Chanzo mimba za utotoni Mkoani Kagera(Makala ya Uchunguzi)

Rutunga M

JF-Expert Member
Mar 16, 2009
1,769
1,382
Wakubwa
Nimesoma kwenye Gazeti moja liitwalo Malengo Yetu la kanda ya ziwa juu ya makala moja ya uchunguzi inayobanisha chanzo cha mimba za utotoni katika mkoa huo.

Nimeipenda makala ile LAKINI cha kusikitisha ni kuwa sidhani kama imesomwa na watu wengi kwa kuwa gazeti halisambazwi sehemu kubwa nchini Tanzania na halimo kwenye mtandao.licha blogspot ya mwandishi huyo kuichapisha.

Hivi ni kwa nini makala kama hii isichapishwe kwenye magazeti kama RAI,Mwanahalisi,Tanzania daima nk badala ya gazeti changa kama hili.

Nimeicop kutoka kwenye blogspot na ni hii hapa

Na Mathias Byabato.
“Nilikutana naye muda mfupi tu baada ya kuhitimu darasa la saba akasema ananipenda,nikakubaliana naye akanioa, lakini nilipojifungua akanifukuza na hivi sasa naishi kwa mama mdogo hapa kijijini na mtoto wangu” .

Hii ni kauli ya Edina Kashaija(20) mkazi wa kijiji cha Nyakazinga ambaye ni mmoja wa wahanga wa mimba za utotoni wakati akifanya mahojiano na gazeti hili katika uchunguzi wa kubaini chanzo cha kukithiri kwa mimba za utotoni na kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika wilaya Karagwe Mkoani Kagera.

Wilaya ya Karagwe inatajwa kuongoza kiuchumi katika wilaya zilizoko mkoani Kagera lakini takwimu kutoka Ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kuwa kuanzia mwaka 2008 hadi sasa wanafunzi 167 wamebeba mimba zinaondoa heshima ya wilaya hiyo hali iliyolazimu nifanye uchunguzi kubaini chanzo cha tatizo hilo.
Kwa mjibu wa mkuu wa wilaya ya Karagwe Bw Fabian Masawe ni kuwa wanafunzi wa shule za sekondari wilayani humo wanaopanga uraiani wanaongoza kwa kubebeshwa mimba kutokana na kurubuniwa na wanaume kwa kuwapatia fedha za matumizi ya kila siku.

Ukubwa wa Tatizo

Kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2002 Wilaya hiyo ina watu 425,476 wakiwemo wanaume 208,620 na wanawake 216,856 Ongezeko la watu la Wilaya ni na kuwa asilimia ya watoto yatima ni 1.35 .
Mwaka 2007 idadi inakadiriwa kuwa 473,128 Me – 232,020, Ke – 241,108. Idadi ya Kaya ni 89,188 na wastani wa watu ni 4.8 kwa Kaya.

Kwa mjibu wa taarifa iliyopataikana kwenye mtandao wa Serikali ya Mkoa wa Kagera ni kuwa athari kubwa ya UKIMWI wilayani Karagwe imesababisha ongezeko kubwa la watoto yatima. Hadi Desemba 2006 watoto yatima wamefikia 44,172 na kuwa wilaya inazo sekondari 43 (zikiwemo 34 za serikali na 9 za binafsi)

Taarifa ya mtandao huo wa www.kagera.go.tz ni kuwa idadi ya wanafunzi waliopata mamba kwa shule za msingi na sekondari kuanzia januari hadi desemba 2009 ni 276 tu na kuwa Chato inaongoza kimkoa kwa kuwa na wanafunzi 74 waliopata mamba kwa kipindi hicho ikifuatiwa na Wilaya ya Karagwe yenye wanafunzi 44 waliopata ujauzito kwa kipindi hicho.

Imebainishwa kuwa wanafunzi wanaongoza kupata ujauzito katika wilaya ya Karagwe ni wa shule za msingi kwani kupitia mtandao huo Serikali imeweka takwimu zinazoonesha kuwa kwa kipindi hicho kati ya 44 waliopata ujauzito wanafunzi 30 walikuwa ni wa shule za msingi .

Kwamba tatizo lilivyo ni kuwa Wilaya ya Biharamulo wanafunzi waliopata ujauzito kwa kipindi hicho walikuwa 12,Manispaa ya Bukoba(4), Bukoba vijijini(41), Chato(74) ,Karagwe(44), Missenyi(29) ,Muleba(36) na Wilaya ya Ngara(36)

Hata hivyo takwimu hizo kwa wilaya ya Karagwe zinatofautiana na zile zilizotolewa na Mkuu wa wilaya ya Karagwe Bw Fabian Masawe wakati akihojiwa na Gazeti hili juu ya tatizo hilo.
Kwa mjibu wa maelezo ya mkuu wa wilaya hiyo ni kuwa tatizo hilo linaathiri sana watoto wa kike katika wilaya yake.

Akidai kuwa mwaka 2008 wanafunzi 102 wa shule za msingi na sekondari walibainika kubebeshwa mimba,mwaka 2009 walibebeshwa mimba wanafunzi 45 na hadi mei 2010 wanafunzi waliobebeshwa mimba walikuwa 20.

Mikakati ya Serikali ngazi ya wilaya kudhibiti mimba

Masawe anafafanua kuwa ili kukabiliana na tatizo,ofisi yake imebuni mkakakati kabambe wa kuwafungulia mashtaka wazazi wa watoto wanaohusika katika njama za kuozesha watoto wao au kuhusika kumaliza kesi kienyeji za waliowabebesha mimba watoto wao.

“Mbali na wazazi tunaowashikilia pia kuna kesi kadhaa za waliohusika kuwabebesha mimba wanafunzi nao tumewafikisha mahakamani ambapo hivi sasa tumeanza mkakakati wa kuwafungulia mashataka hata mabinti wanaobeba mimba ili kuona kama tunaweza kukomesha tabia hii”

DC anaongeza kuwa ofisi yake imetangaza dau la sh 20,000 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa ‘mafataki’ au kutoa taarifa za kuona binti mwenye umri chini ya miaka 18 anayeingia kwenye nyumba ya kulala wageni katika wilaya hiyo.

“Tumetoa taarifa kwa viongozi wa dini ili watusaidie katika kufundisha watu kiroho ili wamrudie Mungu kwa kuacha zinaa na hii itasaidia kuondoa tatizo” anasema DC huyo.

Kwa mjibu wa Fabian Masawe ni kuwa ofisi yake imeagiza wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari kukatazwa kumiliki simu za mkononi ili washindwe kuwasiliana na wanaume wakwale.

Mbali na changamoto zilizopo lakini DC huyo anaona kuwa chanzo cha kuongezeka kwa mimba za utotoni wilayani humo ni malezi duni kutoka kwa wazazi wao,maadili kuporomoka miongoni mwa jamii,wanafunzi wa shule za sekondari za kata kupangishiwa vyumba uraiani maarufu kama ‘geto’ .

Matatizo ya utoaji mimba na UKIMWI kwa vijana.

Kwa mjibu wa maelezo ya mkuu wa wilaya ni kuwa baadhi ya watoto chini ya umri wa miaka 18 wamekuwa wakichoropoa mimba kwa kutumia njia za kienyeji ambapo licha ya kutokuwepo takwimu za madhara ya waliofanya hivyo lakini wanafunzi wanaotoa mimba ili kuendelea na masomo wilayani humo inaongezeka kila siku.

Aidha DC huyo anabainisha kuwa kati ya wanafunzi waliobainika kuwa wajawazito kati ya mwaka 2008 hadi sasa aslimia 85 walibainika kuwa wameathirika hali inayoonesha kuwa katika wilaya hiyo kuna kasi ya maambukizi ya UKIMWI kwa vijana.

Aidha anasema kuwa uongozi wa wilaya hiyo umeamua kila baada ya miezi mitatu wanafunzi wote wa kike wanapimwa ili kubaini kama wanao ujauzito.

Kufuatia mkakati huo wa wilaya wanafunzi wengi walihojiwa walibainisha kuogopa kupata mimba kuliko kupata UKIMWI au madhara mengine yanayotokana na kufanya mapenzi kwa umri mdogo.

Utata katika utekelezaji wa Sheria na kipimo cha DNA

Uongozi wa wilaya ya Karagwe kwa kushirikiana na vyombo vya dola wamekuwa katika harakati za kuwafungulia kesi wote wanaohusika kuwabebesha mimba wanafunzi wilayani humo.

Uchunguzi umebaini kuwa kati ya wanafunzi 167 waliogundulika kubebeshwa mimba kati ya 2008 hadi sasa ni kesi 12 tu zilizoko mahakamani na sita zipo katika kituo cha polisi Karagwe na kati ya hizo hakuna iliyokwisha tolewa uamuzi.

“Kwa kweli kesi na upelelezi vinachukua muda mrefu na nyingine zinachukua mpaka miaka sita hadi nyingine zinafutwa ,lakini vyombo kama mahakama vipo huru hatupaswi kuviingilia”Anasema DC Masawe katika mahojiano na Gazeti hili.

Aidha DC Masawe anaonesha wasiwasi juu ya utata wa sheria kwani sheria ya ndoa ya mwaka 1975 inasema mtoto mwenye umri wa miaka 15 anaruhusiwa kuolewa .

“Changamoto ni sheria ilivyo kimya kwa wasichana wanaojilegeza kwa wanaume kwani tunapowafikisha mahakamani tunashuindwa tuwashtaki kwa kifungu kipi hivyo kuonesha kuwa msichana hawajibiki kwa lolote katika suala ambalo sisi tunadhani linakuwa na dalili za makubaliano kati ya binti na mvulana.

“Hivyo hata juhudi zetu za kuwakamata mabinti wanaobainika kubeba mimba na kuwafikisha mahakamani sheria iko kimya juu yao,hivyo tunawashurutisha tu”anasema

Aidha Mganga wa wilaya Dk Isaya Kamongi alieleza kuwa hata kipimo cha DNA cha kubaini kama mtu anayedaiwa kumbebesha mimba binti ndiye mhusika hakiwezi kufanyika hivi hivi bali ni kwa maagizo ya mahakama na kwa kanda ya ziwa kipimo hicho hufanyika katika jiji la Mwanza pekee katika Hospitali ya rufaa ya Bugando.

Nafasi ya wazazi kwa vijana

Wazazi wengi katika maeneo mbalimbali wilayani humo waliohojiwa walibainisha kutozungumza na watoto wao kuhusu afya ya uzazi hali inayosababisha vijana wengi kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wakiwa na umri mdogo bila kujua madhara yake.

Uchunguzi umebaini kuwa wazazi wengi katika wilaya hiyo wanaona soni au haya kuongea na wanao kuhusu masuala ua uzazi mathalani wazazi wa vijiji vya Ndama,Nyaboigera kata ya Ndama walipoulizwa kama wanawaeleza watoto wao madhara ya kushiriki ngono wakiwa na umri mdogo,walisema kuwa hawafanyi hivyo kwa madai kuwa watoto wa kizazi cha sasa siyo wasikivu na kwamba hata wanaozungumza nao wanadai kutosikilizwa.

Hata hivyo vijana waliohojiwa walisema kuwa hawapati muda wa kuongea na wazazi wao hasa wanaume kuhusiana na afya ya uzazi na kuwa wale wanaopata muda wanaelezwa madhara kwa kugombezwa .

“Mimi siongei na wanangu kwani naona ni kama kuwafundisha mambo ya wakubwa lakini hata nikiwaeleza hawawezi kunielewa kwani watoto wa siku hizi siyo wasikivu,labda kama wanaelezwa na walimu wao huko shuleni” Alisema Kandida Vicent(33) mkazi wa Nyakatuntu.

Beatrice Valentine(18) anasema kuwa yeye amekuwa akielezwa na mama yake juu ya mabadiliko ya kimwili na kwamba maelezo ya mama yake yamemsaidia kujiepusha na vishawishi kutoka kwa wavulana na wanaume wengine.

“Mama huwa ananiita usiku wakati tunapika na kunieleza kwa upole madhara ya kushiriki ngono nikiwa na umri huu mdogo na kwa kuwa nampenda mama huwa nafarijika kwa mama kunieleza ninavyoweza kujikinga na ‘mafataki’(kicheko)” anasema Beatrice.

Walimu kufanya mapenzi na wanafunzi wao wilayani Karagwe.

Wakati DC Karagwe akihojiwa na gazeti hili kuhusu tatizo la mimba katika wilaya hiyo alibainisha kuwa tofauti na mategemeo kuwa walimu wanapasawa kuwa walezi na mabalozi katika kupiga vita mimba kwa wanafunzi lakini katika wilaya hiyo hali ni tofauti kwani baadhi ya walimu wamebainika kufanya mapenzi na wanafunzi wao.

“Hadi sasa kati ya kesi zilizofikishwa mahakamani kwa kuwabaka,kuwaoa au kufanya mapenzi na wanafunzi kati yao tisa ni walimu(wa kiume) hali ambayo imetutia wasiwasi” Anasema Dc Masawe.

Hata hivyo wakihojiwa juu ya madai hayo baadhi ya walimu wilayani Karagwe walibainisha kuwa si wote bali miongoni mwao kuna wasio na maadili ya taaluma hiyo.

Makamu Mkuu wa shule Ndama Danny Bilabamu anasema kuwa walimu ni walezi hivyo madai ya wao kutembea na wanafunzi wao halipo katika shule yake ingawa anasema kuwa mwaka 2009 wanafunzi wawili wa shule hiyo walibainika kuwa wajawazito na kufikia mei 2010 mwanafunzi mmoja amegundulika kuwa mjamzito.

Anaongeza kuwa tatizo la wanafunzi kubebeshwa mimba ni kuishi kwenye nyumba za kupanga uraiani na kwamba iwapo yatajengwa mabweni katika shule za kata wilayani humo tatizo litapungua.

Licha ya uchunguzi wa gazeti hili kubaini idadi kubwa ya walimu ambao ni vijana wanaodaiwa kufanya mapenzi na wanafunzi,mwalimu Dany anasema kuwa hilo siyo sababu ya wao kufanya mapenzi na wanafunzi wao na kama lipo ni la mtu binafsi na siyo utaratibu wa shule.

Walimu Anitha Audax na Prudencia Wilson wa shule hiyo wanasema kuwa umaskini unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vijana kujiingiza katika ngono wakiwa na umri mdogo.

Wanaongeza wao wamekuwa wakitoa elimu juu ya masuala ya afya kwa wanafunzi hao lakini baadhi yao wanapuuza na kwamba wao wanawatambua wanafunzi wanaojihusisha na ngono kwani viwango vya kufaulu kwa wanafunzi hao hupungua.

Maoni ya vijana juu ya wao kujihusisha na ngono kwa umri mdogo

Vijana kadhaa wakiwemo wanafunzi waliohojiwa kuhusiana na mipango ya serikali ngazi ya wilaya katika kudhibiti kasi ya mabinti kubebeshwa mimba kwa kuondoa wanaoishi katika mabweni ya mitaani walionesha wasiwasi wakidai hilo halitakuwa suluhisho kwao kujihusiaha na ngono.

Wengi waliohojiwa walibainisha kuwa kuwa tatizo kwao ni mabadiliko ya kimwili,mapokeo hasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano hasa internet na filamu na kwamba katika maeneo yao kijana kuwa na wapenzi wengi kama wanne au watano inanoesha heshima na sifa miongoni mwao.

Uchunguzi umebaini kuwa wanafunzi walio wengi wanaishi katika vyumba vya kupanga kitu kinachosababisha kuwepo kwa vishawishi vya ngono kwa baadhi ya watoto wa kike kwani wengi wao wanatoka kwenye familia duni hivyo hawana uwezo wa kupata mahitaji muhimu ya kila siku katika maisha yao ya kupanga huku wakisoma.

Wanafunzi Grace David,Adolf Munio na Wabura Kahunzwa wa shule ya sekondari Ndama ambao wanapanga uraiani wakiongelea tatizo hilo walibianisha kuwa wanaishi kwenye vyumba vya kupanga kwani maisha ya kupanga uraiani ni rahisi kwani kwa mwezi wanalipia chumba sh.5,000 kitu ambacho hata wakijengewa hosteli wazazi wao hawataweza kuwalipia gharama za kukaa huko kwani kipato chao ni kidogo.

Wanameongeza kuwa wao wanapanga ili kupunguza umbali uliopo ambao wamesema ni wa mwendo wa masaa mawili hivyo,wao hawategemei kuondoka na badala yake wanamuomba Mkuu wa wilaya aitishe kikao kati ya wazazi wao ambao ndio wamewaruhusu kupangisha vyumba hivyo.

Wakiongelea agizo la DC Masawe kuwa wahame mara moja ili kupunguza kasi ya mimba wanafunzi hao wanafafanua kuwa agizo hilo ni kuwanyima nafasi ya kusoma kwani wanapotoka ni mbali na shule hivyo wakifukuzwa katika maeneo hayo wataacha shule.

Wanaongeza tabia ya uhuni na uzinzi ni la mtu binafsi na wao wasihukumiwe kwa tabia mbaya za baadhi yao kwani wanafunzi wanaopanga uraiani wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo kuliko wanaoishi na wazazi wao.

Kijana Rajabu Abdalah(22) mkazi wa kitongoji cha Nyakatuntu kata ya ndama anabainisha kuwa katika kitongoji chao kijana mwenye wapenzi wengi anaonekana shujaa na yule ambaye hana anaonekana ‘bwege’ au ‘mshamba’.

Rajabu anasema kuwa vijana wanajua madhara ya kufanya ngono kwa umri mdogo na namna ya kujilinda ikiwemo kutumia kinga kama kondomu lakini hawafanyi hivyo kwa kuwa mipira hiyo ya kiume haipatikani katika vijiji vyao na kwamba iliyopo inauzwa sh 500 kwa kasha moja kiasi ambacho vijana wengi hawawezi kumudu.

“Kijana hawezi kutoa sh 500 kununua kondomu kwani sisi tunaona ni bora tununue hata chumba mbili za pombe”alisema Rajabu.

Aidha Beatrice Valentine anasema kuwa ili kujiepusha na masuala ya ngono kwa vijana ni kukwepa makundi na marafiki wenye tabia mbaya na kujikita katika shuguli za kilimo au masomo.
Aidha uchunguzi umebani kuwa baadhi ya vijana hawana elimu ya kutosha juu ya mabadiliko ya kimwili na afya ya uzazi.

“Naona nikuulize ndugu mwandishi ,hivi nikiwa na hamu ya kufanya mapenzi nifanye nini,au nifanye nini ili nisiwe na hamu hiyo kwani hilo ndilo sisi vijana linatuangusha kwani mbali na kurubuniwa lakini hata mabadiliko ya kimwili yanatuathiri sana sisi mabinti” Aliuliza Arodia Anatory(18) wa kijiji cha Nyabwoigera licha ya kwamba hakupata jibu kutoka kwangu.

.Mila na desturi za zamani kupuuzwa

Baadhi ya wazee waliohojiwa kutoka vijiji mbalimbali wilayani humo wameeleza kuwa endapo mila na desturi za zamani zitatumika kikamilifu katika kuhimiza maadili kwa vijana tatizo la mimba za utotoni wilayani humo litamalizika au kupungua.

Bi.Frolence Anatory Mkazi wa kijiji cha Nyaboigwera kata ya Ndama na Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Ndama Bw Erenest Mabula wamesema kuwa mila na desturi za zamani ndizo tu ambazo kwa sasa zitasaidia kuwabadilisha vijana kwani maadili yao yameporomoka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo kulikuwa na adhabu kali zilizokuwa zikichukuliwa kwa wanaobainika kuwa na mimba.

Bw Gorge Rumanyika ambaye ni mratibu Elimu kata ya Ndama amebainisha kuwa njia hizo zinaweza kusaidia kutokomeza tatizo hilo ni pamoja na jamii nzima kuwajibika katika kukemea vitendo viovu vya ngono kwa watoto wao.

“Wakati sisi tulipokuwa vijana tulikuwa tukiambiwa kuwa mtoto atakayemchungulia mtu mzima akioga au akijisaidia atapofuka macho na tuliamini ivyo ambapo wazazi walilenga kuimiza maadili lakini watoto wa sasa wanataka kudhibitisha kwa kutenda na matokeo yake wanakuwa wadadisi wa kila kitu” Anasema.

Aidha wanaongeza kuwa mila za zamani zililenga kuwalinda vijana kwa kuwapatia taarifa za kuogofya hasa kuhusu suala la mahusiano ya kimwili lakini baada ya kupuuzwa kwa mila za zamani katika maeneo yao kumesababisha vijana kujua mambo mengi ya kimahusiano kuliko hata watu wazima.

“Zamani ilikuwa ni nadra kuona mtoto anaongelea masuala ya ngono hadharani kwani hata kijana kutaka kuchumbia au kuchumbiwa ilikuwa ni kazi kweli kweli ukiona aibu mbele ya wazazi lakini hivi leo kijana wa darasa la saba anafika nyumbani kwa wazazi wake kuwatambulisha girl au boy friend wake hii ni hatari kwa kizazi cha leo” Anasema Bi Frolence Anatory.

Mhanga wa mimba za utotoni anasemaje

Edina Kashaija(pichani) akiwa na umri wa miaka 17 tu alibebeshwa mimba akiwa darasa la saba mwaka 2006 lakini licha ya kwamba alifanikiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi lakini ndoto zake zilifuatia baada ya kupata ujauzito.

Katika maelezo yake nami huku akibubujikwa na machozi biti huyu mwenye maelezo ya huruma anasema alikumbana na na askari polisi mmoja akamweleza kuwa anampenda naye akashawishika akaingia katika penzi hilo.

Anasema haikuchukua muda akapata ujauzito na kuolewa na askari huyo muda mfupi baada ya kumaliza elimu ya msingi na kwamba matokeo yalipotoka alikuwa amechaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari lakini tayari alikuwa mke wa mtu.

“Haikuchukua hata miaka miwili tangu niwe kwenye ndoa kwani mambo yaligeuka na hatimaye nikatelekezwa na baadaye nikaamua kurudi kwetu nikiwa na mtoto mchanga ambaye anaishi kwa mama yangu mzazi” anasema Edina

Kwa mjibu wa Edina ni kuwa kilichomponza ni tamaa ya fedha ndogo ndogo,mabadiliko ya kimwili na kutopata nasaha zozote kutoka kwa wazazi,walezi au walimu juu ya madhara ya kujihusisha na ngono au kuolewa kwa umri mdogo.

Anaongeza kuwa hivi sasa anaona ndoto za kujikwamua na umaskini zimeota mbawa kwani hivi sasa ni mkulima wa kijiji mipango ambayo hakuitegemea.

“Nawaomba wasichana wanaosoma wawe makini na vikundi,wawe wavumilivu wasikimbilie kuolewa hakuna jipya huko,mateso matupu kwani kwa umri kama niliokuwa nao sikuwa na uwezo wa kuzungumza na mume wangu juu ya masuala ya mahusiano” Anasema Edina na kuongeza kuwa

“Hivi sasa nimeongezea mama mzigo wa kulea kwakweli najuta kwa kosa nililonifanya na nimekwisha muomba mama msamaha” anasema Edina huku akilbubujikwa na machozi.

Edina anasema kuwa licha ya hivi sasa kuishi kwa mama yake mdogo tofauti na kijiji alipo mama yake anaongeza kuwa amekuwa akisumbuliwa na vishawishi kutoka kwa vijana wa kijiji hicho lakini kwa kuwa anajua madhara hawezi kurudia kosa na kwamba anawaona wavulana kama watu wakatili,waongo na wanaotaka kuwatumia mambinti kwa tamaa zao za kimwili tu.

Wataalamu wa afya wanasemaje

Katibu wa afya wa wilaya ya Karagwe Silvernus Manyinyi ,muuguzi wa Afya wilayani humo Esheza Mwombeki na Bibi afya wa wilaya hiyo Beatrice Laurent wamelieleza gazeti hili kuwa hata wao hawana jibu sahii kuhusu chanzo cha vijana wengi katika wilaya hiyo kujiingiza kwenye vitendo vya ngono wakiwa na umri mdogo.

“Hata sisi juzi tulikuwa tunajiuliza kwenye kikao,kuhusu kasi ya vijana wa wilaya hii kupenda ngono hatujabaini sababu za kitaalumu lakini tunadhani ongezeko la shule za sekondari za kata limechangia kwani baadhi yao wanapanga uraiani hivyo wanakuwa huru mno”anasema Bi Beatrice Laurent.

Anaongeza kuwa hata malezi duni kutoka kwa wazazi wao,mmomonyoko wa maadili na watoto kutazama filamu na picha chafu zilizoko hata kwenye simu za mikononi vinachangia kuharibu vijana.

Aidha wataalamu hao wanasema kuwa wamekuwa wakitoa elimu juu ya masuala ya uzazi kupitia kampeini ya Ishi na kwamba kupitia njia hizo mipira ya kiume husambazwa bure miongoni mwa vijana na katika vituo vya afya ingawa walikiri kuwa usambazaji wa mipira hiyo huwa ni changamoto.

Bajeti ya Ngazi ya wilaya kuondoa tatizo.
Licha ya tatizo la mimba kuwepo wilayani humo tangu mwaka 2008 lakini hakuna mkakakati wa moja kwa moja wa kuondoa tatizo hilo kwani bajeti ya halmshauri ya wilaya ya Karagwe kwa mwaka 2008/2009 kwenye idara za sekta ya afya na elimu hapakutengwa fedha yoyote ya kuondoa tatizo hilo bali walitenga sh 385,818,005 kwa shughuli mbalimbali za afya bila mpango wa kutatua tatizo la mimba mashuleni.

Hata idara ya Elimu iliyotengewa sh 274,500,000 kwa mwaka huo ilijielekeza kwenye utengenezaji madawati,ujenzi wa matanki ya maji,ujenzi wa vyoo,ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu wakati kwenye idara ya ustawi wa jamii walipanga kutumia sh 338,482,000 lakini katika kiasi hicho hakuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya kuondoa tatizo la mimba za utotoni.

Hata hivyo kwa mjibu wa kitabu cha Bajeti cha Halmashauri hiyo kwa mwaka huo ,Halmashauri hiyo ya Karagwe kwenye idara hiyo ya ustawi wa jamii ilipanga pamoja na mambo mengine kutumia sh 10,170,00 ili kusambaza vipeperushi kwa ajili ya watu kubadili tabia juu ya suala la UKIMWI na sh 15,000,000 kwa ajili ya kulipa ada wanafunzi ambao ni Yatima.

Hata Bajeti ya mwaka 2009/2010 ni sawa na bajeti iliyopita kwani kwa mwaka huo tofauti na ya zamani zilitengwa sh 395,347,709 kwa idara ya afya, sh 301,507,000 kwa idara ya elimu na sh 201,568,000 kwa idara ya ustawi na maendeleo ya jamii.

Hata hivyo katika bajeti zote hizo hakuna popote ambapo Halmashauri inapanga kujenga mabweni kwenye shule za kata kama mapendekezo ya wakazi wa wilaya hiyo kwamba yanaweza kupunguza idadi ya mimba wilayani humo.

Uchunguzi kupitia kabrasha la Bajeti ya Halmashauri umegundua kuwa Halmshauri hiyo inajikita zaidi katika kutenga fedha nyingi kupitia idara tajwa katika kuhudumia yatima,wajane na wagonjwa wa Ukimwi wakati vyanzo vya kupatikana kwa yatima ambacho hasa ni mimba za utotoni ambapo wahusika hutelekeza watoto,Wagonjwa wa Ukimwi ambacho ni hasa ngono zembe havitengewi pesa yoyote.

Katika uchunguzi baadhi ya vijana walibainisha kukosa huduma ya mipira ya kiume (kondom) kama njia ya kudhibiti maambukizi ya UKIMWI na mimba lakini katika bajeti ya Halmashauri haikutengwa fedha yoyote ya kusambaza kondomu hizo bure au kwa malipo.

Licha ya ukosefu wa mipira hiyo uchunguzi wa gazeti hili katika maduka wilayani Karagwe umebaini kuwa kasha moja la kondomu (za shirika la PSI) lenye kondomu 72 ndani linauzwa tsh 2,500 tu katika maduka ya jumla katika wilaya hiyo.

Lakini katika Bajeti ya Halmshauri ya wilaya hiyo ya 2009/2010 imetengwa sh 4,000,000 kwa ajili ya kufanya mikutano ya tathimini na wadau mbalimbali wa UKIMWI kiasi ambacho kinatosha kununua makasha 1600 yenye kondom 115,200.

Mkakati wa Wizara ya afya
Wizara ya afya na ustawi wa jamii imekuwa ikitoa matangazo kwenye vyombo vya habari yanayohamasisha jamii kukemea na kuwadharau watu hasa wanaume wanaowarubuni kingoni watoto wa kike .

Wizara inatumia dhana hiyo ambapo mtu anayeitwa ‘fataki’anazomewa au kudhauliwa na jamii ili aogopwe kwa tabia za kufanya mapenzi na mabinti wadogo.
Hata hivyo kupitia tangazo hilo hakuna popote ambapo mabinti wanahimizwa kujilinda wao wenyewe au kuacha tamaa.

Kauli ya Rais Jakaya Kikwete juu ya tatizo hilo Kitaifa
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete alitolea ufafanuzi juu ya tatizo la watoto wadogo kujingiza katika ngono wakiwa na umri mdogo na mimba za utotoni wakati akijibu swali la mtoto Rehema Abbas wa Dar es Salaam ,wakati alipokutana na baraza la watoto kutoka mikoa mbalimbali, ikiwa ni maadhimisho ya kilele cha mtoto wa Afrika ambapo watoto hao walipata nafasi ya kumuuliza Rais maswali mbalimbali hapo Juni 15,2010

Mtoto Rehema alitaka kufahamu Serikali ina mpango gani kwa wanafunzi wanaopata mimba kuendelea na masomo yao hata baada ya kujifungua.

Rais Kikwete alisema kuwa wanaume wasiwe ‘mafataki’ bali wawaache watoto wa kike wasome kwamba wanaume wanapaswa kuwafuata wanawake wakubwa wenzao na si watoto, na kwamba, wanawake wapo wengi.

“Ninacho waomba wanafunzi wa kike washugulike na masomo, mambo ya mimba yaacheni… kina baba waacheni watoto wa shule kina mama watu wazima wamejaa tele acheni kupiga ufataki” Rais Kikwete alisema..

Kuhusu suala la wanafunzi wanaobeba mimba kuruhusiwa kuendelea na masomo alisema kuwa wananchi wana mtazamo tofauti kuhusu suala hilo kwa kuwa,wapo wanaharakati wanaosema sawa na wengine wanaohusika na maadili wanasema suala hilo halifai.

Alisema hoja zote wanazotoa ni za msingi na zenye uzito unaostahili lakini bado hawajafikia mwisho ila inaonyesha kuwa katika hilo wakiruhusiwa wanafunzi hawataogopa kujiingiza katika vitendo vya ngono na kupata mimba.

Mtoto Zulekha Kipupwe kutoka Pwani aliuliza kama serikali inafahamu matatizo ya shule za kata ikiwa ni pamoja na kukosa nyumba za walimu, vitabu, maabara, na waalimu.

Rais alisema, ni kweli mpango wa kujenga shule za kata serikali ilifikiri kama ingechukua miaka mitano kukamilika, lakini fursa hiyo ilisababisha ongezeko la shule nyingi na kusababisha kasi ya ujenzi kuwa kubwa kuliko matarajio ila katika ujenzi huo haukuzingatia kujenga maabara katika shule hizo.

Alisema Serikali inatafuta fedha ili kujenga maabara katika shule nchini,na kwamba,Serikali ya Marekani imekubali kutoa fedha kwa ajili ya kuchapisha vitabu na vingine vitanunuliwa.

Kikwete amesema, kuna mradi mkubwa wa kujenga nyumba za walimu,na kwamba kila mwaka serikali itatenga Sh. bilioni 50 kujenga nyumba za walimu kukabiliana na tatizo hilo hivyo katika miaka mitano ijayo tatizo litapungua.

“Sekta ya elimu hatuna mashaka nayo, tumetenga Sh. trilioni mbili katika bajeti ya mwaka huu 2010/2011 kwa maendeleo ya elimu nchini,” alisema Rais Kikwete.

Mwandishi wa Makala haya anapatikana kwenye simu namba 0754527358,

Chanzo Malengo Yetu,julai 6,2010
 
Back
Top Bottom