#COVID19 China kuisaidia Kenya kutoa chanjo kwa watu milioni 19 ifikapo Juni 2022

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
1644544472995.png


Na Tom Wanjala

Serikali ya Kenya imesema iko mbioni kutoa chanjo dhidi ya virusi vya Corona kwa Wakenya wasiopungua milioni 19 ifikapo mwezi Juni mwaka huu. Taarifa hii inakuja wakati ambapo Wakenya wengi wanazidi kujitokeza katika vituo vya utoaji chanjo kufuatia serikali kuhamasisha kuwa kila mtu anatakiwa kupata chanjo hiyo.

Kenya imepokea misaada ya chanjo kutoka kwa mataifa mbalimbali kama vile China, Marekani, Uingereza na mashirika mengine ya kimataifa.

Akigusia ushirikiano wa China na Kenya katika vita dhidi ya virusi vya Corona, Mwenyekiti wa jopokazi la kitaifa la chanjo dhidi ya virusi vya Corona nchini Kenya, Bw Willis Akhwale anasema, China imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya Kenya, haswa katika utoaji wa chanjo ya virusi vya Corona. Akirejelea ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Chjina Wang Yi nchini Kenya mapema mwaka huu, Akhwale anakiri kuwa Kenya itafaidika mno na ahadi ya mchango wa dozi milioni 10 za chanjo ya Corona kutoka China.

‘Tungependa kushukuru sana China kwa kuendelea kusimama na sisi katika safari hii ya kupambana na janga la virusi vya Corona. Ahadi ya msaada wa dozi milioni 10 ya chanjo kutoka kwa China, itapiga jeki juhudi zetu za kuchanja watu milioni 19 ifikapo mwezi Juni mwaka huu,’ anasema Akhwale.

Aidha tayari Wizara ya Afya ya Kenya imezindua harakati kubwa ya chanjo, ikilenga kuwafikia angalau watu milioni moja kila siku ndani ya wiki mbili.

Akizungumza wakati akizindua zoezi hilo jijini Nairobi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisisitiza kuwa, chanjo imesalia kuwa ya hiari, ingawa wanaotafuta huduma za serikali lazima wapewe chanjo.

‘Hatulazimishaimtu kuchanjwa. Lakini ukijua hujachanjwa, tafadhali usitangamane na watu wengine. Chukua tahadhari,’ alisisitiza waziri Kagwe.

Kuhusu jinsi chanjo kutoka China itakavyosambazwa, Willis Akhwale, anasema kwamba wanaopewa kipaumbele ni wafanyikazi walio kwenye hatari ya kuambukizwa au kusambaza virusi hivi, ambao ni pamoja na walimu, maafisa wa afya, na wale wanaoishi na maradhi mengine.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Kenya, zaidi ya asilimia mia moja ya wahudumu wa afya tayari wamepata chanjo dhidi ya virusi vya Corona, na sasa wito unatolewa kwa walimu wote nchini Kenya kujitokeza kupewa chanjo hii.

Kwa mujibu wa Akhwale, takriban asilimia 90 ya walimu nchini Kenya wamepata chanjo kamili dhidi ya COVID-19. Anaongeza kuwa msaada wa chanjo kutoka China utasaidia kuhakikisha kuwa walimu wengi wanachanjwa.

Kulingana na Wizara ya Afya, walilenga kuwachanja walimu 480,681 na asilimia 89 kati yao tayari wamepata chanjo hiyo. Kenya ina takriban walimu 500,000 katika shule za binafsi na za umma.

Kati yao, 370,000 wameajiriwa na serikali katika shule za chekechea, msingi na sekondari za umma. Kufikia katikati ya Agosti 2021, kulingana na Wizara ya Afya, ni asilimia 33 tu ya walimu waliokuwa wamechanjwa kikamilifu dhidi ya COVID-19.

‘Kupata msaada wa dozi milioni kumi za chanjo dhidi ya virusi vya Corona, kutapunguza pengo kubwa sana kati ya wale waliochanjwa na wale ambao hawajachanjwa. Tunashukuru sana China kwa kuendelea kusimama nasi,’ anasema Akhwale.
 
Back
Top Bottom