China ilikuwa imejenga takribani vituo milioni 1.97 vya msingi vya 5G, kwa miji yote ya ngazi ya wilaya, kaunti na asilimia 96 ya majiji yalikuwa na mtandao wa 5G.
China inaendelea kutoa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu mipya ya mitandao ya 5G, na juhudi pia zinafanywa ili kupanua wigo wa mitandao ya hali ya juu hadi maeneo ya vijijini, na kupanua kikamilifu matumizi ya njia mpya za biashara katika maeneo ya vijijini.
Kutokana na hayo, ni wazi kuwa, China imepata maendeleo makubwa katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege, lakini pia imepata maendeleo makubwa katika sekta ya miundombinu ya mawasiliano kupitia teknolojia ya mtandao wa 5G.