Changamoto ya kufufua mchakato mpya wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

zacha

JF-Expert Member
Feb 28, 2009
1,190
1,828
(na cde Agathon Simba Ulanga)

Baada ya kuisoma Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoitwa “Katiba Inayopendekezwa Oktoba 2014”, nilisema afadhali kuwa mchakato uliishia pale ulipoishia.

Kwani Rasimu ile ingekubaliwa na kupitishwa, historia ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ingetikisika, na historia ya Taifa hili, ingerudishwa nyuma mpaka kabla ya mwaka 1977.

Hii ni, kwa sababu mwaka 1977 una umuhimu wa pekee katika historia ya CCM na Taifa. Mwaka 1977 ulikuwa ni mwaka ambao Mapambano ya kupigania uhuru wa Nchi zetu, Uasisi wa Mataifa yetu na Uasisi wa Taifa la Tanzania kwa kutumia dhana ya Taifa ulifikia mustakabali.

Dhana ya Taifa ilikuwa katika Maono ya Baba wa Taifa, Mwl. J. K. Nyerere, tangu wakati wa kupigania uhuru.

Ndiyo maana baada ya Uhuru wa Tanganyika tarehe 9/12/1961, ilipofika tarehe 22/1/1962, alijiuzulu Uwaziri Mkuu. Mapokeo yanatuambia kuwa:-

a) Alitaka apate nafasi ya kujifunza vitendo katika jamii kwa lengo la kudumisha Uhuru na Umoja.

b) Kufanya Maandalizi ya Kuasisi Taifa kwa kutumia dhana ya Taifa ili nchi ya Tanganyika itoke kabisa kuwa nchi chini ya Taifa la Uingereza.

c) Kuendeleza fikra zake za Mfumo wa Jamii wa kupiga vita ukoloni na mfumo wake wa jamii wa kibepari. Katika hotuba kwa njia ya Radio, tarehe 30/5/1962 aliwaeleza wananchi wa Tanganyika lengo la kufanya nchi ya Tanganyika kuwa Jamhuri – Taifa.

Katika kueleza fikira za Mfumo wa Jamii aliotaka kuasisi ili kupambana na ukoloni na Ubepari katika Taifa jipya, aliandika ile Insha Mashuhuri inayoitwa “Ujamaa – the Basis of African Socialism”. Ilipofika tarehe 9/12/1962, Nchi ya Tanganyika ikawa, Jamhuri – Taifa.

Kupatikana kwa Jamhuri, kulimpa nafasi Baba wa Taifa kuanza safari ndefu na ngumu ya kuasisi Taifa kwa kutumia dhana ya Taifa inayohusu:-

a) Kutofautisha kati ya Nchi na Taifa. Nchi ni Utawala na Taifa ni Uongozi na Siasa.

b) Utambuzi wa Taifa – Katika kuwa katika Jamii ambayo inagawanyika kitabaka, utambuzi wa Taifa lazima uonyeshe ni Mfumo gani wa Jamii utatumika katika Jamii- kuweka lengo la Taifa.

c) Mikakati ya kuwaletea wananchi maendeleo. Taifa husika lazima liwaletee wananchi maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.

Kwa kuwa fikra za ujamaa alikwisha zieleza katika ile insha mashuhuri, ilipofika mwishoni mwa mwaka 1962, Ujamaa uliingizwa rasmi katika Katiba ya TANU.

Aidha fikra hizo zilikifikia chama cha Afro-shirazi-ASP-kule Zanzibar na kwamba ilipofika tarehe 12/1/1964 Chama cha ASP chini ya Uongozi wa Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, kilifanya Mapinduzi na kuifanya Zanzibar kuwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar-Taifa.

Na ilipofika tarehe 26/4/1964 Mataifa mawili – Taifa la Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar – Taifa-waliungana na kuwa Taifa moja – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuliyo nayo sasa.

Kwa hiyo fikra za kuasisi Taifa zikaunganishwa, na kuwa fikra za kuasisi Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa hiyo, katika utaratibu ule, dhana ya tofauti ya Nchi na Taifa ilitumika kwa Taifa la Tanzania kuwa na Nchi mbili kiutawala. Nchi ya Zanzibar na Nchi ya Tanzania Bara. Lakini Taifa moja. Hiyo ndiyo ilikuwa hoja ya Serikali mbili kutawala Nchi na Wananchi na Kuongozwa na Taifa moja.

Katika Utambuzi, ilikubalika kuwa Taifa liitwe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfumo wa Jamii uliokubalika ili uwe Lengo la Taifa ni Ujamaa na badaye ukawa Ujama na Kujitegemea.

Ninasema Lengo kwani jambo hilo lilitegemea Mikakati nitakayoieleza baadaye, ikiwa ni pamoja na Urasimishaji ya Lengo katika Mustakabali wa Taifa, ijapokuwa vyama vya siasa vinaweza kuwa vingi. Mtazamo wa kiyakinifu ni Taifa kwanza na Siasa inafuata, baada ya Ukombozi wa Nchi.

Kuhusu Mikakati ya kuwaletea wananchi maendeleo ilikuwa lazima ielezwe kisheira, Taifa jipya walikubaliana kutumia Katiba ya Muda ili kusubiri Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ilipofika mwaka 1967 Ujamaa na Kujitegemea, ulikabidhiwa rasmi kwa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU). Makabidhiano haya yalifanywa kule Arusha kwa:-

a) Kutoa semina Elimishi na Elekezi kwa Wajumbe wa Kikao Kikuu cha Uongozi na Utendaji katika Chama kinachoitwa Halmashauri kuu ya Taifa.

Kikao kilianza tarehe 26/1/1967 – 29/1/1967 kwa semina elimishi na elekezi kuhusu :-

(i) Imani ya TANU – Ujamaa.
(ii) Sera za msingi za TANU – Madhumuni ya TANU
(iii) Siasa ya TANU – Ujamaa na kujitegemea
(iv) Masharti ya maendeleo.
(v) Uanachama.

Hitimisho la semina ile ilikuwa kuweka Miiko kwa Wanachama wanaotaka kuwa au Viongozi au Watendaji wa Chama. Mambo yote yaliyofanyika katika semina ile yaliandikwa katika kile kitabu kinachoitwa “Azimio la Arusha na Siasa ya TANU juu ya Ujamaa na Kujitegemea.

Mambo mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusu Ujamaa na kujitegemea na Azimio la Arusha, lakini katika Makala hii napenda kusema:-

1. Baba wa Taifa alibuni Ujamaa - ili kuwa na Mfumo wa Jamii wa kupambana na hatimaye kuuondoa ubepari. Uthibitisho upo aliposema, “nilikuwa wa kwanza kutumia neno “Ujamaa” ili kueleza aina ya maisha ninayotaka tuishi katika Nchi yetu …” Alimalizia maelezo haya kwa kusema “Hivi ndivyo tunavyotaka kuishi kama Taifa. Tunataka Taifa lote tuishi kama familia moja”. (Uhuru na Ujamaa uk 137 – tafsiri ni yangu) ona alivyoonyesha tofauti kati ya Nchi na Taifa.

Aidha alisema “kwa hiyo Ujamaa unaeleza mawazo yetu. Unapinga Ubepari ambao shabaha yake ni kuunda nchi zenye raha kwa msingi ya kunyonyana”. (Ujamaa Uk.12).

2. Kuhusu sababu za Ujamaa, Baba wa Taifa alisema, “sababu kubwa ya kuwa na Ujamaa ni maisha bora ya watu, na msingi wake mkubwa ni watu kuukubali usawa wa binadamu” (Ujamaa Uk. 75)

3. “Na Ujamaa - ni kutimiza Imani ya usawa kwa binadamu katika mambo ya uchumi na maendeleo, Imani ambayo ilikuwa msingi wetu wa malalamiko wakati tulipokataa kuwa si haki Taifa jingine lolote kututawala. (Ujamaa Uk. 99).

4. Ujamaa una sura mbili - Baba wa Taifa alisema Ujamaa una sura mbili- Imani na Siasa (Kujitawala ni Kujitegemea Feb.5, 1987 – Dodoma). Sura hizi mbili za Ujamaa hazitenganishwi.

Ujamaa ni Imani kuhusu:-

a) Uhuru-Ukombozi wa nchi kisiasa na kiuchumi, kwa njia ya kujitegemea, uzalendo.

b) Umoja - Uasisi na Utambuzi wa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mikakati ya ujenzi wa Ujamaa kwa njia ya kujitegemea. Ujamaa Vijijini na Sera mbalimbali kama nitakavyoonyesha hapo baadaye.

c) Usawa – Udugu, utu, upendo, uaminifu, ukweli, ushirikiano, utamaduni wa Taifa, uwezeshaji wananchi kiuchumi kijamaa, usimamizi wa sera za kijamaa, kupinga uonevu, unyonyaji, kupuuzwa, ufisadi na jambo lolote la kibepari au kikabaila.

Kwa kuwa Ujamaa ni Imani – ndio maana Azimio la Arusha linasema, “lakini Ujamaa hauwezi kujijenga wenyewe. Kwani Ujamaa ni Imani. Hauna budi kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake”. (Azimio la Arusha uk 7).

Azimio linaendelea, “wajibu wa kwanza wa mwana TANU na hasa kiongozi wa TANU, ni kutii kanuni hizi za Ujamaa hasa katika maisha yake mwenyewe”.

(Azimio la Arusha uk 8). Ndiyo maana Viongozi waliwekewa miiko katika Azimio lile. Azimio liliwataka viongozi wawe waamini wa Uhuru, umoja na usawa. Katika TANU na baadaye CCM Imani kuhusu Ujamaa ni jambo la msingi na halitakiwi kubadilika.

Ujamaa ni Siasa - Aidha Azimio lilisisitiza kuwa Ujamaa ni Siasa ya kutumia dhana ya Uongozi.

Azimio liliwakumbusha viongozi walikotoka katika mapambano ya kudai uhuru kwa kusema “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi, mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena”

Siasa ya Ujamaa inatokana na tafsiri ya Imani na kuiweka katika sera kwa ajili ya utekelezaji – matumizi katika siasa. Ndiyo maana kuna siasa ya ujamaa.

Baada ya Azimio la Arusha TANU ilijipanga kiuongozi ili kuasisi mikakati ya kuitafsiri Imani ya TANU – Ujamaa na kujitegemea na kuuweka katika Sera ili zitumike katika Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Baadhi ya mikakati hiyo ilikuwa:-

1. Uamuzi wa kuitumia Dola- katika kujenga Ujamaa kwa njia ya kujitegemea. Mali za Mabepari zilitaifishwa. Dola ilielekezwa kuingia moja kwa moja katika kuendesha uchumi wa Taifa.

2. Kuimarisha Taasisi za Ujenzi wa Taifa – Jeshi la kujenga Taifa. Viongozi wa TANU na Serikali walishiriki katika mafunzo ya Uzalendo katika kambi za Jeshi la kujenga Taifa.

3. Kuimarisha dhana ya Uongozi - kwa kupanua vyuo vya TANU na kuwateua viongozi wa TANU na Serikali kuhudhuria mafunzo kuhusu Ujamaa na kujitegemea na Uzalendo.

4. Azimio la Arusha baada ya miaka kumi – tathmini iliyofanya Baba wa Taifa ilibaini:-

4.1 Kusimamisha na kuondoa kujigawa katika matabaka ya wanyonyaji na wanyonywaji.

4.2 Kubadili dira ya maendeleo ya Taifa na kufanya rasilimali yetu itumike kwa kutosheleza mahitaji ya Taifa

4.3 Kuanzisha tabia, ya kuwa wajamaa - ndugu.

4.4 Kujenga vyombo vingi vya kujiwekea mikakati na mbinu za kupeleka Taifa kweye Ujamaa.

4.5 Kupiga hatua muhimu katika kuwapatia wananchi huduma za afya, elimu na usafirishaji wa Umma.

4.6 Kujenga utamaduni wa kitaifa kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

4.7 Taifa kuendelea kutimiza wajibu katika ukombozi wa Bara la Afrika.

La kusisitizwa hapa ni kwamba sura mbili za ujamaa hazitanganishwi

Hata hivyo, alitoa tahadhari kuwa Taifa bado lina changamoto nyingi katika kuelekea kwenye lengo la kujenga Ujamaa. Aliwataka wanaotaka kuomba Uongozi wazingatie Miiko ya Uongozi ili waweze kuliongoza Taifa kwenye Ujamaa kwa kuzikabili changamoto za wananchi walio wengi.

Alionya kuwa jambo ambalo linaweza kuharibu maendeleo yetu ni kushindwa kupambana na rushwa, wizi, uharibifu wa mali na fedha za Umma, matumizi mabaya ya vyeo na uzembe.

Baadhi ya Sera zilizotafsiriwa kutoka Imani ya TANU ni:-

i. Ujamaa Vijijini (1967) – Sera hii ilitoa meelekezo na ufafanuzi kuhusu ujenzi wa Ujamaa vijijini. Kuwafanya wananchi waishi mahali pamoja ili iwe rahisi kuwapelekea huduma za jamii, - maji, afya, elimu, umeme, miundo mbinu, ili maisha ya vijijini yafanane na maisha ya mjini ili wananchi wasihamie mijini.

ii. Elimu ya kujitegemea 1967 – Elimu ni chomo cha mabadiliko, kwa hiyo falsafa yake lazima iendane na falsafa na lengo la Taifa ili wananchi katika kuelemika wapate maarifa ya kuyafahamu mazingira yao na ya ulimwengu ili waweze kuishi katika mazingira hayo na kuyatawala kwa mujibu wa lengo la Taifa, ili wajenge Ujamaa na waweze kujitegemea.

iii. Kitabu cha Ujamaa – 1968 – kitabu kile kilitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu mambo ya msingi yanayohusu ujamaa na kujitegemea.

iv. Waraka wa Rais Namba 1 wa 1969 – ulielekeza kwamba rasilimali kubwa ya Taifa ielekezwe vijijini kujenga Ujamaa na kujitegemea.

v. Mwongozo wa TANU 1971 – kwa kutumia kanuni ya wakati na mahali uliwaeleza wafanyakazi kuthamini kazi kuwa ni kipimo cha utu. Kuwa ulinzi wa Taifa ni jukumu la kila Mtanzania na kila Mjamaa – ndiyo chimbuko la Ulinzi wa Mgambo.

Umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika maamuzi ya mambo yanayohusu maendeleo yao. (Ibara za 13, 21, 28).

vi. Siasa ni kilimo – 1972 – ilisisitiza matumizi ya teknologia na kanuni bora za kilimo.
vii. Kila mtu afanye kazi 1976 – ililenga kuondoa uzururaji, unyonyaji na kusisitiza kuwa kila mwananchi na hasa mwana – TANU anakuwa mstari wa mbele katika kujenga Ujamaa na kujetegemea.

Wakati wote huo sera zilikuwa zinatoka kwenye Chama kwenda Serikalini. Aidha sera hizo zilikuwa ni mkakati wa kuurasimisha mfumo wa Jamii wa ujamaa na kujitegemea ili uwe rasmi Mfumo wa Jamii wa Taifa la Tanzania.

Tarehe 21-1-1977, ulifanyika Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP. Katika Mkutano ule, moja ya maazimio Makuu lilikuwa kukabidhi rasmi jukumu la kusimamia na kuendeleza Ujenzi wa Ujamaa kwa Chama kipya, ili kiurasimishe uwe mfumo wa Jamii wa Taifa la Tanzania, kwa kuuweka katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyotarajiwa kutungwa. Lengo ni kutaka Taifa litambulike kuwa ni la kijamaa na kujitegemea.

Ndiyo maana, katika kikao cha Bunge Maalum la Katiba kilichofanyika tarehe 25/04/1977, Baba wa Taifa alisema”. Chama cha Mapinduzi kimetoa maelezo ya mambo makubwa ya kutiwa katika katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Na alionya kuhusu umuhimu wa kuzingatia lengo kuwa, “Tukishindania hadhi na heshima za wongo na kweli tutagongana, tukijitahidi tu, kila mtu kwa uwezo wake, kuwahudumia wananchi tutasaidiana;

Mimi naahidi kwamba Chama kitajitahidi kutimiza wajibu wake wa Uongozi kwa kuzingatia katiba, sheria na utu - na hasa utu”. Lakini alilifananisha Taifa na kijana mwenye afya anayekua.

Alisema kuwa katiba ni kama vazi la huyo kijana anayekua ambaye anaweza kuhitaji vazi jingine kadri anavyokua. Kwa maelezo hayo alitegemea marekebisho ya Katiba kadri Taifa linavyokua.

Ndiyo maana marekebisho ya Katiba yaliyofanywa mpaka toleo la 2005 hayana matatizo katika kutekeleza dhana ya lengo la Taifa kuhusu Katiba. Yalikuwa yanarekebisha au kumshonea kijana vazi jingine akiachwa akiwa hai – hayakuwa marekebisho yaliyofanyika ya kulibomoa Taifa.

Baada ya kuurasimisha Ujamaa, CCM kiliendelea kuliongoza Taifa. Uongozi huo ulitolewa kwa kutumia dhana ya Uongozi wa kijamaa. Baadhi ya mambo yanayohusika na hoja yangu ni:-


1.0 Mwongozo wa CCM 1981 – Mwongozo ule ulifuatia Mwongozo wa TANU 1971. Mwongozo wa 1981, ulikuwa ni fikra madhubuti za CCM na ulifanya uchambuzi wa hali halisi na changamoto katika jamii.


1.1 Ibara 36 - ilichambua changamoto katika jamii, kuongezeka kwa
rushwa hujuma za kiuchumi, wizi, ujambazi na uharibifu wa mali ya Umma.

1.2 Ibara 52- ilionya kuwa ujenzi wa Ujamaa siyo lelemama, bali ni mapambano dhidi ya Ubepari, dhidi ya wapinga maendeleo, wababaishaji wa kisiasa, wahujumu uchumi, majambazi, wezi, wazururaji na wazembe.

1.3 Ibara 108 – Serikali ndiyo chambo kikuu cha kutekeleza sera za Chama. Serikali haibuni sera.

1.4 Ibara 159 – Inakumbusha masharti ya uongozi. Kuwa kiongozi wa CCM lazima awe na msimamo wa kijamaa. Itikadi yake ya Ujamaa, vitendo na tabia yake vidhirihishe kwa anaowaongoza kuwa ni vya kijamaa. Mwongozo unaonya kuwa Imani ya kiongozi inaambukiza anaowaongoza.

1.5 Ibara 160 – Inaonya kuwa msimamo thabiti wa kijamaa lazima uambatane na uwezo.


Uhai wa Chama 1985 – 1987 – Baba wa Taifa alifanya kazi ya kuimarisha Chama na ilipofika mwaka 1987 alifanya mambo yafuatayo:-

a) Kujitawala ni kujitegemea – Hotuba 5-2-1987. Baadhi ya mambo aliyosema ni “Azimio la Arusha ndilo linaloeleza itikadi ya Chama chetu. Ndilo msingi wa maamuzi yote ya sera za chama na serikali” alimaliza hotuba ile kwa kukitaka Chama kitoe ahadi mpya:-

i. Kikiimarisha Chama cha Mapinduzi
ii. Kulitekeleza Azimio la Arusha.
iii. Kujenga Ujamaa kwa njia ya kujitegemea na kwamba, CCM ni Chama cha kuongoza na kuongoza ni kuonyesha njia”.

