Chimbuko la Bongo Fleva, Wasanii na Makundi Yaliyowahi Kutingisha

Hashpower7113

JF-Expert Member
Sep 26, 2011
1,353
2,137
Muziki wa kizazi kipya Bongo au maarufu kama Bongo Fleva, ndiyo unaaoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi kwa sasa nchini Tanzania, hilo halina ubishi. Vijana wengi wamejiajiri kupitia muziki huu, kuna wasanii, maprodyuza na waongozaji wa video.

Japokuwa wengi wanaifurahia Bongo Fleva, ni wachache wanaojua ni wapi hasa muziki huu ulipoanzia, na ni watu gani waliovuja jasho na damu kuufanya ukubalike kwenye jamii.

Historia ya chimbuko la Bongo Fleva, inaturidisha mwanzoni mwa miaka ya tisini. Hapa tunakutana na mtu muhimu sana ambaye kama ukimuita ndiye mwanzilishi wa Bongo Fleva, utakuwa hukosei.

Huyu si mwingine bali Saleh Jabir ambaye kwa mara ya kwanza, mwaka 1991 alirekodi wimbo wa kwanza wa Hip Hop kwa lugha ya Kiswahili, uitwao Ice Ice Baby, akitumia ‘beat’ iliyotengenezwa kwa kugandamizia (sampling) beat ya msanii wa Kimarekani, Vanilla Ice.

Wimbo huo ulikuwa kama kichocheo muhimu cha kuzaliwa muziki wa Rap za Kiswahili. Ikumbukwe kwamba kabla ya Saleh Jabir hajatoa wimbo huo, walikuwepo wasanii wa Kibongo waliokuwa wakirap kwa Kiingereza, walitumia beats za Hip Hop ya Marekani na hata mashairi, wengi walikuwa wakigandamizia yale ya wasanii wa Marekani.

Wakati wimbo huo ukiwa ndiyo habari ya mjini, kulifanyika tamasha kubwa la kwanza la Rap Tanzania, lililopewa jina la Yo! Rap Bonanza lililoandaliwa na Dj Kim na The Boys Promotion, lililofanyika katika ghorofa ya saba ya Hoteli ya New Africa.

Mamia ya wasanii, hasa kutoka jijini Dar es Salaam walichuana vikali kwa muda wa siku mbili kutafuta wakali wenye vipaji, ambapo Saleh Jabir na ngoma yake ya Ice Ice Baby, aling’ara vilivyo kwenye mashindano hayo.
1063997

Saleh Jabir (kulia) akiwa na Ferouz na mdau
Ni katika tamasha hilo ndipo vipaji vingine vilipoibuka, wakiwemo wasanii kama Nigga One, Eazy B, D Rob, KBC Kibacha, Y Thang, Killa B na wengine wengi. Tamasha hili linatajwa kwamba liliweka misingi mipya ya Bongo Fleva na japokuwa nyimbo za wasanii wengi walizokuwa wakiimba zilikuwa ni katika lugha ya Kiingereza, wengi wakikopi staili za makundi ya Marekani kama Niggers With Attitude (NWA) na kadhalika, mashairi ya Kiswahili yalionesha kuwavutia watu wengi sana waliofurika kwenye tamasha hilo.

Baada ya Yo! Rap Bonanza kumalizika, wasanii waliofanya vyema kwenye mashindano hayo, waliungana na kuunda makundi mbalimbali, likiwemo Kwanza Unit, chini yake Ramadhan Mponjika ‘Chief Rhymson’ akiwa na Kibacha (KBC), D-Rob na Eazy B, baadaye wakaongezeka memba wengine kama Bugzy Malone, Papa Sav, Abbas Maunda, Baraka, Ndoti, Fresh-G, Y-Thang na Adili.

Pia lilizaliwa kundi lingine, The Diplomatz lililokuwa likiundwa na Saigon na Dola Soul (Balozi). Mbali na makundi, pia wasanii wengine walianza kufanya kazi kama ‘solo artists’, wakiwemo Joseph Mbilinyi kipindi hicho akiitwa II Proud kabla ya baadaye kuja kubadili jina na kuitwa Mr II (Sugu).

Mawingu Studio iliyokuwa chini ya Mawingu Discotheque (hivi sasa Clouds Media Group), iliyokuwa ikimilikiwa na Joseph Kusaga chini ya prodyuza Bonnie Luv, ilikuwa ndiyo studio pekee iliyokuwa ikirekodi nyimbo za wasanii. Baadaye waliibuka maprodyuza wengine kama Sound Crafters na Don Bosco.

Makundi mengi yakazidi kuibuka, wasanii nao wakawa wanazidi kuongezeka na miongoni mwa wasanii wa mwanzo kuingia studio na kurekodi, walikuwa ni Othman Njaidi, Sindila na Pamela ambao walirekodi wimbo uitwao Msela.
1064002

Joseph Kusaga (kulia), Ruge Mutahaba na Dj Mind Motion wa San fransisco

Kwanza Unit nao wakarekodi albamu yao waliyoipa jina la Tucheze, Hard Blasters Crew iliyokuwa ikiundwa na Nigger Jay (Prof Jay), Fanani na Biggy Willy nao wakarekodi ngoma iitwayo Mambo ya Mjini, Mr II akarekodi Chini ya Miaka 18 kwa prodyuza Don Bosco na kufanya muziki wa kizazi kipya wenye mashairi ya Kiswahili, uzidi kupasua anga.

Kundi la Weusi Wagumu Asilia (WWA) pia lilirekodi ngoma zao kama Rumba Kali, Sauti ya Wagumu, Twasafiri na Kua Ukomae kwa prodyuza Don Bosco, hiyo ilikuwa ni mwaka 1994.

“Kulikuwa na changamoto nyingi, nakumbuka kwa mara ya kwanza nilipoingia studio za Don Bosco na kufanya kazi na prodyuza Marlone Linje nilipata kazi kubwa. Marlone alikuwa akirekodi muziki wa injili na hakuwa akijua sana kuhusu muziki wa Rap, kwa hiyo nikawa namuelekeza kila kitu, kuanzia beats zinavyotakiwa kuwa mpaka albamu yangu ya kwanza, Ni Mimi ilipokamilika. Marlone alikuwa kama injinia wa sauti lakini prodyuza nilikuwa ni mimi, watu wengi hawakuwa wakiielewa midundo ya Hip Hop, kwa hiyo nikawa namuelekeza kila kitu,” anasema Joseph Mbilinyi (Sugu) ambaye alikuwa miongoni mwa wasanii wa mwanzomwanzo kurekodi albamu nzima.

Licha ya kurekodiwa kwa nyimbo nyingi, bado changamoto kubwa ilikuwa ni namna ya kuugeuza muziki kuwa biashara. Wengi waliichukulia Rap kama muziki wa kihuni, na hata redio zilizokuwapo kipindi hicho, ikiwemo Redio Tanzania, Radio Onena East Africa FM, hazikuwa zikipiga muziki huo.
1064005


Mapinduzi ya mwanzo, yalifanywa na msanii Mac Muga ambaye kwa mara ya kwanza katika historia, mwaka 1995 aliingiza sokoni albamu yake iliyokuwa ikiitwa The Mac Mooger na kuwapa Mamu Stores (Wahindi) kazi ya kuuza tape nchi nzima.

Baada ya Mac Muga kufanikiwa kusambaza kazi zake kwa kuwatumia Mamu Stores, wasanii wengi walipata moyo wa kukamilisha albamu na kuanza kuzisambaza kwa kuwatumia Mamu, ambapo Sugu na Kundi la Rough Niggaz lililokuwa linaundwa na Eddy T and Easy S (Steve 2k) nao waliingiza albamu yao ya Maisha sokoni mwaka huohuo, 1995.

Mpaka hapo, njia tayari ilishaanza kufunguka, wasanii wakaongeza juhudi kwa sababu sasa walikuwa na uhakika na soko la kazi zao, vituo vya redio navyo vikaanza kuutazama muziki wa Rap kwa jicho tofauti.

Kituo cha kwanza kupiga Rap za Kiswahili kilikuwa ni Radio One, na mchango wa watangazaji na Madj kama Taji Liundi, Mike Mhagama na Dj John Dilinga hauwezi kusahaulika kwani ndiyo walioupeleka muziki huo hewani kupitia vituo vya redio vya Redio One na baadaye East Africa FM.

Mike Mhagama ndiye aliyeubatiza muziki wa Rap jina la Bongo Fleva na hiyo ilikuwa ni mwaka 1996 ambapo kupitia kipindi chake cha DJ Show, mtangazaji huyo alianza kulitumia neno ‘Bongo Fleva’ akimaanisha muziki wa kizazi kipya Tanzania. Kuanzia hapo Bongo Fleva ikazidi kushika kasi, nyimbo zikawa zinapigwa redioni, albamu zinauzwa sokoni na wasanii wengi wakazidi kuikuka kila kukicha, mpaka leo hii Bongo Fleva inapopepea kimataifa.

MAKUNDI KUMI YALIYOWAHI KUTINGISHA KWENYE BONGO FLEVA

WEUSI WAGUMU ASILIA (WWA)

Achana na hawa Weusi wa Arusha, Joh Makini na wenzake. Miaka ya 1992 kulikuwa na kundi lililoitwa WWA (Weusi Wagumu Asilia) waliokuwa na makazi yao pande za Kijitonyama. Hawa ni miongoni mwa wanaharakati wa mwanzo kabisa wa Bongofleva, huku ngoma zao kama Rumba Kali, Sauti ya Wagumu, Twasafiri na Kua Ukomae zikiamsha ari miongoni mwa vijana wengi ya kuanza kurap kwa Kiswahili.

HARD BLASTERS CREW (HBC)

Hili ni miongoni mwa makundi ya mwanzomwanzo kabisa lililofanikiwa kuwa na mashabiki lukuki. Lilikuwa likiundwa na Nigger Jay (Prof Jay), Fanani na Biggy Willy. Miongoni mwa nyimbo zilizowahi kubamba ni pamoja na Chemsha Bongo, Mam Sapu, Funga Kazi, Nusu Peponi Nusu Kuzimu, Fanani, Pata Potea na kadhalika.

KWANZA UNIT

Hili ni miongoni mwa makundi ya mwanzo kabisa ya Bongo Fleva na mwanzilishi wake ni Ramadhan Mponjika ‘Chief Rhymson’ akiwa na Kibacha (KBC), D-Rob na Eazy B, baadaye wakaongezeka memba wengine kama Eazy-B, Bugzy Malone, Papa Sav, Abbas Maunda, Baraka, Ndoti, Fresh-G, Y-Thang na Adili.

Ngoma kama Msafiri, Kwanzanians zililitambulisha vyema kundi hili.

EAST COAST TEAM

East Coast Team lilikuwa likiundwa na wasanii wakali enzi hizo, wakiwemo King Crazy GK, AY, Mwana FA, O Ten, Buff G, Snare na wengineo. Makazi yao yalikuwa ni Upanga jijini Dar es Salaam na wamewahi kutamba na ngoma zao kama Ama Zangu Ama Zao, Itikadi na kadhalika.

TMK WANAUME

Kundi hili lilikuwa likuundwa na Juma Nature, KR, Doro, D Chief, Mh Temba, Chegge, Stico, YP, Y Dash na wengineo. Lilianzishwa mwaka 2002 na lilikuwa na makazi yake Temeke jijini Dar es Salaam. Ngoma zao zilizowahi kutamba, wakitumia staili ya kucheza ya ‘mapanga’ ni pamoja na Ndio Zetu, Dar Mpaka Moro, Chai, Nyumbani ni Nyumbani na kadhalika. Wapinzani wao wakubwa walikuwa ni East Coast Team.
1064007


DAZ NUNDAZ

Daz Nundaz lilikuwa likiundwa na Ferooz, Daz Baba, Critic, La Rumba na Sajo na miongoni mwa ngoma zao ambazo mpaka leo ikipigwa haichakai, ni Kamanda. Ngoma nyingine ni Maji ya Shingo na Barua.

SOLID GROUND FAMILY

Kundi hili lilikuwa likiundwa na wasanii kama Big Black, GZ, Hummer Guy na Master V na ngoma ambayo mpaka leo huwa haisahauliki, ni Bush Party. Nyimbo zao nyingine ni pamoja na Baba Jeni, Athuman Akishalewa, Mechi Kali na kadhalika.

USWAHILINI MATOLA

Kundi hili lililokuwa na maskani yake jijini Mbeya, lilikuwa likiundwa na wasanii watatu, Dr Drito, Mashu Guy na Badi na ngoma iliyowatambulisha ni Kosa la Marehemu waliyorekodi na prodyuza Mika Mwamba.

GANGWE MOB

Gangwe Mobb lilikuwa liliundwa na Inspekta Haroun na Luteni Kalama, lilikuwa na maskani yake pande za Temeke na miongoni mwa ngoma ambazo mpaka leo huwa hazisahauliki, ni Asali wa Moyo, Mtoto wa Geti kali, Pamba Nyepesi, Rap Katuni na kadhalika.

WATEULE

Hili lilikuwa likiundwa na wakali kama Jay Moe, Mchizi Mox, Solo Thang, Mack 2B Simba, Jaffarai na wengine wengi, ngoma zilizowatambulisha vyema ni pamoja na Watu Kibao, Msela na kadhalika. Maskani yake yalikuwa ni Makumbusho, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

MAKUNDI MENGINE

Makundi mengine yaliyofanya vizuri na kuingia kwenye historia ya Bongo Fleva ni pamoja na The Diplomatz, X Plastaz ya Father Nelly, Unique Sisters, Manduli Mobb, Ngoni Tribe, Park Lane, B.D.P (Big Doggy Pose), Mabaga Fresh na Uswahilini Matola.

Wengine ni Wangoto Click, Bantu Pound, Gangsters With Matatizo (GWM), Manzese Crew, Watengwa, Wandago Family, Waswahili, Kikosi cha Mizinga, UVC, Hardcore Unity, Chemba Squad, Wagosi wa Kaya na mengine mengi.

When Bongo Fleva was Bongo Fleva!


Hashpower7113
 
Safi sana
Umejaribu kuelezea kama vyote...
Namjua sana Marlone Linje

Kwa II PROUD, albamu yake ilimpandisha ilikuwa "Ndani ya Bongo", nadhani alihusisha wasanii kadhaa, mpaka leo huwa naisikiliza
Na G Unit ulikuwa nyimbo ya "Msafiri"
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom