Mwezi Agosti mwaka 2021, China ilizindua Mpango wa China na Afrika wa Kujenga Jumuiya yenye mustakbali wa pamoja kwenye mambo ya mtandao wa internet, na kuwa jukwaa la kwanza la Maendeleo na Ushirikiano kwenye mambo ya mtandao wa Internet kati ya China na Afrika. Ushirikiano huo ni mwendelezo wa juhudi ambazo tayari zimefanywa kati ya pande mbili, kuwawezesha watu wa Afrika kuwa na huduma ya Internet.
Tehama ni moja kati ya sekta zenye maendeleo ya kasi kwenye nchi za Afrika. Licha ya maendeleo yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kufikisha mkonga wa mawasiliano (optic fibre) katika sehemu nyingi na kuongezeka kwa watu wanaotumia internet kwa njia ya simu na internet, usalama wa internet bado ni eneo ambalo nchi nyingi za Afrika ziko nyuma.
China ambayo jamii yake kwa kiwango kikubwa imeunganishwa na mtandao wa internet, imepitia changamoto mbalimbali za kiusalama kwenye eneo hilo na sasa kimsingi mtandao wa internet wa China ni safi. Kwenye nchi za Afrika changamoto kama ukatili wa kimtandao, wizi wa kimtandao, habari za kupotosha na za uzushi zinazoleta taharuki, na hata wizi wa pesa zimekuwa zinajitokeza mara kwa mara.
Wakati huo huo nchi nyingi za Afrika zinatambua umuhimu wa mtandao wa internet kwenye maswala ya uchumi, kwa hiyo zimekuwa zikihimiza maendeleo ya uchumi wa kidigitali. Kutokana na mahitaji ya maendeleo katika eneo hilo, kwenye mkutano wa Mawaziri wa Kuratibu Utekelezaji wa Hatua za ufuatiliaji na Ushirikiano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (2025-2027) uliofanyika mwaka jana, China ilitangaza kuwa iko tayari kutoa msaada na kushirikiana na nchi za Afrika kuendeleza mtandao wa internet ulio wa haki, wenye usawa, wazi, jumuishi, salama na thabiti zaidi, na kuharakisha juhudi za kujenga Jumuiya yenye mustakbali wa pamoja kati ya China na Afrika kwenye masuala ya mtandao wa Internet.
China ilitangaza kuwa tayari kushirikiana na nchi za Afrika katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa vifaa vya mawasiliano na kufanya mawasiliano na ushirikiano mkubwa zaidi na wenzao wa Afrika, na kuwezesha makampuni yenye uwezo ya China kuwekeza kwenye maendeleo ya miradi ya mikonga ya mawasiliano kwenye baharini za kimataifa barani Afrika. Makampuni hayo pia yatahimizwa kufanya kazi na watoa huduma za mawasiliano wa Afrika katika usambazaji wa huduma ya 5G.
Katika hatua nyingine China pia ilitangaza kuwa itaunda “mtandao wa Ushirikiano wa Makampuni ya Internet ya China barani Afrika” ili kuruhusu makampuni zaidi ya internet ya China kupanua biashara zao za ushirikiano barani Afrika, ili kuweka jukwaa la mawasiliano kati ya makampuni ya internet kutoka pande zote mbili kwa ajili ya kubadilishana na ushirikiano wa kina wa internet kati ya China na Afrika.
Mbali na hayo, China pia iko tayari kufanya kazi na nchi za Afrika kupanua ushirikiano wa “Njia ya Hariri ya Biashara ya Mtandao wa Internet” ili kuanzisha mfumo wa ushirikiano wa biashara ya mtandao wa internet. Ikiwa ni sehemu ya juhudi hizo, China imefanya aina mbalimbali za sherehe za ununuzi wa bidhaa bora za Afrika na shughuli za kuhimiza biashara ya utalii.