b) Kufungua mkutano Mkuu – 22-10-1987 – Katika mkutano ule alizieleza kazi tatu za CCM

i. Kiendelee kusisitiza uhalali wa misingi na mwelekeo wetu wa Ujamaa na kujitegemea.

ii. Kikao kijadili jinsi ya kufikia malengo ya ujenzi wa Ujamaa na kujitegemea.

iii. Kukiimarisha Chama na hasa demokrasia ndani ya Chama.

Dhana ya Makada wa Chama – 1987 – kutolewa kwa mafunzo ya kwanza kwa Makada wa Chama (Training of Trainers – TOT) ili kuimarisha dhana ya uongozi wa kijamaa ndani ya Chama. Nilikuwa moja ya wanafunzi hao.

Program ya CCM 1987 – 2002 – Utekelezaji wa Azimio la Arusha katika kipindi cha Mpito. Nilikuwa moja ya wakufunzi.

Maamuzi ya Zanzibar – Inaelekea kuwa Manunuzi yale “Twende na Wakati” ndiyo yaliyoliondoa Azimio la Arusha katika Ujamaa na kubakiza siasa ya Ujamaa na kujitegemea.

Katika Azimio la Arusha –Ujamaa ni Imani. Nilisoma Gazeti la Mwananchi la April 2022, lililoandika,” kifo cha Azimio la Arusha kilivyomsononesha Mwalimu”.

Mwelekeo wa sera za CCM katika miaka ya Tisini – Mwelekeo ule:

i. Ndiyo uliobadilisha mkakati wa Ujenzi wa Ujamaa uwe wa kuwatumia wananchi badala ya kutumia Dola.

ii. Ijapokuwa ulisema katika Ibara ya Tano kuwa, siasa ya msingi ya CCM itaendelea kuwa ujamaa na kujitegemea, tafsiri yake ni kwamba uliacha sura moja ya ujamaa ambayo ni “Imani” iliyowekwa katika Azimio la Arusha.

Mfumo wa vyama vingi vya siasa – 1992 – Mfumo huu ulirudishwa wakati ambapo dhana ya Uasisi, Utambuzi na Urasimishaji wa lengo katika katiba Taifa, ulifikia mustakabali.

Katiba ikiwa ni Chombo kikuu cha Uongozi wa Taifa, cha kuongoza Taifa katika kutunga sheria za kutumiwa na serikali katika kutawala nchi na wananchi.

Kwa bahati mbaya, karibu vyama vyote vya siasa vilivyoanzishwa vilikataa katiba na kudai katiba mpya. Hii ina maana kuwa waliikataa dhana ya Taifa iliyotumika katika kutunga katiba. Waliikataa dhana ya taifa kwanza na siasa baadaye katika dhana ya taifa.

Kwa bahati mbaya kama nilivyosema hapo juu, ndani ya CCM ilikwisha ingia changamoto ya Azimio la Arusha, Mamuzi ya Zanzibar na mwelekeo wa sera.

Hali hiyo ilizaa kutoelewana ndani ya chama – kushindania hadhi katika Muungano na changamoto ya Uongozi. Nilisoma, “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” (Julius Kambarage Nyerere 1994).

Hata Tathmini ya Miaka 20 ya CCM 1977 – 1997, ilisema,” matatizo ya ndani ya Chama yamezaa matatizo makubwa zaidi katika utekelezaji wa sera za CCM” uk. 34).

Kuondolewa kwa Ujamaa kulijionyesha katika Mapendekezo ya katiba kutoka CCM kwenda Tume ya Jaji warioba.

Ujamaa haukuwemo. Ndiyo maana Rasimu ya katiba 2013 na katiba Inayopendekezwa 2014 – Ujamaa haumo. Ujamaa uliotajwa katika Utangulizi – Misingi ya katiba, Ibara 3(I) na ibara 9(a)-(k)-ya katiba 1977-toleo la
2005-haumo.

Katika Makala hii nimetoa maelezo marefu kuhusu maono ya Baba wa Taifa kuhusu uasisi wa Taifa.

Nimeeleza jinsi Baba wa Taifa alivyofanikisha maono yake kwa kuasisi Taifa kwa kutumia dhana ya Taifa na Uongozi.

Katika Uasisi na Utambuzi, aliweka lengo na kulirasimisha katika katiba ya Taifa ili kuwaletea wananchi maendeleo kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Katiba ni Chombo Kikuu cha Uongozi wa Taifa kwa ajili ya kuongoza utungaji wa sheria kwa ajili ya kutawala nchi na wananchi.

Katika kufanya kazi hiyo, Baba wa Taifa alitumia Uongozi ndani ya TANU na baadaye ndani ya CCM. Alikitumia Chama cha TANU na baadaye CCM kwa kuwa alijua kuwa katika ulimwengu wa kitabaka kazi ya kuliongoza Taifa lazima iwe na wenyewe.

Nijuavyo mimi lengo la Taifa likisha rasimishwa katika katiba huwa halibadilishwi, bali kuboreshwa kulingana na mazingira na kanuni ya wakati na mahali.

Hata Bwana Yesu alipoulizwa iwapo alikuja kuibadilisha Torati alisema hapana ila Kuimarisha.

Lengo la Taifa la Marekani tangu liwekwe katika katiba, halijabadilika. Hivyo ndivyo ilivyo kwa China na Mataifa mengine yaliyo makini.

Katika Tanzania lengo la Taifa ni kujenga Ujamaa kwa mujibu wa Azimio la Arusha. Baba wa Taifa alionya kuhusu kushindania hadhi katika kutunga katiba.

Ukisoma “katiba inayopendekezwa” linaloonekana ni kushindania hadhi katika Jamhuri ya Muungano. Lengo la Taifa limeondolewa.

Nimetiwa moyo baada ya kusoma baadhi yaliyomo katika Sura ya Kumi ya Mwelekeo wa Sera za CCM miaka 2020 – 2030:-


1. Ibara 164- Sehemu ya Kwanza inaeleza umuhimu wa kushinda katika Chaguzi za Serikali za Mitaa na Serikali Kuu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sehemu ya Pili ya Ibara hiyo ina maneno yasemayo “… pia katika Ibara ya 5 (3) CCM inalo lengo la kuhimiza Ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea.


Kwa kuzingatia Malengo hayo ya Kikatiba ni wazi kwamba, chimbuko la Sera za CCM linatokana na Siasa yake ya Ujumaa na kujitegemea”.

Ningekuwepo wakati wa kuandika ningeandika –“… ni wazi kwamba chimbuko la siasa za CCM zinatokana na Imani na sera zake za Ujamaa na kujitegemea”. Kuandika hivi ni kuelewesha Sura mbili za Ujamaa alivyotueleza Baba wa Taifa.

2. Ibara 166- Inazungumzia Utekelezaji wa Majukumu ya kihistoria na Kimapinduzi ya kuongoza Mapambano ya kulinda na kudumisha uhuru wa nchi yetu na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na watu wake.

Hapa vile vile lengo la Ujamaa ni kudumisha uhuru wa nchi zetu au wa Taifa letu na Umoja. “Uhuru na Umoja” ni maneno yaliyomo katika nembo ya Taifa.

Uhuru utukumbushe Mapambano ya kuzikomboa nchi zetu – Tanganyika na Zanzibar. Umoja tukumbuke uasisi wa mataifa Mawili – Taifa la Tanganyika na Taifa la watu wa Zanzibar na hatimaye Taifa la Tanzania.

Nimefurahi kusoma kuwa Mapambano hayo ya kihitoria ni pamoja na kuwakomboa wananchi kutoka kwenye unyonge na umaskini na kuwapeleka kwenye maendeleo na maisha bora.

