Machi 24, Siku ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu Duniani

Sildenafil Citrate

JF-Expert Member
Jan 29, 2021
573
2,553
Kifua kikuu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya bakteria na huenezwa kwa njia ya hewa. Mtu mwenye maambukizi ya kifua kikuu akikohoa, kupiga chafya au kutema mate ovyo husambaza vijidudu hivyo hewani, huweza kumwambukiza mtu mwingine.

Siku hii huadhimishwa Machi 24 kila mwaka ili kuongeza ufahamu na nguvu katika kupambana na janga hili la kidunia. Ni kumbukumbu ya Machi 24, 1882, siku ambayo bakteria wanaosababisha ugonjwa huu waligunduliwa rasmi na Dr. Robert Koch

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Ndiyo, tunaweza kukomesha Kifua Kikuu"

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2021, watu milioni 10.6 waliugua ugonjwa huu huku wengine milioni 1.6 wakipoteza maisha.

Akizungumza na HabariLeo, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma jijini Dar es Salaam, Dokta Mbarouk Seif Khaleif Machi 15, 2023 alisema Tanzania kila mwaka watu 137,000 huugua TB na husababisha vifo 32,000, sawa na vifo 87 kila siku ambapo kati ya vifo hivyo, 33 ni vya waliokuwa wanaishi na virusi vya ukimwi (WAVIU). Alisema Kifua Kikuu ni janga linaua kimya kimya na hugharimu wastani wa asilimia 7 ya pato la taifa huku Dar es Salaam ikiwa kinara kwa asilimia 17.

Dalili za ugonjwa huu-
  • Kukohoa kwa muda wa wiki 2 au zaidi
  • Maumivu ya kifua
  • Homa za usiku
  • Kutoka jasho kwa wingi usiku
  • Kupungua uzito
  • Kukohoa damu
  • Kukosa hamu ya kula na mwili kuwa dhaifu
Bacille Calmette-Guérin (BCG) ni chanjo inayotumika katika kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu. Kwa Tanzania, chanjo hii huchomwa kwenye bega la mkono wa kuume.

Hutolewa baada ya mtoto kuzaliwa au pindi anapofika kliniki kwa mara ya kwanza. Kutokutokea kwa kovu baada ya kuchomwa sindano hutoa ishara kuwa chanjo husika haikuonesha ufanisi hivyo hupaswa kurudiwa katika kipindi cha miezi 3.

Ugonjwa wa kifua kikuu ni hatari. Mzazi au mlezi hakikisha kila mtoto anapozaliwa anapata chanjo ya kuzuia ugonjwa huu.

Aidha, matibabu ya ugonjwa huu huchukua muda mrefu kati ya miezi 6, 12 au hata zaidi ya hapo. Ni muhimu kwa wagonjwa kutumia dawa vizuri ili kuepusha madhara makubwa ya ugonjwa huu ikiwemo kifo.
 
Kuna umuhimu wa kichomwa chanjo ya ndui ikiwa ugonjwa huu ni kama haupo tena?
Walao kupunguza sindano kwa watoto wetu , maana zina karibia sindano 9 chink ya miaka 3
 
Kuna umuhimu wa kichomwa chanjo ya ndui ikiwa ugonjwa huu ni kama haupo tena?
Walao kupunguza sindano kwa watoto wetu , maana zina karibia sindano 9 chink ya miaka 3
Boss hii siyo sindano ya ndui (small pox). Hii ni sindano ya kifua kikuu ambayo ndiyo huitwa BCG.
 
basi kuna wajinga huku mitaani wanakwambia hio ni alama ya kuonesha wewe ni Mtanzania.

kama huna hio basi wewe ni mkimbizi.

hii Nchi 🙌
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom