Changamoto ya Mazingira kwenye miradi mikubwa, maeneo yanageuzwa dampo

Changamoto ya Mazingira kwenye miradi mikubwa, maeneo yanageuzwa dampo

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
28
Reaction score
19
WhatsApp Image 2026-05-14 at 14.23.19.jpeg
Wakazi wa Kata ya Chamwino, Manispaa ya Morogoro, wameendelea kuishi katika mazingira yenye hatari kubwa za kiafya, kiusalama na kimazingira kufuatia kutofanyiwa usafi wa mara kwa mara maeneo yaliyopitiwa na miradi mikubwa ya serikali ikiwemo Bomba la Mafuta la TAZAMA na Grid ya Taifa ya Umeme inayosimamiwa na TANESCO.

Maeneo hayo yamegeuka kuwa vichaka vinene na dampo lisilo rasmi la taka, hali inayosababisha harufu kali ya mizoga, uchafuzi wa hewa na mazingira, pamoja na kuibua hofu ya mlipuko wa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, homa ya matumbo na magonjwa ya mfumo wa hewa. Baadhi ya wananchi wanasema hali hiyo imeathiri maisha yao ya kila siku, shughuli za kiuchumi na ustawi wa kijamii.

‘‘Kiukweli tunateseka sana na harufu ya mizoga ambayo huwa inatupwa kwenye vichaka na afya zetu zinakuwa hatarini, na tunakosa amani hatuwezi hata kufanya ujasiriamali wa kuuza maandazi kwa sababu ya harufu’’ anasema Metruda mkazi wa mtaa wa Mwembeni kata ya Chamwino.

“Kulingana na hali ilivyo katika eneo hili tulikuwa tunawaza kuna siku tungekuta maiti kwasababu tulikua tunaona vituko vya kila aina, kuna siku tunakuta mbwa katupwa, taka zimetupwa pakawa kama dampo tukaamua kuchoma moto” anasema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Mbali na hatari za kiafya, vichaka hivyo vimekuwa tishio la kiusalama. Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwembeni, Bi. Hadija Salum Madegwa, anasema vichaka virefu vimekuwa makazi ya nyoka na sehemu ya kujificha wahalifu, hali inayowaweka wakazi katika hatari ya kushambuliwa au kuibiwa.
WhatsApp Image 2026-05-14 at 14.23.18 (1).jpeg

WhatsApp Image 2026-05-14 at 14.23.18.jpeg
“Ndani ya mitaa hali ya usafi iko sawa, lakini kwenye maeneo ya TAZAMA na TANESCO majani yanakuwa makubwa sana. Nyoka wanatokea, vibaka wanajificha, na wananchi wanapata hofu kubwa,” alisema Bi Hadija.

Mwenyekiti wa mtaa wa Malipula kata ya Chamwino Shaban Issa Kikova moja ya mitaa iliyopitiwa na mradi huo amesema mtaa wake ni moja ya mtaa iliyosaini mkataba wa usimamizi wa ulinzi katika mkuza wa TAZAMA, na amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kwamba huwataarifu wahusika kupitia ripoti zao za kila mwezi na hatua stahiki za kufanya usafi huchukuliwa, na kwamba wananchi nao wanaruhusiwa kusaidia kudumisha mazingira kuwa safi bila kuharibu bomba au miundombinu mingine.

Amesema kwa mujibu wa Mkataba wa TAZAMA eneo lililopita mradi huo mwananchi haruhusiwi kufanya shughuli zozote za kiuchumi au kilimo, kuvamia na kujimilikisha maeneo, kutokana na hilo wameweka walinzi maalum wa kulinda maeneo hayo ili wananchi wasifanye uharibifu, maana hapo awali wananchi walikuwa wanafanya shughuli za kiuchumi na kilimo katika maeneo hayo ya TAZAMA na TANESCO.

Kifungu cha 81(1) cha sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 kinatoa jukumu kwa mmiliki wa mradi au mradi wa maendeleo kuhakikisha uhifadhi wa maeneo yanayopitiwa na mradi, ili kupunguza uharibifu wa ardhi, maji, hewa na misitu na hivyo kulinda mazingira na afya ya wananchi walioko jirani.

Naye mtendaji wa kata ya Chamwino, Rajabu Wanyamale amekiri uwepo wa changamoto hiyo hasa katika eneo linalosimamiwa na Tanesco kutokana na kushindwa kusafisha maeneo yao kwa wakati.

“Tanesco wamekuwa kikwazo kikubwa kwasababu hawasafishi maeneo yao kwa wakati na kama hawasafishi maeneo yao kwa wakati kuna taka ambazo moja zinapeperushwa na upepo na kunasa kwenye hayo maeneo, lakini vilevile watu kutokaa maeneo mengine wanaenda kutupa taka zao na kuzidampo pale” alisema Wanyamale.

Amesema wameshafikisha malalamiko hayo ngazi husika na yanaendelea kufanyiwa kazi, na kuongeza kuwa kwa upande wa TAZAMA wao wamekuwa wakijitahidi kusafisha maeneo yao mara kwa mara.

Kwa upande wake mhandisi wa kusafirisha umeme Mkoa wa Morogoro Amani Mbamba akijibu malalamiko hayo ya wananchi wanaoishi jirani na maeneo yaliyopitiwa na njia kubwa za umeme kwamba wanao utaratibu wa kusafisha maeneo hayo kila baada ya miezi miwili lakini kwa maeneo yaliyo mbali na makazi ya watu hufanya mara 1 kwa mwaka kulingana na bajeti iliyopo.

“Sisi wajibu wetu tunafanya usafi mara kwa mara, na kumbuka tunahudumia kilomita nyingi, haiwezi kuwa sawa na mtu mwenye shamba dogo kwamba kila siku unafyeka, tunakuwa na ratiba zetu lakini kwa wale wenyeviti wakiona tumejisahau eneo lao lile limekuwa critical (hali mbaya) wana namba zangu wengi wanaweza kunipigia, mbona wengi wanapigaga aaaaah! mhandisi huku umetusahau nawaambia ok watu wanakuja, na watu wanaenda kufanya usafi” alisema Mhandisi Mbamba.

Ameongeza kuwa baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakitaka kutumia maeneo hayo kufanya shughuli za kilimo au biashara jambo ambalo ni hatari kwao kutokana na maeneo hayo kuwa na umeme mkubwa voltage laki mbili na elfu ishirini (220,000) na huruhusiwi maeneo yale kama barabara bali eneo la kukatiza mara moja.

KAULI YA NEMC
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro-Rufiji, Arnold Mapinduzi anasema kwa mujibu wa kifungu cha 81 cha sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 ni lazima miradi yote ifanyiwe tathmini ya athari za mazingira (EIA) kabla ya mradi kuanza na kwa miradi ambayo ilianza kabla ya sheria ya mazingira sheria inawataka kufanya ukaguzi wa mazingira (Environmental Audit).

Anasema, “iwe miradi ya TAZAMA ina maana TAZAMA wana jukumu hilo, iwe miradi ya TANESCO wana jukumu, tutampa cheti TANESCO sasa TANESCO jukumu lake ni kuhakikisha ule mpango wa usimamizi wa mazingira aliyojiwekea na yale masharti anayazingatia, ambayo kimsingi ndio yanayompa cheti na ndio mkataba kati yake na serikali na sisi ndio wafuatiliaji wa huu mkataba” alisema Mapinduzi.

Mapinduzi amesema ikiwa mwenye mradi anaenda tofauti watamkumbusha kutekeleza na kuzingatia masharti ya kibali chake, wanamkumbusha kwa barua na akionekana mtu huyo ameamua kutokuelewa basi wanaweza kumpiga faini ili kumsaidia yeye kukumbuka kuwa anatakiwa azingatie nini kwenye mambo ya mazingira katika mradi wake.

Hata hivyo aliongeza kuwa hajapokea malalamiko yoyote kwenye ofisi yake kuhusiana na miradi hiyo.

"Tukipata malalamiko kama hayo tunafuatilia na tunawahusisha wahusika wenyewe wafanye, sababu ni jukumu lao sheria inasema kila anayechafua au anayeharibu ni jukumu lake kusafisha, ni jukumu lake kutengeneza, lazima ahakikishe kwamba haathiri maisha ya watu na viumbe wengine ndo sababu sheria imewekwa hivyo” alisema Mapinduzi.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na usafirishaji Manispaa ya Morogoro Hezron Ligala amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano na mamlaka nyingine na kuna maeneo ambayo mamlaka zenyewe zinatakiwa kufanya usafi ikiwa ni pamoja na Barabara za TARURA, TANROADS, maeneo ya hifadhi za reli na maeneo mengine pamoja na Bomba la mafuta TAZAMA.

“Tumekuwa tukiwaandikia barua tunapoona changamoto hiyo, tunawaandikia barua ambapo pia hata kata wana mamlaka hayo, kwamba wanapoona eneo lao lina changamoto ya kuota nyasi na mambo mengine na ni taasisi fulani wanaiandikia barua kukumbusha usafi huo ufanyike” alisema Ligala.

Ameongeza kuwa Manispaa ya Morogoro ina jumamosi ya kila mwisho wa mwezi ambayo sasa inamtaka kila mwananchi kufanya usafi katika eneo lake, wamekuwa wakitumia siku hiyo kufanya uhamasishaji kwa njia ya matangazo na barua za kuhamasisha ambazo zinatumwa kwa watendaji wa kata na makundi sogozi mbalimbali ya wananchi ili kila taasisi na kila mwananchi afanye usafi kwenye eneo lake na kuimarisha zaidi hali ya usafi.

ANDIKO LA: Na Elizabeth Tanzania
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.

Pia soma ~ Tani 100 za taka zinavyobaki mitaani Morogoro
 
Back
Top Bottom