Ninakubaliana kabisa na lengo (a) la Ibara 166. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba misingi ya Uchumi wa Taifa letu imejengwa na inatakiwa iendelee kujengwa juu ya Imani na Sera za Ujamaa na Kujitegemea na kuimarisha demokrasia kama alivyosema Baba wa Taifa tarehe 22-10-1987 na Demokrasia hiyo ianze ndani ya Chama.

Baada ya kueleza haya, sasa naomba nirudi kwenye hoja, ambayo ni kwamba iwapo tulisahau au adui kuingia ndani ya Chama, basi tusome ibara 58, 59, 60, 61 na 62 ya Mwongozo wa CCM 1981, inayosema kuwa kujikosoa na kukosoana ni silaha ya Mapinduzi.

Ujamaa ulikwisha rasimishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba CCM ishiriki katika kuondoa changamoto kubwa katika kuendeleza misingi aliyotuachia Baba wa Taifa na maendeleo ya Taifa hili.


Hivi kuna maana gani kufanya Kumbukizi na huko misingi aliyotuachia hatuifuati? Alituonya kuwa katika kutunga Katiba tusishindanie hadhi kama nilivyosema hapo awali.

Nasikia Bungeni Mhe. Gwajima akisema Taifa halina lengo – lengo la taifa hili ni kujenga Ujamaa na kujitegemea.

Wasomi wa Taifa hili wako wapi? Pamoja na Maandishi mengi aliyotuachia Baba wa Taifa, imeshindikana kupata Mitala ya kufundisha Ujamaa shuleni mpaka Vyuo Vikuu!

Leo tunahangaika na Falsafa ya Elimu, baada ya kuiacha “Elimu ya kujitegemea”. Ilikuwaje Taifa likawa halina mitala ya kufundisha” Artizans and Technicians”? huko tunataka maendeleo ya viwanda?

Kuhusu Ujamaa – Azimio la Arusha katika mazingira ya vyama vingi – Karne ya Ishirini na moja – Cde. Mihanjo – hivi ule” Mwongozi wa utekelezaji wa Azimio la Arusha katika Mazingira ya siasa/mfumo wa vijana vingi vya Siasa tulioanzisha pale REPOA mwaka 2012 – uliishia wapi? Baba wa Taifa hakukataza marekebisho ya uchumi.

Mbona alisema “lakini marekebisho hayo yasiruhusu kabisa kufifia kwa lengo lenyewe la Ujamaa na kujitegemea, wala kufunga njia ya hatua ya baadaye ya kuelekea kwenye Ujamaa na kujitegemea”.

Iwapo CCM, kitasoma Ibara za Mwongozo wa 1981, kama nilivyoeleza, hapo awali, nakiomba kichukue nafasi yake ya Uongozi, kwa kuzingatia lengo la Taifa ujenzi wa Ujamaa kwa kutumia Kanuni ya Wakati na Mahali.

CCM kiache kujiita Chama Tawala – hiki siyo Chama tawala; kwa mujibu wa ibara 106 ya Mwongozo wa CCM 1981, CCM ni chombo kikuu cha Uongozi wa Taifa letu.

Katika Uongozi, Chama kiache Uliberali. Uliberali unaingizwa ili kudhoofisha mapambano dhidi yao kwani bado wanatafuta kila njia za kutudhoofisha ili waendelee kututawala kiuchumi.

Aidha ninaomba tuache tabia ya kutosoma Maandishi yetu.

Ni matumaini yangu kuwa hoja yangu imeeleweka.

Kidumu Chama cha Mapinduzi – Kidumu ili kazi Iendelee.
 
Bila machafuko huu uhuni uliopandikizwa na CCM ndani ya nchi hii hauwezi kuondoka. Nchi imewekewa matambiko kibao kiasi kwamba CCM wanadhani wana haki miliki ya nchi hii. Kusimama kwenye mstari wa kura ni kupotezeana muda, kwani CCM hawaheshimu tena uchaguzi.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom