Changamoto za uteuzi wa wagombea na matakwa ya kisheria

Kinjekitile junior

JF-Expert Member
Apr 20, 2015
4,404
581
Uteuzi wa wagombea ni moja ya hatua muhimu katika mchakato wa Uchaguzi na katika chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni na umekuwa ukiibua changamoto kwa baadhi ya vyama vya siasa.

Changamoto hizo zimejitokeza kuhusiana na sifa binafsi za mgombea, masharti ya uteuzi wa wagombea na ujazaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi kwa muda unaokubalika kisheria.

Kwa kuwa uteuzi wa wagombea unafanyika mintaarafu Sheria za Uchaguzi, baadhi ya wagombea wamejikuta wakienguliwa wakati wa uteuzi kutokana na kushindwa kukidhi matakwa ya kisheria.

Kanuni ya 31 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na ile ya 21 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani (2015) zinamtaka mtu anayetaka kugombea ubunge au udiwani kuwasilisha barua ya utambulisha kwa msimamizi wa Uchaguzi.

Barua hii huandikwa na Katibu wa Mkoa au Wilaya wa chama cha siasa anachotoka mtu huyo anayetaka kugombea ambayo huthibitisha kwamba mtu huyo ni mwanachama wa chama hicho.

Hata hivyo, ianapokosekana Katibu wa Mkoa au Wilaya ni lazima kuwepo kielelezo cha kuthibitisha kuwa aliyetajwa kwenye barua ya utambulisho ndiye kiongozi halali anayekaimu nafasi hiyo.

Baada ya mgombea kuwasilisha barua ya utambulisha au kwa kumtumia mwakilishi yeyote kwa niaba yake kwa Msimamizi wa Uchaguzi, atakabidhiwa fomu Namba 8 ya uteuzi.

Fomu ya uteuzi hujumisha maelezo binafsi ya mgombea na iwapo amewahi kushtakiwa na kuhukumiwa kwa kosa la jinai, uthibitisho wa chama cha siasa wa kumteua mgombea, idadi ya majina na namba za kadi za wapigakura waliomdhamini, tamko la kisheria la mgombea na uthibitisho kwamba mgombea ameweka dhamana.

Changamoto iliyopo kuhusu nukta hii ni kwamba baadhi ya wagombea wamekuwa wakiamini kuwa kuhukumiwa kwa kosa lolote la jinai (lisilokuwa la kukwepa kulipa kodi) ni kukosa sifa.

Matokeo yake mgombea anatoa taarifa zisizo za kweli kukwepa kile anachofikiria ni kosa lakini kwa upande wa pili anajitia hatiani kwa kutenda kosa la kusema uongo na hivyo kujikuta akienguliwa.

Ni jambo la kisheria wakati wa kujaza fomu ya uteuzi, mgombea akathibitisha tamko la kisheria la mgombea kwa saini ya Hakimu na muhuri wake, badala ya kutumia saini na muhuri wa Wakili.

Kuhusu sifa, ili mtu aweze kuteuliwa kugombea ubunge au udiwani anatakiwa kuwa mwanachama wa chama cha siasa, awe na umri kuanzia miaka 21, awe raia wa Tanzania, na anayejua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza.

Ni lazima awe mkazi wa Halmashauri yenye kata anayogombea (udiwani), awe na kipato halali kinachomwezesha kuishi (udiwani) na awe hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa la kukwepa kulipa kodi kwa miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Pamoja na kuwa na sifa hizo, mgombea anaweza kupoteza sifa iwapo anatumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita gerezani au yuko uhamishoni (Deportation Ordinance) au amezuiliwa na sheria yoyote kujiandikisha kuwa mpiga kura.

Mgombea pia atapoteza sifa iwapo ana maslahi katika mkataba na Halmashauri au kampuni yenye mkataba na Halmashauri na hajaitangaza kwenye magazeti ya Kiswahili au Kiingereza yanayopatikana katika Halmashauri husika juu ya maslahi hayo.

Ili mgombea aweze kuteuliwa kugombea ni sharti awe amedhaminiwa na wapigakura walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapigakura wasiopungua kumi (udiwani) au wapigakura 25 (ubungea) walioandikishwa ndani ya kata au jimbo analogombea.

Mgombea anatakiwa kuambatanisha picha nne za passport zilizopigwa ndani ya miezi 3 kabla ya siku ya uteuzi, atatakiwa kulipa dhamana ya Sh. 5,000 (udiwani) na Sh. 50,000 (Ubunge).

Mgombea atawasilisha fomu ya uteuzi katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi au Msaidizi wake si chini ya saa kumi kamili jioni ya siku ya uteuzi.

Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutoa nafasi kwa wagombea kupeleka fomu zao siku tatu kabla ya siku ya uteuzi ili zikaguliwe na kuona kama zimekidhi vigezo na masharti ya uteuzi na kasha kurudishiwa ili kusubiri siku ya uteuzi.

Pamoja na nafasi hiyo, wagombea wengi wamekuwa wakirejesha fomu dakika za mwisho na matokeo yake baadhi hujikuta wakikosa nafasi ya kugombea kwa sababu ya kushindwa kukidhi masharti ya kisheria hasa pale wanapohitaji kufanya marekebisho.

Suala la idadi ya wadhamini na uthibitisho wa mpigakura anayemdhamini mgombea nalo limekua likiibua changamoto kwa baadhi ya wagombea kutumia wadhamini wasiokubalika kisheria.

Mbali na kuwasilisha fomu ya uteuzi, mgombea hutakiwa kujaza Fomu Namba 10 ya kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 iliyojazwa kwa Usahihi.

Iwapo mgombea anataka kumuwekea pingamizi mgombea mwenzake sheria zinamtaka awasilishe pingamizi ndani ya saa 24 baada ya uteuzi na kueleza sababu zinazokubalika kisheria.

Mgombea anapowekewa au kuweka pingamizi anatakiwa kuwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi majibu yenye vielelezo vya kisheria ndani ya saa 24 baada ya kupokea pingamizi hilo.

Kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kikanuni katika uteuzi wa wagombea, changamoto zilizojitokeza katika hatua hii muhimu ya mchakato wa uchaguzi zinaweza kupata ufumbuzi.
 
Back
Top Bottom