China itaendelea kushirikiana na Afrika kupambana na malaria baada ya kuidhinishwa na WHO kuwa nchi isiyo na ugonjwa huo

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,006
1,026
VCG111327159511.jpg

Mapema wiki hii mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani WHO Bw. Tedros Ghebreyesus aliitangazia dunia kuwa China imetokomeza ugonjwa wa Malaria. Taarifa iliyotolewa na WHO inasema Bw. Tedros amepongeza mafanikio hayo ambayo ametaja kuwa yamepatikana kutokana na kazi ngumu iliyofanyika kwa zaidi ya miaka 70.

Pamoja na kuwa ni wiki hii China imetangazwa kupata cheti cha kutokomeza ugonjwa wa Malaria, ukweli ni kuwa China ilitokomeza Malaria mapema zaidi. Mwaka 2020, baada ya kuripoti miaka minne mfululizo ya kutokuwepo kwa mgonjwa wa malaria, China iliomba idhini rasmi ya WHO ya kupata cheti hicho. Jopo huru la kuthibitisha lilifanya safari ya ukaguzi mwezi Mei mwaka huu, ili kuthibitisha hali ya kutokuwepo kwa malaria nchini China, na kukagua uwezo wa China wa kuzuia kurudi tena kwa Malaria. Jopo hilo liliidhinishwa kutolewa kwa cheti hicho baada ya kuridhdika.

China ni nchi ya kwanza katika Kanda ya Pasifiki ya Magharibi ya WHO kupewa cheti cha nchi iliyotokomeza malaria katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu. Nchi nyingine katika kanda hii zilizopata cheti hicho ni pamoja na Australia iliyopata cheti hicho mwaka 1981, Singapore mwaka 1982 na Brunei Darussalam mwaka 1987.

Kama alivyosema Bw. Tedros mafanikio ya China katika kutokomeza Malaria hayakupatikana kwa urahisi, kwani yanatokana na juhudi za miaka ya 50 zikihusisha wataalamu wengi na raslimali nyingi. Mwaka wa 1967, Serikali ya China ilizindua "Mradi namba 523" ambao ulikuwa ni mpango wa utafiti wa taifa wenye lengo la kupata matibabu mapya ya malaria. Wanasayansi 500 kutoka taasisi 60 walifanya kazi kwa kushirikiana, mafanikio ya awali yalipatikana kwenye miaka ya 70, baada ya kugunduliwa kwa mmea wa artemisinin – ambao umekuwa ni msingi wa dawa bora ya malaria inayotumiwa leo duniani.

Katika miaka ya 1980, China ilikuwa moja ya nchi za kwanza duniani kujaribu matumizi ya vyandarua vyenye dawa (ITNs) kama moja ya njia za kuzuia malaria, baadaye njia hiyo ilipendekezwa na WHO kuwa ni moja ya njia zenye ufanisi katika udhibiti wa malaria. Hadi kufikia mwaka 1988, vyandarua milioni 2.4 vilikuwa vimesambazwa kote nchini China, na kuonyesha ufanisi mkubwa kwenye kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo katika maeneo vilikopelekwa.

Mwisho wa 1990, idadi ya wagonjwa wa malaria nchini China ilikuwa imepungua hadi kufikia laki 1.17, na vifo vilipunguzwa kwa 95%. Kwa msaada kutoka kwa Mfuko wa Ulimwenguni wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, kuanzia mwaka 2003, China iliongeza mafunzo kwa wataalamu wake, matibabu, kuboresha vifaa vya maabara, dawa na udhibiti wa mbu, juhudi ambazo zilisaidia kupunguza zaidi wagonjwa wa malaria, na ndani ya miaka 10 idadi ya watu walioambukizwa malaria ilipungua hadi karibu 5000 kwa mwaka.

Kwa sasa China inaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali za Afrika zinazosumbuliwa na ugonjwa wa Malaria. Kupitia ushirikiano kwenye sekta ya afya, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, China imeandaa semina na programu za mafunzo kwa maofisa wa afya wa Afrika. Taasisi za afya ya umma za China kama Idara ya Magonjwa ya Vimelea (NIPD) ya Kituo cha Kichina cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) iliandaa warsha tano za mafunzo zinazohusu 'kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza' na 'Kuzuia na kudhibiti malaria na kichocho katika nchi zinazoendelea. '. Zaidi ya wataalamu wa afya 150 na maofisa wa afya kutoka nchi zaidi ya 20 za Afrika wamepata mafunzo nchini China ikiwa ni sehemu mikakati na hatua za kuzuia na kudhibiti malaria barani Afrika.
 
Back
Top Bottom