Cheka, simulia, lakini usiombe yakukute

Umesoma hadithi hii mwanzo hadi mwisho?

  • Ndio

    Votes: 3 50.0%
  • Hapana

    Votes: 3 50.0%

  • Total voters
    6

Mlenge

R I P
Oct 31, 2006
2,125
2,291
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute

Jamaa kaamka asubuhi kajikuta kageuka mdudu. Hii hapa simulizi yake, Die Verwandlung, imefasiriwa kwa Kiswahili. Ilichapishwa kwa Kijeremani mwaka 1915, mwandishi akiwa Franz Kafka.


Asubuhi fulani, wakati Grego Samsa akiamka toka kwenye ndoto za kutisha, alibaini kwamba hapohapo kitandani alipo, amekwisha kubadilishwa kuwa lidudu kubwa, baya.
Franz.png


Alilalia mgongo wake mgumu mithili ya deraya, akiinua kidogo kichwa chake, tumbo lake la kahawia, likijigawa vipandevipande kuwa visehemu mithili ya pinde. Kutoka urefu huu liliko blanketi, likiwa karibia kabisa kudondoka toka mwilini mwake, alipata shida kubakia alipo. Miguu yake mingi, myembamba vya kusikitisha ukilinganisha na mzingo wa mwili wake, ilijitikisa huku na kule akiitizama.

“Kimenisibu nini,” aliwaza. Haikuwa ndoto. Chumba chake, chumba hasa kwa ajili ya binadamu, japo kidogo sana, kilitulia baina ya kuta nne alizozifahamu vyema. Juu ya meza, ambako kulikuwa na rundo la bidhaa za nguo (Samsa alikuwa ni mfanyabiashara asafiriye) palining’inia picha ambayo alikuwa ameikata toka kwenye jarida la mapicha muda mchache uliokuwa umepita na kuwekwa kwenye fremu ya rangi ya dhahabu. Ilikuwa ni picha ya mwanamke mmoja aliyevaa kofia ya ngozi na kitambaa kizito cha kufunika shingo. Alikaa wima, akiinua uelekeo wa mtazamaji ngozi yenye manyoya mazito ambamo mkono wake wote ulikuwa umezama.

Kisha macho ya Grego yakaelekea dirishani. Hali ya hewa ilikuwa mbaya (matone ya mvua yalidondokea kingo za dirisha kwa kelele) ilimfanya ajihisi ni mwenye huzuni. “Kwa nini silali kwa muda mwingine wa ziada kidogo na kusahau wehu huu wote,” aliwaza. Lakini hili lilikuwa haliwezekani aslani, kwa vile alikuwa na mazoea ya kulalia upande wake wa kulia, na kwa hali yake ya sasa hangeweza kujigeuzia upande wake wa kulia. Hata alipojirusha kwa nguvu zake zote ageukie upande wa kulia, mara zote aliviringika na kurudi chali.


INAENDELEA

 
Mbona munaharibu uzi wawatu😡😡😠😠😠

Brother hao achana nao we endelea😊😊😊😁
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 2

Itakuwa alijaribu mara mia, akifunga macho, ili asione miguu yake ikining’inia, na alikubali matokeo pale tu alipoanza kuhisi maumivu kidogo, yaliyosambaa ubavuni, maumivu ambayo hakuwahi kuyapata hapo kabla.

“Mungu wangu,” aliwaza, “jinsi ilivyo ngumu kazi niliyochagua kuifanya! Kutwa kucha barabarani Msongo wa mawazo ni mkubwa kuliko kazi za ofisini makao makuu, na zaidi ya hayo, inanibidi kupambana na changamoto za safarini, wasiwasi wa kuachwa na treni, chakula kibovu cha njiani, na mahusiano yasiyodumu yasiyotoka moyoni aslan. Nimechoka nayo yote!”

Alihisi muwasho juu ya tumbo. Polepole alijisogeza hivyohivyo chali mpaka kwenye mchago wa kitanda ili aweze kuinua kichwa chake kwa urahisi, akaona sehemu inayomuwasha, ambayo ilikuwa ni madoadoa madogo meupe (hakuyaelewa maana yake), na alitaka apakune na mguu wake mmoja. Lakini aliurudisha mara moja, kwani kujikuna kwa mguu kulileta hisia mwili mzima mithili ya aliyemwagiwa maji baridi.

Alijisogeza tena polepole kurudi alipokuwa awali. “Kudamka mapema hivi,” aliwaza, “kunamfanya mtu awe juha. Mtu shurti autulumue usingizi. Wachuuzi wengine wasafiripo huwa mithili ya machangudoa. Kwa mfano, niliporejea gesti kuandika oda muhimu, mijamaa ile ilikuwa ndio imefika kupata kiamsha kinywa. Ningejaribu mimi kufanya hivyo, bosi angenitimua kazi papo hapo.

Hata hivyo, nani ajuaye iwapo hilo lisingekuwa la manufaa kwangu. Kama nisingevumilia kuajiriwa ili niweze kuendelea kuhudumia wazazi, ningeshaacha kazi zamani sana. Ningemfuata bosi na kumwambia yote yaliyomo ndani kabisa ya moyo wangu. Angezirai na kudondokea mezani mwake! Uliona wapi bosi anaketi juu ya meza na kuamrisha watumishi akiwa hapo juu. Bosi wetu ana shida kidogo ya kusikia, kwa hiyo mtumishi humbidi kujongea karibu naye kabisa.

Lakini, bado sijakata tamaa kabisa. Pindi nikishajikusanyia pesa za kutosha kulipa madeni anayowadai wazazi wangu -- na hilo litachukua miaka mitano au sita hivi mingine -- nitafanya hivyo hakika. Kisha nitajipa mapumziko marefu. Kwa vyovyote vile, sasa hivi inanibidi niamke. Treni inaondoka saa kumi na moja kamili juu ya alama.”

Kisha akaangalia kwenye saa yake yenye kengele ya kumwamsha ilipo kwenye madroo. “Mungu wangu,” aliwaza. Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu, na mishale ya saa ilikuwa ikiendelea kutiki. Ilikuwa imeshapita saa kumi na mbili na nusu, na sasa inakaribia saa moja kasarobo. Inawezekana kengele leo iligoma kulia? Aliweza kuona toka pale kitandani alipokuwa kwamba ilitegeshwa sawasawa saa kumi usiku. Ni wazi kengele ililia. Ndio, lakini ingewezekana kuendelea kulala kwenye kelele hii kubwa iliyofanya fenicha zitikisike? Sawa, ni kweli hangelala, lakini ni wazi alilala fofofo. Kwa hiyo, nini afanye sasa? Treni inayofuata ni ya saa moja kamili. Ili aiwahi, ingembidi atimue mbio mithili ya kichaa. Sampo za bidhaa hazikuwa zimeandaliwa tayari, na hakujihisi mchangamfu wala mwenye nguvu. Na hata akiiwahi treni, hakuna namna ya kukwepa tafrani na bosi, kwa vile tarishi wa kampuni atakuwa tayari amekuja kumpokea kwenye treni ya saa kumi na moja na saa nyingi kumpa ripoti bosi kuchelewa kwake. Alikuwa ni msaidizi wa bosi, bila msimamo wala akili. Sasa, labda aripoti kuumwa? Lakini hiyo ingekuwa mbaya na yenye kuibua mashaka, kwa sababu katika kipindi chote cha miaka mitano ya utumishi wake, Grego hakuwahi kuumwa hata siku moja.

Bila shaka bosi angekuja na daktari kutoka kampuni ya bima ya afya na angewagombeza wazazi wake kwa ugoigoi wa mtoto wao na kukataa hoja zozote watakazomwambia, kwani yeye huona kila mtu ni mwenye afya ila analeta maringarin kutega kazi. Juu ya hayo, kwenye hili dokta angekuwa amekosea? Ukiondoa mawengewenge baada ya usingizi mrefu, Grego alijihisi vema kabisa na hata alijiona ana hamu kubwa ya kula.

Wakati akifikiria hayo yote kwa haraka sana, na bila kuweza kufikia uamuzi wa kutoka kitandani (saa ya kengele ilikuwa inaonyesha ni saa moja kasorobo) palikuwa na hodi iliyopigwa kwa machale pale mlangoni ulikokuwa mchago wa kitanda.


“Grego,” sauti iliita (ilikuwa ni mama yake!) “ni saa moja kasorobo. Hutaki kuanza kuondoka?” Sauti mororo! Grego alijistaajabia alipojisikia sauti yake mwenyewe wakati anamjibu. Ilikuwa wazi kabisa na bila ubishi sauti yake ya siku zote, lakini ilikuwa imevurugika, kana kwamba kutokea chini, mitetemo iumizayo iliruhusu kwanza maneno yasikike kisha ikayavuruga kwa mwangwi, ili mtu asiamini anachosikia ni sahihi.

Grego alitaka kujibu kwa kina na kueleza kila kitu, lakini kwa mazingira aliyokuwapo alijikuta akisema, “Ndio, ndio, asante mama. Naamka sasa hivi.”

Inaendelea Sehemu ya 3
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 3

Kutokana na mlango wa mbao, mabadiliko kwenye sauti ya Grego hayakuweza kubainika nje ya chumba, hivyo mama yake akatulizwa na maelezo hayo na kuondoka. Hata hivyo, kutokana na mazungumzo hayo, wanafamilia wengine wakafahamu kwamba Grego alikuwako nyumbani bado isivyotarajiwa, na tayari baba yake alikuwa akigonga upande mmoja wa mlango, kidogokidogo lakini kwa kutumia ngumi. “Grego, Grego,” aliita, “Kunani pale?” Na baada ya muda mfupi alirudia tena kwa sauti nzito zaidi. “Grego!” Grego!” Hata hivyo, kwenye upande mwingine wa mlango, dada yake aligonga mlango polepole. “Grego! Umeamkaje? Wahitaji chochote?”

Grego aliekeza majibu yake pande zote mbili. “N’takuwa tayari sasa hivi.”

Alifanya juhudi kwa uangalifu mkubwa na kwa kuweka pozi ndefu baina ya neno mojamoja ili kuficha chochote cha tofauti kwenye sauti yake.

Baba yake akarejea kuendelea kunywa chai. Lakini dada yake akanong’ona, “Grego, fungua mlango, nakusihi.” Grego hakuwa na mpango wa kuufungua mlango, bali alijipongeza kwa tahadhari ile, aliyoipata kutokana na kuwa ni mtu wa safari, akifunga kwa funguo milango yote usiku, hata kama yu kunyumba.

Kwanza alitaka kusimama wima kimyakimya bila kusumbuliwa, kuvaa nguo, na muhimu kuliko yote kupata kiamshakimya, na hapo ndipo angeweza kufikiria mengine ya kufanya, kwani (alibaini hili wazi kwamba) kwa kufikiria mambo akiwa kitandani hangeweza kufikia hitimisho la busara.

Alikumbuka pia kwamba alikuwa tayari mara nyingi anasikia maumivu mepesi haya au yale kitandani, pengine yakiwa ni matokeo ya namna anavyolala, ambayo baadaye ilikuja kubainika ni mawazo tu ya kufikirika pale aliposimama wima, na alikuwa na hamu ya kuona namna gani matarajio aliyonayo, na alikuwa na hamu ya kuona mafikara yake yakipungua taratibu.

Mabadiliko hayo ya kwenye sauti yake hayakuwa ya maajabu zaidi ya ujio wa homa wa baridi, ugonjwa ukumbao wachuuzi wanaosafiri mara kwa mara, na kwa hilo hakuwa na chembe ya shaka.

Ilikuwa ni vyepesi sana kutupa kule blanketi. Alichohitaji ni kujituma kidogo zaidi tu, na likaanguka. Lakini kuendelea ndio ikawa shida, na hasa kwa vile alikuwa ni mpana isivyo kawaida. Alihitaji mikono na viganja kumsaidia awe wima.
Badala ya hivi, hata hivyo, alikuwa tu na viguu vidogo vingi ambavyo muda wote vilikuwa vinapepea huku na kule na ambavyo, kwa nyongeza, alikuwa hawezi kuvidhibiti apendavyo. Akitaka kuukunja mmojawapo, basi ulikuwa ndio wa kwanza kujinyoosha, na kama akifanikiwa hatimaye kuuongoza mguu huu apendavyo, wakati huohuo miguu yote mingine iliyobaki, kana kwamba imeachwa huru, ilichezacheza huku na kule na kumpa maumivu. “Lakini inanibidi nisiendelee kuwepo kitandani kizembezembe,” alijiambia bwana Grego.

Kwa kuanzia, alitaka kutoka kitandani kwa kutumia sehemu ya chini ya mwili wake mpya, lakini sehemu hii ya chini (ambayo hata hivyo hakuwa ameiangalia bado na ambayo hakuweza kuiona vizuri) ilimuwia vigumu kuijongeza. Jitihada zake zilienda polepole sana.

Pale ambapo, alipokuwa karibu ya kuchanganyikiwa, hatimaye alijirusha kwa nguvu zake zote na bila kujali, alichagua uelekeo kwa makosa, na kujigonga kwenye mchago wa kitanda. Maumivu makali aliyoyasikia yalimfanya atambue kwamba eneo la chini la mwili wake lilikuwa pengine ndilo la kulichunga zaidi.

Kwa hiyo, alijaribu kutumia sehemu ya juu ya mwili wake kuanza kujiondoa kitandani, na aligeuza kichwa chake kwa uangalifu kuelekea pembeni mwa kitanda. Hili alifanikiwa kwa urahisi, na licha ya upana na uzito wa mwili wake, hatimaye polepole nao uligeuka kufuata uelekeo wa kichwa. Lakini pindi hatimaye alipoinua hewani kichwa chake nje ya kitanda, alihofia kuendelea namna hii, kwani angeruhusu hatimaye kudondoka kwa mtindo huu, ingehitaji muujiza kuzuia kichwa chake kisijeruhiwe. Na kwa gharama zote ni lazima ajilinde ufahamu wake. Hivyo akapendelea kuendelea kubakia kitandani.

Hata hivyo, baada ya jitihada kama hizo, wakati akilala hapo na kuendelea kutafakari, kwa mara nyingine tena aliiona miguu yake ikipambana yenyewe kwa yenyewe, kana kwamba ni zaidi ya ilivyokuwa awali, na hakuona namna yoyote ya kurejesha amani na utulivu kwenye miguu hiyo, na alijiambia tena pengine hangeweza kuendelea kubakia kitandani na kwamba ingekuwa ni jambo la busara sana kujitoa muhanga ili kupata matumaini japo madogo ya kujikwamua toka kitandani. Wakati huohuo, hakusahau kujikumbusha mara kwa mara ukweli kwamba utulivu (yaani utulivu wa hali ya juu) ungekuwa ni bora kuliko maamuzi yaliofikiwa kwa muhemuko. Kwa nyakati hizo, alielekeza macho yake kadiri alivyoweza uelekeo wa dirisha, lakini angeweza kupata furaha kidogo sana kutoka kwenye ukungu uliotanda nje, ambao ulifunika asiweze hata kuona upande wa pili wa mtaa mwembamba. “Tayari ni saa moja kamili” alijiambia aliposikia kengele ya saa, “saa moja kamili na bado kuna ukungu hivi.” Kwa muda zaidi aliendelea kujilaza kimya akivuta pumzi kidhaifu, kana kwamba akisubiri hali ya hewa irudi kuwa nzuri kama ilivyo kawaida baada ya kimya chake.

Lakini kisha alijiambia mwenyewe, “Kabla haijafika saa moja na robo, liwalo na liwe, lazime niwe nimetoka kitandani. Na tena, mpaka wakati huo mtu kutoka ofisini atakuwa ameshafika nyumbani
Kuniulizia, kwa sababu ofisi hufunguliwa kabla ya saa moja kamili.” Ndipo alipofanya juhudi ya kuujongeza mwili wake wote nje ya kitanda kwa wakati mmoja. Kama akijiachia namna hii, kichwa chake alichokusudia kukiinua juu kwa ghafla wakati akidondoka, pengine kingebaki bila kujeruhiwa. Mgongo wake ulionekana ni mgumu; hakuna ambacho kingeupata kutokana na kudondoka. Wasiwasi wake ulibakia kwenye sauti kubwa itakayotokana na kudondoka na ambayo itaamsha, ikiwa si hofu, basi mashaka upande wa pili wa milango yote. Hata hivyo ilibidi kujaribu.

Wakati Grego akiwa kwenye mchakato wa kujiinua kutoka kitandani (mbinu hii ilikuwa ni kama anayecheza kuliko ilivyokuwa ni jitihada; alihitaji kujiinua tu kwa kurudiarudia) wazo lilimjia ambavyo ingekuwa rahisi tu kama mtu angekuja kumsaidia. Watu wawili wenye nguvu (alimfikiria baba yake na dada wa kazi) wangeweza kutosha kabisa. Wangehitaji tu kuweka mikono yao chini ya mgongo wake na kumuinua kutoka kitandani, kuchutama, na kisha taratibu kwa uangalifu kumgeuza sakafuni, mahali ambapo vigulu vyake, aliamini, vingekuwa na manufaa. Sasa, mbali na ukweli kwamba milango ilikuwa imelokiwa, kwani alijihitaji kuita msaada? Licha ya masaibu yote yaliyompata, alishindwa kujizuia kutabasamu alipowaza haya.

Tayari alikuwa amefikia mahali ambapo, kwa kujijongeza kwa nguvu zaidi, uwezo wake wa kujidhibiti ulipungua, na punde ingembidi afanye maamuzi ya mwisho, kwani ziibaki dakika tano tu ifike saa moja na robo.

Kisha palikuwa na hodi nje ya nyumba. “Atakuwa mtu kutoka ofisini” alijiambia, na alitulia tuli mwili mzima, isipokuwa vigulu vyake vilivyozidi kuchezacheza haraka zaidi. Kwa sekunde moja kila kitu kiliku wa tuli. “Hawamfungulii,” Grego alijiambia, akianza kujipa matumaini ya kijinga. Lakini kama kawaida, dada wa kazi alipiga hatua za nguvu kwenda mlangoni na kuufungua. Grego alihitaji kusikia tu neno la kwanza la mgeni ili kujua ni nani, bosi meneja mwenyewe.

Kwa nini Grego alikuwa ni mtu pekee aliyeadhibiwa kufanya kazi kwenye kampuni ambapo kukosekana kidogo tu kunaibua tuhuma kubwa? Je wafanyakazi wote, mmojammoja na kwa pamoja, walikuwa ni mabaradhuli? Hakukuwa hata na mmojawao ambaye hujituma kiukweli ambaye, akikosekana masaa kidogo tu asubuhi, atajisikia vibaya nafsini na kushindwa hata kutoka kitandani? Haikutosha kwa tarishi kuja kuulizia kulikoni, kama hilo lingekuwa la lazima? Lazima aje bosi meneja mwenyewe, na kwa kufanya hivyo kuionyesha familia isiyo na hatia kwamba uchunguzi wa mazingira haya ungeweza kuaminiwa kwa bosi meneja pekee?

Zaidi ni muhemuko uliotokana na mafikara haya, na katu si uamuzi uliotokana na tafakuri, Grego alijirusha kwa nguvu zake zote kutoka kitandani. Palikuwa na kishindo kikubwa, lakini hakuumia.

Kudondoka kule kulisharabiwa kiaina na zulia, na mgongo wake ulikuwa ni laini kuliko alivyoudhania Grego hapo awali. Kwa sababu hiyo, sauti iliyotoka haikuwa haikusikika mbali.

Lakini hakukikinga kichwa chake kwa uangalifu wa kutosha na alikipigiza. Aligeuza kichwa chake, kwa kero na maumivu, akakifutafuta sakafuni.

“Kuna kitu kimeanguka,” alisema meneja aliyekuwa chumba cha jirani kushoto. Grego akajaribu kujiwazia iwapo masaibu kama haya yaliyompata leo yangeweza kuja kumpata bosi meneja. Walau ilibidi kukubali kuwepo uwezekano wa jambo kama hilo.

Na kama vile ilikuwa ni kutoa jibu kwa swali lile, bosi meneja sasa alichukua hatua kadhaa madhubuti kuelekea chumba kingine, viatu vyake vilivyobrashiwa vema vikitoa sauti.

Na kutokea chumba jirani cha upande wa kulia, dada yake alikuwa akinong’ona kumuarifu Grego: “Grego, bosi meneja amekuja.”
“Najua!” Grego alijiambia mwenyewe. Lakini hakuthubutu kusema kwa sauti kubwa ambayo dada angeisikia.

“Grego,” baba yake sasa alisema kutokea chumba jirani cha upande wa kushoto,”Bwana Meneja amekuja na anauliza kwa nini hukuja na treni ya kwanza. Hatujui la kumjibu. Na kisha, anataka kusema na wewe. Kwa hiyo tafadhali fungua mlango. Atakuwa na busara ya kutojali mvurugiko wa chumbani kwako.”

Wakati yote haya yakiendelea, bosi meneja alimuita kwa upole, “Salbakheri Bwana Samsa.”

“Hajisikii vizuri,” mama alimjibu bosi meneja, wakati baba bado alikuwa akiongea mlangoni, “Hayuko vizuri, niamini, Bwana Meneja. Vinginevyo, Grego anaanzaje kukosa kupanda treni! Bwana mdogo hana kitu chochote kichwani mwake isipokuwa kazi tu! Ananiudhi hatokagi kwenda viwanja usiku. Na hapa yuko mjini siku nane, lakini kila usiku yuko nyumbani tu. Hukaa hapa kimya na sisi mezani na kusoma magazeti au kupitia ratiba zake za safari. Starehe yake ni kuchonga vitu. Kwa mfano, alikata kipande cha fremu ndani jioni mbili tatu. Utashangaa kilivyo kizuri. Utakiona pindi Grego akifungua mlango. Tumefurahi lakini kukuona hapa Bwana Meneja. Tungekuwa wenyewe tusingeweza kumfanya Grego afungue mlango. Ni mbishi kweli, na japo hajisikii vizuri, alikanusha hayo asubuhi hii.”

Inaendelea Sehemu ya 4
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom