China inatoa msaada kwa nchi za Afrika, ili nchi za Afrika zisiombe msaada tena katika siku za baadaye

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,008
1,030
VCG11460419963.jpg


Fadhili Mpunji

Moja ya mada zinazojadiliwa katika uhusiano kati ya China na Afrika ni msaada. Hivi karibuni, ofisa mwandamizi wa shirika la misaada ya kimataifa la China (CIDCA) Bw. Liu Junfeng kwenye mkutano uliofanyika Beijing alieleza kwa kina utaratibu wa China katika kutoa misaada kwa nchi za nje kupitia CIDCA

Bw. Liu alikumbusha kuwa sio miaka mingi iliyopita China ilikuwa ni nchi inayopokea misaada, na alieleza jinsi China ilivyokuwa inasimamia misaada hiyo, ili kuhakikisha kuwa inakuwa msingi wa kujitegemea na kutoomba tena msaada katika siku za baadaye. Usimamizi huo umeleta matokeo yaliyotarajiwa, na sasa China sio nchi inayopokea msaada tena, bali ni nchi inayotoa misaada.

Bara la Afrika limekuwa mpokeaji mkubwa wa misaada kutoka nje. Kumekuwa na maswali yanayoulizwa na wanazuoni, ni kwanini misaada ambayo imekuwa ikitolewa kwa miaka mingi kwa nchi za Afrika haijaleta mabadiliko yoyote makubwa? Kuna sababu nyingi zilizofanya misaada inayopelekwa kwenye nchi za Afrika isiwe na ufanisi mkubwa kwenye kuleta maendeleo kwa Afrika.

Kwanza misaada mingi kutoka nchi za Magharibi, sio hisani, bali ni biashara kubwa ambayo inazinufaisha zaidi nchi zinazotoa msaada kuliko zinazopokea misaada hiyo. Jarida la The Journal la Ufaransa liliwahi kutoa makala moja inayoonesha kuwa tangu miaka ya 70 nchi za magharibi zilipoanza kutoa msaada kwa nchi za Afrika kusini mwa Sahara GDP ya nchi hizo ilipungua, lakini zilipounguza misaada GDP ilikuwa ikiongezeka. Na kibaya zaidi ni kuwa misaada hiyo huwa iliambatana na masharti ambayo yanahatarisha uhuru na hata usalama wa nchi.

Pili, nchi za magharibi zinapendelea kutoa msaada kwenye maeneo ambayo kimsingi sio msingi wa maendeleo endelevu, bali ni fursa kwao kujiwekea mazingira ya kuonekana wanahitajia zaidi na wana maana zaidi kwa wanaohitaji msaada. Mfano mkubwa unaotumiwa kuonyesha hali hii ni pale wanapoombwa kutoa msaada kwenye sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula, wanakataa, lakini wanakuwa mstari wa mbele kutoa msaada wanaposikia kuna janga la njaa, kwa kuwa kisiasa hali hiyo ina manufaa zaidi kwa nchi zao, na hata ina manufaa kiuchumi kwa watu wao.

Tatu, kwenye baadhi ya nchi za magharibi wanasiasa huvutia kura za watu kutoka watu wenye asili ya Afrika kwenye nchi zao, kutokana na ahadi wanazotoa kuhusu kusaidia bara la Afrika.

Lakini tukiangalia utaratibu wa China wa kutoa msaada uko tofauti sana na wa nchi za magharibi. Kwanza msaada unaotolewa na China hauna masharti ya kuhatarisha uhuru au usalama wa nchi zinazopokea msaada, na China imekuwa inarudia kauli hii mara kwa mara kuwa nchi inayopokea msaada haitapewa masharti yoyote.

Lakini pili China inatoa kwa mtindo wa “kumpatia mtu ujuzi wa kuvua samaki” na sio kumpatia samaki. Nchi za magharibi zinapenda kutumia mtindo wa kumpatia mtu samaki, kwa sababu samaki huyo akiisha, basi mtu huyo ataenda kuomba samaki tena, na mtoaji wa samaki ataendelea kuwa na utukufu wa kuombwa na hata kuweka masharti ya ajabu ajabu kabla ya kutoa msaada huo.

Hivi karibuni Bw. Liu Junfeng alisema China inatoa msaada kwa nchi za Afrika ili nchi za Afrika zisiombe tena msaada katika siku za baadaye. Alirudia kuwa China haisahau kanuni ya kutoa msaada kwa mtindo wa kumfundisha mtu kuvua samaki na sio kumpa samaki.

Bw John Demiyakor kutoka Ghana, anaona shirika la misaada ya kimataifa la China lina mipango mingi mizuri ya kutoa misaada kwa Afrika, lakini kwa upande wake anaona mtindo wa China wa kutoa mafunzo kwa watu wa Afrika ni njia nzuri ya kuweka msingi wa Afrika kujitegemea, na angependa sana msaada huo ufikie hatua ya kuimarisha sekta ya viwanda kwenye nchi yake ili iweze kujitegemea zaidi.

Kwenye mkutano huo, baadhi ya wanafunzi walimwuliza Bw. Liu maswali mengi ili kujua kama China imejifunza kutokana na makosa yanayofanywa na nchi za magharibi kwenye kutoa msaada. Kama vile kuwepo kwa usimamizi mbaya wa misaada hiyo. Ukweli ni kuwa sehemu kubwa ya misaada hiyo kwanza hurudi kuwanufaisha watu wa nchi zinazotoa msaada huo, na hata ukifika kwenye nchi zinazopokea msaada huo, sehemu kubwa inaishia mifukoni mwa baadhi ya maofisa, na walengwa wanapata kiasi kidogo sana ambacho hakina ufanisi mkubwa katika kubadilisha maisha ya watu.

Bw. Liu Junfeng alisema China itahakikisha kuwa misaada inayotolewa kwa nchi za Afrika, kwanza ni lazima ijadiliwe na pande mbili, na China itaridhia kutoa msaada huo kama ina uhakika ni msaada wenye manufaa kwa umma wa nchi husika. Lakini pia sasa China ina utaratibu wa kuhakikisha kuna usimamizi madhubuti ili msaada huo uwafikie walengwa, na uwe ni msaada ambao utahimiza kujitegemea na sio kuwa msingi wa kuomba msaada mwingine.

Bw. Victor Kihagi Ngatia kutoka Kenya anaona China tayari ina mwelekeo mzuri wa kutoa msaada kwa Afrika. Yeye anasema tatizo ni kuwa baadhi ya watu wa nchi za magharibi wanadhani vijana wa Afrika wanahitaji pesa, yeye anasema wanachohitaji ni kuwa na njia za wao kujiendeleza. Anasema reli ya SGR ya Kenya, au barabara zinazojengwa na China kwenye nchi za Afrika zimewapa vijana wa Kenya fursa ya kuonyesha uwezo wao wa kujiendeleza. Anaona msaada wa namna hiyo ndio unawapa vijana uwezo wa kuvua samaki na sio kuwapa samaki.
 
Afrika tutaendelea kuomba omba milele amina maana tuko proud na kuomba omba
 
Tatizo siyo misaada au mikopo tatizo ni viongozi wetu mikopo Mingi wanayopata huishia mifukoni mwao imagine mtu anakopa ili akajenge Choo cha shule au anakopa ili pesa zitumike kwenye uchaguzi wakati ivyo ni vitu ambavyo mnaweza kujiumiza wenyewe na mkavifanya viongozi wengi WA afrika hawana uchungu na nchi zao Bali wanajali familia zao na matumbo Yao Tu
 
Huyo mjumbe kutoka China kaongea vizuri Sana, lakini shida ipo kwa wapokeaji mikopo , Je Wana hiyo vision ya kubadilisha Mataifa yao kiuchumi !?
 
Back
Top Bottom